Martin Bryant na mauaji ya kutisha….!

Mtambuzi

Platinum Member
Oct 29, 2008
8,806
15,379
tumblr_m2sx4b2hwv1rtz32io1_500.jpg



tumblr_m80p5ff7gC1qc7z29o1_500.jpg


Ilikuwa ni siku ya Jumapili ya April 28, 1996, Bryant aliamshwa na mlio wa alam ya saa yake ambayo aliitega ili imuamshe majira ya saa 12:00 asubuhi. Mpenzi wake na ndugu zake walishangazwa na huo utaratibu wake mpya wa kuamshwa na alam ya alfajiri wakati haikuwa kawaida yake kwa sababu alikuwa hafanyi kazi na hakuwa na majukumu yoyote.

Majira ya saa 8:00 za asubuhi mpenzi wake aliondoka hapo katika nyumba ya urithi ya Bryant aliyoirithi kutoka kwa mwanamke mmoja aitwae Helen Harvey kwenda kuwatembelea wazazi wake. Bryant naye aliondoka hapo nyumbani majira ya saa 9:47 na gari lake aina ya Volvo ya njano akiwa amebeba boti ndogo ya kuchezea baharini maarufu kama Surfboart. Alikuwa na begi kubwa kama la wanamichezo. Majira ya saa 4:00 asubuhi alisimama katika duka moja na kununua sigara na kisha kulipa kiasi kikubwa cha pesa na kuondoka bila kusubiri chenji. Kabla ya hapo aliingia katika duka hilo na kuuliza kama wanauza kiberiti cha kuwashia sigara na baada ya kuambiwa kwamba wanauza alirudi katika gari lake na kurudi na kiasi hicho cha fedha.

Aliendesha gari lake hadi katika duka moja maarufu kama Sorell Supermarket ambapo alinunua chupa ya tomato sauce ambapo alilipa na kuondoka kuelekea kijiji cha jirani kiitwacho Forest ambapo aliwasili kijijini hapo majira ya saa 5:00 asubuhi. Alingia katika kituo cha mafuta cha Shell na kununua kahawa. Wakati anakunywa kahawa katika kituo hicho alimweleza mmoja wa wahudumu wa mghahawa huo kwamba anaenda kufanya surfing katika ufukwe wa Roaring lakini mhudumu huyo aliashangaa kwa sababu hali ya hewa ilikuwa shwari na haingefaa kwa kufanya surfing.

Aliondoka hapo na kuendesha hadi katika eneo la Eaglehawk Neck ambapo alisimama kwenye kituo cha mafuta na kujaza mafuta ya kiasi cha dola 15. Aliendelea na safari yake kuelekea katika eneo la Port Arthur majira ya saa 5:45 ambapo alisimama katika nyumba moja ya wageni iitwayo Seascape ambayo awali ilikuwa inunuliwe na baba yake lakini ikanunuliwa na mmiliki mwingine mtu na mkewe waitwao David na Noelene Martin. Inaelezwa kwamba Bryant hakufurahishwa na kitendo cha David kumzunguka baba yake na kwenda kuinunua nyumba hiyo ya wageni wakati alikuwa anafahamu dhahiri kwamba baba yake alikuwa kwenye hatua za mwisho za kutaka kuimiliki nyumba hiyo. Bryant aliingia ndani ya nyumba hiyo ya wageni na kufyatua risasi kadhaa ambapo alimfuata mmiliki wa nyumba hiyo na kumchoma kwa kisu mara kadhaa. Wakati akiwa humo ndani walikuja wateja flani mtu na mkewe wakitaka kuangalia vyumba, lakini Bryant aliwazuia kwa kuwambia kwamba wazazi wake hawapo na aliyepo ndani ni mpenzi wake. Inaelezwa kwamba majibu yake yalikuwa ni kifedhuli kiasi kiasi cha kuwakera wale wateja na hivyo kuondoka katika nyumba hiyo kwa hasira.

Inaelezwa kwamba Bryant aliondoka katika nyumba hiyo ya wageni ya Seascape majira ya saa 6:35 kuelekea katika eneo hilo la Port Arthur akiwa amechukua funguo za nyumba hiyo baada ya kuifunga milango yote. Bryant alionekana akiwa amesimama baada ya kuona gari moja likiwa limesimama kutokana na kuchemsha kutokana na joto. Alionekana akiongea na watu hao wawili waliokuwa kwenye hilo gari ambapo inadaiwa aliwaalika wakutane katika mghahawa wa Port Arthur kwa ajili ya kupata Kahawa pamoja. Kutoka hapo aliendesha gari lake kupitia eneo la kihisoria la Port Arthur. Alipofika aliingia katika mghahawa maarufu uitwao Broad Arrow na kuagiza chakula. Waliomuona walishangazwa na jinsi alivyochukua chakula kingi, lakini aliwambia kwamba anajisikia njaa sana.

Baada ya kumaliza chakula chake aliinama chini na kufungua zipu ya begi lake na kisha na kutoa bunduki aina ya Armalite AR-15 Semi automatic na kuanza kufyatua risasi hovyo huku akicheka kama vile amepagawa. Watu wote waliokuwa kwenye huo mghahawa ambao wengi ni watalii walianza kukimbia huku na huko wakitafuta namna ya kujificha ili kuepuka kuuawa, wengine waliingia chini ya meza lakini Bryant aliwafuata na kuwafyatulia risasi huko huko walipo, na wale waliokuwa wakikimbia waliishia kupigwa risasi za mgongoni. Kwa muda mfupi wa dakika tano Bryant alikuwa ameuwa watu 20 ambao walikuwa ni wanawake, wanaume na watoto. Baada ya kuridhika na watu aliowaua ndani ya huo mghahawa, Bryant alitoka nje na kuanza kuwashambulia kwa risasi za mgongoni watalii waliokuwa wakikimbia kutoka katika eneo hilo.

Bryant aliingia kwenye gari lake na kuendesha kwa kasi huku akiendelea kufyatua risasi kupitia dirishani kuua kila mtu aliyemuona mbele yake. Baaada ya kuendesha kwa mwendo mrefu kidogo alimuona mwanamke mmoja aitwae Nanette Mikac aliyekuwa akikimbia. Alikuwa amembeba binti yake wa miaka mitatu aitwae Madeline na bintiye mwingine aitwae Allanah aliyekuwa na umri wa miaka 6. Bryant aliwafyatulia risasi na kumuua Nanette na bintiye Madeline. Allanah alikimbia umbali wa mita 18 na kujificha nyuma ya mti. Bryant alishuka kutoka kwenye gari na kumfuata binti yule na kumwambia, "hakuna hata mtu mmoja aliyefanikiwa kunikimbia…." Kisha alimfyatulia risasi ya kichwa na kumuua pale pale.

Dakika tano baadae Bryant aliingia katika Hotel ya Fox and Hounds ambapo kama alivyofanya katika mghahawa wa Broad Arrow, alianza kufyatua risasi hovyo. Mabinti wawili waliuawa kwa kupigwa risasi za kichwa na wateja wengine kadhaa walijeruhiwa vibaya. Bryant alitoka nje ya Hotel hiyo na kuendelea kuwafyatulia risasi za mgongoni watalii waliokuwa wakikimbia hovyo kunusuru maisha yao. Bryant alirudi kwenye gari lake na kuendesha kwa mwendo wa taratibu huku akiendelea kumfyatulia risasi kila aliyemuona barabarani.

Aliendesha umbali wa kilomita 32 hadi alipofika kwenye kituo cha mafuta. Alipofika hapo alibadilisha gari lake kwa kupora gari aina ya Toyota Corola lililokuwa likiendeshwa na mwanasheria wa Sydney aitwae Zoe Anne Hall aliyekuwa akiendesha kuelekea Port Arthur akiwa na mfanyakazi mwenzie aitwae bwana Glen Pears. Bryant alimwamuru bwana Glen Pears kuteremka kutoka kwenye gari na kumlazimisha aingie kwenye buti la gari hilo na kumfungia kisha akamgeukia Zoe na kumfatulia risasi na kumuua na kuutupa mwili wake barabarani. Aliondoka na gari hilo huku akiwa na mateka wake.

Aliendesha umbali wa kilomita 3.2 hadi ilipo nyumba ya wageni ya Seascape. Aliingia katika hoteli hiyo akiwa amemshika Glen mkono na kumkokotea ndani na kuwashikilia mateka pamoja na wamiliki wa nyumba hiyo ya wageni David na Sally. Alipanda moja kwa moja hadi ghorofa ya juu kabisa na kukaa dirishani na kuanza kuifyatulia risasi Helikopta iliyokuwa inafanya kazi ya kubeba miili ya watu waliokufa kutokana na tukio hilo na majeruni ili kuwawahisha hospitalini. Kwa muda usiozidi nusu saa, Martin Bryant alikuwa maeuwa watu 32 na kujeruhi watu 21 wengi wao wakiwa ni watalii. Lilikuwa ni tukio ambalo halijawahi kutokea nchini humo.

Muda mfupi baadae askari Polisi wa kikosi maalum wakiwa na silaha nzito walifika na kuizingira nyumba ile ya wageni ambapo ndipo alipojificha Bryant. Baada ya kuona amezingirwa Bryant alianza kuwafyatulia risasi askari wale na alitishia kuwaua wale mateka wake iwapo ombi lake la kutaka apatiwe Helikopta na kuhaklikishiwa usalama wa kuondoka katika eneo hilo halitatekelezwa. Byant alikuw akiwasiliana na askari hao kwa mnjia ya simu ya mkononi na alikuwa akiwatisha kuwauwa mateka wale kila alipowaona askari wale wale wakijaribu kuisogelea nyumba ile. Askari waliamini kwamba Bryant alikuwa na darubini ambayo ilimwezesja kuona kila kilichokuwa kikiendelea pale chini. Polisi waliamua kucheza mchezo wa kupoteza muda ili ifikapo usiku ndipo wafanye kazi ya kumkamata Bryant na kuwaokoa wale mateka.

Je huyu Martin Bryant ni nani na ni kitu gani kilimsukuma hadi kufikia kufanya mauaji haya ya kutisha kwa kuuwa watu wasio na hatia?

Martin Bryant alizaliwa hapo mnamo Mei 7, 1967 huko katika kisiwa cha Tasmania nchini Australia akiwa ni mtoto wa kwanza kwa wazazi wake Maurice na Carleen Bryant, (Tasmania ni kisiwa kinachomilikiwa na Australia lakini kikiwa kama nchi kamili inayojitegemea). Baba yake alikuwa ni mhamiaji kutoka mji wa Dunston nchini Uingereza. Bryant alizaliwa na kukulia ktika mji wa Hobart, mji mkuu wa Tasmania. Ingawa nyumba ya familia yao iko katika eneo la Lenah Valley Tasmania lakini maisha yake ya utotoni alikulia katika nyumba yao nyingine iliyoko katika ufukwe wa Carnavon Bay, Tasmania.

Bryant aliacha shule akiwa na umri wa miaka 15. Vijana wa rika lake waliokuwa naye karibu walimwelezea kama kijana mwehu na mvivu. Waalimu wake walimwelezea kama mtu asiyependa kuambiwa ukweli na mwenye hisia chungu. Alikuwa ni mkorofi kwa wanafunzi wenzie na ndio sababu ya yeye kushindwa kujenga urafiki. Kutokana na ukorofi wake huo.

Mnamo mwaka 1977 alisimamishwa shule. Taarifa za kisaikilojia zilionyesha kwamba Bryant alikuwa na tabia ya kutesa wanyama pia. Alirudishwa shuleni mwaka mmoja baadae baada ya kuonyesha mabadiliko makubwa ya kitabia, lakini hata hivyo alishindwa kuendelea na shule kutokana na wanafunzi wenzie kumtania na kumfanyia vitendo vya kejeli. Alihamishiwa katika shule maalum kwa wanafunzi wenye matatizo ya kisaikolojia hapo mnamo mwaka 1980, lakini maendeleo yake kielimu na kitabia yaliendelea kuwa duni.

Maisha yake ya ujana yalikuwa bado ni ya matatizo na alikuwa ni mtu mwenye kuchokozeka kihisia haraka sana na baada ya kufanyiwa vipimo vya kisaikilojia alionekana kama alikuwa ana dalili zote za kuwa na mtindio wa ubongo na hata alipofanyiwa vipimo vya IQ alipata alama ya 66 ambayo ni sawa na alama ya mtoto wa miaka 11 tofauti na umri wake. Kutokana na maoni ya wanasaikolojia Bryant aliwekwa kwenye orodha ya watu wenye matatizo a akili na hivyo kunufaika na mafao yanayotolewa na watu wenye hali hizo kila mwezi. Hata hivyo alikuwa akijishughulisha na kazi ndogo ndogo za kutunza bustani kwa malipo na shughuli nyingine zisizo rasmi. Kwa kifupi maisha ya Bryant hayakuwa ya kawaida.

Mnamo mwaka 1990, Bryant na baba yake walihamia katika nyumba ya Helen Harvey, mwanamke mzee ambaye alikuwa ni mcheza kamari asiye wa kawaida. Minong'ono ilienea kwamba Bryant alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na hicho kizee, na kilimgeuza kama mdoli wake akitembea naye huku na huko kujionyesha huku akimnunulia zawadi kemkem za thamani. Mnamo mwaka 1993 Maurice Bryant, baba yake Bryant alifariki na kifo chake kilikuwa ni cha kutatanisha. Mwili wake ulikutwa ukiwa kwenye kisima na ulipotolewa, ulikutwa na jeraha la risasi, lakini uchunguzi wa awali ulionyesha kwamba alikuwa amejiuwa, lakini baada ya tukio la mauaji alilolifanya Bryant, polisi wameanza uchunguzi upya wa kifo hicho. Mwaka huo huo wa 1993, baada ya kifo cha Maurice, Helen Harvey alikufa kwa ajali ya gari katika mazingira ya kutatanisha ambapo Bryant alikuwa ni abiria huku mwanamke huyo mzee akiwa ndiye dereva. Taarifa ya Polisi ulionyesha kwamba kifo chake kilitokana na ajali, lakini pia Polisi wameanza uchunguzi upya wa kesi hiyo baada ya Bryant kufanya mauaji ya kutisha.

Baada ya kifo cha Helen Harvey, Bryant alirithi nyumba zake na mamilioni ya dola ya mwanamke huyo yaliyokadiriwa kufikia dola 550,000 na hivyo kijana huyo kuwa na uwezekano mdogo wa kulazimika kutafuta kazi au kutofanya kabisa kwa sababu hela alizokuwa nazo zilikuwa ni za kutosha. Pamoja na uwezo mkubwa kifedha aliokuwa nao na sura na umbo la kuvutia, lakini Bryant alikuwa na tatizo la kujenga mahusiano. Alikuwa anautumia muda mwingi akiwa peke yake.

Kuanzia mwaka huo wa 1993 alifanya safari za kitalii katika nchi mbalimbali zipatazo 14 lakini kote huko aligundua kwamba watu walikuwa wakimwepuka kama vile ilivyokuwa nchini mwake Tasmania, hata hivyo alikuwa akifurahia safari za ndege na kuna wakati aliwahi kusimulia jinsi alivyovutiwa na mazungumzo yake na abiria mwenzake ndani ya ndege kitu ambacho kilimfurahisha sana kutokana na abiria huyo kuonyesha kumkubali. Hata hivyo mwishoni mwa mwaka 1995 alifikia ukingoni na kutaka kujiuwa. Katika ujumbe wake aliandika hivi: "Nadhani watu wako dhidi yangu, kila ninapojaribu kuwa nao karibu au kujenga nao urafiki, wao wananikwepa……….." hata hivyo hakutimiza adhma yake hiyo.

Majirani zake wanamwelezea kwamba alikuwa ni mtu mwenye mapenzi makubwa na silaha na alikuwa ana kawaida ya kuwatisha majirani zake kwa kufyatua risasi hovyo akiwinda vicheche. Jirani yake mmoja alikwenda mbali zaidi kwa kwenda katika kituo kidogo cha polisi na kuripoti kuhusu vitendo hivyo vya Bryant na kuwaeleza polisi kwamba huenda Bryant akawa ni Mtu hatari kwa usalama wa raia wema, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yake.

Ukweli ni kwamba, bado watu walikuwa na kumbukumbu ya wauaji wa halaiki. Kwa mfano Thomas Hamilton ambaye wiki sita zilizopita alifanya mauaji ya kinyama kwa kuuwa watoto wa shule wapatao 16 huko Dunblane, Scotland, au James Hubert ambaye aliuwa watu 21 katika mghahawa wa McDonalds huko San Diego nchini Marekani mwaka 1984, au Michael Ryan ambaye aliuwa watu 16 huko Hungerford nchini Uingereza mwaka 1987. Wauaji woe hao walielezwa kuwa ni watu waliokuwa wakiishi katika upweke kutokana na kushindwa kujenga mahusiano na watu. Wote walikuwa na mapenzi makubwa na silaha.Mpaka inakaribia alfajiri ya April 29, askari polisi bado walikuwa wameizingira nyumba hiyo ya wageni ya Seascape. Walikuwa, hawajasikia chochote kutoka kwa Bryant kwa muda wa saa kadhaa baada ya simu aliyokuwa akitumia kuisha chaji.Lakini baadae waliona moshi wa moto ukitokea katika dirisha la chumba kimojawapo cha nyumba hiyo ya wageni. Muda mfupi baadae waliona moto ukiwa umezingira chumba hicho. Mtu wa kwanza kutoka katika chumba hicho alikuwa ni Bryant na nguo zake zilikuwa zimeshika moto. Polisi walifanikiwa kuzima moto ule na kumkamata na kisha kumkimbiza katika kitengo cha kuhudumia watu walioathiriwa na moto cha hospitali ya Royal Hobart, ambapo alilazwa kwa matibabu chini ya ulinzi mkali.

Baadae mwili wa Glen Pears na wamiliki wa ile nyumba ya wageni ilikutwa ikiwa imeungua. Wote walikuwa wameuawa kwa kupigwa risasi. Kupatikana kwa miili hiyo kulifanya idadi ya watu walioawa na Bryant kufikia 35 idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na mauaji yaliyowahi kutokea katika nchi hiyo ya Tasmania kwa miaka mitano iliyopita.

Misa ya kumbukumbu ya watu waliopoteza maisha katika mauaji hayo ilifanyika katika kanisa la St. David's Cathedral, Hobart. Huduma hiyo ilihudhuriwa na Gavana wa Australia wa wakati huo Sir William Deane na waziri mkuu John Howard.

Salaam za rambirambi zilimiminika kutoka nchi mbalimbali duniani, akiwemo aliyekuwa rais wa Marekani wa wakati huo Bill Clinton, Malikia Elizabeth wa Uingereza na aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza wa wakati huo John Major ambao nao walipata kushuhudia aina hiyo ya mauaji katika nchi zao. Nchi yote ya Australia ilikumbwa na simanzi, lakini wiki zilivyozidi kupita tangu tukio hilo litokee, simanzi hizo zilibadilika na kuwa hasira. Wananchi wa nchi hiyo walitaka Serikali irejeshe hukumu ya kifo kwa watu wanaokutwa na hatia za kesi za mauaji na kuzuia watu binafsi kumiliki bunduki za automatic. Kilio hicho cha wananchi kilisikilizwa. Wakati serikali ikiangalia namna ya kubadilisha sheria hiyo ya hukumu ya kifo, lakini ilitambulisha sheria mpya inayohusiana na kumiliki silaha.

Kesi ya Bryant ilianza kusikilizwa hapo mnamo Novemba 7, 1996 katika mahakama kuu ya kisiwa hicho cha Tasmania. Alishitakiwa kwa makosa 72 yakiwemo mashitaka 35 ya mauaji na mashitaka mengine 20 ya kujaribu kuuwa. Wakati akisomewa shitaka moja baada ya lingine Bryant alikuwa akitabasamu na kujibu, ‘sina hatia'. Katika hali ya kushangaza, mara baada ya mwendesha mashitaka kumaliza kumsomea mashitaka, Bryant aliangua kicheko pale mahakamani, kisha akabadilisha kauli yake na kukiri makosa yote. Kwa hiyo kufanya kusiwe na kesi ya kusikilizwa. Kilichobakia ni Mahakama kutoa hukumu.Kulikuwa na maoni kutoka kwa mawendesha mashitaka kwamba Bryant ahukumiwe kifungo cha maisha bila uwezekano wa kuachiwa kwa kifungo cha nje (parole).

John Avery, wakili aliyekuwa akimtetea Bryant alimwambia Jaji, "Mteja wangu ana msongo wa mawazo na amekuwa kama amechanganyikiwa. Ingawa hana matatizo ya akili, lakini amekuwa hana furaha na mwenye hasira kutokana na kutokuwa na marafiki kiasi cha kufikia hatua ya kutaka kujiuwa, lakini hasira hizo za kutaka kujiuwa zilibadilika na kupanga kufanya kufanya mauaji a kutisha kama kulipa kisasi. Alinieleza kwamba hakuhofia kupoteza nyumba yake, bali wazo alilokuwa nalo akilini mwake ni kwenda katika Bandari ya Arthur na kuuwa watu wengi."

Lilikuwa ni jukumu la Jaji wa mahakama hiyo William Cox kusoma hukumu. Katika hukumu yake Mheshimiwa Jaji alimhukumu Martin Bryant kifungo cha maisha jela pamoja na kifungo kingine cha miaka 1,035 jela bila uwezekano wa Parole. Akifanyiwa mahojiano na gazeti moja nchini humo hapo mnamo mwaka 2011, mama yake alisema kwamba mwanaye alikuwa ana dalili zote za ukorofi na ukatili tangu alipokuwa mtoto. Alikuwa ni mkorofi kwa watoto wenzie na ukubwani hakumudu kudumu katika ajira kutokana na ukorofi wake.

 
I am back again, baada ya kuwapunja wiki iliyopita.
Sina mengi ya kueleza na ni naamini kwa kesi hii mtajifunza mengi. nawatakia siku njema na mapumziko mema ya mwishoni mwa juma.
 
I am back again, baada ya kuwapunja wiki iliyopita.
Sina mengi ya kueleza na ni naamini kwa kesi hii mtajifunza mengi. nawatakia siku njema na mapumziko mema ya mwishoni mwa juma.

Mkuu mintarudi kuisoma, sasa hivi sijatulia napapalika kama pop con kwenye kikaango, usione kimya ile insue naishughulikia
 
Nashukuru sn kwa post yako mkuu mtambuzi kwani umeifanya wikend yangu kuwa fupi sn..nitaisoma hii na tafakuri juu yake ntaizingatia..!!
 
tangu nijiunge Jf nimekuwa navutiwa sana na hiz makala zako za kiharifu,please mzee keep on coz nyingizinajenga nakutambua maisha wanadamu wa dunia nyingine,most of them they have everything except true and peace,selfishness mbaya sana..
I am back again, baada ya kuwapunja wiki iliyopita.
Sina mengi ya kueleza na ni naamini kwa kesi hii mtajifunza mengi. nawatakia siku njema na mapumziko mema ya mwishoni mwa juma.
 
Mtambuzi ina maana polisi hawakung'amua sababu za kifo cha baba yake? Pia kifo cha yule kizee?
 
Last edited by a moderator:
Maisha ya wazungu yamejaa upweke na ubinafsi sana.Kuna uwezekano mkubwa Martin Bryant ndiye muuaji wa kibibi kizee na Baba yake mzazi.

Asante Mtambuzi kwa simulizi zako zenye msisimko wa ajabu.Nimesoma kisa kizima huku napata hizi nazo za Radio One.
 
Last edited by a moderator:
So sad yaani mauaji ni yakutisha sana.
Ndio hapo tunapokumbuka hujui saa wala dakika ambapo mauti yatakufika !

Eh mungu tunusuru

Pepo la uaji ni baya sana.
Thanks Mtambuzi
 
Last edited by a moderator:
Mkuu Mtambuzi upweke ni kitu kibaya sana aise
Yote aliyafanya kwa kuwa alikuwa mpweke na kila aklikoenda hakubahatika kuw ana marafiki kitu ambacho ni kibaya sana
Kwa simulizi hili ni kuwa kuna uwezekano ni yeye aliwauwa baba yake na yule bibi kizee
 
Last edited by a moderator:
Bryant aliingia kwenye gari lake na kuendesha kwa kasi huku akiendelea kufyatua risasi kupitia dirishani kuua kila mtu aliyemuona mbele yake. Baaada ya kuendesha kwa mwendo mrefu kidogo alimuona mwanamke mmoja aitwae Nanette Mikac aliyekuwa akikimbia. Alikuwa amembeba binti yake wa miaka mitatu aitwae Madeline na bintiye mwingine aitwae Allanah aliyekuwa na umri wa miaka 6. Bryant aliwafyatulia risasi na kumuua Nanette na bintiye Madeline. Allanah alikimbia umbali wa mita 18 na kujificha nyuma ya mti. Bryant alishuka kutoka kwenye gari na kumfuata binti yule na kumwambia, "hakuna hata mtu mmoja aliyefanikiwa kunikimbia…." Kisha alimfyatulia risasi ya kichwa na kumuua pale pale.

khaaa inasikitisha kujichanganya inaondoa msongo wa mawazo asante mtambuzi
 
Last edited by a moderator:
1035 years?duh,nashukuru sana kuishi Tanzania,marafiki kibao,wangemleta huku angeshobokewa na kina .............,tena ni mzungu,ana nyumba,ana gari,wale dada zetu wasingemchoka....mkuu thread yako imenifanya ni-skip lunch leo,perfect
 
Aisee upwek ni noooma kabisa......tena mtu akioneshwa anakataliwa na jamii..hahaha ni worse zaidi!!!Thanks again for the tremendous true story!!
 
Maisha ya wazungu yamejaa upweke na ubinafsi sana.Kuna uwezekano mkubwa Martin Bryant ndiye muuaji wa kibibi kizee na Baba yake mzazi.

Asante Mtambuzi kwa simulizi zako zenye msisimko wa ajabu.Nimesoma kisa kizima huku napata hizi nazo za Radio One.
Kweli Mkuu Ngongo hawa jamaa wana saikolojia ya ajabu sana labda mwana saikolojia Mtambuzi atanisaidia kama ni kweli au la...

Imekuwa jambo la kawaida sana kukutana na mikasa ya mtu anapenda kuua wenzake, yaani yeye ni starehe yake kuona mtu anakata roho na kupigania uhai, haya matukio ni adimu sana kwenye jamii isiyo na vita!

Maana kwenye nchi zenye machafuko, ni suala la kawaida kesi hizi.... Mfano wale watoto wanajeshi waliofundishwa uanaharamu ni kawaida wao kuwa na hamu ya kuua mtu na kutaka kuona viungo vya mtu vimeumbwaje, na ukikitoa kimoja huyo mtu anakuwaje!

Lakini kwa wazungu hali ni tofauti sana, sijui wanakuwa na vita za kwenye nafsi zao tu??

Ila pia hicho kitongoji kilikuwa kimejisahau sana kwa usalama wake, yaani huyo dogo anazunguka na kuua tu kwa mda mrefu hadi police wanakuja kutokea madhara yeshatokea sana hata polisi wa bongo (wa vituo vidogo) wangekuwa wesharipoti na kupambana naye.



 
Last edited by a moderator:
Asante Mtambuzi kwa uzi huu tena. Ila ni hakika maisha ya wazungu ni ya kipweke sana kiasi kwamba ukiwa na tatizo unajiuliza maswali na kujijibu mwenyewe!! Imagine jirani wa mlango wa pili unaweza ukapita bila hata kusema Hi na anaweza augulie ndani au kufa aoze na hakuna wa kujali kuuliza mbona jirani haonekani. Maisha haya yanawagharimu sana na sisi Waafrika tubataka kuyaiga!!! Halafu suala la Silaha liangaliwe upya maan siku hizi tunazipata Tanganyika Arms na sijui kama kuna ufuatiliaji mzuri wa who is who owning it? Pole kwa waliopeteza maisha!!
 
11 Reactions
Reply
Back
Top Bottom