Nawatukana vijana wote wa Kiafrika2

musicarlito

Senior Member
Dec 29, 2020
176
289
NAWATUKANA VIJANA WOTE WA AFRIKA
(Sehemu ya pili)

3. Kama kweli “SISI TUNA WATU” tunalia nini umaskini na kukosa mitaji? Si vijana mwatume baba zenu na mama zenu waruke usiku wa kesho hadi China na Ujerumani na vyuma ulete vyao wakazichomoe hela za mabilionea huko? Kwa nini kama kuna “chuma ulete” kwa nini hamwapi mawaziri wa fedha, ambao wengi ni vijana, wakaenda kutumbukiza kwenye benki kuu za Ulaya, China, Japan au Marekani tukarudi kuzikinga pesa katika benki zetu kuu tukajiepusha na tozo na ushuru tunavyokamuana pasipo huruma?

Ninyi vijana mnaoamini habari za chuma ulete na uchawi, kwa nini hamwibii Mark Zuckerberg CEO wa Facebook au akina Bill Gates wa Microsoft wanaotuchukulia pesa zetu kila siku? Utajiri wao sana unawafanya matajiri namba tano na namba mbili mtawalia ulimwenguni na wamempita Aliko Dangote wetu zaidi ya mara sita, sasa kwa nini hamwaaliki hao mnaowaamini kwamba wana vitu wakawaibia kwa vyuma ulete utajiri huo mkagawana na hata sisi wazee mkatupa “hasusa” kidogo?

Halafu makampuni ya kimataifa matajiri kabisa, kwa mfano, Facebook, Microsoft, Apple, Amazon, Barshire Hathaway, Exxon Mobil, General Electric, Alphabet, Johnson and Johnson na China Mobile, yana pesa za kunuka. Hamyajui?

Au kwa nini hawaendi kuyaibia makampuni makubwa ya kimataifa yanayolinyonya bara la Afrika hata kujipatia pesa nyingi kupita nchi zetu nyingi? Vipi hao watu wenu wenye vyuma ulete mnaosadiki kwamba wapo wanawaibia akina mama ntilie, wauza matembele na wakulima wa mpunga wa Ushirombo na sehemu zingine kama hizo? Basi, sisi wazee wenu na ninyi vijana wetu, wote wajinga sana!

Hivi vijana hamwaambii hao “wachawi” mnaoamini kuwapo kwamba licha ya makampuni kuna matajiri wenye pesa binafsi, ambao wakienda kuwaibia hata sisi tutambulia kitu? Hamwajui akina Elon Musk, tajiri namba moja na mkurugenzi wa Tesla, Musk’s Rocket Company na Space X; Jeff Bezos wa Amazon; Bernard Anault & Family wa LVHM; Bill Gates wa Microssoft; Mark Zuckerberg wa Facebook; Zhong Shanshan, mfanyabiashara mkubwa; Larry Ellison wa Oracle Company; Warren Buffet wa Barkshire Hatthaway; Larry Page wa Google na Sergey Brin wa Google pia? Matajiri hawa wana pesa “za kunuka” ambazo “vyuma ulete” vingeweza kutuletea na siyo pesa za akina mama ntilie maskini na wachoma vitumbua na maandazi wa Makoroboi, Kariokoo au Sokomjinga. Vijana mpo hapo? Niambieni vijana!

4. Kama kweli “SISI TUNA WATU” tunaliaje njaa barani mwetu? Wenye uwezo wa kuiba vyakula kutoka kwenye mashamba ya wenzao kwa vipi hawatuibii vyakula kutoka mashamba ya Wazungu, Wamerikani, Wachina na kadhalika tukapumzika kulima kwa majembe ya mkono? Je, kwa utaalamu wa kuiba vyakula vya wengine tusingeweza kuzika kwa milele sera na kauli mbiu za “Kilimo ni Uti wa Mgongo”, “Siasa ni Kilimo”, “Kilimo Kwanza” na kadhalika? Hizo ni sera na kauli mbiu tunazoweza kubishania ufanisi wake.

5. Kama kweli “SISI TUNA WATU” tunalia nini maradhi? Hivi watu wetu hawezi kuroga bacteria, virusi, vimelea, amoeba na kadhalika, yaani visababishi vya magonjwa vikakoma nasi tukawa na afya mwanzo mwisho? Aidha, kama kweli tuna watu, wenye uwezo wa kutoa maiti makaburini pasipo kufukua, kwa nini hawatoi sehemu zilizovimba za wagonjwa wa saratani huko Ocean Road, wagonjwa wakapata nafuu kwa haraka na kwa bei wanayoimudu?

6. Kama kweli “SISI TUNA WATU” kwa nini tunalia kuogopa Wazungu watatuua kwa chanjo zao, kwa namna ya pekee chanjo ya UVIKO 19? Si tuwawahi sisi kabla hawajatuwahi? Jambo la kwanza watu wetu kwa uchawi wao wavuruge maabara za Wazungu zinazotengeneza chanjo hizo. Kesho wakiingia wakute nyoka tu humo au wakute vitu na vifaa vyao vyote vimegeuka konokono wasijue la kufanya zaidi. Jambo la pili labda tuwatie wendawazimu wasambaratike kama walivyosambaratika wajenzi wa mnara wa Babeli. Kama hivyo havitoshi, tuwaroge kabisa watafiti na watu hao wanaotengeneza chanjo zilizodhamiriwa kutuua. Maana yake tuwawahi kabla hawajatuwahi kutuua. Je, si mbinu ya kijeshi hii, ya kumuua adui kabla hajakuua wewe? Kama hatuwezi kujiokoa kwa mtindo huu, basi sisi wajinga, tena wajinga mno. Mtu una uwezo wa kumuua adui yako, unamwacha tu hata akuue, si ujinga huo?

7. Kama kweli “SISI TUNA WATU” kwa nini hatujawahi kuchukua kombe la dunia? Katika kila mashindano ya kombe la dunia wawakilishi wetu hupigwa mabao na kurudi mikono mitupu, watu wetu wanakuwa wapi? Tunaamini kweli kwamba wanazidiwa na wazungu na Wamarekani wa kusini kwa juju? Sisi kweli wajinga. Hivi hatuamini kwamba mpira ni sanaa inayokwenda kwa nidhamu, stamina, mbinu, uzalendo na moyo wa mapambano?

8. Kama kweli “SISI TUNA WATU” tunalia nini vita? Najua wapo wanaotamani kunibisha vijana kwa watu wazima. Wao wananibisha kwa utetezi kwamba watu tulio nao ni balaa katika mambo hasi tu. Sasa lakini, tukijitetea kwa kusema nguvu za wachawi zinatumika katika kutendea mambo ya kikatili na kihalifu tu, vipi basi mbona hatutumii nguvu hizo kuwazimia Al Shabaab, Boko Haram, ADF na ISIS wanaotuua wenzao huko Somalia, Msumbiji, Nigeria, Niger, Mali, Cameroon, Chad, Congo na kadhalika? Makundi ya kigaidi yanatuua Waafrika, kwa maelfu, kututia vilema, kutuacha pasi makazi na kutusababishia adha zinazolifedhehesha bara zima la Afrika. Je, hatuwezi kujisaidia wenyewe kwa uchawi? Mimi nang’aza ujinga mwingine hapo ! Basi, nawatu- kana vijana wote pamoja na watu wazima na wazee wote wa Afrika!

Umoja wa Afrika umepitisha tamko la KUNYAMAZISHA BUNDUKI barani mwetu lakini bado zinarindima. SADAC na hata ECOWAS wameakisi mwangwi wake wake pia, ndiyo maana wameamua kuingilia katika vita dhidi ya magaidi huko Msumbiji na Nigeria. Kama ndivyo, kwa nini kama tuna watu wasijitokeze kwenda kuzima bunduki zote hizo kwa ulozi? Nauliza tena. Kwa nini “watu tulio nao” wasinyamazishe vita barani mwetu ama kwa ulozi baridi basi au kwa ulozi wenye nguvu zaidi ya AK 47? Watu wetu, yaani wachawi wetu, walioko Ngende, Sumbawanga, Tanga, Msumbiji, Gambosi, si wawaroge Al Shabaab, kule Somalia na Msumbiji wafe wote? Si wawaroge Boko Haram kule Nigeria na pande zote za nchi za Sahel bunduki zinyamaze? Si wawaroge Wazungu wanaochochea vita Kongo katika mbinu za kuiba madini, kama vile dhahabu na coltan, kule pamoja na makundi yote ya waasi wakiwamo na ADF? Wajinga sisi! Au kama si wajinga sisi, tunafeli wapi kuwatumia watu tulio nao kutuletea maendeleo ya mwili?

Kwa jinsi nilivyotoa changamoto ambazo bila shaka zimefanikisha kuonesha upuuzi wa imani katika uchawi, ninaweza kukuulizeni swali la aina yake: Hivi maombi ya wachungaji dhidi ya nguvu ya wachawi yana faida gani? Wanatoa jasho kwa mantiki gani? Ni nguvu au uwezo gani wanaotirizana nao? Siyo kivuli na chui wa karatasi tu? Hao wachungaji na wanamaombi wanatuombea Waafrika tupate nini au dhidi ya kitu gani? Hatujaona nguvu chanya wala nguvu hasi isipokuwa hewa tu. Sasa wachungaji au manabii wanaamini nini hasa? Basi, hapo napo pana ujinga wa kiwango cha lami.

Hapa napatukana vile vile! Watu wa mabara mengine, vijana, watu wazima kwa wazee, wanapokuna vichwa namna ya kupata roketi na roboti bora kwa kuzikabilia anga za juu, Waafrika tupo bado chini tukihangaika na mabimkubwa na wazee wenye macho mekundu na hadithi zetu za fisi, mbweha, kenge, mijusi na magamba ya miti! Kweli sisi wajinga!

Tutawapataje hapo watu wa mabara mengine wakati hata kuwafukuza hatuwafukuzi? Kumbe, ulofa huu ndio unawaobainishia wenzetu kwamba tuna Hisa ndogo kabisa ya Akili (IQ) na ndiyo kisa hawaogopi kuja kuchukua madini, urani, coltan na raslimali zetu zingine mchana kweupe. Na kwa ujumla siku hizi nchi zetu zinatangaza zenyewe na kuwaalika watu wa mabara mengine waje wachukue wanachokitaka kwani “tumewawekea masharti nafuu”. Uuuuuwiiiiiiiii! Mwenzenu nanyong’onyea!

Namalizia kwa kuwapozeni vijana wangu. Tusi nililowatukana linakuja kwetu wazee wenu pia. Kama zamani hizo TULIKUWA NA WATU mbona hatukuwaroga Wazungu waliotukamata utumwa? Mbona hatukuwaroga wakoloni walijinyakulia nchi zetu? Mbona hatukuwaroga wakoloni waliokuwa wanatulimisha pamba kwa viboko? Mbona AKILI YA KINJIKITILE, akili ya kukabiliana na risasi za moto kwa kuzitamkia “MAJI, MAJI, MAJI, MAJI!” zilifeli wakafa watu chungu nzima? Mbona nchi zetu nyingi zilitumia bunduki za Wazungu wenyewe hao hao kuwatimulia Wazungu wenyewe? Kumbe, kwa namna hii hata sisi wazee wenu tulikuwa wajinga na ndiyo maana tumekurithisheni ujinga nyie pia. Tulikuwa wajinga wakati ule, yaani wala hatukuwa na watu wowote, sawa na tulivyo wajinga sasa na wala hatuna watu wowote sasa.

Kumbe, vijana mnapotuua vikongwe na maajuza kwa tuhuma za uchawi tunavuna tu tulichopanda. Kwa kweli ilitupasa tusilie wakati nyie watoto na wajukuu wetu mnapouawa kwa sababu kama tulikuwa tunawafundisheni na kuwasadikisheni habari za uwapo wa wachawi na vigezo vyao, mnapotuua ni siku ya “graduation” kwa sababu tuliyowafundisheni yamewafikisheni mahali pa kutuona sisi wenyewe ndio wachawi na walimu huwa hawalii siku ya “graduation” ya wanafunzi wao wenyewe.

Hata hivyo, msifurahie kutuua sisi maana nanyi itawafika zamu ya kuuawa vile vile kwa sababu tumetengeneza “mzunguko mshenzi” tu. Msifurahie kutumaliza sisi leo kwani sina mashaka kwamba itakapofika zamu yenu kuuawa na watoto na wajukuu wenu kwa tuhuma za uchawi mtalia vile vile, maana wakati huo mtafundishwa kwa vitendo maana ya methali ya MKUKI KWA NGURUWE KWA BINADAMU UCHUNGU.

Nimeandika mengi na bado ningeweza kuandika mengi zaidi. Lakini aheri nikomee hapa ili atakaye kusoma arudie makala hii kwa urahisi. Kwa hayo yote, hivi sisi, ninyi vijana na sisi wazee wenu si wajinga na waongo? Hivi kweli sisi wazima? Naona aibu lakini nauliza. Papo hapo nimewatukaneni nyote.
Mzee wenu Pd. Titus Amigu. MWISHO.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom