Mawaziri 12 kuwakutanisha wawekezaji, wafanyabiashara Ruvuma

diana chumbikino

JF-Expert Member
May 29, 2018
428
368
Mawaziri 12 wa Serikali ya Tanzania leo Jumanne Septemba 24, 2019 watahudhuria mkutano wa wawekezaji na wafanyabiashara mkoani Ruvuma. Lengo la mkutano huo ni kusikiliza kero za wawekezaji na wafanyabiashara na kuzitafutia ufumbuzi ili kutengeneza mazingira ya kuwekeza zaidi na kukuza uchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumatatu Septemba 23,2019 mkoani Ruvuma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu –Uwekezaji, Angellah Kairuki alisema katika kutekeleza dhamira ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, Serikali Kuu ngazi ya za Ofisi ya Rais Tamisemi na ofisi ya waziri mkuu pamoja na wizara za kisekta wamepanga mkutano huo.

Alisema mikutano hiyo ya mashauriano kati ya Serikali na sekta binafsi ambayo itafanyika ngazi za mikoa nchi nzima Waziri Kairuki alisema awamu ya kwanza ya mikutano hiyo itafanyika katika mikoa mitatu ambayo ni Ruvuma (leo), Mtwara kesho Jumatano na Lindi Alhamisi ya Septemba 26, 2019. Aliwataja baadhi ya mawaziri watakaoshiriki mkutano wa leo Ruvuma ni; Innocent Bashugwa (Viwanda na Biashara), George Simbachawene (Mungano na Mazingira) na Jenista Muhagama (Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu). Wengine ni; Willium Lukuvi (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Dk Medard Kalemani (Nishati), Doto Biteko (Madini) na Dk Philip Mpango wa Fedha na Mipango.

Waziri Kairuki alisema maandalizi ya mikutano hiyo imeshirikisha kwa kiasi kikubwa taasisi na vyama vya sekta binafsi vilivyopo kwenye mikoa husika kwa utaratibu wa sekretariati za mikoa hiyo. Alisema Serikali imedhamiria kukuza mchango wa viwanda hasa vinavyohusiana na kilimo ili kutoa soko la mazao ya kilimo hivyo kukuza ajira kwa watu wa kawaida hasa vijijini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme alisema tayari mkoa umejipanga kimkakati ambapo mkoa umeanza kunufaika kwa kupata wawekezaji katika sekta mbalimbali baada ya kufanya kongamano la uwekezaji na kuzindua mwongozo wa uwekezaji Ruvuma. Alisema tayari wamepata wawekezaji kwenye sekta ya kilimo, afya, elimu na utalii pamoja na viwanda ili kuweza kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.
 
Back
Top Bottom