Simulizi: Mauaji ya Kifo

Kudo

JF-Expert Member
Nov 2, 2017
1,809
6,081
RIWAYA; MAUAJI YA KIFO

MTUNZI; BAHATI MWAMBA

SIMU;0758573660.



Mwaka 2012

CHAYA-


Kikundi chao kilikuwa na watu wanne. Kikundi hiki kilikuwa na watu wanaopenda kujiongeza, bila kujali matokeo yatakayopatikana baadae. Kwa lugha yao ya utani kambini; kikundi hiki kiliitwa Nanga.

Kikundi hiki kikiwa kimejiondoa kwenye mstari wa mazoezi, kiliingia porini kwa mbwembwe nyingi, kwa nia ya kutafuta maji ya kujipooza koo.

Walikuwa ni vijana waliyokuwa wameamua kutotii amri ya kamanda wa msafara. Amri iliyowataka vijana wote waliyokuwa kozi, kutogawanyika mstarini; wala kutoroka wakiwa katikati ya pori lile kubwa, ambalo walilitumia kufanya mazoezi ya utayari na ulengaji shabaha. Mbali ya kuwa ni pori lenye wanyama wakali,pia lilikuwa ni pori lilioaminika kuwa na jini mla watu.

Wenyeji wa kijiji cha Chaya kilicho wiliyani Manyoni mkoani Singida, walikuwa wametoa tahadhari kwa viongozi wa mafunzo kwa vijana wa jeshi la kujenga taifa, waliyokuwa wamepiga kambi katika pori lile la kutisha, kwa wenyeji wa kijiji cha Chaya.

Kanali Bengo Ndaya aliyekuwa mkuu wa mafunzo rgt 84KJ,aliamua kuwapeleka vijana wa operesheni Nyerere kwenye pori lile, kwa nia ya kuhakikisha vijana wanakuwa na utayari wa kutosha, kukabiliana na aina yoyote ya ugumu, wawapo kwenye uwanja wa vita, au wawapo kwenye maisha ya kawaida wakiwa kama jeshi la akiba.

Vitisho na tahadhari za wenyeji hazikutiliwa mkazo na wakufunzi, wala vitisho vile havikuarifiwa kwa vijana waliokuwa kozi ya wiki sita. Vitisho viliiishia kwa wakufunzi pekee na hawakuonekana kujali.
Wiki mbili ziliisha salama na vijana walionekana kushika vema mafunzo. Wengi walielewa vizuri kile walichofundishwa.

Siku zote palipo na wengi hakukosekani wajanja wajanja. Wajanja ambao hawapendi kushindwa au kuonekana wao ni wa mwisho katika wengi.

Mbali na kutakiwa kuishi pamoja na kufuata amri ya kamanda wa mafunzo, lakini kuliibuka kundi la vijana ambao wao, hawakutaka kufuata amri ya wakufunzi. Vijana hawa waliona ni mateso kukimbia kilomita kumi bila kunywa maji. Waliona ni mateso pale walipozuiwa kunywa maji baada ya kukimbia umbali mrefu.

Vijana hawa walizua tabia ya kutoroka kabla ya kufika kambini, ili wajipatie maji. Siku ya kwanza kutoroka hawakufanikiwa kupata kile walichokitarajia, walirudi kambini wakiwa wamechoka maradufu zaidi, kuliko wale waliotii amri ya kufuata utaratibu wa kanuni za kimazoezi. Lakini wao hawakuona tatizo, badala yake walitamani kurudi tena kwa mara nyingine, kwa lengo la kuhakikisha wanapata chemichemi au kisima cha maji ndani ya pori.

Wahenga walisema ‘mwanakulitafuta, mwanakulipata’. Vijana wanne kati ya kumi wenye nia ya kupata kisima, walijitolea kwenda kukitafuta kisima kwa niaba ya wenzao, huku wakiweka makubaliano ya zamu, endapo wao wangekikosa tena.

Siku hiyo ilikuwa ni siku maalumu kwa zoezi la ulengaji shabaha. Kila mmoja alipewa silaha yake na risasi zake bandia. Kule walikoelekea kwa ajili ya ulengaji, ndiko walitarajia kutorokea baada ya zamu zao za ulengaji kuisha.

Kama walivyopanga, baada ya kumaliza ulengaji shabaha, ilitakiwa waanze safari ya kurudi kambini.

Nao hawakuwa mbali na lengo lao, nafasi ilipopatikana waliishia porini, wakiwa na silaha zao begani, huku vibuyu vya maji vikining’inia kiuononi.

