Mawakili Tanesco kuanika hukumu ya Dowans

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
219,470
911,173
Mawakili Tanesco kuanika hukumu ya Dowans
Saturday, 11 December 2010 21:00

Sadick Mtulya

JOPO la mawakili waliokuwa wakilitetea Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika kesi dhidi ya Kampuni ya Dowans, limesema litazungumzia hukumu ya kesi hiyo wiki ijayo.
Hukumu hiyo imeitaka Tanesco kuilipa Dowans fidia ya mabilioni ya fedha. Hata hivyo Tanesco imetahadharisha kuwa kuna siri nyingi zilizo kwenye kesi hiyo ambazo ikibidi watalazimika kuziweka hadharani.

Novemba 15, mwaka huu Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC), iliitia hatiani Tanesco na kuitaka ilipe fidia ya zaidi ya Sh185 bilioni kwa Dowans baada ya kukatisha mkataba wa kuzalisha umeme mwaka 2008 bila kufuata taratibu.

Katika kesi hiyo, Dowans iliwakilishwa na Kampuni ya uwakili ya ALN ya Afrika Kusini ambayo inafanya kazi zake nchini Kenya(Nairobi) ikiwa na wakili Roderick Cordara na Ricky Diwan.

Tanesco iliwakilishwa na Kampuni ya Uwakili ya Reed Smith LLP ya nchini Uingereza iliyopo katika Jiji la London ikiwa na wakili Antony White na Kampuni ya Uwakili ya Rex Attorneys iliyopo jijini Dar es Salaam ikiwa na mawakili Dk Eve Hawa Sinare na Dk Alex Thomas Nguluma.

Alipoulizwa na gazeti hili kuhusu ajali hiyo jana, Dk Sinare alisema hawezi kukurupuka kuzungumzia suala hilo hiv sasa.


“Sisi ni wataalamu na si wanasiasa, kutokana na unyeti wa suala hili, hatuwezi kulizungumzia kupitia simu. Kuanzia Jumatatu (Kesho) tutakuwa katika mazingira mwafaka kulizungumzia suala hilo,’’ alisema Dk Sinare

Dk Sinare alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya jopo la mawakili kukubaliana mambo ya kuzungumza pamoja na kushauriana na wateja wao.

Wakili huyo alikwenda mbali na kusema walijihadhari kulizungumzia suala hilo kutokana na ukweli kwamba taarifa nyingi kuhusu mwenendo wa kesi hiyo hadi kufikiwa kwa hukumu kwa kiasi kikubwa, zimepotoshwa.

Baada ya gazeti hili kuripoti hukumu hiyo,Tanesco ilitoa maelezo na kwamba wakata rufaa.

Hata hivyo, shirika hilo lilisema inasubiri ICC isajili hukumu hiyo kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, ili shirika hilo liweze kutathmini na kuamua hatua nyingine za kuchukua.
“Tumeiomba ICC iandikishe uamuzi wake katika Mahakama Kuu ya Tanzania kama inavyotakiwa kisheria ili tuweze kuchukua hatua nyingine yoyote katika suala hili ikibidi,” ilieleza Tanesco katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Tanesco ilieleza kwamba imeamua kuweka hadharani maelezo ya hukumu hiyo licha ya sheria za ICC kutaka iwe siri baada ya kuona taarifa hizo zimeanza kuvuja kwenye vyombo vya habari.

“Pamoja na sheria za usuluhishi zinazotaka maelezo ya uamuzi kuwa siri, Tanesco imebidi kutoa hadharani maelezo ya uamuzi kutokana na taarifa ambazo zimetolewa katika vyombo vya habari (Mwananchi na gazeti dada la The Citizen),” ilieleza shirika hilo.

Tanesco ilileza kuwa baada ya taarifa hizo kumekuwepo na mijadala ambayo inaashiria kupotosha, hivyo ikaona kuna umuhimu wa kufanya hivyo na huenda baadaye ikazidi kuweka wazi siri nyingine.

“Tanesco ina haki ya kutoa maelezo ya maamuzi kutokana na ulazima wa kulinda maslahi yake. Tanesco bado inapitia uamuzi wa ICC kwa kina na baadaye ikibidi itatoa taarifa zaidi kuhusu suala la maamuzi haya ili kusiwe na upotoshwaji,” ilieleza taarifa hiyo.

Tanesco ilifafanua kuwa hukumu iliyotolewa Novemba 15 ilihusu mashauri mawili ya kampuni za Richmond Development Company/Dowans Holdings SA (Costa Rica) na Dowans Tanzania Limited dhidi ya Tanesco na kwamba Richmond walipeleka ombi la usuluhishi ICC Septemba, 2008 na madai yao yalikuwa ni fidia ya dola za Marekani 169 milioni ikiwa ni madai ya kukashifiwa na kusitishwa kwa mkataba wao.

“Pamoja na kutolewa hukumu hiyo na kutaja fidia ambazo Tanesco inapaswa kuilipa Dowans na hata Richmond kulilipa shirika hilo, bado kiwango halisi hakijafahamika hadi hapo Mahakama Kuu itakapopitia na kutoa tafsiri halisi,” inaeleza sehemu hiyo oya Tanesco.

Lakini, kulingana na maelezo ya hukumu hiyo, Tanesco itailipa Dowans dola 24.2 milioni za Kimarekani (takriban Sh36.3 bilioni) na riba ya asilimia 7.5 kwa mwaka kulingana na limbikizo la dola milioni 20 milioni, (Sh 30 bilioni) kuanzia Juni 15, 2010.

Pia Tanesco italipa dola 40 milioni (Sh 60 bilioni) na riba ya asilimia 7.5 kwa mwaka kulingana na limbikizo la jumla ya dola 36.7 (takriban Sh 55 bilioni) kuanzia Juni 15, 2010.
 
kpleo.jpg
 
Back
Top Bottom