Marekebisho makubwa ya sheria za jinai nchini

Makonyeza

Member
Feb 2, 2020
69
252
Marekebisho makubwa katika sheria za Jinai nchini Tanzania:



Na. M. Majaliwa, Esq.


Tulikwishapoteza mwelekeo, hatukuwa tena nchi yenye kustahili kujinasibu kwa tunu za Uhuru, Haki, Udugu na Amani ambazo kimsingi zimetajwa kama sehemu ya misingi ya katiba yetu, rejea sehemu ya Utangulizi ya katiba yetu ya mwaka 1977.

Mfumo mzima wa haki jinai katika nchi yetu ulichafuka na ikawa kila mmoja anafanya analotaka kwa yeyote na hakuna aliyemuuliza, tukaishia kuumizana, kutesana, kuoneana, na kunyanyasana na hatimaye vyote hivyo viliishia kuharibiana maisha miongoni mwetu kwa watu kuwekwa magerezani muda mrefu bila ya hatia, ikafanywa ni tabia, tabia ikajenga mazoea, na mazoea yakaonekana kama ndio sheria.

Na nyenzo ya kufanya uovu huo ikawa ni zile sheria zetu mbovu au zenye makengeza, basi ikawa kila unayepishana naye kimawazo au kimaslahi basi akijuana na wenye mamlaka au yeye ndiye mwenye mamlaka utazawadiwa mashtaka ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha hata kama tuhuma zako za msingi ilikuwa ni kupishana tu maneno na mkeo.

Ilikuwa ni vilio kila kona, magereza zenye uwezo wa kulaza watu mia saba zikalaza watu elfu mbili, na ikaonekana ni jambo la kawaida. Wenye imani walikesha wakimuomba na kumlilia Mungu na walioweza walifunga swaumu, na hatimaye Mungu akawasikia akamleta Jemedari mwenye jinsia ya kike mwenyehuruma na maono na maamuzi ya Kijemedari kweli, mwenye kufanya mambo kwa faida ya wote, mwenye hofu ya Mungu kutoka moyoni mwake, akatoa tamko moja, kwamba “..hatuwezi kuwa watumwa wa sheria tulizozitunga wenyewe”.

Leo ninaandika haya nikishuhudia athari za kauli yake ile ndani ya kipindi kifupi kabisa, na bila ya shaka ni kwa kauli yake hiyo wataalamu wa sheria serikalini waliingia ‘Field na mnamo tarehe 19th October 2021 Mwanasheria mkuu wa serikali Mheshimiwa Ezekiel M. Felesh akasaini Mswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali unayosomeka kama ‘Written Laws (Miscellaneous Amendments)(No. 7) Act, 2021.

Na kwa kupitia mswada huo endapo utapitishwa na bunge ambalo naamini litaupitisha tu, sheria zifuatazo zinakwenda kurekebishwa na ahueni ya ukweli kupatikana kwa watuhumiwa na wananchi kwa ujumla.

  • Marekebisho kifungu no. 4 CPA:
  • Kifungu no.4 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai(CPA) kinazungumzia sheria zitakazotumika kusikiliza makosa ya jinai yaliyoainishwa na Sheria ya Kanuni ya adhabu(Penal Code) kwamba yatachunguzwa na kusikilizwa kwa mujibu wa CPA na huku ikisisitiza kwamba makosa yote mengine yaliyotajwa na sheria zingine basi sheria hizo zilizotaja makosa hayo ndizo zitakazotumika kuendesha mashauri dhidi ya makosa hayo na wakosaji wake.
  • Lakini sasa kwa mujibu wa mabadiliko yanayokwenda kufanyika, nyongeza inakwenda kufanyika kwa kuongeza kifungu kidogo cha (3) kinachotaka kesi zote zenye asili ya madai au masuala ya kiutawala ziamuliwe kwanza huko kwenye mfumo na sheria ongozi za madai au utawala kabla ya kuzifanya jinai.
  • Hii maana yake ni kwamba sasa kwa wale wenye kesi zenye asili ya madai mfano zitokanazo na mikataba ya biashara, ndoa na mirathi zitatakiwa kwanza kukamilika huko chini ya sheria za mwenendo wa madai kwanza kabla ya kufunguliwa jalada la jinai.
  • Zaidi inamaanisha kwamba sasa kubambikiana kesi za jinai itakuwa historia.

  • Marekebisho ya kifungu no.91(Nolle Proseque)
  • Kifungu hiki cha sheria ndio kile ambacho mkurugenzi wa mashtaka huiambia mahakama kwamba hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya mshtakiwa na kwa kauli hiyo mahakama humuachia huru mshtakiwa. Lakini japo si kwa kesi zote, baadhi ya kesi hutokea baada ya mahakama kumwachia mtuhumiwa hukamatwa tena na kupandishwa mahakama ileile na kusomewa mashtaka yaleyale na kwa hakimu yuleyule hali ambayo hutafsirika kama ni matumizi mabaya ya sheria kusababisha usumbufu tu kwa mtuhumiwa kwa sababu baada ya hapo mwenendo wote wa kesi husika ikiwe dhamana kama alipewa hufutika na kila kitu kutakiwa kuanza upya.
  • Mengi ya hovyo yalikuwa yakifanyika kwa kutumia kifungu hiki japo nikiri kwa wakati huu wa zama za Mama haikufanyika na hata kama ilifanyika ni kwa nia njema.
  • Sasa mabadiliko yanayokwenda kufanyika kupitia mswada huu ni kwa kuongeza kifungu kidogo cha (3) kinachozuia mshtakiwa kukamatwa tena kwa kosa lilelile baada ya kuachiwa na mahakama isipokuwa tu kama itathibitika kwamba kuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kesi yake. Na zaidi si hivyo tu bali pia italazimu kesi husika ianze kusikilizwa maramoja baada ya mshtakiwa kukamatwa tena.
  • Hii ni namna mujarabu kabisa kuzuia baadhi ya maafisa wasio waaminifu kutoka kwa ofisi ya waendesha mashtaka kutokuitumia sheria hii vibaya.
  • Kwa hivyo baada ya mswada huu kuwa sheria endapo mtuhumiwa akiachiwa kwa Nolle Proseque atoke mahakamani bila ya wasiwasi kwa sababu hiyo hitaji la kuithibitishia mahakama kwamba kuna ushahidi wa kutosha kuweza kuestablish kesi si suala la siku moja, litahitaji Mlalamikaji ambaye ni jamhuri kuleta maombi ya kuthibitisha jambo hilo ili kupata ruhsa ya kumkamata tena kwa ajili ya kuendelea na kesi ilipoishia.

  • Marekebisho/nyongeza ya kifungu namba131A:
  • Kifungu hiki kinazungumzia hitaji la kukamilika kwa Upelelezi wa makosa ya jinai. Marekebisho yanatanabaisha kwamba kwa sasa hakutoruhusiwa kesi ya jinai kusajiliwa mahakamani kama upelelezi haujakamilika, isipokuwa tu kwa kesi za makosa kubwa(serious offences). Na hayo makosa makubwa kwa mujibu wa sheria yametajwa na kutafsirika kwamba ni pamoja na kumsababishia mtu maumivu makubwa ya mwili(Grievous bodily harm), ubakaji, unyang’anyi wa kutumia silaha(armed robbery), usafirishaji haramu wa binaadam(human trafficking), kukutwa na silaha bila kibali na makosa yote ambayo kwa mujibu wa sheria hutakiwa kusikilizwa na mahakama Kuu.

  • Marekebisho kwenye sheria ya ‘Plea Bargain’ :
  • Hapa mswada unalenga kurekebisha baadhi ya vifungu vinavyohusiana na bargain (maridhiano) kama ifuatavyo:
  • Kifungu namba 194F CPA:
  • Kifungu hiki kwa ujumla kinazungumzia na kubainisha aina ya makosa ambayo maridhiano hayaruhusiwi. Mfano mzuri ni Kifungu kidogo cha (c) ambacho kilitaja au kusomeka kwamba kwa makosa ya “kukutwa nazo au kuingiza dawa za kulevya zenye thamani ya shilingi Milioni Ishirini(Tshs. 20,000,000/-) basi kesi hiyo mshtakiwa hakuruhusiwa kubargain.
  • Lakini sasa kwa minajiri ya marekebisho au maboresho ya sheria zetu, Mswada huu katika kuimarisha ufanisi wake unalenga kurekebisha kifungu hicho kwa kukiondoa kabisa na kuweka ingizo mbadala la kifungu hicho linalosomeka “ kukuta au kusafirisha dawa za kulevya zenye thamani ya shilingi za kitanzania Milioni Mia moja(Tshs. 100,000,000/-).
  • Hii maana yake ni kwamba, kwa mshtakiwa wa makosa ya usafirishaji au kukutwa na madawa ya kulevya yenye thamani chini ya shilingi milioni mia moja ataruhusiwa kubargain chini ya sheria hiyo.
  • Lakini zaidi kwa wale wenye mashtaka ya usafirishaji au kukutwa na madawa ambayo hayajaainishwa thamani yake basi kigezo kitakachotumika ni uzito na kwa makosa ya dawa za kulevya yenye uzito wa zaidi ya Kilo Moja(1Kg) haitoruhusiwa kubargain. Lakini kwa minajiri ya marekebisho hayo sasa mashtaka ya madawa ya kulevya yenye uzito chini ya Kilo moja(1Kg) au yenye thamani ya chini ya shilingi Milioni Miamoja sasa wataruhusiwa kubargain.

  • Bhangi na mirungi:
  • Kwa wale wenye mashtaka ya mimea isiyoruhusiwa, yaani Bhangi na Mirungi wataruhusiwa kubargain kama makosa yao yanahusisha mmea we uzito wa chini ya Kilogram mia moja.

  • Marekebisho ya sheria ya Uhujumu Uchumi(Dhamana)

  • Kimsingi makosa yote ya uhujumu uchumi kwa mujibu wa sheria husikilizwa na mahakama kuu ya Tanzania. Na kwa mujibu wa sheria ya sasa ya Uhujumu Uchumi sura ya 200 maombi ya dhamana kwa kesi za uhujumu uchumi zenye kudhaminika kifungu namba 29(4) kinataka maombi ya dhamana yanayohusisha makosa yenye thamani ya chini ya shilingi milioni Kumi maombi hayo kusikilizwa na mahakama ya wilaya au mahakama ya hakimu mkazi.
  • Lakini kwa mujibu wa Mswada huu utakapopitishwa na bunge na kuwa sheria basi kesi zote za uhujumu uchumi zenye kuhusisha Mali yenye thamani ya Tshs. Milioni Mia Tatu.
  • Maana ya hii ni kwamba muswada huu ukipitishwa basi kesi zote za uhujumu uchumi zenye thamani chini ya Milioni Mia tatu maombi yake ya dhamana yatafanyika na kusikilizwa na mahakama za wilaya na zile za hakimu mkazi.
Nikimsifu mama na kumshukuru kwa kazi kubwa aliyoifanya ndani ya muda mfupi nitakuwa nimekukera, Allah amjaalie maisha marefu mama yetu na amlinde dhidi ya kila amfikiriaye, kumuombea na kumuwazia vibaya, Aaaaaaamin!!

Kazi iendelee..
 
Kuna wapuuzi watakwambia nchi inataka sheria ziwe za kikatili kama ilivyokuwa wakati Magufuli.
 
Back
Top Bottom