Vijana hawa maarufu kama Nanga, waliongozwa na William Kondo. Wenzake walipenda kumuita Willy Kondo.
Alikuwa ni kijana mrefu na mweusi tii, huku akiwa na kichwa kidogo kilichonyolewa kwa wembe, bila kuacha salia hata kidogo.
Kijana huyu alikuwa na mikono imara huku akiwa na kifua kipana. Alipendwa na watu wengi kwa kuwa mthubutu kila wakati, huku mara chache akigeuka msanii na kuwaburudisha wenzake, wakati wa mapumziko.

Willy alipendwa na wengi kwa ucheshi wake na pia wengi walimpenda kwa kuwa walitamani kuona kichwa kidogo, kikiwa kwenye mwili mpana huku sauti ikiwa nzito kupindukia. Licha ya sauti yake kuwa nzito; aliweza kuimba vizuri na kuigeuza kuwa burudani tosha kwa wenzake.

Kifupi Willy alikuwa ni burudani tosha, wakati u mtazamapo au wakati umsikilizapo.

Lakini mbali na hayo yote; Willy alikuwa ni miongoni mwa vijana wanaopenda kujiongeza, bila kuwaza matokeo ya baadae.

*****

Walitembea umbali wa kilomita nne bila kufanikiwa kukutana na kisima au chemichemi ya maji. Waliona muda unazidi kwenda bila mafanikio, hapo ndipo walipoamua kubadilisha mbinu, mbinu ambayo ilileta kizaazaa kwa vijana wale.

Baada ya kukubaliana kugawanyika, walikubaliana sehemu ya kukutana ndani ya nusu saa baadae.

Willy Kondo alikuwa na bunduki yake mkononi na, ilikuwa na risasi tatu za bandia(blanko). Risasi hizi zilibaki baada ya kuwa amelenga kwa usahihi risasi saba, kati ya kumi alizokuwa amepewa. Baada ya hapo alichezesha kidogo mgongo wa bunduki na risasi hazikutoka tena. Kwa kuwa alilenga kwa usahihi alipewa alama zake na kuruhusiwa kutoka eneo la ulengaji, huku akiingia kwenye orodha ya wapigaji wazuri, watakao jaribiwa tena wakati mwingine, ili kuupima uwezo wao.

Alikuwa anatembea kwa hatua ndefu, huku akijaribu kufuata nyasi fupi zilizonawiri. Kichwani mwake aliamini nyasi zile zilipokea maji karibu, au kuna mto unaopita kwenye mazingira yale.
Alikuwa anatembea kwa kufuata njia za wachunga ng’ombe. Aliamua kufuata njia hizo akiwa na lengo la kukutana na wachungaji, au sehemu ambayo wachungaji walinywesha mifugo yao. Aliendelea kujipa tumaini hilo kwa sababu ya nyasi fupi alizoziona kwenye njia alizopita.

Akiwa ametembea zaidi ya nusu kilomita, alikutana na njia nyingine kutoonekana kutumika mara kwa mara. Njia ile halikuonesha kuwa fupi na haikuonekana kususwa, bali ilipitisha viumbe hai kila wakati.

Alisimama kwa dakika mbili huku akijaribu kutafari ukubwa wa njia ile. Alitizama alikotoka na alitizama aendako.

Kote kulikuwa ni pori na ni ndege pekee walisikika wakiimba kwa furaha, huku wengine wakirukaruka na kumshukuru Mungu kwa uhai aliowapa.

Alijikuta akianza kuwa na wasiwasi bila kutarajia, huku nafsi ikimtuma aifuate njia ile.

Hakujua ni kwa nini aliingiwa na wasiwasi, lakini aliamini kuna kitu hakikuwa sawa kuhusu njia ile.

Kwa nini?

Kwa sababu njia ile ilianzia pale alipokuwa na haikuonekana kuwa na mwanzo upande mwingine, uliyoiunganisha.

Wazo la kuendelea kuifuatilia njia ile ya wachunga ng’ombe liliishia pale. Na likaibuka wazo jipya la kuifuatilia njia ile iliyopitika mara kwa mara.

Aliifuata taratibu huku akijikuta anaongeza umakini bila kupenda. Kadiri alivyoendelea kwenda, ndivyo mapigo yake ya moyo yalivyozidi kudunda kwa kasi, huku miguu yake nayo ikianza kuwa mizito.

Alisimama!.

Alivuta pumzi nyingi na kuziachia taratibu. Alirudia tena mara mbili, kisha alitulia na kusikiliza udundaji wa mapigo yake ya moyo.

Yalidunda kawaida na hata alipojaribu kusogeza mguu, ulienda bila uzito wowote.
Licha ya mwili wake kukubali kuendelea, lakini akili yake ilikuwa inapigana na mambo mawili.
Jambo la kwanza akili yake ilikuwa inakubaliana na mwili wake, kuendelea mbele; lakini wakati huohuo akili yake ilikuwa inapingana na uamuzi wa mwili kukubali kwenda na ilitaka arudi alikotoka mara moja.

Sasa ilibidi akubali kufuata moja kati ya hayo mawili.

Alijikuta akipiga mluzi usio na maana huku mikono yake ikichomoa magazini na kuziangalia zile risasi tatu alizosalia nazo.

Ujasiri ukamvaa na alipiga hatua kusonga mbele, bila kujali matokeo ya mgongano wa nafsi yake.

Lakini siku zote ninge huja yakishatokea. Na endapo Willy angelijua nini maana ya mgongano wa nafsi, asingeliendelea na safari yake, kwenye ile njia ya ajabu.


****


Ungana nami kesho!
a653e8736584abaea153ac18769f4210.0.jpg
 
RIWAYA; MAUAJI YA KIFO.

NA; BAHATI MWAMBA.

SIMU; 0758573660


SEHEMU YA PILI

Aliifuata taratibu huku akijikuta anaongeza umakini bila kupenda. Kadiri alivyoendelea kwenda, ndivyo mapigo yake ya moyo yalivyozidi kudunda kwa kasi, huku miguu yake nayo ikianza kuwa mizito.

Alisimama!.

Alivuta pumzi nyingi na kuziachia taratibu. Alirudia tena mara mbili, kisha alitulia na kusikiliza udundaji wa mapigo yake ya moyo.

Yalidunda kawaida na hata alipojaribu kusogeza mguu, ulienda bila uzito wowote.
Licha ya mwili wake kukubali kuendelea, lakini akili yake ilikuwa inapigana na mambo mawili.
Jambo la kwanza akili yake ilikuwa inakubaliana na mwili wake, kuendelea mbele; lakini wakati huohuo akili yake ilikuwa inapingana na uamuzi wa mwili kukubali kwenda na ilitaka arudi alikotoka mara moja.

Sasa ilibidi akubali kufuata moja kati ya hayo mawili.

Alijikuta akipiga mluzi usio na maana huku mikono yake ikichomoa magazini na kuziangalia zile risasi tatu alizosalia nazo.

Ujasiri ukamvaa na alipiga hatua kusonga mbele, bila kujali matokeo ya mgongano wa nafsi yake.

Lakini siku zote ninge huja yakishatokea. Na endapo Willy angelijua nini maana ya mgongano wa nafsi, asingeliendelea na safari yake, kwenye ile njia ya ajabu.


Willy Kondo alizidi kuifuata njia ile bila uoga wowote. Alivyozidi kuifuata ndivyo alivyoukaribia mlima fulani mdogo. Alitembea zaidi na kuanza kuupanda mlima ule mdogo.

Hakutumia dakika nyingi kuupanda mlima ule. Dakika tano zilitosha kumfikisha kwenye kilele cha mlima. Alipofika kileleleni alisimama na kutizama chini ya mlima. Macho yake yaliishia kuona miti mingi ikiwa imefungamana,huku milio ya ndege ikisikika kwa mbali.

Maamuzi yake yalikuwa ni kuendelea kushuka kilima kile, akiwa anaifuata njia iliyoonekana kuendelea mbele zaidi.

Alifika chini ya mlima ule mdogo, kisha aliendelea kufuata njia ile bila wasiwasi wowote. Lakini kila alivyozidi kutembea, mazingira yalianza kuonesha dalili za uwepo wa shughuli za kibinadamu. Kulikuwa na vifusi vya udongo mbichi na kulionekana mawe yaliyochimbwa na kukusanywa pamoja.

Alisimama na kujaribu kuotea aina ya kazi iliyofanywa mazingira yale. Wakati akiendelea kuwaza na kuchunguza vifusi, aligundua udongo ule uliletwa na haukuchimbwa maeneo yale aliyokuwa.

Aliangaza kushoto na kulia kwa lengo la kuona mtu au watu, waliokuwa wanaifanya kazi ile. Lakini hakuona dalili ya uwepo wa mtu na, kitu pekee alichoona ni njia nyingine nyingi, zikiwa zimejiotesha bila mpangilio. Kwa haraka haraka alihisi njia zile zilitumiwa na watu waliomwaga mawe na vifusi alivyoviona. Alipochunguza vizuri aligundua njia zile zilitokea sehemu moja na sehemu ile ilikuwa ni bondeni zaidi.
Akiwa bado hajui afanya jambo gani, masikio yake yalihisi hatua za watu wakija pale alipokuwa. Hajui ni kwa nini, lakini alijikuta akikwepa kuonana na watu hao. Haraka alikimbilia upande wake wa kulia kulikokuwa na mwinuko na nyasi nyingi na miti ya kuhesabu.

Hakupata shida ya kujificha kwa sababu alifundishwa mbinu za kujificha katika mazingira kama yale.

Alitulia kimya baada ya kuwa amelelala katikati ya nyasi nyingi, huku bunduki yake akiwa ameiweka tayari kwa lolote.

Vishindo vilizidi kukaribia na hatimae lilitokea kundi la watu sita, wakiwa na karai kichwani zenye udongo mbichi.

Baada ya kuwaona watu wale alitamani kujitokeza, lakini alisita baada ya kuwaona vizuri wakati wakimwaga udongo.

Walikuwa ni watu waliochoka na afya zao hazikuonekana kuwa imara; nyuso zao zilitota uchovu na kukata tamaa.

Mwonekano wao ulimpa maswali, hawakuonekana kuwa na furaha na kazi waliyokuwa wanaifanya.
Kwa nini!

Hilo lilibaki kuwa ni swali lisilo na jibu.

Alisimama na kuwasindikiza kwa macho, kisha nafsi ilimshawishi kuwafuatilia watu wale.

Alianza kuwafuata kwa uangalifu mkubwa, huku bunduki yake ikiwa imara mkononi mwake na alipanga kuitumia kwa lolote, endapo lingetokea la kuhatarisha usalama wake.

Alitembea nyuma ya watu wale kwa umakini mkubwa, hakutaka kutoa sauti yoyote licha ya kuvaa viatu vizito, miguuni mwake. Watu wale hawakuonekana kugundua uwepo wa mtu nyuma yao na walizidi kusonga mbele huku wakiwa kimya bila kuongea.

Wakiwa wametembea umbali wa mita mia, Willy alianza kusikia sauti za vishindo vizito. Aliposimama ma kusikiliza kwa umakini, aligundua ni vishindo vya nyundo au sururu.

Wakati akiwa amesimama na kusikiliza vishindo; watu wale walipanda mwinuko fulani na kupotelea huko. Haraka alikimbia ili awahi kuwaona vizuri, lakini kabla hajapiga hatua mbili, alidakwa na mikono imara ya mtu, kisha alizibwa mdomo na kupigwa mweleka safi uliyomtupa kando ya kichaka cha miba. Alipotaka kunyanyuka alijikuta akiwahiwa na kushikwa shingo, kisha alionyeshewa ishara ya kutulia kimya.

Willy Kondo alibaki akitweta kwa hasira iliyochanyika na woga, huku akijaribu kumtizama mtu aliyempa shambulizi la gafla namna ile. Mtu yule alikuwa amechuchumaa mbele yake, huku akiwa amempa mgongo ingali bado mkono wake wa kulia, ukiwa umeishika shingo yake.

Willy alijipa utulivu japo aliendelea kusikia maumivu kwa kukabwa na mkono imara wa mtu ambae, hakuwa amemuona vizuri usoni, licha ya kuiona ishara iliyooneshwa kwa kasi kubwa.

Akiwa anajaribu kumtafakari mtu yule, mara alisikia vishindo vya watu wakikimbia na walipofika kando ya kichaka kile, walisimama.

Watu wale walisimama kwa dakika mbili, kisha waliendelea kukimbia kuelekea kule alikokuwa ametokea.

Baada ya watu wale kuondoka, mtu aliyekuwa amemkaba alimwachia na kumgeukia.

Willy alijikuta akitazamana na mwanaume wa makamo. Mwanaume yule alikuwa na macho mekundu na mazito yalioonekana kukosa usingizi kwa siku kadhaa. Mwanaume yule alikuwa na kamera ndogo aliyokuwa ameining’iniza shingoni mwake.

Walitazamana kwa dakika nzima bila kusemeshana; lakini Willy aligundua mtu yule alikuwa na maumivu makali kwa sababu kila wakati alikuwa akifinya macho yake, huku akikaza fizi. Alipotaka kuendelea kumchunguza, alisita baada ya kuona mtu yule akiivua kamera yake haraka haraka.

“Unaitwa nani?” Aliuliza mtu yule.

“Naitwa William Kondo.”

“Unajitolea au upo kozi kwa mujibu wa sheria?”

“Nimejitolea”

“Kwa nini unatoroka kambini, wakati umejitolea kujiunga na jeshi?”

Midomo ya Willy ikawa mizito kijibu .

“Sehemu hii ni hatari sana kwa wewe kuwepo hapa!”

“Kuna nini?”

“Ukiendelea kuuliza kuna nini nitakuacha ufe. Hapa si sehemu salama hebu nifuate” Mtu yule alisema huku akisimama na kuanza kuondoka pale mafichoni na Willy alimfuata nyuma.

“Bunduki yako ina risasi ngapi?” aliuliza huku akizidi kutembea kwa kasi, licha ya kuchechemea.

“Ina risasi tatu”

“Hizo ni blanco na hazifanyi kazi!” Mtu yule alisema huku akipanda mwinuko na kulala juu ya mwinuko ule, huku akiwa na kamera yake. Willy nae akipanda na kulala, kisha alitizama kule ambako mtu yule alikuwa anatizama.

Lol! Willy aliona jambo ambalo hakuwahi kudhani kama bado linafanyika katika karne hii. Alimgeukia mwenyeji wake na kisha alirudi kutizama kule alikotizama mwanzo.

Kulikuwa na kundi la watu zaidi ya thelathini. Watu wale walikuwa wanachimba kwa kutumia sururu, huku wengine wakipiga mawe kwa nyundo na wengine wakitumia bereshi kupakia udongo, kwenye karai.

Hilo si jambo lilomshangaza, bali alishangazwa kwa kitendo cha kuona kuna watu watatu, wakiwa wamesimama na bakora mikononi mwao na wakiwachapa baadhi ya watu walioonekana kuwa wavivu.

“Kuna nini hapa!?” Alijikuta akiuliza.

“Hii inawahusu watu wanastahili kujua, ila kwako itabidi ujue wale ni watumwa”

“Watumwa!?”

“Ndiyo”

“Watumwa wa nani?”
“Sikia bwana mdogo. Pori hili lina jini mla watu na yeyote anaeingia humu, hupotea na baadae huletwa kuwa mtumwa wa yale majini yenye viboko”

Willy Kondo alibaki mdomo wazi, hakuwahi kusikia hadithi za jini kula watu, kisha kuwarejesha kama watumwa.

“Lakini majini hawaonekani!” Alisema kwa kushangaa.

“Lakini hao ni majini watu siyo majini unayoimuliwa wewe”

“Majini watu!?”

“Ndiyo, si unaona wanaonekana?”

Willy alibaki njia panda kwa jibu lile. Inakuwaje kuwe na jini afu kuwe na jini mtu.

Hata! Alijikatalia.

“Twende nikusaidie kuvuka maeneo haya bwana mdogo.” Mtu yule alisema huku akisimama na kutoa kadi ndogo ndani ya kamera yake na kuishika vizuri mkononi mwake.
“Kwa nini unachechemea?” Willy aliuliza wakati walipoanza kuondoka.

“Nimepambana na jini watu na nimewatoroka.”

“Sasa kwa nini umeendelea kuwa maeneo haya?”

“Huoni mi kuwepo maeneo haya nimekuokoa?”

Willy alikaa kimya kwa sekunde kadhaa, kisha aliuliza.

“Unaitwa nani?”

“Naitwa Kifo.”

“Heh!” Willy aliguna na kusimama. Alichanganywa na yule jamaa. Dakika chache alitoka kumpa habari za jini mla watu, wakati huu yeye anajiita kifo.

Hata!

Alijikuta anasita kuendelea kumfuata.
437579d25fbe7249e9605fb551675ba9.0.jpg
 
RIWAYA; MAUAJI YA KIFO.

NA; BAHATI K MWAMBA

SIMU; 0758573660

SEHEMU YA TATU

Willy alibaki njia panda kwa jibu lile. Inakuwaje kuwe na jini afu kuwe na jini mtu.

Hata! Alijikatalia.

“Twende nikusaidie kuvuka maeneo haya bwana mdogo.” Mtu yule alisema huku akisimama na kutoa kadi ndogo ndani ya kamera yake na kuishika vizuri mkononi mwake.
“Kwa nini unachechemea?” Willy aliuliza wakati walipoanza kuondoka.

