SoC01 Mateso na manyanyaso wanayopata wajawazito mahospitalini mwanzo hadi mwisho wa mimba

Stories of Change - 2021 Competition

Martin wa Tanga

New Member
Sep 14, 2021
1
1
Inashauriwa kuwa mara tu mwanamke apatapo mimba [ujauzito] aanze kuhudhuria kliniki kwa ajili ya kupatiwa vipimo, ushauri pamoja na kujua maendeleo ya mimba [ujauzito] wake kwa kuendelea kuhudhuria kliniki katika siku alizopangiwa hadi siku atakayo zaa [jifungua]. Binafsi ninaona kuwa utaratibu huu ni mzuri sana maana unaweza kupunguza au kuondoa kabisa hatari ambazo zingeweza kujitokeza kwa mama au mtoto endapo utafuatwa ipasavyo. Lakini pamoja ya kuwa utaratibu ni mzuri kwa afya ya mama na mtoto, kumekuwa na malalamiko lukuki toka kwa mama wajawazito wenyewe lakini pia kwa watu wengine waliowahi kuhudumiwa kupitia utaratibu huu juu ya mateso na manyanyaso wanayopata mara wanapoanza kliniki hadi siku ya kujifungua toka kwa manesi wa kawaida hadi kwa manesi wakunga hasa kwenye zahanati au hospitali za serikali. Kwenye andiko hili nitaeleza namna wajawazito wanavyopata mateso na manyanyaso lakini pia nitatoa pendekezo la nini kifanyike ili kukomesha tabia hizi zisizo za kiutu. mjadala huu nimeugawa katika maeneo mawili ambayo ni, mateso na manyanyaso wakati wa kliniki, na sehemu ya pili ni mateso na manyanyaso katika siku za kujifungua.

1. Mateso na manyanyaso wakati wa kliniki
Ukitembelea maeneo ya kliniki ya wazazi utagundua kuna kitu kama uadui umejengeka kati ya watoa huduma [manesi] dhidi ya wapokea huduma [wajawazito] kutokana na kauli mbaya zinazotoka upande mmoja kwenda upande mwingine. Siku moja nilimsindikiza mke wangu hospitali fulani kwa ajili ya kuanza kliniki mara alipopata mimba [ujauzito]. wakati tukiwa kwenye foleni kusubiri zamu yetu ifike kuna kitu niligundua pale maana karibu robo tatu ya wakina mama wajawazito waliokuwepo pale walikuwa wakiendesha mijadala ya kuwasema manesi vibaya na hata wakati mwingine kuwabeza. Vivyo hivyo na kwa upande mwingine, maana manesi na wao walionekana kuwa wakali na wenye lugha zisizo za upendo. Katika hili niliona kuwa upande wa wajawazito ulielemewa maana pamoja na hasira walizokuwa nazo juu ya hao wahudumu wa afya hata hivyo hawakuweza kuwafanya chochote maana wao ni kama wameshika kwenye makali wakati wenzao wameshika kwenye mpini.

Nadhani hii ni moja ya sababu zinazosababisha wanawake wengi kuanza au kuendelea na kliniki kwa kujivuta sana kwa kuwa tayari wameshajenga fikra vichwani mwao kuwa kliniki si mahali pa amani. Wakati mwingine mama mjamzito anapokosa kuhudhuria kliniki kutokana na sababu mbalimbali hujawa na hofu. Ukimuuliza hofu ni ya nini atakwambia kuwa anaogopa kliniki inayofuata watamfokea. Hali hii wakati mwingine hupelekea baadhi ya wakina mama kuamua kujijazia baadhi ya taarifa kwenye kadi zao hasa wale ambao tayari wameshapata watoto, jambo ambalo si jema hata kidogo. Je, nani alaumiwe? Binafsi ningelitupa lawama kwa watoa huduma [manesi] wenye tabia hizo maana wao ni wana taaluma ambao kwa kipindi fulani wameandaliwa wakiwa vyuoni juu ya namna ya kukabiliana na changamoto wakati wakati wanatekeleza majukumu yao, wakati wajawazito walio wengi hawana ufahamu huo.

2. Mateso na manyanyaso wakati wa kujifungua
Baada ya miezi kadhaa kupita na siku ya kuzaa [kujifungua] kukaribia, mjamzito hupaswa kurudi tena zahanati au hospitali kusubiri tukio tarajiwa la kuzaa [kujifungua]. Katika kipindi hicho mama mjamzito hupata uchungu pamoja na dalili nyingine za kujifungua. katika hali hizo mama mjamzito anahitaji maneno/kauli nzuri zenye faraja, lakini badala yake inaelezwa kuwa huko "labour" kuna manyanyaso yanayoambatana na kauli mbaya kinyume kabisa na matarajio ya wengi zikitoka kwenye vinywa vya wahudumu wa afya wasiofuata maadili ya kazi yao. Inaelezwa kuwa kuna baadhi ya wakunga hutengeneza mazingira ya rushwa kwa kutowajali kabisa wajawazito ambao tayari wamefika hospitalini wakisubiri wakati wa kujifungua ufike kwa sababu kuna baadhi ya ndugu wa wajawazito hutoa chochote [rushwa] ili ndugu ama jamaa zao wapewe uangalizi wa karibu hali ambayo imewafanya hao wakunga wasio waaminifu kufanya kuwa huo ndio mtindo wa maisha na hivyo kujenga chuki na unyanyasaji kwa wale wasiotoa hiyo rushwa. Pia, inaelezwa kuwa kuna baadhi ya mama wajawazito hupoteza maisha au watoto wao kufia tumboni kwa sababu ya kukosa huduma kwa wakati kwa kuwa tu hawakutoa rushwa. Mfano mjamzito anaona dalili za hatari na kuanza kumwita mhudumu ila kwa kuwa mhudumu huyo hakupewa rushwa anaamua kupuuza tena wakati mwingine kwa maneno ya dhihaka na yasio ya-kiutu mpaka mjamzito anapoteza uhai, halafu kiurahisi tu pasipo hofu wanakuja kumfunika shuka kwamba tayari amekufa. Hii haikubaliki hata kidogo. Inawezekana mjamzito aliyepoteza maisha kwa kutopatiwa huduma stahiki kwa kuwa tu hakutoa rushwa ni masikiniambaye hata hapo hospitali aliletwa kwa usafiri wa baiskeli kwa kuwa hakuwa na pesa ya kudodi tax halafu ndani kuna mtu mwenye taaluma amekaa anasubiri rushwa toka kwake. Ni dhambi kubwa!

Nini kifanyike?
Inawezekana yakawepo mambo mengi ambayo yakifanyika yanaweza kuwa mwarobaini wa tatizo ama tabia hizi mbaya mahospitalini lakini hapa nimejaribu kueleza kwa ujumla kama ifuatavyo:

1. Uongozi
Katika nchi yetu bado kuna tatizo la udhaifu wa uongozi au usimamizi kwenye idara ama taasisi mbalimbali. Hii inapelekea baadhi ya watendaji kufanya watakavyo maana wanajua kuwa nafasi ya kufanya hivyo wanayo maana hawafuatiliwi ipasavyo hasa kwenye taasisi za serikali. Rai yangu kwa serikali ni kwanza itambue kuwa ukatili na unyanyasaji wa aina hii upo na umeshamiri katika hospitali zetu hapa nchini. Hivyo, kupitia wizara husika na idara zingine itafute namna bora ya kukomesha vitendo hivi visivyo na utu kwenye zahanati pamoja na hospitali zetu kwa ujumla. Pendekezo langu ni kuwa utumike utaratibu wa kuweka mabango mahospitalini yanayokemea rushwa na unyanyasaji. Katika mabango hayo ziwekwe namba za simu ambazo watu watatoa malalamiko yao pale watakapofanyiwa vitendo hivyo kama vile ilivyo kwa jeshi la polisi walivyotoa namba maalumu kwenye vyombo vya usafiri wa umma ili kuwadhibiti madereva wasiofuata sheria za barabarani. Ni imani yangu kuwa angalau wakianza kufahamu kuwa serikali inafuatilia mienendo ya utendaji wao wataanza kujirekebisha na manyanyaso na mateso haya ya wakina mama wajawazito yatapungua sana kama si kwisha kabisa.
 
Back
Top Bottom