Maswali ya Msingi juu ya taifa letu - u must read this!

Mwanamayu

JF-Expert Member
May 7, 2010
11,347
6,471
Misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 (Toleo la 20 Juni 2005)

KWA KUWA SISI Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani.

NA KWA KUWA misingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia, ambayo serikali yake husimamiwa na Bunge lenye wajumbe waliochaguliwa na linalowawakilisha wananchi, na pia yenye Mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga wala upendeleo wowote, na hivyo kuhakikisha kwamba haki zote za binadamu zinadumishwa na kulindwa, na wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu.

KWA HIYO, BASI, KATIBA HII IMETUNGWA NA BUNGE MAALUM LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, kwa niaba ya Wananchi, kwa madhumuni ya kujenga jamii kama hiyo, na pia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Tanzania inaongozwa na serikali yenye kufuata misingi ya kidemokrasia, ujamaa na isiyokuwa na dini.

{kwa misingi hii ya katiba yetu basi masharti au ibara zote zisizofuata misingi hii minne uhuru, haki, udugu na amani yafutwe mara moja kwa kutumia Bunge Maalum kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015 bila mjadala mrefu baada ya kukusanya maoni ya wananchi kutoka kwenye kila jimbo la uchaguzi}

Baadhi ya masharti au ibara zinazofuata misingi ya katiba

Ibara ya 3
(1) Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa

Ibara ya 8
(1) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia na haki ya jamii; na kwa hiyo:
(a) Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa katiba hii
(b) Lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi
(c) Serikali itawajibika kwa wananchi

Ibara ya 13
(1) watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kuptata haki sawa mbele ya sheria
(2) ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake
Ibara ya 107A
(1) Mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa in Mahakama.

Baadhi ya masharti/ vifungu/ibara ambazo hazifuati misingi ya katiba
Ibara ya 41
(7) Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.

[ibara hii inapinga ibara ya 3(1), 8(1), 13 (1) and (2), na 107A(1) na kwa maana hiyo inapinga misingi ya katiba yetu bila kuwa na sababu yoyote aidha ya sababu ya ovyo au msingi.
Maswali ya Msingi: Je, wagombea wa Urais wa vyama vingine kama ibara ya 3 (1) inavyosema wakinyimwa haki waitafute vipi wakati/ waipate vipi? Kwenda msituni? Kuandamana barabarani? Wabunge wao kutoka nje ya Bunge wakati Rais akitoa hotuba? Matokeo ya Udiwani na Ubunge yanachunguzwa mahakamani kwa sababu wagombea ni zaidi ya mmoja, sasa iweje haya ya Urais yenye mgombea zaidi ya mmoja yasichunguzwe kama haki ambayo ni msingi wa katiba kama imetendeka?]

Ibara ya 74
(12) Hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya katiba hii.

[ibara hii inapingana na ibara ya 3(1), 8(1), 13 (1) and (2), 74 (5) na 107A(1) lakini hasa ibara ya 107A(1) bila sababu yoyote aidha ya msingi au ya ovyo.
Maswali ya Msingi: Je, haki isipotendeka itajulikana vipi, na itatafutwa vipi hasa kwa wagombea Urais wakati mahakama ndio chombo cha kutoa haki (ibara ya 107A(1)? Sasa kama mahakama ndio chombo chenye kauli ya mwisho kwenye utoaji haki, haki ya hawa wagombea wa Urais iliyopokonywa itatolewa na nani? Rais? Kama Rais, mbona katiba haisemi? Je, Tume ya Uchaguzi inaendeshwa na ‘malaika wema waliotelemka kutoka Mbinguni’? Kama ndio, misingi ya katiba inasema nchi yetu aina dini! Rais atajuaje kama Tume ya Uchaguzi haitendi haki bila mahakama ili aweze kutimiza masharti ya ibara ya 74 (5)? ]

Je, viongozi wafuatao wamevunja katiba?

I. Makamu wa Rais, Dr. Ghalib Bilal
Wakati akiongea kwenye maazimisho/ sherehe/ sala ya Idd El Hajj ya kitaifa kwenye Msikiti wa Simbambali uliopo wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam tarehe 17/11/2010, alitoa ahadi kwa umma wa waislamu ya kushughulikia kwa kuanzishwa kwa mahama ya kadhi Tanzania Bara (Mwananchi/ Majira/Mtanzania, 18/11/2010)

Katiba inasema:
Ibara ya 3
(1) Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa

Ibara ya 6
...neno ‘serikali’ maana yake ni ... na pia mtu anayetekeleza madaraka au mamlaka yoyote kwa niaba ya serikali yoyote

Ibara ya 19
(2) kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi, na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi
(4) kila palipotajwa neon ‘dini’ katika ibara hii ifahamike kwamba maana yake in pamoja na madhehebu ya dini, na maneno mengineyo yanayofanana au kuambatana na neon hilo nayo yatatafsiriwa kwa maana hiyo

Ibara ya 20
(2) ...haitakuwa halali kwa chama chochote cha siasa kuandikishwa ambacho kutokana na katiba au sera yake:
(a) Kukusudia kukuza au kupigania maslahi ya:
(i) Imani au kundi lolote la dini

Ibara ya 26
(1) Kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii katiba hii na sheria za Jamhuri ya Muungano


[Maswali ya Msingi: Katiba kama isemavyo na ahadi ya Makamu wa Rais kwa Umma wa Waislamu kwa niaba ya serikali ya CCM na Chama cha Mapinduzi sio kuvunja katiba huko? Huyu Kiongozi si amevunja katiba ndani ya kama wiki mbili baada ya kushika madaraka na kuapa kuilinda, kuitetea na kuhifadhi katiba hii, je baada ya miaka miwili itakuaje? Je, serikali ya CCM na Chama Cha Mapinduzi au mamlaka ya nchi in dini?]



II. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Semamba Makinda

Baada ya jina la Waziri Mkuu kusomwa na Spika, Mwanasheria Mkuu wa serikali alipewa nafasi ya kutoa hoja au kuongea; Mheshimiwa Tundu Lissu alimuuliza Spika kuhusu kanuni ya Bunge 53 (6) (c) ambayo inamtaka kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani kuongea mara hoja ya serikali inapotolewa; Spika alijibu kuwa hakukuwa na hoja ya serikali kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali kuongea kwa sababu Baraza la Mawaziri lilikuwa halijaundwa.

Katiba inasema:

Ibara ya 6
Katika sehemu hii ya sura hii; isipokuwa kama maelezo yahitaji vinginevyo, neno ‘serikali’ maana yake ni pamoja na serikali ya Jamhuri ya Muungano, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, serikali za mitaa na pia mtu anayetekeleza madaraka au mamlaka yoyote kwa niaba ya serikali yoyote

[Maswali ya Msingi: Je, Mwanasheria Mkuu hakuwa mtu ambaye anatekeleza madaraka au mamlaka ya serikali? Hivi huko kutoa maana nyingine ya serikali, yaani ni Baraza la Mawaziri si kuvunja katiba na kanuni ya Bunge 50(6)(c)?]

III. Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Mrisho Khalfani Kikwete
Rais kwa mujibu wa katiba hii anatakiwa kufanya mambo kwa maslahi ya nchi na ustawi wa wananchi. Mambo hayo yasipofanyika ni sawa na kwenda kinyume na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katiba inasema:

Ibara ya 74
(4) (a) Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi atakoma kuwa mjumbe ukimalizika muda wa miaka mitano tangu alipoteuliwa

[Maswali ya Msingi: Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Ben Mkapa hakuwahi kubadilisha wajumbe wa Tume ya Uchaguzi; pia Rais JK hajafanya hivyo mpaka sasa, je wamekuwa na ajenda gani ya siri hapa? Kama kusema Tume haichunguzwi mahakamani, basi ndio hata wajumbe hawabadiliki? Wajumbe wamekuwa wale wale tu – Jaji Lewis Makame, Rajabu Kiravu, Prof. Chaligha – zaidi ya miaka mitano! Je, kwa maana hiyo wajumbe wa Tume wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, 2005 na 2010 hawakutakiwa kwenye Tume kwa mujibu wa katiba na hivyo Tume kuwa batili?]

Ibara ya 74
(5) Rais aweza tu kumwondoa katika madaraka mjumbe wa Tume ya Uchaguzi kwa sababu ya kushindwa kutekeleza kazi zake, ama kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote, au kwa sababu ya tabia mbaya au kupoteza sifa za kuwa mjumbe

[Maswali ya Msingi: Kwa nini Rais hajawaondoa baadhi au wajumbe wote ambao wamesababisha utendaji kazi mbovu; kuonyesha tabia mbaya ya kuchakachua kura za Urais na baadhi ya wabunge wa upinzani hasa CHADEMA wakati kukiwa na ushahidi tosha kuwa matokeo ya kwenye majimbo ni tofauti na yale yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi? Je, waangalizi wa uchaguzi mkuu mfano wale wa Umoja wa Ulaya kuona namna Tume ya Uchaguzi ilivyochelewesha matokeo bila sababu za msingi kuwa walakini wa uchaguzi haukuwa wa haki ni mkubwa? Kuairisha uchaguzi kwenye majimbo saba, si kasoro hizo za utendaji wa Tume? Je, haya si yamekuwa yakitokea kila uchaguzi mkuu unapofanyika?]

IV. Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
Tumeona jinsi Rais na Makamu wa Rais pia Spika wakivunja baadhi ya masharti ya katiba yetu licha ya kula kiapo cha kuilinda, kuitetea, kuifuata, kuitii na kuihifadhi lakini Bunge kwa niaba ya wananchi lenye mamlaka kikatiba kupitisha azimio la kuwaondoa viongozi hawa madarakani kushindwa kufanya hivyo.

Katiba inasema:
Ibara ya 46A
(1) ... Bunge linaweza kupitisha azimio la kumwondoa Rais madarakani endapo itatolewa hoja ya kumshtaki Rais na ikipitishwa kwa mujibu wa masharti ya ibara hii
(2) ..., hoja yoyote ya kumshtaki Rais haitatolewa isipokuwa tu kama inadaiwa kwamba Rais:
(a) Ametenda vitendo ambavyo kwa ujumla vinavunja katiba
(b) Amekiuka ibara ya 20(2)

Ibara ya 50
(3) Bunge litakuwa na madaraka ya kumuondoa Makamu wa Rais madarakani kama yale lililyonayo kuhusiana na Rais, isipokuwa kwamba hoja yoyote ya kumshtaki Makamu wa Rais itatolewa tu kama inadaiwa kwamba:
(b) Ametenda vitendo ambavyo kwa ujumla vinavunja Katiba au sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma
(c) Ametenda vitendo ambavyo vinakiuka maadili yanayohusu uandikishwaji wa vyama vya siasa yaliyotajwa katika ibara ya 20(2) ya katiba


[Maswali ya Msingi: Je, wabunge hawaoni kama hawa viongozi wanavunja katiba mapema kiasi hiki baada ya kushika madaraka yao? Kama viongozi hawa wanavunja katiba na wao wanabaki kimya basi `ni dhahiri nao wanavunja katiba walioapa kuilinda na kuifuata au hawaijui katiba na kuapa tu ilimradi wameapa? Kama wawakilishi wetu wanavunja aktiba, je si sahihi kwa wananchi kuwaadhibu watakapokuja kuomba kura zetu kwenye uchaguzi mkuu? Je, tusipofanya hivyo na sisi wananchi tutakuwa tunavunja katiba hasa ukiangalia Ibara ya 26 (1) Kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii katiba hii na sheria za Jamhuri ya Muungano?]


V. Wabunge wa CHADEMA
Mara baada ya Rais kuanza kuhutubia Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano tarehe 18/11/2010 wabunge wa Chadema ambao wanaunda kambi rasmi ya upinzani Bungeni walitoka nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma

Katiba inasema:
Ibara ya 26
(1) kila mtu anawajibu wa kufuata na kutii katiba hii na sheria za Jamhuri ya Muungano

Ibara ya 28
(4) uhaini kama unavyofafanuliwa na sheria utakuwa ni kosa la juu kabisa dhidi ya Jamhuri ya Muungano

Ibara ya 18
(a) kila mtu anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake

Ibara ya 71
(1) Mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge litokeapo kati ya mambo yafuatayo:
(c)ikiwa Mbunge atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika

Ibara ya 100
(1) kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano; au katika Mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge
(2) Bila ya kuathiri katiba hii au masharti ya sheria nyingine yoyote inayohusika, Mbunge yeyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya Bunge au alilolileta Bungeni kwa njia ya maombi, muswada, hoja au vinginevyo

[Maswali ya Msingi: Je, wabunge hawa wamevunja katiba kwa kutoka nje ya Bunge? Hapana kwa sababu ibara ya 100 (2) inawalinda vizuri tu na hakuna ibara yoyote iliyovunjwa kwani tukio hilo limetokea ndani ya ukumbi wa Bunge na haiwezekani kuwashtaki kokote kule zaidi ya kuamuliwa ndani ya Bunge. Je, wamevunja kanuni yeyote ya Bunge? HAPANA na hakuna kanuni yoyote inayoongelea suala hilo. Nini Spika atafanya? Spika atatumia kanuni ya 5(1) inayosema: katika kutekeleza majukumu yakeyaliyotajwa katika ibara ya 84 ya katiba, Spika ataongozwa na kanuni hizi na pale ambapo kanuni hazikutoa mwongozo, basi Spika atafanya kazi kwa kuzingatia katiba, sheria nyingine za nchi, kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya awali ya Maspika wa Bunge pamoja na mila na desturi za Mabunge mengine yenye utaratibu wa Kibunge unaofanana na utaratibu wa Bunge la Tanzania. Kanuni ya 5(4) inasema mbunge yeyote ambaye hataridhika na uamuzi wa Spika anawezakuwasilisha malalamiko hayo kwa Spika. Basi wabunge wa Chadema watapangua uamuzi wowote kandamizi wa Spika kwa kutumia kanuni hii. Kama kanuni mpya itatungwa basi lazima kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani ni mjumbe kama kanuni ya 3(1) ya Bunge inavyosema.


Je ni sahihi wabunge wengine hasa wa CCM kupeleka hoja Bungeni ya kuwaondoa wabunge wa Chadema? Kanuni ya 50(1) Mbunge anaweza kutoa hoja binafsi Bungeni kuhusu jambo lolote linalomhusu na lililoifikia jamii; je, wabunge wa Chadema watajinasua vipi na hoja hii? Kanuni ya 54(5) inasema taarifa yoyote ya hoja ambayo inakiuka masharti ya katiba au ya kanuni hizi haitakubaliwa; kanuni hii ndio itakayowanusuru wabunge wa Chadema kutolewa Bungeni kwani hoja ya Chiligati ni kinyume na ibara ya 71(1)(c); na baadhi ya kanuni za Bunge kama 14, 15, 16, 53(5)(c) kwani itakuwa vigumu kwa shughuli au vikao vya mikutano ya Bunge kufanyika bila kambi rasmi ya upinzani. Pia Mbunge upelekwe Bungeni na wananchi na sio Chama cha Siasa hasa chama tawala – CCM.

Wabunge wote ula kiapo cha utii – kuilinda na kuifuata katiba, basi kama wabunge wa Chadema wamevunja katiba kwa kutoka nje ya ukumbi wa Bunge wakati Rais alipoanza kuhutubia – kitu ambacho tumeona ni HAPANA – je, wale wabunge walioshiriki kurekebisha katiba na kufuta ibara ya 10, 80 na 82 hawakula kiapo wakati ibara hizo zikiwemo kwenye katiba?


Je, jambo hilo ni kuvunja katiba? Je, Chadema kama timu ya mpira wa miguu wangewezaje kucheza mechi za ligi kuu bila wachezaji wao kusajiliwa? Mechi inapigwa baada ya usajili na ndicho walichokifanya Chadema pale Bungeni na kuandika historia nzuri ya kufuata misingi ya kidemokrasia kama misingi ya katiba yetu inavyosema, kwa kfupi wameonyesha kwa jinsi gani wanafuata misingi hiyo ya katiba yetu].

VI. Kamati Kuu ya CCM
Wakati wa mchakato wa kumpata mgombea Uspika kwa tiketi ya CCM, iliamua kutoa upendeleo kwa wanawake kwenye kiti hicho na kuwaengua wanaume wote akiwemo Mhe. Sitta na Chenge. Wanawake waliobaki ni Anna Semamba Makinda, Anna Abdallah na Kate Kamba na hatimaye Anna Makinda kupata fursa hivyo.

Katiba inasema:

Ibara ya 20
(2) ...haitakuwa halali kwa chama chochote cha siasa kuandikishwa ambacho kutokana na katiba au sera yake:
(a) Kukusudia kukuza au kupigania maslahi ya:
(i) Imani au kundi lolote la dini
(ii) Kundi lolote la kikabila, mahali watokeapo, rangi au jinsia

[Swali la Msingi: hivi hawa CCM hawajavunja kweli kifungu cha 20(2)(ii) kwenye kipengele cha jinsia? Je, Spika huyu sio batili kwa mujibu wa ibara hii ya katiba?]
 

Attachments

  • Misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.docx
    28.7 KB · Views: 151
good analysis; sote tunapaswa kuchunguza na kuielewa katiba sawasawa kama huyu mzalendo Mwanamayu. I am challenged to read kwa umakini ili tukitoa hoja tuwe well versed
 
Back
Top Bottom