kyalankota
JF-Expert Member
- Jul 27, 2014
- 2,560
- 1,399
Masheikh mbalimbali nchini wamejikusanya na kupiga kambi mjini Dodoma maeneo ya bunge ili kuhakikisha mahakama ya kadhi inapitishwa na bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
==========================
==========================
Chanzo: Jambo leo
MASHEIKH na Wanazuoni wa Kiislamu nchini wameamua kupiga kambi mjini Dodoma ili kuhakikisha wakati Bunge linajadili Mahakama ya Kadhi wawe eneo hilo kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.
Uamuzi huo umekuja baada ya kauli ya Maaskofu kuingilia madaraka ya Bunge kwa kulitaka lisijadili Mahakama ya Kadhi ambapo Tasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania wamesema wamesikitishwa na kauli hiyo na sasa wameamua kuweka kambi Dodoma ili kuona Bunge litaamua nini wakati wanajadili Mahakama ya Kadhi.
Taasisi mbalimbali za Kiislamu nchini zimeungana katika kuhakikisha Bunge linatoa fursa kuhusu Mahakama ya Kadhi ambayo imekuwa kilio cha Waislamu walio wengi kwa muda mrefu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, kabla ya kuanza safari ya kwenda Dodoma, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazouni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Khamisi Mataka alisema kauli ya maaskofu kupitia Jukwaa la Wakristo Tanzania, ndilo limesababisha waweke kambi Dodoma ili kuwa karibu na Bunge.
Sheikh Mataka alisema hawakuwa na nia ya kwenda kuweka kambi Dodoma wakati Bunge litakapokuwa linajadili Mahakama ya Kadhi wiki hii, lakini kauli ya maaskofu imewafanya wafanye hivyo ili kuhakikisha haki inatendeka.
Alisema ikumbukwe ahadi ya marekebisho ya sheria kuitambua Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara , ni ahadi ya Serikali , hivyo alisema taasisi yao inawaomba maaskofu waachie uhuru wabunge waumini wa dini ya Kikristo kuujadili muswada huo bila shinikizo la kiimani na kuukataa.
"Tumeamua kwenda Dodoma kwa ajili ya kuwa karibuni na jikoni ambako wabunge wetu wote walio Waislamu na Wakristo watakupokuwa wanajadili Mahakama ya Kadhi , tuwe karibu.
"Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge wiki hii moja ya muswada utakaojalidiliwa ni pamoja na Mahakama ya Kadhi.Hivyo hatuwezi kuwa mbali katika jambo ambalo linatuhusu,"alisisitiza Sheikh Mataka.
Wakati huo huo, Anicetus Mwesa anaripoti kuwa Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR Mageuzi), amesema Serikali inafanya ulaghai hata kwenye taasisi za dini.
Amesema kutokana na ulaghai huo ndiyo maana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda mwaka jana alisema Serikali itapeleka bungeni vifungu vitakavyoifanya mahakama ya kadhi itambulike katika Katiba.
Mkosamali alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza kwenye kipindi cha tuongee asubuhi kinachorushwa na Staa Tv kilichokuwa kinazungumzia Katiba inayopendekezwa.
"Wiki hii kutatokea jambo kubwa sana bungeni, Waziri Mkuu aliwahaidi Waislamu kuwawezesha kupata mahakama, sasa wameleta bungeni vifungu viwili vitatu sasa moto wake watauona.
"Yaani serikali iko tayari kuvuruga amani ya nchi kwa kulazimisha mambo kwenye suala la Katiba wakati ukweli wanaujua kuwa mchakato huu unaoendelea si halali kisheria na kikanuni," alisema Mkosamali.
Kuhusu suala la ucheleweshaji wa kuigawa kwa wananchi Katiba pendekezwa, Mkosamali alisema Serikali inafanya makusudi ili wananchi wasijue kilichomo kwenye katiba hiyo na kwamba Watanzania wasitegemee kama itasambazwa kwani mpango uliopo ni kusambazwa chache.
Aidha, alisema mwaka huu, Ukawa watashinda uchaguzi mkuu na kwamba mwakani wataanzisha mchakato wa katiba ambao utakuwa umehusisha wananchi na wadau wote.
Naye, Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba alisema Ukawa wasitegemee ushindi wowote kwani dalili za kushindwa uchaguzi mkuu zimeonekana kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika Desemba 14, mwaka jana.
"Wananchi waliopiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa ni wale wale watakaopiga kura uchaguzi mkuu hivyo Ukawa waendelee kusubiri maumivu," alisema Nkumba.
Pia, aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kueleza umma kama muda wa kura ya maoni unatosha au hautoshi na si kukaa kimya kama ilivyo sasa.
"Tume inapaswa kueleza kama muda unatosha ama hautoshi ili Serikali iseme uamuzi mwingine. Pia, serikali inatakiwa kupeleka kwa wananchi Katiba pendekezwa ili waisome waelewe maudhui yake," alisema.
Kwa mujibu wa sheria namba tatu ya mwaka 2014, ambayo inahusu kura ya maoni inaeleza kuwa jambo la kwanza kufanyika ni uboreshaji wa daftari la wapiga kura ambao utafuatiwa na elimu kwa umma kwa miezi miwili kisha kampeni kwa mwezi mmoja.
Kura ya maoni kuhusu Katiba pendekezwa inatarajiwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu.