Marupurupu ya wabunge Afrika Mashariki ni haya; Kenya ni kufuru tupu, inazizidi Sweden, Ufaransa, au | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Marupurupu ya wabunge Afrika Mashariki ni haya; Kenya ni kufuru tupu, inazizidi Sweden, Ufaransa, au

Discussion in 'Kenyan News and Politics' started by nngu007, Jun 24, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Jun 24, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  [h=1][/h]
  *Kenya ni kufuru tupu, inazizidi Sweden, Ufaransa, Australia
  *Wabunge Uganda wafuatia, Tanzania ndiyo wanaoshika mkia
  *Sitta mwasisi wa posho nono, mzimu wa maamuzi yake waitafuna CCM
  *Mbowe aibua mjadala, wananchi wataka ruzuku za vyama pia zifutwe

  Na Mwandishi Wetu

  MJADALA mzito ulioibuka kuhusu posho za vikao kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sasa unaingia katika wiki yake ya tatu, huku viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakisisitiza ziondolewe na kwamba iwapo zitaendelea kutolewa, msimamo wao wa kuzisusia upo pale pale.

  Hivi sasa wabunge hao wanakuna vichwa kuona namna watakavyotekeleza mpango wao wa kusuia fedha hizo, baada ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, kukataa kuziondoa wakati alipokuwa akihitimisha hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2011/12 Jumanne jioni wiki hii.

  Kwa Tanzania, hii ni mara ya kwanza kwa kundi kubwa la wabunge kupinga hadharani posho zinazowagusa moja kwa moja, ukichilia mbali mwaka jana wakati aliyekuwa Mbunge wa Karatu, Wilbroad Slaa, alipojitokeza kupinga marupurupu mengi aliyosema yanatolewa kwa wabunge, akisema wanajichotea kiasi cha Sh milioni 7 kwa mwezi.


  Utamaduni uliokuwa umejengeka kwa miaka yote, hasa katika Bunge la Tisa lililokuwa chini ya Spika Samuel Sitta ni kwamba mara zote maslahi ya wabunge yalipokuwa yakijadiliwa, hakuna mbunge hata mmoja (hata wale wa kambi ya upinzani) aliyekuwa tayari kupinga ili kutetea maslahi ya mpigakura maskini wa Tanzania.

  Sitta ndiye aliyesimamia uboreshaji wa marupurupu ya wabunge kwa maelezo kuwa alitaka angalau yalingane na wenzao katika nchi jirani za Kenya na Uganda na kati ya masuala atakayokumbukwa kuyasimamia ni pamoja na kuanzisha kwa Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDF), pamoja na ujenzi wa ofisi za wabunge katika majimbo yote ya Tanzania, ambako awali, ofisi za wakuu wa wilaya zilikuwa zimetenga ofisi za wabunge.

  Utafiti uliofanywa na gazeti la The Guardian la Uingereza Oktoba mwaka jana, unaonyesha kuwa wabunge wa Kenya ndio wanaoongoza kwa kujichotea marupurupu manono zaidi kuliko wabunge wengine wote katika nchi za Afrika Mashariki za Kenya, Uganda na Tanzania.

  Kwa mujibu wa utafiti huo, wabunge wa Kenya na Uganda pia wanapata marupurupu makubwa kiasi cha kuwazidi wabunge katika mataifa mbalimbali yaliyoendelea, yakiwamo Ufaransa, Sweden, Australia na hata Italia, ingawa wabunge wa Uingereza wanaelezwa kuwa ndio vinara wanaoongoza kwa kupata marupurupu makubwa zaidi kuliko wabunge wengine katika Jumuiya ya Madola na nchi nyingine duniani.

  Hata hivyo, wachunguzi wa mambo wanasema kuwa kelele zinazopigwa na wabunge wa kambi ya upinzani Tanzania zinatokana na ukweli kwamba takwimu za kiuchumi zinazotolewa kila mwaka bado hazijajitafsiri katika maisha ya Mtanzania wa kawaida ambaye anaendelea kufunikwa na blanketi la umaskini na kwamba pamoja na kuwa wabunge wa Tanzania wanapata marupurupu kidogo ikilinganishwa na wenzao wa Kenya na Uganda, ukwasi wao unaonekana kuwa mkubwa mno kulinganisha na kipato cha mwananchi wa kawaida.

  Kwa mujibu wa utafiti wa gazeti hilo, Mbunge wa Kenya anajikusanyia kitita cha Sh 15,318,000 kwa mwezi, fedha ambazo zinajumuisha mshahara pamoja na posho za aina mbalimbali anazopewa, wakati yule wa Uganda anajikusanyia Sh 10,989,000 kwa mwezi. Kwa mujibu wa utafiti huo, ambao haukuihusisha Rwanda, Mbunge wa Tanzania anaondoka na wastani wa Sh 7,740,000 kwa mwezi.

  Hii ina maana kwamba Mbunge wa Kenya anapata marupurupu mara mbili zaidi ya Mbunge wa Tanzania, lakini wanaojenga hoja wanasema ukiangalia utamaduni uliojengeka Kenya tangu baada ya uhuru, ni jambo la kawaida kwa mwanasiasa kujilimbikizia mali kwa kuwa wakati siasa nchini Kenya zinaangaliwa kama sehemu ya wanasiasa kujinufaisha binafsi, Tanzania imejijengea utamaduni wa mwanasiasa kuonekana mtumishi wa wanyonge.

  Kwa mantiki hiyo, baadhi ya watu wanasema iwapo kutakuwa na tofauti kubwa sana ya kipato kati ya Mbunge na mpigakura wake, dhana ya utumishi inatoweka na watu wanaanza kukimbilia siasa kama sehemu ya kwenda kujitafutia ukwasi.

  Mapema mwaka jana, kuliibuka mjadala mzito nchini Kenya pale wabunge walipokula njama kutaka kujiongezea marupurupu hadi Sh 21,600,000, lakini Waziri Mkuu, Raila Odinga, Waziri wa Fedha, Uhuru Kenyatta na waziri mwingine, Joseph Nyagga, walisimama kidete kupinga ongezeko hilo, wakisema linaweza kukwamisha mpango wa maendeleo wan chi hiyo unaojulikana kama ‘Vision 2030.’

  Hata nchini Uganda, mara zote wabunge wamekuwa wakiungana kuishinikiza Serikali kuongeza marupurupu yao mara kwa mara na ndio maana hadi sasa wanaingiza mfukoni kwao kiasi hicho cha fedha wakati uchumi wao bado ni mdogo kuweza kuhimili mzigo mzito kama huo.

  Wakati Mbunge wa Kenya akijikusanyia zaidi ya Sh milioni 15, kwa mwezi, utafiti wa gazeti la The Guardian unaonyesha kuwa Mbunge wa Ufaransa anajichotea kiasi cha Sh 9,468,000 kwa mwezi zikiwa ni mshahara pamoja na posho mbalimbali, huku Mbunge wa Italia akijikusanyia kiasi cha Sh milioni 9.9 kwa mwezi.

  Mbunge wa Sweden, ambalo ni moja ya mataifa wafadhili wakubwa wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki, anaweka kibindoni Sh 10,440,000 kwa mwezi zikiwa ni mshahara pamoja na marupurupu mengine yote, fedha ambazo ni kidogo zikilinganishwa na zile anazolipwa Mbunge wa Uganda na Kenya.

  Gazeti hilo limedokeza kuwa Uingereza ndiyo nchi yenye wabunge matajiri kuliko nchi nyingine zote duniani kutokana na donge nono wanalojikusanyia kila mwezi kama mishahara pamoja na posho mbalimbali zilizoainishwa kama stahili za Mbunge.

  Kwa wastani, Mbunge wa Uingereza anajikunjia kiasi cha Sh 37,800,000 kwa mwezi, wakati yule wa Marekani akiambulia kiasi cha Sh 21,600,000 kwa mwezi, kiasi ambacho ndicho kilichokuwa kikidaiwa na wabunge wa Kenya mwaka jana na kukwamishwa na Waziri Mkuu Odinga na wenzake Kenyatta na Nyagga.

  Kwa upande mwingine, wabunge wa Australia, moja ya nchi tajiri na kubwa duniani wanalipwa Sh 13,860,000 kila mwezi kama mshahara na posho za aina mbalimbali, fedha ambazo pia ni kidogo kuliko zile anazolipwa mbunge kutoka Kenya.

  Nchini Tanzania, Mbunge analipwa Sh milioni 2.5 kama mshahara, huku akikabidhiwa pia kitita cha Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo kinachotolewa kila mwezi na wakati huo huo akilipwa posho ya kujikimu ya Sh 80,000 kwa siku anapokuwa kazini, hasa kwenye vikao vya Bunge na kamati za Bunge pamoja na Sh 70,000 ya kikao (sitting allowance).

  Ni Sh 70,000 ya vikao ndiyo iliyozua mjadala mkali bungeni ambazo Chadema wanasema zinatakiwa kuondolewa kwa kuwa haina mantiki yoyote na kwamba ni moja ya vyanzo vya matumizi mabaya ya fedha za Serikali kwa kuwa mtu hawezi kulipwa posho kwa kufanya kazi aliyoajiriwa kuifanya.

  Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, ambaye ndiye mwasisi wa hoja hiyo anasema haiwezekani Mbunge alipwe fedha hizo kwa kufanya kazi yao ya mijadala bungeni na katika kamati za Bunge, wakati mwalimu halipwi posho kwa kushika chaki darasani.

  Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, anasema posho za aina hiyo ziko nyingi miongoni mwa watumishi wa umma na kwamba ingefaa wabunge waanze kuzikataa ili wapate mamlaka ya kukemea matumizi ya posho za aina hiyo katika taasisi nyingine za Serikali.

  Si hivyo tu, bali katika kuonyesha mfano wa uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma, Mbowe ameamua kurejesha gari la Serikali alilokabidhiwa kama Kiongozi wa Upinzani Bungeni kwa maelezo kuwa tayari amekwisha kukopeshwa Sh milioni 90 kwa ajili ya kununulia gari lake kama ilivyo kwa wabunge wengine wote.

  Lakini wakati hayo yote yakifanyika, baadhi ya watu wameibua hoja kuwa hatua ya wabunge wa Chadema kususia posho za wabunge haitoshi, bali wanataka ruzuku zinazotolewa kwa vyama vya siasa zifutwe ili fedha hizo zitumike kwa ajili ya mradi mblimbali ya maendeleo ya wananchi.

  Watu hao wanasema fedha zitakazopatikana kutokana na kufutwa kwa ruzuku kwa vyama vya siasa ni nyingi zaidi kuliko zile zitakazopatikana kutokana na kuondolewa kwa posho za wabunge wa chama hicho na vyama bingine vya upinzani.

  Hoja hiyo inajengwa katika mazingira kwamba vyama vingi vya siasa duniani vinaendeshwa na fedha za miradi ya vyama, michango na ada za wanachama pamoja na wafadhili wa ndani na nje ya nchi wanaoamini katika misingi ya sera zinazosimamiwa na chama husika.

  Hivi sasa Chadema inapata rukuzu ya inayofikia Sh bilioni 3.6 kwa mwaka, huku CCM, chama ambacho ndicho chenye wabunge na madiwani wengi, kikijikusanyia Sh bilioni 9.6 kwa mwaka. Vyama vingine vinavyopata ruzuku ni pamoja na Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha NCCR-Mageuzi, Chama cha United Democratic (UDP) na Chama cha Tanzania Labour (TLP). Vyama vyote hivyo vina wawakilishi wake bungeni.
   
 2. Narubongo

  Narubongo JF-Expert Member

  #2
  Jun 24, 2011
  Joined: Nov 3, 2010
  Messages: 1,922
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 135
  vipi kuhusu mishahara ya wafanyakazi wengine ktk sekta za uma huko kenya na uganda ili tuilinganishe na hapa tz mf. mshahara wa mwalimu/dr/etc kwa kila nchi
   
 3. K

  Kamundu JF-Expert Member

  #3
  Jun 24, 2011
  Joined: Nov 22, 2006
  Messages: 2,109
  Likes Received: 455
  Trophy Points: 180
  Kenye na Tanzania ni pwagu na pwaguzi
   
 4. Kichuguu

  Kichuguu Platinum Member

  #4
  Jun 24, 2011
  Joined: Oct 11, 2006
  Messages: 7,203
  Likes Received: 865
  Trophy Points: 280
  Wakati mbunge wa marekani akipokea Shs 21,600,000 kwa mwezi, daktari wa kawaida (siyo Bingwa) analipwa kiasi cha Tsh20,000,000 hadi TSh 32,000,000 kwa mwezi. Je Tanzania na Kenya mambo yakoje kwa madakari?
   
Loading...