Nitawasiliana na mshana atakutumia moja leo usikuNdoto za malaika waovu zikoje?
RIWAYA; MAUAJI YA KIFO.
NA; BAHATI MWAMBA
SIMU; 0758573660
SEHEMU YA TANO
Mapigo ya moyo wake yaliongeza kasi kuliko awali, kuikuta pale bunduki ya aina ile, ilimaanisha rafiki yake yuko matatizoni na ndiye aliyekuwa anaburuzwa.
Alijaribu kupiga hatua kwenda mbele, alijikuta anashindwa na alipojaribu kupiga kurudi nyuma, pia alishindwa.
Kichwani mwake aliwaza sifa za Cholo na Podo, hakika aliogopa.
Hakujua aende mbele au arudi nyuma, hakujua aokote bunduki ile ambayo haikuwa na risasi au afanye kitu gani.
Alibaki njia panda.
***
Akili yake ilifanya kazi kwa kasi kubwa, alihitaji kufanya uamuzi sahihi bila kuathiri lolote. Akili yake ilifikiria kurudi nyuma na kuichukua silaha yake, kisha atokomee na kurudi kambini. Lakini alipomfikiria mtu aliyejiita Kifo, aliona si jambo jema kurudi kule na kukutana nae tena.
Alifikiria kuichukua silaha ile iliyokuwa imeachwa na rafiki yake, kisha akimbie na kurejea kambini, lakini alipokumbuka namba za silaha ile na namba za silaha yake havifanani, aliamua kugairi kuichukua na alibaki na uamuzi wa kwenda mbele kuufuatilia mburuzo uliyokuwa mbele yake.
Aliona kurudi nyuma ni kumdhalilisha mkufunzi wake, ambae aliwafundisha kusonga mbele bila kujali ukubwa wa vita inayopiganwa na; kurudi nyuma ni ishara ya kushindwa mapema kabla ya kujaribu kushinda.
Yeye aliamua kushinda na ujasiri ilikuwa ni silaha muhimu kuliko bunduki. Alihitaji kujua kilichomsibu mwenzake na ikibidi amuokoe au kufa wakiwa pamoja. Kurudi nyuma ni uoga ambao mwanajeshi hajawahi kuufikiria kirahisi na akirudi nyuma, kuna mbinu anazipanga.
Ujasiri ukamvaa na taratibu alianza kupiga hatua zake kuelekea mbele, huku akiufuata mburuzo aliyouona.
Alitembea zaidi ya hatua ishirini na, alipoanza kuzihesabu hatua nyingine zaidi; macho yake yaliona kibuyu cha maji kikiwa kimetelekezwa chini. Kibuyu kile kilikuwa sawa na kile kilichokuwa kiunoni mwake na, ilimaanisha kibuyu kile kilikuwa ni cha rafiki yake.
Midomo ilimtetemeka kwa hasira; kuikuta bunduki na kisha kibuyu, ilimaanisha usalama kwa rafiki yake ulikuwa ni asilimia chache kati ya nyingi za kudhurika. Haraka alianza kukimbia kuelekea mbele na kabla hata ya kumaliza mita ishirini, alikutana na kile ambacho alidhania japo hakukitarajia.
Mbele yake kulikuwa na mtu akiwa amelala chini na kuitanua miguu yake. Mtu yule alikuwa amelala kwenye dimbwi la lita zaidi ya tatu za damu,huku akiwa ametenganishwa kichwa na kiwiliwili chake.
Mtu yule alikuwa amechinjwa.
Willy alipiga magoti kwa unyonge huku machozi yakimtoka kwa wingi bila kupenda. Rafiki yake wa karibu alikuwa ameuwawa kikatili kwa kutenganishwa kichwa chake. Kilio cha kwikwi kilimtoka huku kamasi nyepesi zikiunda mifereji kuelekea kwenye papi za midomo yake.
Majuto yalimzonga huku akishindwa kuelewa ni hatua gani achukue kwa haraka ndani ya pori lile lenye mauza mauza ya kutisha.
Alijuta kwa sababu yeye ndiye aliyetoa wazo la wao kuingia porini na kutafuta maji, baada ya maji waliyopewa kuisha na wakizuiwa kunywa maji tena, kwa sababu walifanya mazoezi makali ya kukimbia na mazoezi mengine ya viungo, kabla ya kuingia kwenye uwanja wa ulengaji.
Kama si yeye basi pengine wangelikuwa salama na wakati huo wangelishaingia kambini na kuoga kisha kupumzika.
Kilio kisingeweza kuyapunguza machungu na majuto aliyokuwa nayo .
Alihitaji kutoka ndani ya msitu ule na kwenda kutoa taarifa kambini, huku akiwa tayari kwa adhabu yoyote huko kambini, lakini taarifa itoke na utaratibu mwingine ufanywe. Alikuwa tayari kwa lolote na kikubwa zaidi alitamani kuona msako kwa Podo na Cholo unafanyika, ili watiwe nguvuni kwa kile walichokuwa wamekifanya.
Alisimama kisha akayafuta machozi yake na kugeuka.
Lahaulal!!
Willy hakuwa peke yake, macho yake yalikutana na watu wawili wakiwa wanamtizana kwa macho ya chuki na dhihaka. Watu wale walikuwa na sura za kuogofya; macho makali na uso uliyojaa makovu makubwa. Mmoja alikuwa ni mkubwa wa mwili na kichwa kidogo mithili ya monjo. Mwili wake ulikuwa mkubwa kama mcheza mieleka maarufu kwa jina la Bigshaw. Mwingine alikuwa ni mrefu na mwili uliyojaa kimazoezi kama walinda milango kwenye kasino.