“Nimepambana na jini watu na nimewatoroka.”

“Sasa kwa nini umeendelea kuwa maeneo haya?”

“Huoni mi kuwepo maeneo haya nimekuokoa?”

Willy alikaa kimya kwa sekunde kadhaa, kisha aliuliza.

“Unaitwa nani?”

“Naitwa Kifo.”

“Heh!” Willy aliguna na kusimama. Alichanganywa na yule jamaa. Dakika chache alitoka kumpa habari za jini mla watu, wakati huu yeye anajiita kifo.

Hata!

Alijikuta anasita kuendelea kumfuata.

Mtu yule nae aligeuka na kumtazama, kisha alisema..
“Unahisi naweza fanana na huyo jini? Usiogope endelea kunifuata.” Kifo alimaliza kuongea na kugeuka, kisha alianza kupiga hatua zake kuelekea upande ule kulikokuwa na kilima, alichotokea Willy.

Wasiwasi ulianza kuivaa nafsi yake, mwili wake uliingiwa na ubaridi kwa jina la yule mtu na habari aliyompa kuhusu jini mla watu, huku yeye akijiita Kifo.

Hata!

Roho yake ilikataa na wakati huohuo aliikoki silaha yake, ambayo alikuwa nayo wakati wote.
Sauti ya chuma ilimfanya Kifo agaeuke taratibu na kumtazama.

Macho yao yaligongana na kila mmoja alipepesa mara mbili na kumkazia mwenzake. Utazamanaji wao haukuchua sekunde nyingi; Kifo alifinya macho yake kama mtu aliyekuwa anapitia maumivu makali, wakati huo huo mkono wake wa kulia ulishika tumbo lake.

Macho ya Willy yaliyokuwa makini yaliufuata mkono ule, hadi ulipoishia tumboni mwa yule mtu aliyejiita Kifo.

Damu!

Macho yake yaliona damu ikiwa imelowesha shati la yule bwana, hapo ndipo alipogundua kwa nini mtu yule alikuwa anachechemea. Mtu yule alionekana kupitia maumivu makali kutokana na jeraha lilokuwa tumboni mwake, upande wa kulia pembeni kidogo ya mbavu changa.

Kwa haraka hakujua kilichomjeruhi mtu yule kwa kiasi kile, pia hakujua ni muda gani mtu yule alikaa na jeraha hilo na kwa nini muda wote lilikuwa halitoi damu.

“Na wewe unataka kuniongeza jeraha lingine?” Kifo aliongea kwa upole huku akijitahidi kuyakabili maumivu yake.

Willy alishusha silaha yake chini huku akijitahidi kuikabili aibu iliyomvaa, baada ya kufanya kitendo alichohisi ni cha kipuuzi. Huruma ilizonga nafsi yake na haraka alipiga hatua na kwenda kumdaka mtu yule, baada ya kuyumba na kutaka kudondoka. Kifo aliangukia mikononi mwake, huku akihema kwa kukwama kwama kwa sababu ya maumivu.

“Hilo jeraha umefanywa nini?” Aliuliza huku akijitahidi kumuinua kwa nguvu zake zote.

Kifo alihema taratibu huku akiyafinya macho yake na kung’ata papi za midomo yake.

“Ni hadithi ndefu ambayo haiwezekanani kusimuliwa katika mazingira kama haya. Lakini nitakuelekeza jambo fulani.” Aliongea huku akijitahidi kujiweka mbali na mikono ya Willy Kondo.

“Nifuate bwana mdogo. Lakini jitahidi kuudhibiti uoga, kifo hakikimbiwi na kwa kuwa umetukana na Kifo mimi, basi jua utanuka harufu yangu kila uendako.” Aliongea huku akipiga hatua zake kwa mwendo wa haraka, japo hakuonekana kuwa katika utimamu wa mwili.

“Hebu tembea taratibu maana una jeraha bichi” Willy alimwambia huku akiweka sawa bunduki yake begani na, kichwani mwake akiitafakari kauli ya mwisho ya bwana yule.

“Unapokuwa katika harakati zozote inabidi ujali muda. Usifikirie maumivu yako bali fikiria muda wako, ukiyafikiria majeraha utakufa na kuuacha muda ukitumiwa na wenye uhitaji, wawe wazuri ama wabaya.” Kifo aliongea huku akianza kupanda kilima kile alichopita Willy.

Maneno ya mtu yule aliyejiita Kifo, yalikuwa na utata mkubwa kwenye ubongo wa Willy. Hakuna neno ambalo aliongea na likaeleweka kirahisi. Kila neno lilikuwa limejawa na fumbo ndani yake.

Willy hakuwa na la kufanya zaidi alikubali kumfuata mtu yule, kila sehemu aliyopita na hatimae walikimaliza kilima na kufika kwenye kilele chake na walisimama, huku wakitizama pande mbili za mabonde; bonde moja ni kule walikotokea na bonde lingine ni kule Willy alitokea mwanzo kabla ya kukutana na mtu yule mwenye jina la ajabu.

“Wakati unakuja mlikuwa wangapi?” Kifo aliuliza.
“Tulikuwa wanne”

“Watatu wako wapi?”

“Tuligawana njia na tulikubaliana kukutana baada ya nusu saa”

“Tatizo hilo!” Kifo aliongea taratibu huku akitizama mteremko ambao walikuwa wanautazama mbele yao.

Kauli ile ilimfanya Willy amtazame kwa mashaka makubwa.

“Unamaanisha nini!?”
“Unakumbuka habari ya jini mla watu?” Kifo aliuliza badala ya kujibu.

“Ndiyo nakumbuka.”

“Na unawakumbuka wale watu wawili waliokuwa wananikimbiza ndipo nikakukatana na wewe?”

“Ndiyo nakumbuka”

“Ni asilimia sabini kukutana na vijana kuruti wenzako wakikusubiri, kwa sababu wamepita njia hii uliyopita, wakati unakuja.”
“Ooh shiit!” Willy aliropoka huku akipiga hatua kuanza kuushuka ule mlima, ili aende kule walikokuwa wenzake.
Kwa ustadi mkubwa alidakwa ukosi wa gwanda lake lililokuwa limechafuka kwa vumbi na tope.

“Kwa hiyo unahisi unaweza kuwakomboa kama kweli wapo matatizoni? Bado huwezi kupambana na wale watu, bado hautoshi kwenye mikono yao.” Alisema huku akitabsamu kwa maumivu.

Lilikuwa ni tabasamu liloeleza uhalisia wa kile alichokimaanisha. Walitazamana na kila mmoja alizungumza kwa lugha ya macho na Kifo alitikisa kichwa kwa masikitiko makubwa.

“Kuna jitu huko linaitwa Podo. Jitu hilo hata hizo risasi zako baridi, haziwezi kulitekenya. Ni katiri na haliogopi kuua kabisa, yaani kwako ni kama linakuwa kumbikumbi tu.” Kifo aliongea huku akianza kupiga hatua ndogo kushuka ule mlima.

“Kwa hiyo unanitisha au!” Willy alisema huku akianza kumfuata nyuma.

“Sasa kama hutishiki nenda ukutane na Podo.”

Ukimya ulipita na walizidi kukishuka kilima taratibu, kwa sababu wasingeliweza kutumia nguvu wakati mmoja anajeraha linalovuja damu.


Dakika nane zilitosha kuwafikisha hadi bondeni. Muda wote hakuna aliyemsemesha mwenzake na kila mmoja alikuwa anawaza jambo lake. Willy alikuwa anawaza kuhusu mtu yule wa ajabu waliyekutana katikati ya pori nene. Aliwaza kuhusu uwepo wake ndani ya pori, akiwa amejeruhiwa vibaya. Aliwaza kuhusu jina lake la ajabu, kwa sababu hajawahi kusikia mtu anaitwa Kifo.

“Wewe ni nani hasa na unafanya nini kwenye hili pori?” Aliuliza.

“Mimi ni kifo na nipo humu porini kufa. Yeyote atakaekuja kuuliza kuuliza kuhusu kifo mwambie ‘follow the money’..”

“Follow the money!”

“Ndiyo, follow the money”

“Unamaanisha nini sasa na inauhusiano gani na wewe?”

“Bwana mdogo follow the money, okey!” Kifo aliendelea kusisitiza zaidi kuhusu hilo neno, ambalo lilimwacha njia panda. Akili yake ilichanganyikana na lindi la maswali mengi yenye mshangao ndani yake.
Walikuwa bado wanatembea katikati ya pori nene, kama ungebahatika kuwasikiliza, ungedhani hawaelewani japo waliongea lugha moja ya kiswahili. Wakati Willy anaomba kufafanuliwa uhusiano wa Kifo na neno ‘follow the money’; Kifo yeye alizidi kusisitiza uhusiano wa jina lake na hilo neno na, kusisitiza endapo angeliulizwa na mtu yeyote amwambie hivyo.

