Mawaziri, wabunge na wananchi kulilia misaada kwenye ziara za Rais Magufuli kwazua mjadala

Hivi punde

JF-Expert Member
Apr 1, 2017
2,554
8,552
Kuna usemi wa wahenga kwamba unapobahati kukutana na mfalme, basi eleza shida zako zote. Hekima nyuma ya usemi huu ni kwamba huenda fursa hiyo isipatikane tena kwa kuwa mfalme kutokana na majukumu yao.

Hivyo ndivyo ilivyo hata kwa wananchi wanapobahatika kukutana na viongozi wao hususan Rais. Wengi wamekuwa wakitumia fursa hiyo kutoa vilio vyao juu ya kero mbalimbali zinazowakabili.
Lakini katika siku za karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la maombi hayo si kutoka kwa wananchi tu, bali hata baadhi ya mawaziri, wabunge na viongozi mbalimbali wa Serikali, taasisi zake na wanasiasa.

Katika ziara zake mbalimbali, Rais Magufuli amekuwa akitoa nafasi kwa mawaziri, wabunge na wananchi kuzungumza, nafasi ambayo wengine wamekuwa wakiitumia kumuomba awasaidie miradi iliyokwama, ikiwamo ujenzi wa barabara, shule, zahanati na umeme.

Katika ziara yake ya siku tatu mkoani Morogoro, Rais Magufuli wakati akielekea katika uzinduzi wa Daraja la Magufuli katika Mto Kilombero, alitoa Sh5 milioni za ujenzi wa shule katika Kijiji cha Mkula na Sh3 milioni za ujenzi wa vyoo kwenye Shule ya Sekondari Mang’ula baada ya kusimamishwa njiani na wananchi waliomueleza kero zao.

Pia, wakati akizindua daraja hilo na stendi ya mabasi ya Msamvu, wabunge wa Mkoa wa Morogoro walipewa nafasi ya kuzungumza na karibu kila mmoja alimuomba kusaidia kutatua shida mbalimbali.
Akizungumza katika uzinduzi wa daraja hilo, Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali alimuomba Rais Magufuli kuzungumza na askofu wa Kanisa Katoliki ili aridhie kuliachia eneo lake ambalo limevamiwa na wananchi.

Hakuwa Lijualikali pekee ambaye alitoa maombi hayo pekee, bali wabunge karibu wote waliozungumza baada ya kupewa fursa hiyo na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.

Hata alipokuwa mkoani Dodoma, katika uzinduzi wa Barabara ya Kondoa – Babati, Naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji alimuomba kusaidia ujenzi wa barabara ya kuelekea Itotoro yenye urefu wa kilomita sita inayoungana na barabara hiyo kuu.

Naibu waziri huyo pia alikumbushia ombi lake la kumaliza mgogoro wa mashamba ya wananchi wa Kondoa yaliyopo katika pori la Mkongonero.

Kauli za wasomi.

Baadhi ya wasomi waliotakiwa kutoa maoni yao juu ya maombi hayo yanayoelekezwa kwa Rais walitoa maoni tofauti, wakati wengine wakisema jambo hilo halina ubaya wowote kwa kuwa Rais ndiye kiongozi mkuu wa nchi wapo waliosema kwamba hali hiyo inatokana na mamlaka ya Serikali za Mitaa kukosa nguvu.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha (Ruco), Gaudence Mpangala alisema hali hiyo inatokana na msimamo wa kiongozi huyo kutoa uamuzi papo kwa papo.
“Wananchi wanakaa na madukuduku yao wakimsubiri Rais kwa kuwa watapata majibu ya uhakika. Jambo hili ni zuri, lakini halitaleta usawa wa maendeleo na muda mwingine fedha zinazotolewa zinakuwa nje ya mfumo wa bajeti inayopitishwa na Bunge,” alisema Profesa Mpangala.

Kuhusu wabunge alisema wanafanya hivyo kwa sababu wanajua Rais ndiye mtoa uamuzi wa mwisho kutokana na msimamo wake wa kusikiliza na kutoa majibu papo kwa papo.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana alisema hilo ni jambo jema kwa sababu Rais ndiye mwenye ya kutoa uamuzi wa kero husika.

“Wananchi na wabunge wanajua wakipeleka maombi kwa Rais watapatiwa majibu papo kwa papo, kuliko kupeleka kwa wakurugenzi ambao wanafanya kazi kwa niaba ya mkuu wa nchi,” alisema Profesa Bana.
Hata hivyo, Profesa Bana aliwakosoa baadhi ya mawaziri wanaowasilisha maombi kwa Rais ambayo alisema wanaweza kuyashughulikia wenyewe kwa ngazi ya uwaziri, “Waziri sio lazima useme hadharani, unaweza kulimaliza jambo kwa kuzungumza na waziri mwenzako.”

Katika ufafanuzi wake, mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Hamad Salim alisema wananchi wanajisikia faraja kuzungumza na kuwasilisha kero au maombi yao moja kwa moja na moja kwa Rais.

Alisema hali hiyo inatokana na mamlaka za Serikali za mikoa na mitaa kukosa meno, “Ndio maana baadhi ya shughuli ikiwamo kodi ya majengo inafanywa na Serikali kuu kupitia TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) badala ya manispaa au halmashauri.”

Salim alisema kutokana na hali hiyo, wananchi wamejijengea fikra kuwa ili maombi yao yashughulikiwe, lazima wayawasilishe kwa Rais ambaye atatoa majibu badala ya kwenda ngazi za chini ambako watendaji wake huwa wanapata kigugumizi kutoa uamuzi.

Mhadhiri mstaafu wa Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam, Balozi Ahmed Kiwanuka aliungana na Profesa Bana akisema hatua hiyo ni nzuri kwa sababu inawapa fursa wananchi kuzungumza moja kwa moja na mkuu wa nchi.

“Kwa Kihaya tunasema mfalme ni yule anayemaliza shida hapohapo kwa mtu anayemlilia. Ukimkuta maliza shida zako, ukisubiri utachelewa,” alisema.
Alisisitiza, “Wajibu wa mfalme ni kutembelea, kuangalia wananchi wake na kutatua matatizo yanayowakabili. Hiki ndicho anachokifanya Rais na wananchi, wabunge, mawaziri hawajakosea kueleza maombi yao kwake.”

Mhadhiri wa UDSM, Dk Richard Mbunda alisema Katiba ya nchi inampa madaraka makubwa Rais ya kuendesha Serikali.
Alisema wabunge na mawaziri wanawasilisha maombi kwa mkuu huyo wa nchi kwa sababu wanamuona ni mchapakazi na jambo lao litafanikiwa.

“Tanzania ni maskini na bajeti za baadhi ya wizara zinakuwa finyu ndio maana upungufu mwingi unajitokeza. Mbunge hana bajeti, anaishi kwa ushawishi ili atekeleze miradi yake ya maendeleo. Rais akiwa mchapakazi anayependa maendeleo, lazima wananchi wajitokeze kumuomba kwa sababu yeye ndio mtu wa mwisho wa kutoa kauli,” alisema.

“Tutarajie kuona maombi zaidi katika maeneo yote atakayopita Rais kutokana na hali halisi. Watu wanafuatilia ziara za Rais anakopita na wana historia ya namna anavyowasaidia wale wanaojitokeza kuomba msaada kwake ikiwamo fedha lakini ukiniuliza kisheria limekaaje hapo sina jibu.
 
Maskini waziri wa msimu huu hawana amani,ni kama wanawaambi wananchi semeni wenyewe sisi pia hatusikilizwi hoja zetu.
 
Hii ni kwakua tumeaminishwa mwenye kutoa pesa kwa sasa ni rais, hivyo akipita lazima watu waeleze matatizo yao!
 
Ni aibu kwa taifa (Serikali?) na hasa pale Waziri anaposimama kumwomba Rais kusaidia mradi fulani mkoani au jimboni mwake (auhata sehemu yoyote ile). Hii inaonyesha Baraza la Mawaziri halifanyi kazi zake maana Waziri alipaswa kujua uwezo wa Serikali. Inaonyesha pia kuwa maamuzi yako kwa mtu mmoja (Rais) ambayoni tatizo la kimfumo na Waziri anaonyesha kuwa madaraka yako kwa mtu mmoja! Waziri katika hali yoyote ile hapaswi kuomba hadharani kwa mkuu wa serikali aliyomo. Yeye ni mmoja wa watoa maamuzi.
 
Back
Top Bottom