Mauaji yaliyofanywa na polisi yaitia doa heshima ya Tanzania

Tankthinker

Member
May 1, 2011
58
9

ZAIDI ya nchi 50 duniani zimejadili ripoti ya haki za binadamu iliyowasilishwa na Tanzania katika Baraza la Umoja wa Mataifa mapema wiki hii na kuielezea kuwa licha ya kuonyesha mafanikio, lakini ina kasoro nyingi zinazopaswa kusahihishwa.

Miongoni mwa mambo ambayo waliitaka Tanzania kuyarekebisha ni pamoja na kufuta adhabu ya kifo, kukomesha mauaji na vitendo vya kikatili vinavyofanywa na polisi dhidi ya raia, ukatili dhidi ya wanawake, kutoa uhuru kwa vyombo vya habari na kukomesha ndoa za utotoni.

Kwa upande mwingine, Tanzania ilipongezwa kwa kufanikisha malengo ya millennia kwa kuongeza nafasi za elimu kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu, kupokea na kutunza wakimbizi, kufanikisha usawa wa kijinsia na kuweka mkakati kabambe wa kupambana na ugonjwa wa malaria.

Katika mjadala huo ulioongozwa na Makamu wa Rais wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, Gulnara Iskakova, nchi nyingi zilionyesha shauku ya kuchangia ripoti hiyo iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe.Kwenye mjadala huo, Chikawe aliwatetea polisi kuwa hawaui raia kwa makusudi na kwamba wanafanya hivyo pale inapobidi kuokoa maisha yao na ya raia wengine.


Mwakilishi wa Finland akitumia ripoti ya mwaka huu ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, aliitaka Serikali ya Tanzania ieleza hatua ilizochukua dhidi ya polisi waliohusika na mauaji ya raia.

Mwakilishi huyo alisema kwa mujibu wa ripoti hiyo watu 20 waliuawa na polisi katika katika kipinid cha miezi sita ya mwaka huu.Kwa upande wao, wawakilishi kutoka Norway, Denmark, Marekani na Djibut, waliitaka serikali kukomesha vitendo vya kikatili vinavyofanywa na vyombo vya dola dhidi ya raia.

Norway iliitaka serikali kukomesha machafuko ya mara kwa mara katika maeneo ya migodi ya madini, kutatua migogoro ya ardhi na kuwapa wananchi haki ya kufanya mikutano bila kuingiliwa.

Marekani ilisema serikali inapaswa kuhakikisha kuwa hayatokei tena mauaji kama yaliyotokea mkoani Arusha miezi kadhaa iliyopita ambako watu wawili waliuawa na polisi kwenye maandamano ya kisiasa.

Pia ilishauri polisi wafundishwe namna ya kuepuka vitendo vya mauaji, ukatili na kuhakikisha kuwa raia wote wanakuwa na uhuru na haki ya kukutana bila kizuizi.

Ingawa ripoti ya Tanzania ilionyesha kwamba moja ya mambo yaliyokomesha mauaji ya maalbino ni kutoa onyo la kutumia sheria yake ya kunyonga watu watakaopatikana na hatia, nchi nyingi ziliiomba serikali kuachana na utaratibu huo.

Nchi kadhaa ziliitaka Tanzania kukubaliana na azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu la kuchana na adhabu ya kifo. Miongoni mwa nchi hizo ni Hungary, Ujerumani, Ubelgiji, Uingereza, Hispania na Romania.

Baadhi ya nchi pia ziliilaumu serikali kwa kushindwa kutatua tatizo la mrundikano wa mahabusu na wafungwa wa umri wa utu uzima kuchanganywa na watoto na hivyo kuchochea unyanyasaji, ukiwamo kulawitiwa.

Hali kadhalika Marekani iliitaka serikali kuchukua hatua zitakazokomesha maofisa na watendaji wake kujihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi wa mali za umma.Ingawa ripoti ya Tanzania ilionyesha kwamba uhuru wa vyombo vya habari unazingatiwa kikamilifu na kuna muswada unaoondaliwa kuimarisha zaidi haki hiyo, baadhi ya nchi zilipinga vikali.Marekani, Uholanzi, Sweden zilikuja juu na kuitaka serikali kutunga sheria itakayolinda haki ya mtu kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari na haki ya Watanzania kupata habari.

Uholanzi ilitoa mfano wa sheria ya utangazaji ya mwaka 1993 ambayo hadi sasa inasimamia vyombo vya habari nchini kuwa haifai kwa sababu inakandamiza sekta hiyo, hivyo akaitaka serikali ibadili.Marekani iliiitaka Serikali kuhakikisha kuwa inafanya mabadiliko ya sheria zote zinazogandamiza vyombo vya habari ili kumfanya mwandishi wa habari kufanya kazi yake kwa uhuru.

Hata hivyo, nchi kadhaa ziliisifu Tanzania kwa kuwezesha usawa wa jinsia hususani katika vyombo vya maamuzi kama vile Bunge, lakini baadhi zikasema kuwa bado kuna vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake.

Sweden ilitoa mfano ikisema pamoja na kuwapo kwa sheria, bado wanawake wengi wamejikuta wakinyanyaswa katika suala la kumiliki ardhi kutokana na mila na desturi potofu kuendelea kuendekezwa na baadhi ya makabila.

Akijibu hoja hizo kwa jumla hoja Chikawe alisema serikali itazifanyia kazi kama ilivyoelekezwa na nchi wanachama wa Baraza wa Haki la Umoja wa Mataifa.Alisema kwa sasa Tanzania ipo katika mchakato wa kuandika katiba mpya na kwamba hicho ni kipindi kizuri kwa Watanzania kuingiza mambo yanayoonekana kuwa hayazingatii haki za binadamu.

“Ni matumaini yangu kwamba katika ripoti ijayo, tutalileza Baraza hatua ambazo tumechukua katika kutekeleza mapendekezo haya,” alisema Chikawe.



 
Back
Top Bottom