Ilikuwa ni wakati mgumu kwa kijana yule ambae hakuwa anajua lolote kuhusu mafumbo, wala hakujua nini maana ya maneno hayo ambayo yalikuwa ni kama fumbo na ni fumbo ambalo halikuwa likimhusu.

“Huyu mtu ananitakia nini lakini? Mbona simuelewi na hadithi zake; mara jini mara aseme anaitwa Kifo mmh” Willy Kondo aliwaza huku akizidi kumfuata mtu yule ambae alionekana kuwa na wasiwasi mkubwa.

Wasiwasi wa nini?

Hakika hakujua.

Wakati akiwa kwenye lindi la tafakuri, alishangaa akidakwa kwa mtindo wa aina yake, kisha akazungushwa na kutandikwa teke maridadi lilotua katikati ya mgongo wake na kumsukuma kwa nguvu hadi kwenye kichaka, kilichokuwa katikati ya nyasi ndefu.

Alianguka kwa kutanguliza mikono huku akitoa kilio cha hamaniko. Kabla hajageuka ili ajue anajitetea vipi, alijikuta akijaa vema kwenye mikono ya Kifo, huku akizibwa mdomo kwa utaalamu wa aina yake.Alipojaribu kufurukuta alikutana na jicho kali lilomuonya asifurukute tena.

Willy Kondo alitulia huku akihema kwa hofu, hakuwa na imani tena na mtu yule mwenye jina la ajabu na maneno yasiyoeleweka. Lakini aliwaza kutokukubali kirahisi endapo angelijaribu kuendelea kumdhuru, japo aliuhusudu uwezo wake mtu yule, uwezo ambao ulimtofautisha mbali na yeye na hata angelijaribu kupigana nae, katu asingeliweza.

“Nahisi kuna hatua za watu mbele yetu, ndiyo maana nimekushambulia namna hii ili tujifiche” Kifo alisema huku akimwachia na kumwacha huru, huku macho yake yakimtizama.

“Umefundishwa namna ya kujificha dhidi ya adui?” Aliuliza.
“Ndiyo” Willy alijibu.

“Basi huu ni wakati ambao inabidi uziweke vema kichwani mwako mbinu hizo.”

“Kwa nini?”

“Kwa sababu zitakusadia humu porini au hata huko nje ya kambi. Naamini kuanzia leo hautakuwa kuruti tena”

“Una maana gani!?”

“Maana yangu utaipata baada ya kutengana mimi na wewe.”

Willy alibaki kukodoa macho bila kujua aseme nini. Moja ya mambo ambayo kamwe hakupenda hata kuyasikia ni; kuwa siku moja ataiacha kambi ya jeshi na kurudi uraiani. Sasa kuyasikia maneno hayo kwa mtu yule asiyeeleweka, ilikuwa ni kama kuchomwa na ncha ya mshale utosini. Jasho la woga na majuto lilimtoka.

“Nakuomba kitu kimoja bwana mdogo” Kifo aliongea na kumtoa mawazoni. Aliinua kichwa chake na kumtazama.
“Chaza hoteli iko Dodoma na kwenye kibao cha kuhifadhia funguo, kuna ufunguo upo na hautumiki. Ufunguo huo ni namba 105. Hakikisha unaupata ufunguo huo, kisha follow the money” Aliongea kwa utulivu mkubwa na alimaanisha. Lakini maneno yake yalimwacha njia panda aliyeambiwa.

Midomo ilimwanguka tena kwa mshangao, maneno aliyoambia hakuyaelewa kabisa na hakujua kwa nini mtu yule alikuwa anamwambia habari zile. Maswali mengi yalipita kichwani mwake na aliamua kuchagua swali moja alilohisi ni sahihi kuliuliza wakati kama ule.
“Kwa hiyo unamaanisha nikiupata huo ufunguo, nitazifikia hizo pesa?” Aliuliza.

“Pesa!? Pesa zipi bwana mdogo!”

“Haah!” Ulikuwa ni mshangao wa karne kwa Willy Kondo. Kichwani mwake alijua tafsiri ya follow the money, ni fuata pesa kwa lugha ya kiswahili sasa vipi tena bwana yule aseme siyo pesa, wakati na ufunguo upo Chaza?

Aalah! Ajabu hii
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom