Kuna ukweli gani kuhusu vinywaji vya Energy Drink kusababisha Madhara kwenye Figo?
- Tunachokijua
- Unywaji wa vinywaji vya kuongeza nguvu (Nishati) umekuwa ukiongezeka kwa kasi katika miongo miwili iliyopita, hasa miongoni mwa vijana. Vinywaji hivi hudaiwa kuwa na uwezo wa kuboresha utendaji wa mwili na akili. Hata hivyo, tafiti zinazounga mkono madai haya ni chache.
Madhara kadhaa ya afya yamehusishwa na kinywaji cha nishati hivyo kuzua maswali mengi iwapo vinywaji hivi ni salama.
Kwa mujibu wa Kituo Cha Udhibiti na Kinga ya Magonjwa (CDC), matumizi makubwa ya vinywaji hivi yanaweza kusababisha athari kubwa kwenye mfumo wa kati wa fahamu.
Athari zingine za vinjwaji hivi ni Kuufanya mwili upoteze kiasi kikubwa cha maji, Magonjwa ya mfumo wa damu na moyo, Wasiwasi uliopitiliza na Kukosa usingizi.
Madhara ya Energy Drinks kwenye Figo
JamiiCheck ilimtafuta Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo JKCI, Pedro Pallangyo kuhusiana na suala hili ambapo alisema husababisha kufeli ghafla kwa figo pamoja na kuongeza nafasi ya kutengenezwa kwa mawe kwenye kiungo hicho.
Aidha, kwa mujibu wa tafiti, Energy Drinks huufanya mwili upoteze kiasi kikubwa cha maji. Hii inaweza kuongeza nafasi ya kupatwa na magonjwa ya figo.
Utafiti uliowahi kufanyika Tanzania kuhusu Energy Drink
Aprili 2023, Taasisi ya Moyo ya JKCI ilichapisha utafiti wake ukimhusisha kijana wa Kitanzania mwenye umri wa miaka 28 aliyeziba mshipa wa moyo kutokana na kutumia kiasi kikubwa cha Energy Drinks cha kopo 5 ndani ya masaa 4.
Pamoja na mambo mengine, utafiti huo ulionya kuwa mtu asinywe zaidi ya kopo moja lenye ujazo wa mililita 250 ndani ya saa 24, huku ukisisitiza kama kuna uwezekano wa kuviepuka, ifanyike hivyo kulinda afya ya mhusika.
Baadhi ya viambato vinavyotumika kutengeneza vinywaji hivi ni maji, sukari, ladha, caffeine, tauline (amino acid), protini, vitamini, madini. Inaelezwa kuwa caffeine pamoja na mambo mengine, hufanya kazi ya kuzuia uzalishwaji wa kichocheo cha mwili kinachohusika na kulala ama kuhisi uchovu.
Maelezo ya Kitaalamu
JamiiCheck imezungumza pia na Dkt. Anthony Gyunda, Bingwa wa Magonjwa ya Figo ambaye ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Figo kutoka Hospitali ya Muhimbili – Mlonganzila, Dar es Salaam anaelezea:
"Vinywaji vingi vya ina hiyo vimetengenezwa zikiwa na caffeine nyingi pamoja na kemikali zingine ambazo zina madhara makubwa kwenye kila kiungo au viungo vya mwili wa Mwanadamu.
Kwa ujumla ‘energy’ hazifai kwa matumizi ya kila siku kwa binadamu, kwani kuna vimelea vya uraibu, hali ambayo inaweza kusababisha mtu kulazimika kunywa vinyaji kadhaa kila siku.
Vinywaji kama vya Energy ni hatari, vikiendelea kuachiwa bila kudhibitiwa vinaweza kuwa na madhara makubwa zaidi kwenye jamii. Organs zote kwenye mwili zinaweza kuathiriwa na vinywaji hivyo kutokana na wingi wa caffeine"
Kuhusu madhara ya vinjwaji hivi, Dkt. Gyunda amefafanua vinaweza kuwa na athari kwenye mishipa, moyo, ubongo, mishipa ya fahamu, figo na hata mapafu pia.
- Moyo: Moyo kupiga hovyo, shinikizo la juu la damu, kifua kuuma na hata kifo cha ghafla kinachosababishwa kwa moyo kusimama ghafla.
- Ubongo: Sonona, kifafa, kichaa, uraibu.
- Figo: Figo kushindwa kufanya kazi kupelekea kuhitaji dialysis.
- Uzazi: Zinapunguza madini muhimu ya kuzalisha mayai kwa Wanawake na mbegu za kiume, hivyo hili tatizo la ugumba na utasa kwa vijana, zinahusika sana.
Kwa nini Energy nyingi zinaandikwa hakuna kunywa kabla ya kulala?
Dkt. Gyunda: Unapokunywa Energy inamaanisha ubongo wako uwe active, hivyo unapokunywa kisha ukaenda kulala hauwezi kupata usingizi vizuri.
Kuna madhara gani ya Energy kwa watoto na vijana wadogo?
Dkt. Gyunda: Mtoto mdogo ana nafasi ya kukua kwa viungo na hata ubongo wake, hivyo anapotumia Energy inamaanisha analazimisha viungo vyake vifanye kazi juu zaidi ya umri wake, hiyo inasababisha viungo vithirike.
Kibaya zaidi kuna vijana huchanganya energy na pombe kali, hili linakuwa kama bomu la nyuklia kabisa.
Unashauri mtu anywe energy ngapi kwa siku?
Dkt. Gyunda: Mimi binafsi ningekuwa na mamlaka ningepiga marufu uuzaji na kuingiza kwa kuwa madhara yake ni makubwa. Kuniambia anywe kwa kiwango fulani ni sawa na kumwambia mtu aonje sumu.