ACT Wazalendo
JF-Expert Member
- May 5, 2014
- 620
- 1,543
Maswali na Majibu ya Kizalendo Kuelekea Kongamano la Rasilimali Madini [Swali la Kwanza]
Swali: Mnamuunga Mkono Rais Magufuli kwenye hili suala la Madini?
Jibu: Msimamo wetu upo wazi katika kupigania taifa kulinda raslimali za nchi ikiwemo madini. Jambo lolote linahusu maslahi ya Tanzania tutashirikiana na yoyote katika kulifanya liwe na tija zaidi. Kuhusu Rasilimali Madini, tumepinga siku zote serikali kuwa mkodishaji na kubaki kuwa mkusanya kodi pekee, jambo ambalo linatufanya tusinufaike na Rasilimali zetu.
Tunaamini serikali lazima iwe ni sehemu ya mmiliki na muendeshaji wa uvunaji wa raslimali za taifa letu, jambo hilo ndio msimamo wetu kwenye 'AZIMIO LA TABORA' - ambalo ndilo tamko la kiitikadi na kisera la chama chetu. Tume ya Rais (Kamati ya Mruma) imethibitisha tu kile ambacho tumekisema siku zote kwamba: tulitengeneza mikataba ya kuwezesha kuibiwa kisheria!
Sasa swala hapa sio kumpinga au kumuunga mkono Rais, ambaye amekuwa sehemu ya sera, maamuzi na utendaji wa Serikali ya chama cha CCM zilizofanikisha wizi unaoendelea nchini kwa zaidi ya miaka 17 sasa.
Suala la msingi hapa ni kutumia matokeo haya kwa akili ili kupitia upya mahusiano yetu ya kimkataba na wawekezaji. Ni muhimu sana tutumie akili nyingi katika hatua ya sasa ili isije tukaharibu juhudi za miaka 20 za kuvutia wawekezaji katika nchi yetu. Lakini jambo lililo dhahiri ni kuwa, ni LAZIMA tuwe sehemu ya UMILIKI wa madini yetu.
Rasilimali Madini ni mali ya Taifa, ni muhimu Taifa lizungumze juu ya suala hili nyeti. ACT Wazalendo tumejipa jukumu la mstari wa mbele katika kuongoza mazungumzo ya Taifa juu ya namna njema ya kufaidika na rasilimali madini za Taifa. Huo ndio msingi wa Kongamano letu la Jumamosi, Juni 3, 2017 jijini Dar es salaam.
Karibuni Sana
Ado Shaibu
Katibu wa Itikadi, Mawasiliano ya Umma na Uenezi
ACT Wazalendo