Matokeo mabaya darasa la saba 2007: Walimu wakuu wampinga Sitta

Keil

JF-Expert Member
Jul 2, 2007
2,214
803
Matokeo mabaya darasa la saba 2007: Walimu wakuu wampinga Sitta

*Wasema usimamizi mbovu si sababu
*Wamwambia uhaba wa vitendea kazi
*Waeleza walimu vijini ni hohehahe
*Wanena wa mjini wanafaidi twisheni


Na Francis ole Rikanga, Arusha

BAADHI ya walimu wakuu wa shule za msingi mkoani Arusha wamepingana na kauli ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bibi Margret Sitta, aliyoitoa kwa vyombo vya habari kuhusu wanafunzi wa darasa la saba kufeli mtihani mwaka huu kwa asilimia 16.3.

Walimu hao walisema jana kuwa sababu iliyosababisha wanafunzi wengi kufeli ni uhaba wa vitendea kazi, upungufu wa walimu na wingi wa wanafunzi madarasani na wala si usimamiaji wa mtihani kama alivyosema Waziri Sitta.

Wakizungumza na Majira mkoani hapa kwa masharti ya kutotajwa majina, walimu hao walisema shule nyingi na hasa za vijijini, zimekuwa na walimu wachache huku vitabu vikikosekana, hali inayowafanya wanafunzi kushindwa kujisomea na kufanya mazoezi wenyewe.

Walifahamisha kuwa walimu wengi wamekuwa wakikimbia shule za vijijini, kutokana na mazingira magumu yaliyopo na kuwafanya wachache wanaobaki kubeba mzigo mkubwa ambao wanashindwa kuumudu.

"Walimu wengi hawataki shule za vijijini, unakuta shule ina walimu wanne wakati wanafunzi ni 1,400, sasa hao walimu wanne watafanyaje kazi hiyo? Hapa wanafunzi wataweza kusoma vizuri kweli?," alihoji mmoja wa walimu hao.

Aliongeza:"Katika kuwafundisha wanafunzi, wapo wanafunzi makundi matatu, wanaofahamu zaidi, wanaofahamu kiasi na wasiofahamu kabisa. Sasa kwa uhaba huu wa walimu na wingi wa wanafunzi darasani, kila darasa unakuta lina wanafunzi 150 sasa unatarajia kweli mwalimu mmoja aweze kuhudumia vizuri hao wanafunzi wote na baadaye wafaulu vizuri?"

Akieleza sababu ya wanafunzi kufeli somo la Hisabati, mmoja wa walimu hao alisema wanafunzi wamekuwa wakifeli masomo hayo kutokana na walimu walio wengi wanaopangwa katika shule za msingi kutopenda kufundisha masomo hayo.

Alisema hivi sasa walimu wengi katika shule za msingi wamekuwa wakilikimbia somo la Hisabati na Kiingereza, hivyo Serikali haina budi kubuni mbinu itakayowafanya walimu wengi kupenda masomo hayo ili wa kufundisha masomo hayo wapatikane kwa uhakika na wanafunzi wapate kuelewa masomo hayo vizuri.

"Mimi labda ningependa kuishauri Serikali ingewalipa walimu kufuatana na masomo wanayofundusha, kwa mfano walimu wa Hisabati na Kiingereza wangelipwa kulingana na masomo hayo; nafikiri Serikali kama itafanya hivyo, wanafunzi watakaokwenda vyuo vya ualimu naamini kabisa watapenda Hisabati na kwa njia hii, tutapata walimu wengi wa masomo hayo," alishauri mwalimu huyo.

Aidha, walimu hao pia waliitaka Serikali kutoa kipaumbele kwa walimu wanaofundisha vijijini, ili walimu wengi wapende kukaa katika shule hizo, kwani wamekuwa wakikimbia kutokana na mazingira magumu yaliopo na wengi kukosa kazi za ziada, kama twisheni, ikilinganishwa na walimu wa mjini ambao katika saa ya ziada, huzama katika kufundisha twisheni na kufanya wapate kipato cha ziada.

"Lazima Serikali iwalipe walimu wa shule za vijijini mshahara wa tofauti na mwalimu wa mjini, sisi hatuna twisheni tunaofanya hapa tunategemea mshahara tu, tofauti na wenzetu wa mjini wao jioni utawakuta wanafundisha twisheni wanapata kipato cha ziada, ndiyo sababu wakipangiwa kuja kufundisha kijijini, wakikaa mwezi mmoja tu wengine wanatoroka au wanatafuta kwenda kusoma," alifafanua mmoja wa walimu hao.

Pampja na hilo, walimu hao pia waliwataka wazazi kuwa na tabia ya kuwanunulia wanafunzi vitabu vya kujisomea, badala ya kutegemea Serikali, kwani hivi sasa Serikali inashindwa kumudu gharama hizo.

Source: Majira
 
Mama Sitta anayajua yote haya, ila sasa hawezi kuyasema kwa kuwa yuko "miongoni mwao". Akiondoka tu utamsikia anaanza kuyasema hayahaya kama vile hakuwahi kupata nafasi ya kuyashughulikia. Tumewaona akina Tabitha Siwale na Jackson Makwetta wakilalamikia mambo ambayo walipokuwa mawaziri wa wizara hiyohiyo waliyakalia kimya kama vile hayakuwepo. Sijui ni ile ya "nyani haoni kitugani" au tuseme "Mzigo wa mwenzio ni ganda la sufi"?
 
Back
Top Bottom