Mawaziri wanaotoswa waache kujidhalilisha

OSOKONI

JF-Expert Member
Oct 20, 2011
10,971
2,000
KATIKA siku za hivi karibuni umeanzishwa utamaduni wa ajabu katika nchi yetu, ambapo mawaziri wanaoondolewa au kuachwa katika Baraza la Mawaziri wanakimbilia katika majimbo yao ya uchaguzi siyo tu kwa lengo la kupata huruma ya wapigakura , bali pia kujenga dhana kwamba kutemwa kwao na mamlaka iliyokuwa imewateua kumetokana na fitina na wivu wa washindani wao kisiasa katika chama tawala na serikali yake.

Mawaziri hao waliotemwa wamewatumia wapambe wao kuandaa maandamano makubwa katika majimbo husika, huku mabango makubwa yenye ujumbe wa kuwatukuza na kuwasifu mawaziri hao waliotemwa, ambayo yatatumika wakati wa maandamano hayo, yakitengenezwa kwa gharama kubwa. Lengo ni kuwathibitishia wapigakura kuwa, pamoja na kuondolewa katika nyadhifa zao za uwaziri bado wana nguvu na uwezo mkubwa wa kifedha kama ilivyokuwa wakati wa kampeni, hivyo wasianze kufikiria au kushawishiwa kutafuta mbadala wao katika majimbo hayo katika uchaguzi ujao.

Kinyume na ilivyokuwa huko nyuma, mawaziri waliotemwa siku za hivi karibuni wamegeuza matukio hayo kuwa mapokezi ya kishujaa mithili ya askari wanaopigana vita na kurudi nyumbani kidedea. Ndiyo maana mapokezi hayo yamefanywa ili kuwasafisha kwa kuwaandalia sherehe kubwa, ambapo wananchi walicheza, wakanywa, wakala na kusaza. Ni ujumbe kuwa, pamoja na kutemwa uwaziri, wao bado ni wabunge. Hivyo, lengo ni kudhihaki , kuasi, kubeza na kupimana nguvu na mamlaka iliyokuwa imewateua ili ighadhibike na kudhani kuwa, nyuma ya mawaziri hao iliowatosa ipo nguvu kubwa ya umma.

Pengine yafaa tukumbushane hapa kwamba utamaduni huo wa ajabu uliasisiwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na kufuatiwa na Edward Lowassa aliyelazimika kuachia kiti cha uwaziri mkuu. Hali hiyo imeshika kasi hivi sasa baada ya mawaziri William Ngeleja, Ezekiel Maige, Omari Nundu, Cyril Chami na Mustafa Mkulo kuondolewa katika nyadhifa zao. Ni Dk Haji Mponda pekee aliyeachishwa uwaziri pamoja na wenzake hao watano hivi karibuni lakini akaamua kukaa kimya.

Hayo ndiyo matokeo ya kutojifunza kutokana na historia, kwa maana kwamba watu hao walioachishwa uwaziri walishindwa kutambua kuwa, hawakuwa mawaziri wa kwanza kupokonywa nyadhifa zao hizo. Tunadhani wangefanya vyema iwapo wangetambua kwamba cheo ni dhamana tu, hivyo hawatazamiwi kutaharuki pindi mwenye dhamana yake anapoamua kuichukua. Hivyo ndivyo walivyofanya watangulizi wao, wakiwamo Iddi Simba, Juma Ngasongwa, Simon Mbilinyi na Ali Hassan Mwinyi ambaye alikuja kuchaguliwa katika vipindi tofauti kuwa Rais wa Zanzibar na baadaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mawaziri wanaoondoshwa na kupatwa ghadhabu na mfadhaiko kama hao tuliowataja wanashindwa kuelewa kwamba waliomba ubunge na siyo uwaziri, hivyo aliyewapa uwaziri huo anaweza kuuchukua pasipo kulazimika kutoa maelezo. Ni jambo la kushangaza kuona kuwa, baadhi ya mawaziri hao waliong’olewa wametoa vitisho kadhaa, ikiwa ni pamoja na kwamba wafuasi wao watahamia kambi ya upinzani.

Je, tumejifunza nini kutokana na sarakasi hiyo ya mawaziri waliotolewa katika Baraza la Mawaziri? Bila shaka wananchi watakuwa wamejifunza mengi, lakini pengine somo kubwa zaidi ya yote ni kwamba idadi kubwa ya watu wanaogombea ubunge wanafanya hivyo ili baadaye wateuliwe kuwa mawaziri. Hapo ndipo inapozuka hoja katika kujadili sheria ya mabadiliko ya Katiba kuwa, ili kuhakikisha wabunge wanaochaguliwa na wananchi kuwawakilisha bungeni wawe wawakilishi wao kweli, ipo haja Katiba Mpya itamke kwamba mawaziri wasiwe wabunge ili yeyote atakayeomba ubunge ajue fika kwamba anaingia bungeni kuwakilisha wapigakura wake na siyo vinginevyo.

Mawaziri hao waliotupwa wametufumbua macho kwamba walipewa uwaziri pasipo kuwa na dhamira ya kuwatumikia wananchi na ndiyo maana wanalia kwa madai ya kuhujumiwa kana kwamba kwao uwaziri ni urithi wao wa kuzaliwa. Ndiyo maana wanaona uwaziri ni ngazi ya kupata ulaji kwa faida yao, ndugu zao na washirika wao. Wananchi kamwe wasikubali kudanganywa na watu hao kwa kupewa pombe na shibe ya siku moja.

 

Jujuman

JF-Expert Member
Dec 7, 2008
248
0
Osokoni:
Mambo mengine watu hufanya kwa mwelekeo potofu "Bendera Hufuata upepo"
Niliposikia Wanajimbo fulani wakijipanga kumlaki Mbunge wao kwa hiyoyo (baada ya kuondolewa Uwaziri) Nilihoji juu ya Lengo, Madhumuni na Tija itakayopatikana kwa kufanya hivyo sikupata jibu lenye mwelekeo. Nikauliza kama muhusika ameataarifiwa na nini maoni yake. Wakadai ametaarifiwa na Amefurahia jambo hilo.
Kwa hiyo maandamano yanafanyika muhusika anapata fursa labda ya kujisafisha au kujitetea na kujinadi upya kuwa yeye ni Ngangari kwa jimbo lake. Then What.....................!!
 

m_kishuri

JF-Expert Member
Jan 27, 2010
1,485
1,225
Binafsi sioni ubaya wowote wa hao mawaziri kwenda kujitetea majimboni kwao. Why? Kwa sababu ni haohao wananchi waliomchagua kama mbunge wako kabla ya uwaziri. Kwa hiyo. ni lazima awaeleze yaliyotokea. Vinginevyo. Itawabidi waamini Yale waliyosikia kutoka kwenye vyombo vya Habari.
 

Jujuman

JF-Expert Member
Dec 7, 2008
248
0
Kuna makala inayodai Polisi Tanga walisitisha Maandamano ya kupokewa kwa Mbunge wa jimbo hilo Mh.Omari Nundu. Tukio hilo linaleta mtazamo tofauti. ( Mh. Nundu ni mmoja wa Mawaziri walioondolewa katika wadhifa huo)
 

Mbinga

Member
Apr 1, 2012
68
70
Kuna makala inayodai Polisi Tanga walisitisha Maandamano ya kupokewa kwa Mbunge wa jimbo hilo Mh.Omari Nundu. Tukio hilo linaleta mtazamo tofauti. ( Mh. Nundu ni mmoja wa Mawaziri walioondolewa katika wadhifa huo)
Hawasomi alama za nyakati hao.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom