Mawaziri na leseni zao za kuboronga

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,039
Mawaziri na leseni zao za kuboronga

Lula wa Ndali-Mwananzela Desemba 26, 2007
Raia Mwema

MOJA kati ya filamu nyingi za James Bond (007) ambayo ilitolewa mwaka 1989 na kuvutia watu wengi ilikuwa inaitwa “License to Kill”.

Katika filamu hiyo James Bond alikataa maagizo rasmi ya ‘M’ ya kwenda kufanya kazi yake ya kipelelezi huko Uturuki na badala yake aliamua kujiuzulu na kwenda kulipiza kisasi cha rafiki yake aliyeuawa mikononi mwa kigogo wa madawa ya kulevya Franz Sanchez.

Kitendo cha James Bond kukaidi agizo la mkuu wake kilisabaisha leseni yake ya kuua (bila kuomba kibali au kwa kupewa amri) isimamishwe. Maafisa wengi wa usalama (wanajeshi, polisi n.k) kutokana na wajibu wao wa kazi wanakuwa na uwezo huu wa kuweza kutumia nguvu hata za kuua wanapotekeleza majukumu yao lakini katika masharti yanayoeleweka.

Ni kwa sababu hiyo basi polisi au maafisa usalama wanaweza kujikuta wakilazimika kuua mtu katika kutekeleza wajibu pasipo kushitakiwa. Wanafanya hivyo kwa vile kutokana na wajibu wao wanacho kile tunachoweza kukiita ‘leseni ya kuua’.

Niliposikiliza maelezo ya Rais Jakaya Kikwete alipozungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita na kutangaza wazi kuwa licha ya baadhi ya mawaziri wake kuboronga kwa kiasi kikubwa na licha ya utafiti wa hivi karibuni wa REDET kuonyesha kuwa Serikali yake imepoteza umaarufu, yeye aliamua kuwakingia kifua mawaziri wake na kwa kufanya hivyo kuwahakikishia kuwa wanaendelea kuboronga pasipo hofu ya kupatwa na matatizo yoyote.

Uamuzi wa Rais wa kuamua kuchukulia malalamiko na manung’uniko ya wananchi juu ya utendaji kazi wa baraza lake kuwa “ni matakwa ya watu” tu ni kuwapa kichwa mawaziri wake ambao sasa wanajua kuwa Rais yuko upande wao.

Ni wazi kuwa kuna baadhi ya mawaziri ambao kwa hakika si tu wamemuangusha Rais lakini kwa hakika haingii akilini ni kwa nini bado wako kwenye nafasi zao na ni kwa nini Rais amewapa hizi leseni za kuboronga. Kwa tunaofuatilia kwa karibu utendaji kazi wa baraza, jambo tunalojiuliza sana ni ‘mpaka lini?’, mawaziri hawa wataendelea na nafasi hizi?

Hivi ni kweli kuwa katika Tanzania mawaziri tulionao sasa ndio wanafaa kuliamsha Taifa na kulipeleka kule kwenye neema? Hivi kati ya watu wote ambao Rais Kikwete angeweza kuwateua kwenye nafasi mbalimbali, hawa 60 ndio kwa kweli tunaweza kuweka matumaini yetu kwao?

Binafsi ninaona kuwa kitendo cha Rais kuwakingia kifua ni kitendo cha kuwapa ‘leseni ya kuboronga’ ili waendelee kuboronga kwa kadiri wanavyoweza kwa kutumia kauli mbinu ya utawala wake. Yaani, kuboronga kwa ‘ari mpya, kasi mpya, na nguvu mpya’.

Tuwaangalie basi baadhi ya mawaziri hawa ambao kwa hakika ni shaka kuendelea kupepewa na bendera ya Taifa. Ni kama kejeli na dhihaka kwa umma. Viongozi wafuatao ni viongozi ambao neno ‘uongozi’ halistahili kuwekwa kwenye sentensi moja na majina yao. Ni hawa ambao kwa hakika wamemuangusha Rais Kikwete na kwa hakika hata kama hatavunja Baraza lake la Mawaziri kama alivyosema lakini kwa vile ameacha mlango wazi wa kulifanyia mabadiliko basi watu hawa wataonyeshwa mlango wa kutokea na kutimuliwa bila kupewa Uenyekiti wa Bodi au ‘kauteuzi’ kengine kama ilivyo kawaida ya watawala wetu.

Wa kwanza bila ya shaka ni Waziri wa Madini na Nishati Nazir Karamagi. Waziri huyu ni kwa hakika hawezi kusameheka katika historia ya madini nchini. Kitendo chake cha kuhalalisha mkataba wa Buzwagi na kulidanganya Bunge bila adhabu yoyote ni kitendo ambacho hakimstahilishi hata kidogo kuendelea kushika wadhifa wowote serikalini.

Yeye ni mfanyabiashara na wakati umefika arudi kwenye biashara zake. Aachane na madini yetu. Hata hivyo kabla ya kumtimua itakuwa vizuri kama tutaambiwa na yeye kama Daniel Yona, hajaanzisha ka kampuni na Rais Kikwete ambako kataanza kuuza umeme baada ya kuvunja Shirika la Tanesco.

Leo hii wanaposimama kuleta mswada wa kulivunja shirika la Tanesco (kama alivyosema Rais kwenye mkutano wa waandishi wa habari) hatuna budi kujiuliza kuwa kwa miaka yote hilo si lengo lao? Kwamba wameliingiza shirika hili kwenye madeni hadi shingoni ili lishindwe na badala yake wao wapate nafasi ya kuingia (na vikampuni vyao) katika biashara ya umeme? Je, si kweli kuwa rais msitaafu, Benjamin Mkapa, Yona na wenzao waliingia mikataba mibovu kwenye shirika hili ili Kiwira ipate nafasi ya kuanza kuuza umeme?

Je, Karamagi hana hisa yoyote kwenye makampuni ya nishati (yeye au familia yake?). Kuna uhalali gani wa kulivunja shirika la Tanesco ili wao waje na vikampuni vyao kuanza kutuuzia umeme? Kwa vile Karamagi ndiyo mwenye dhamana hii na kusimama kwake kulivunja Tanesco ni kitendo cha usaliti wa ofisi yake na kuliandaa Taifa kwa ushindani ambao Tanesco tayari imeshindwa! Sasa amepewa leseni ya kuboronga.

Mwingine ni Dk. Ibrahim Msabaha. Waziri Msabaha ndiye aliyetuingiza kwenye Richmond yeye na marafiki zake. Yeye na Rais Kikwete, Balozi Andrew Daraja, na hata kina Waziri Mkuu ndio wanajua kwa hakika nini kiliendelea hadi Taifa la watu wenye akili timamu likaingia mkataba wa ukichaa wa Richmond.

Baada ya watu kulalamika, Dk Msabaha alihamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki. Yeye, kutokana na sakata hiyo ya Richmond, ni miongoni mwa ambao hawakustahili kuendelea kuwamo kwenye Baraza la Mwaziri. Lakini naye alipewa leseni ya kuendelea kuboronga.

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, sasa Waziri wa Miundo Mbinu Andrew Chenge naye ni mtu aliyelindwa na kupewa leseni ya kuendelea kuboronga. Kati ya Watanzania ambao kwa hakika wanastahili kubanwa na kulazimishwa kutoa maelezo ya kwa nini nchi yetu imeingia kwenye mikataba mibovu na kuwa na sheria za ajabu ajabu ni Chenge.

Yeye amekuwa mshauri mkuu wa mambo ya Kisheria wa Serikali ya Muungano na ni chini ya uongozi wake ndipo Taifa limeingia kwenye mikataba ya ajabu ajabu. Ni yeye ambaye ofisi yake haikujipanga kukabiliana na sheria za matumizi mabaya ya ofisi kiasi kwamba rais na waziri wake wanafungua biashara wakiwa Ikulu huku Mwanasheria Mkuu akiona.

Siyo hivyo tu, Mwanasheria huyo Mkuu alishindwa kuhakikisha kuwa Bunge linatekeleza amri za mahakama kwa kuandika sheria ambazo zinaakisi maamuzi ya mahakama.

Kitendo cha Chenge kutokusimamia haki ya wananchi ya kuchaguliwa kama wagombea huru na sasa miaka imepita huku Bunge likiendelea kusua sua ni kitendo kinachoonyesha kuwa si mtu wa kuaminiwa katika dhamana ya uongozi nchini.

Akiwa Mwanasheria Mkuu Chenge alifumbia macho sheria mbovu zilizoletwa bungeni (kama ile iliyohalalisha rushwa kwa jina la Takrima). Akitumia nafasi yake hiyo alishindwa kuweka maslahi ya Taifa mbele na badala yake aliangalia maslahi ya chama chake ambacho baadaye kilimzawadia kumteua kugombea Ubunge na baadaye kumpa Uwaziri wa Miundo Mbinu.

Leo hii wakati Tanzania inahangaika na jinsi gani miundo mbinu yetu imedorora yeye ameamua kusaka umaarufu kupitia kwa Mahujaji. Ameshindwa kusimamia ujenzi wa barabara kwa kiwango kinachostahili, ameshindwa kusimamia uendeshaji wa vyombo mbalimbali vya usafiri na ameshindwa kuilinda miundo mbinu.

Kuna mtu kweli anaweza kutuambia ni kwa nini Chenge bado ni Waziri? Ni kitu gani amekifanya kwenye Taifa kiasi kwamba hawezi kuondolewa?

Waziri mwingine Profesa Peter Msolla wa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu. Huko nyuma Watanzania tuliamini kuwa mtu akiwa msomi basi yawezekana kuwa ni kiongozi mzuri. Mara nyingi tukisikia mtu ni ‘pofesa’ basi tunaamini kwa haraka kuwa ‘anaweza kuongoza’. Mfano wa Msolla ni mfano unaoonyesha kuwa usomi na uongozi si kitu kimoja na havifanani.

Mtu anaweza kuwa kiongozi mzuri na asiwe profesa wa fani yoyote ile na mtu anaweza kuwa profesa aliyebobea lakini akawa kiongozi mbovu na mbaya. Profesa Msolla ni ushahidi wa jambo hili. Chini ya uongozi wake Tanzania imekabiliwa na changamoto na matatizo makubwa zaidi katika elimu ya juu yawezekana kuliko wakati wowote ule katika historia.

Migomo na ucheleweshaji wa mikopo ni baadhi tu ya matatizo makubwa ambayo Profesa Msolla na timu yake wameshindwa kuyashughulikia. Profesa Msolla ni aibu ya wasomi nchini na kitendo cha Rais kusema kuwa ‘hakuna tatizo’ kwenye baraza lake ni kukejeli akili za Watanzania.

Alionyesha kiburi chake cha madaraka na ubabe wa uongozi pale alipotumia mabavu kuwarudisha vijana wa Kitanzania waliokuwa masomoni toka Ukraine. Cha kuudhi na kukera ni kuwa kila akipata nafasi ya kuhutubia hachoki kusema ‘Taifa letu liko nyuma kwenye elimu ya juu, kulinganisha mataifa mengine’.

Binafsi naamini kabisa kuwa kati ya watu ambao wamelitendea vibaya Taifa mwaka huu, wa kwanza bila ya shaka ni Karamagi na wa pili ni Msolla! Wameweka mbele maslahi ya chama chao kuliko maslahi ya wana na mabinti wa Taifa hili. Kwa nini leo wanaendelea kukalia ofisi zao ni suala ambalo linasumbua fikra za wengi.

Kuna wengine ambao kuwataja mmoja mmoja na mambo yao kutajaza kurasa. Yupo Edward Lowassa, kiongozi mahiri, shujaa aliyetamba bungeni; yupo Basil Mramba, mtu ambaye bila ya shaka amefungwa katika muda akifikiria uchumi na biashara bado zinaendeshwa kama miaka ile 1980; yupo Joseph Mungai (msiniulize kwanini alirudi kwenye Baraza); yupo Kingunge Ngombare Mwiru (mkomonisti mbepari wa kijamaa), na wengine wengi.

Ni wazi kuwa wapo mawaziri ambao wamefanya vizuri na kitendo cha Rais kuwakingia kifua kinaweza kukubaliwa. Hata hivyo kuendelea na baraza hili jinsi lilivyo bila kulipangua ni kuwapa kiburi mawaziri kuwa wao ni kama miti mitakatifu isiyokatwa hata kama mizizi yake ina sumu inayoharibu shamba.

Tunapoelekea mwaka 2008 Rais Kikwete anakabiriwa na changamoto moja kubwa, kuonyesha uongozi pale unapohitajika. Kama baraza la watu 30 hivi na manaibu wao limeshindwa kuwapa watu matumaini, kwanini asijaribu na baraza dogo ambalo msingi wake ni uwajibikaji?

Inakuwaje leo mawaziri wasiwasiliane ndani kwa ndani na badala yake siri za Serikali zinavuja kuliko magunia ya machungwa katika soko la Makorola au yale ya dagaa pale Mwaloni Mwanza? Ni kitu gani hadi kitokee ndipo Rais Kikwete atatambua kuwa baraza alilolanalo ni baraza butu, lisilowajibika na lililojaa wasanii wa kisiasa?

Ninapowatakia salamu za mwaka mpya ni matumaini yangu kuwa Rais Kikwete hatawaacha Watanzania waendelee kukata tamaa jinsi walivyokata tama mwaka huu. Ni matumaini yangu na bila shaka ya wengine kuwa Rais Kikwete ataamua kuonyesha kuwa katika Tanzania Taifa linapendwa zaidi kuliko mtu, na hakuna mtu binafsi.

Endapo Rais Kikwete ataendelea kuitetea hii leseni ya kuboronga na kuwaacha viongozi butu waendelee na nafasi zao, basi ajue kabisa ya kuwa mwisho wa siku ni yeye na chama chake ambao watalipa gharama kubwa kwenye sanduku la kura. Kama anadhani Watanzania, katika hali hii ya uborongaji, wataendelea kumchekea chekea na kumshangilia anadanganya nafsi yake.

Kwa vile anaamini kuwa ana miaka mingine mitatu ya kutekeleza ahadi za CCM na hivyo wananchi waache mchecheto basi ajue kabisa kuwa kuna watu ambao wanataka ashindwe na aboronge ili ifikapo 2010 waweze kuonyesha ni kwa nini Watanzania walifanya makosa kumpa Urais.

Baadhi ya waliomo kwenye baraza lake wanataka ashindwe na afeli ili watengeneze mazingira ya kumfanya Rais Kikwete kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kutawala kwa mhula mmoja. Kama anafikiri hilo haliwezekani arejee methali ya Kuswahili: Adhaniaye kuwa amesimama, aangalie asianguke.
 
Nice piece overall,ninashangaa anaongelea kukerwa na "siri za serikali kuvuja".Serikali nzuri ni ile isiyo na siri.

Natumaini KLowassa hatatuma vikaragosi wake kumfuatilia mwandishi.Inatia imani kuona tuna semblance ya uhuru wa vyombo vya habari, miaka michache tu iliyopita wangem-katabalo.
 
Sasa huyo naye anataka kujipandisha chati tu. Huko nyuma wenzio walikuwa wanazungumza kwa ujumla jumla. Sasa tangu wapinzani wataje watu majina naona kila mtu anataka na yeye ataje majina. Ufisadi kama alivyosema Baba Askofu Kilaini kwenye misa ya usiku juzi, "ni wetu sote".

asante
 
Sasa huyo naye anataka kujipandisha chati tu. Huko nyuma wenzio walikuwa wanazungumza kwa ujumla jumla. Sasa tangu wapinzani wataje watu majina naona kila mtu anataka na yeye ataje majina. Ufisadi kama alivyosema Baba Askofu Kilaini kwenye misa ya usiku juzi, "ni wetu sote".

asante

Hebu fafanua unaposema ufisadi ni wetu sote una maana gani? Natanguliza shukrani.
 
Sasa huyo naye anataka kujipandisha chati tu. Huko nyuma wenzio walikuwa wanazungumza kwa ujumla jumla. Sasa tangu wapinzani wataje watu majina naona kila mtu anataka na yeye ataje majina. Ufisadi kama alivyosema Baba Askofu Kilaini kwenye misa ya usiku juzi, "ni wetu sote".

asante

Wetu sote wewe na nani? unaweza kuwataja wenzako hapahapa tuwafuatilie?

Naelewa cocept nzima ya "uongozi ni reflection yetu" lakini Askofu Kilaini naye anakuja na apologists arguments kwa sababu mimi sijapigia kura uozo huu na wala sijisikii responsible kwa aina yoyote, sasa utaniambiaje ufisadi ni wetu sote wakati wengine wanabwia matunda ya Kiwira wakati mimi sina ngawira?
 
Statement ya Kilaini ni msimamo wa Pengo.Lazima waseme hivyo kwa kuwa wote wanaacha kuhubiri dini na wanafanya biashara kwenye nyumba za Ibada . Kwa miaka kadhaa sasa Pengo aliwasimamia maaskofu kuhakikisha CCM inashinda ili kumuenzi Nyerere kwa kuwa yeye nu Muumini wa mwalimu sana na mwana CCM mkubwa.Sasa lazima waanze na hayo maana wanajua wanavyo shiriki kuwapa kura mafisadi wenzio .
 
Labda anamaanisha "like begets like", yaani kwa kuwa sisi sote (ama wengi wetu) tu mafisadi, basi hata kiongozi tutakayemchagua ana chances kubwa sana za kuwa fisadi kwani amezaliwa na kulelewa katika jamii ya mafisadi. Hata viongozi wetu wa dini wametoka katika jamii ya mafisadi, nao pia ni mafisadi. Hata viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani wametokana na jamii ya mafisadi!

Unajua kwa nini wamarekani wa jimbo moja (silikumbuki, lakini lilitangazwa sana) walimchagua mchungaji "shoga" kuwa askofu? Mtaalamu mmoja alieleza kuwa askofu hutoka katika jamii, hivyo watachagua anayewakilisha vema jamii hiyo. Na kwa kuwa wengi katika sehemu hiyo ni mashoga, wakaona huyo ndiye mwakilishi sahihi wa "majority", palepale "like begets like", jumuiya ya kishoga kupata askofu shoga kwao ni sawa, kwa wasio mashoga ndio tunashangaa hadi tunakaribia kuzimia!

Conclusion: "Fisadi begets fisadi"! Kwa hiyo tufute kwanza "ufisadi" miongoni mwa jamii, ili idadi ya mafisadi watakaogombea uongozi ipungue, na hata wakiwepo washindwe kura kwa maana wapiga kura watakuwa hawana ufisadi, hawatapiga kura kifisadi, na ndivyo tutakavyoondoa ufisadi nchini. Huu ufisadi inaelekea ni "systemic", uko katika mishipa ya damu zetu. Wale ambao hawajadhihirisha ufisadi mbele ya umma ni kuwa tu hawajapata nafasi hiyo. Yaani tunahitaji dawa kali kabisa, sindano ya mshipani (ile wataalamu wanaingizia kwa dripu), izunguke kwenye system yetu hadi ufisadi ututoke!
 
I understand your rationale, lakini kuutokomeza ufisadi completely ni a Selassian abstract, to be proverbially "pursued, but never attained".

This is a terrible breed of pessimistic resignation.Viongozi wanatakiwa ku-inspire hope.

Mbona Papa John Paul pamoja na labels zote alizovikwa aliweza kukemea tyranny Poland na kuchangia sana kuangusha ukomunisti?

Je angesema tu, "ukomunisti umezaa ukomunisti" na kumlaumu victim leo Lech Walesa na Solidarity wangeweza ku-make history?

Viongozi wa kidini wanatakiwa ku-inspire the struggle, sio kuwa apologists wa mafisadi.
 
The right to call for accountabilit is not the right for Politicians only. Infact katika nchi zilizoendelea, Waandishi wa Habari ndiyo nguzo kubwa kuhakikisha Serikali (Kuu, Bunge na Mahakama) wanakuwa wawajibikaji kwa wananchi.

Je kwa ni siri kuhusu hayo majina aliyoyataja na jinsi alivyoyachambua? Nope, infact it is fair game!
 
hapa kuna maneno mazito.. ila hao raia mwema sijui wanasilimika vipi. Naona tuendeleze mapambano kwani ni yetu sote.
 
Sasa huyo naye anataka kujipandisha chati tu. Huko nyuma wenzio walikuwa wanazungumza kwa ujumla jumla. Sasa tangu wapinzani wataje watu majina naona kila mtu anataka na yeye ataje majina. Ufisadi kama alivyosema Baba Askofu Kilaini kwenye misa ya usiku juzi, "ni wetu sote".

asante

unantisha(ga) sijui kwa nini!
 
Unajua kwa nini wamarekani wa jimbo moja (silikumbuki, lakini lilitangazwa sana) walimchagua mchungaji "shoga" kuwa askofu? Mtaalamu mmoja alieleza kuwa askofu hutoka katika jamii, hivyo watachagua anayewakilisha vema jamii hiyo. Na kwa kuwa wengi katika sehemu hiyo ni mashoga, wakaona huyo ndiye mwakilishi sahihi wa "majority", palepale "like begets like", jumuiya ya kishoga kupata askofu shoga kwao ni sawa, kwa wasio mashoga ndio tunashangaa hadi tunakaribia kuzimia!

Hapa umekosea, mkuu! Kinachotumika kwa wenzetu ni kuchagua mtu bila kuangalia kama ni shoga au la. Kinachoangaliwa ni uwezo wake wa kuongoza na kutetea maslahi ya waliomchagua. Ushoga, kama vile gender na rangi vimeondolewa kuwa kikwazo kwa mtu kutumikia. Ni hilo tu, sasa turudi kwenye mada.
 
Back
Top Bottom