Mbali na ukubwa wa miili yao, mikononi mwao walibeba silaha aina ya Uzi12, silaha ambazo hazikuonekana kutumiwa na jeshi lolote hapa nchini.
Willy Kondo alitetemeka kwa uoga na kuanza kurudi nyuma. Kwa hofu iliyomjaa alisahau kiwiliwili cha rafiki yake kilichokuwa nyuma yake, badala yake alijikuta akijikwaa na kuanguka huku akipiga kelele za hamaniko, kisha alianza kusota chini kwa makalio yake.
Wakati akiendelea kurudi nyuma kwa nia ya kujiweka mbali na watu wale ambao hawakuonekana kuwa na nia njema, jitu lile lenye mwili mkubwa na kichwa kidogo kama monjo, lilianza kumfuata huku likikenua kinywa chake kilichogoma kuota meno. Jitu lile lilikuwa kibogoyo. Sura yake iliyokosa muonekano kamili kwa sababu ya kichwa kidogo, ilizidi kuonekana mbaya kwa sababu ya kinywa kukosa meno.
Jitu lile alilitambua kwa jina la Podo kwa sababu lilikuwa na sifa sawa na zile alizoambiwa na mtu aliyejiita Kifo.
Willy Kondo aliendelea kusota chini huku akijaribu kupapasa kitu chochote, ambacho kingeweza kumsaidia kujitetea mbele ya watu wale ambao, hawakuonekana kuwa na nia njema kwake.
Mkono wake wa kulia uligusa kipande cha mti, alikishika vizuri na kutulia huku akimtizama Podo alivyokuwa akimsogelea kwa hatua zake nzito.
Alimhesabia hatua kwa nia yakutaka kumshambulia, ili apate upenyo wa kutoroka mikononi mwa watu wale wabaya.
Podo alipomkaribia kwa haraka alijinyanyua chini kwa wepesi na kumtandika kichwani na kile kipande cha mti hadi kilivunjika.
Licha ya kipande cha mti kuvunjika, lakini Podo hakuonesha dalili ya kuingiwa na pigo lile la kushitukiza, badala yake alianza kucheka kwa dharau na kumdaka Willy kwa mikono yake yote miwili na kumnyanyua juu kama karatasi. Willy Kondo alijaa vema kwenye mikono imara ya Podo na, kila alipojaribu kufurukuta alishindwa na kubaki akilia kama mtoto mdogo aliyetishiwa na nyoka wa kuchonga.
Willy alizidi kufurukuta kwa kurusha miguu yake huku na huko, lakini mbavu zake zilibanwa nusu ya kuvunjika, kisha alitupwa chini kama jiwe la kuua nyoka. Alianguka chini na kusambaratika kama mlevi wa choya, huku akilia kwa uchungu.
Akiwa bado anajizoazoa chini, macho yake yaliona Cholo akimfuata kwa kasi na kumtandika teke zito usoni na kumpasua midomo yake. Alilia tena kwa uchungu uliyochanganyika na woga wa kuingia kwenye mikono ya wauaji.
Akili yake ilianza kumkumbuka Kifo ambaye alimuonya kuhusu watu wale wabaya. Lakini hakuwa na la kufanya wakati huo ili kuwakimbia, hali ilizidi kuwa tete na tayari walimsogelea na kumweka katikati yao, kisha Cholo akatoa kisu kutoka kwenye soksi za miguu yake na kwenda kukiweka shingoni mwake. Willy alitumbua macho huku akihema kwa shida, mwili ulimtetemeka huku akilini akijenga picha ya kutenganishwa kichwa chake na kiwiliwili.
Mikono ya Cholo iligawana majukumu; mkono wa kushoto ulimziba mdomo Willy huku mkono wa kulia ukitafuta shabaha ya kuinasa shingo ya Willy. Podo nae hakuwa nyuma kuitumia mikono yake kuidhibiti miguu na mikono ya Willy, ambae alikuwa akitapatapa kutaka kuinusuru roho yake.
“Usilie haiumi.” Cholo aliunguruma huku akimtizama kwa macho ya dhihaka.
“Unatekenywa tu hapo shingoni, usilie.” Podo nae alimwambia huku akizisukutua fizi zake kwa ulimi,huku mate yakimtoka kwa raha ya kutaka kuiona damu ya mtu inavyoruka.
Hakika maneno ya Kifo yalikuwa sahihi kuwaita majini watu.
Willy alilowesha suruali yake kwa mkojo, wakati kisu kilipoanza kuipekenyua ngozi ya shingo.
****
KWAKO MSOMAJI......
HITAJI LA RIWAYA HII LIMEKUWA KUBWA, HIVYO BASI, NAOMBA KWA YEYOTE ANAEHITAJI KITABU CHA RIWAYA HII, AWASILIANE NA MIMI KWA 0758573660, 0624155629... AU 0658564341WHATSAPP TU.
KITABU KITAUZWA KWA TSH 12000, LAKINI ATAKAE WAHI KUTOA ODA, ATAPEWA PUNGUZO HADI TSH 8000/= NA WALE WANAOTAKA KUNUNUA KWA SOFT COPY NI TSH 5000.
UNACHOTAKIWA KUFANYA UNAPOKUJA KUTOA ODA TANGULIZA MALIPO YA TSH 5000 ILI KUWE NA UHAKIKA WA ODA YAKO.
WANAOTAKA KUNUNUA SOFT COPY PIA UNATAKIWA KULIPA NA KUSUBIRI HADI MWISHO WA WIKI, AMBAPO NDIYO ITAKUWA MWISHO WA KUPOKEA ODA NA PESA YA SOFT COPY.
NB; KAMA KUNA MTU ANAHITAJI KUDHAMINI KOPI KADHAA UNAKARIBISHWA KWA MAZUNGUMZO.
KARIBUNI.....View attachment 1323725