Matumaini kupata tiba ya Ukimwi yaongezeka

Jemmie

JF-Expert Member
Mar 6, 2018
216
285
Juhudi za kusaka tiba ya ugonjwa wa Ukimwi zinaendelea miongoni mwa wanasayansi ulimwenguni, huku taarifa za matumaini kuhusu upatikanaji wake zikizidi kujitokeza. Tanzania haijaachwa nyuma katika jitihada za kukabiliana na Ukimwi baada ya watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kutoa taarifa hivi karibuni kuhusu hatua walizofikia katika kusaka chanjo dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Kwa zaidi ya miongo mitatu sasa, wanasayansi kutoka Muhas wamekuwa wakitafiti chanjo ya VVU, wakihusisha maofisa wa polisi katika utafiti wao. “Matokeo ya awali ya utafiti huo yanaashiria kwamba Tanzania inaweza kufikia hatua ya kuvumbua chanjo dhidi ya VVU ikiwa tafiti za ziada zitafanyika,” alisema Profesa Eligius Lyamuya, mratibu wa utafiti huo, wakati akiwasilisha mada yenye kichwa kisemacho “Tulipotoka, Tulipo na Tunapoelekea”.
Huku wataalamu nchini wakiendelea kusaka chanjo, habari za matumaini kutoka jijini London, Uingereza zilisema juzi kuwa mgonjwa aliyekuwa akiishi na VVU ameonekana kupona Ukimwi baada ya kupandikizwa uboho (bone marrow) kutoka kwa mtu mwingine.
Kiongozi wa jopo la madaktari waliomtibu mgonjwa huyo, Profesa Ravindra Gupta, ambaye ni mtaalamu wa baiolojia ya VVU, ameeleza kuwa mgonjwa aliyepewa huduma ya kupandikizwa uboho, ameondolewa virusi lakini akaonya kuwa ni mapema kusema amepona kabisa.

“Hakuna Virusi vya Ukimwi ndani yake ambavyo tunaweza kuvipima na kubaini. Hatuwezi kuona chochote… lakini ni mapema kusema kuwa amepona kabisa,” alisema Profesa Gupta kama alivyokaririwa na AFP.
Jumanne ijayo, wataalamu waliomtibu mgonjwa huyo wanatarajiwa kutoa undani wa taarifa hizo katika jarida la kisayansi la Nature na pia kuwasilisha mada kuhusu ‘uponaji’ katika mkutano utakaojadili virusi aina ya retrovirues na maradhi nyemelezi, utakaofanyika Seattle, Marekani.

“Hii inaonyesha kwamba tiba si ndoto,” alisema mmoja kati ya wanayansi hao, Dk Annemarie Wensing wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Uholanzi. Hii ni kwa mara ya pili dunia inajulishwa uwezekano wa mgonjwa mwenye VVU kuonekana amepona. Mgonjwa wa sasa ambaye ni wa London, Uingereza na wa Berlin, Ujerumani aliyekuwa anatibiwa saratani 2007 wote walipandikizwa uboho ili kutibu saratani na si VVU. Hata hivyo, watafiti wametahadharisha kwamba upandikizaji wa uboho hauwezi kuwa suluhisho la kutokomeza virusi vya Ukimwi kiuhalisia katika siku za usoni.

Hapa Tanzania, taarifa hizi zimepokewa kwa mitazamo tofauti miongoni mwa jamii, huku baadhi wakihoji ‘inawezeakanaje mtu kupona kabisa VVU?’Hata hivyo, Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema taarifa za mgonjwa wa Ukimwi kupona “ni habari njema katika makabiliano yanayoendelea dhidi ya ugonjwa huo”. “Imani yangu ni kwamba hii ripoti itahamasisha utafiti zaidi kuhusu tiba na chanjo dhidi ya VVU,’’ alisema. “Licha ya habari hizi za matumaini, napenda kuwashauri Watanzania kuendelea kutumia huduma zilizopo hapa nchini, hasa katika kuzuia maambukizi. Ugonjwa wa Ukimwi mpaka sasa hauna tiba.” Karibu watu milioni 37 duniani wanaishi na VVU, lakini ni asilimia 59 tu wanapata dawa za kufubaza virusi hivyo, huku watu milioni moja wakipoteza maisha kila mwaka kwa ugonjwa huo.
 
Back
Top Bottom