SoC01 Mateso ya Binti wa Shule yaliyopuuzwa na Jamii

Stories of Change - 2021 Competition

Geo C Starfish

New Member
Jul 17, 2021
4
6
Katika familia nyingi za kiafrika hasa ndani ya nchi yetu ya Tanzania, kuzaa watoto inachukuliwa kama baraka kubwa sana na hasa watoto hao wakiwa wa jinsia zote mbili, watoto wa wakiume na watoto wakike. Na hata inapotokea familia imepata watoto wote wa jinsia moja, wazazi huiona kama haijakamilika, hivyo huthubutu kuitafuta jinsia nyingine bila kujali idadi ya watoto iliyonayo kwa wakati huo. Yote ni kutafuta amani na baraka ndani ya familia na kwenye jamii kwa ujumla.

Kwa kawaida sisi binadamu kuzaa watoto huwa ni swala lisilo na ugumu wowote, ila shida kubwa kwetu huja kwenye upande wa kuwalea. Tunapenda watoto wa jinsia zote lakini tunashindwa kuelewa kuwa malezi yao kamwe hayafanani. Na huwa tunafanya hivyo labda kwa kutokujua au kwa kusahau kuwa mtoto wa kiume malezi yake ni tofauti kabisa na malezi ya mtoto wa kike. Na hapa ndipo familia na jamii zetu nyingi hujikuta zinamuweka matatani mtoto wa kike kwa kujua au hata kwa kutokujua. Kuna mambo mengi sana ya kujiuliza juu ya mitazamo ya familia na jamii zetu kuhusu mtoto wa kike.

Hivi ulishawahi kujiuliza maswali haya;
Jamii inamchukuliaje mtoto wa kike?
Au jamii imewekeza nini kwenye maisha ya mtoto wa kike?

Hebu mfikirie kwa kina binti huyu ambaye ni mwanafunzi.

Asubuhi binti anaamka kwa kukurupuka akihisi amechelewa kuamka baada ya kulala usingizi mzito uliotokana na uchovu wa kazi nyingi alizozifanya jana yake shuleni na nyumbani. Akili yake ikiwa imejaa mawazo mengi juu ya majukumu anayotakiwa kuyafanya hapo nyumbani huku akitakiwa pia kufanya baadhi ya maswali aliyopewa shuleni na walimu kama kazi ya nyumbani.

Wazazi wake wote wakiwa tayari wamedamka alfajiri na mapema na kuondoka kuelekea kwenye shughuli zao za kila siku za kutafta riziki, hivyo ni jukumu lake yeye kama binti kuhakikisha nyumba yote inakuwa safi kwa kufagia, kudeki, kuosha vyombo na hata kuwaandaa wadogo zake ili nao waende shule na ikiwezekana kuwaandalia na kifungua kinywa ambacho watakula wakati huo na kingine watakikuta baadae watakaporudi kutoka shule wakati ambao yeye dada yao atakuwa hajarudi.

Anapambana kufanya kazi zote lakini sababu ya muda kumtupa mkono swala la kufanya kazi aliyopewa na walimu jana shuleni linashindikana hivyo anaamua na yeye kujiandaa ili aweze kuwahi shule asije akachelewa na kukumbana na adhabu kali za wachelewaji. Licha ya changamoto ya umbali mrefu wa kutoka nyumbani mpaka kufika shuleni, njiani anakutana na changamoto nzito zaidi za vijana na hata watu wazima wa umri wa baba yake ambao humsumbua kila siku kwa vishawishi kibao vya fedha na vizawadi wakitaka awe nao kimapenzi. Japo kila siku huwakatalia na kuwatukana kwa sababu ya kuamini watamuharibia maisha yake na ndoto zake za kufanikiwa kielimu, lakini hawakomi kumsumbua.

Kwa bahati nzuri kutokana na mwendokasi mkubwa wa kutembea leo anajitahidi na kufika shuleni kwa wakati japo kachoka lakini inakuwa si sawa na siku zingine ambazo huchelewa. Shuleni anakutana tena na kazi kadhaa za kufanya usafi wa mazingira ya shule. Muda wa kuingia darasani unapofika na walimu kuanza kuingia kwenye vipindi.

Anajikuta matatani kwa kukutana na adhabu ya kila mwalimu ambaye aliwapatia kazi jana yake ya kufanya wakiwa nyumbani sababu yeye hakufanya kazi hizo kwa kukosa muda. Na baadhi ya walimu wanaamua kumpa adhabu kali zaidi wakidai anadharau sababu ni mara nyingi huwa hafanyi kazi zao.

Anajitahidi kufanya adhabu hizo ambazo ni fimbo na kazi za nje huku wanafunzi wengine wakiendelea na vipindi. Anapobahatika kumaliza na kurudi darasani, mwili wote na ubongo vinakuwa vimechoka kiasi cha kushindwa kabisa kuelewa masomo yanayoendelea darasani.

Wakati akiwa hapo shuleni, bado pia kuna walimu kadhaa wa kiume ambao humfatilia kila siku kwa vitisho vya viboko na vishawishi mbalimbali kama vya kumpa majibu ya mitihani ili awakubalie kimapenzi. Msimamo wake wa kuwakatalia kila siku humfanya aambulie viboko na adhabu zisizo na sababu kutoka kwa walimu hao. Na hii humuongezea zaidi mateso na majuto ya kuwa binti.

Muda wa kurudi nyumbani unapofika, binti hujikuta akiwa hoi bin taabani kwa adhabu na viboko vya shuleni pasipo kujifunza chochote kipya walichojifunza wenzake. Na bado anapokuwa njiani kurudi nyumbani hukutana tena na wale wanaume wanaomuhitaji kimapenzi wakiwa wanamvizia njiani ili kuendeleza ushawishi wao kwake. Kwa msimamo wake hufanikiwa kuwakwepa na kufika nyumbani salama bila shida.

Akifika nyumbani huwakuta wadogo zake wakiwa wanamsubiri huku wazazi wake wakiwa bado hawajarejea kutoka mihangaikoni, hivyo kutokana na njaa ya kutwa nzima waliyonayo humlazimu kuingia jikoni na kuandaa chakula chake na wadogo zake. Huku akiwa na kazi nyingine inayomsubiri ya kufua sare zake za shule na za wadogo zake ili kesho siku ya usafi shuleni wasikumbane na adhabu za wanafunzi wachafu.

Mpaka anamaliza shughuli zote tayari jioni inakuwa imeingia, na hivyo kumfanya aanze kuandaa chakula cha usiku cha familia nzima ikiwa wazazi wake hasa mama yake ambaye huwa anamsaidia mara moja moja anapowahi kurudi nyumbani anakuwa hajarudi.

Hii humfanya azidi kuchoka zaidi na kukosa kabisa muda mzuri wa kupumzika na kufikiria masomo yake hasa maswali waliyopewa shuleni na walimu. Na ikitokea akajikaza aweze kufanya maswali hayo, kwa uchovu wa mwili na akili akiwa mezani, usingizi unampitia na mwisho anaamua kwenda kulala akijipa moyo kuwa ataamka mapema ili aweze kufanya maswali hayo kabla ya kufanya kazi nyingine yoyote.

Asubuhi anashtuka amechelewa kama ilivyokuwa jana yake sababu ya usingizi mzito aliolala uliotokana na uchovu wa kazi nyingi alizofanya. Na mambo hubaki hivyo hivyo kila siku kwa binti huyu.

Wazazi wapo mbali nae na familia kwa ujumla kwa kisingizio cha kutafuta riziki. Na hata ikitokea binti anahitaji pesa kwa ajili ya mahitaji yake muhimu ya kimwili na kielimu bado wazazi wake wanakuwa mbali nae kwa kutomsikiliza na kumpatia fedha hizo. Hii inamfanya binti aanze kuzifikiria pesa ambazo huwa anazikataa kutoka kwa wanaume na walimu wanaomuhitaji kimapenzi.

Mwisho uvumilivu unamshinda, anapoteza msimamo wake na kuamua kuwakubalia wanaume hao ili aweze tu kupata pesa za kutatua changamoto zake. Pia ili kuwalizisha wazazi wake juu ya maendeleo yake shuleni anajikuta ameingia kwenye mahusiano na walimu ili tu wamsaidie kumpa alama za uongo kwenye mitihani yake aonekane amefaulu vizuri.

Kutokana na hali hiyo, binti anabadili tabia kabisa na kuamua kutembea na mwanaume yeyote anayeweza kumpatia chochote anachohitaji. Matokeo yake binti anaambulia mimba na/au magonjwa ya zinaa. Anafukuzwa shule na wazazi pia wanaamua kumfukuza nyumbani na asijue pa kwenda sababu aliyemlaghai na kumpa mimba kamkimbia au kamkataa. Zaidi ya yote jamii inaanza kumuona mhuni na malaya asiyefaa kuwa katika jamii hiyo. Lakini ni nani alikuwa nae katika mateso yote aliyokuwa anapitia?

Ni nani alikuwa tayari kumsikiliza na kumtengenezea mazingira salama kwa elimu yake na maisha yake?
Wazazi waliopaswa kuwa nae karibu zaidi ndio walimtenga na kumfanya mlezi wa familia ilhali ni mwanafunzi.

Walimu waliopaswa kumfundisha na kumshauri juu ya kuepukana na matendo mabaya ndio hao hao waliomtesa kwa adhabu na kumtumia kingono. Wanaume wa jamii yake waliopaswa kumchukulia kama mtoto wao au dada yao na kumlinda ndio hao hao pia waliomtumia kimapenzi.

Hayo ndiyo mateso ambayo wanayapitia mabinti na dada zetu wengi wa shule huku sisi kama jamii tukipuuza na kutokujari chochote wanachokipitia. Wapo mabinti wanaofanya uhuni kwa tamaa na maamuzi yao binafsi, lakini asilimia kubwa ya mabinti hufanya kutokana na kukosa kimbilio la kuwatetea, kuwasikiliza na kuwasaidia shida zao. Na bila shaka katika kila shule ndani ya nchi hii huwezi kumkosa binti kama huyu anaepitia mateso haya.

Tukumbushane kama jamii. Ni wajibu wetu kama jamii kuwasikiliza, kuwajali na kuwalinda mabinti na dada zetu walioko mashuleni kwa faida yao, faida ya familia zetu na jamii zetu na hata taifa kwa ujumla.
 
Back
Top Bottom