Dong Samuel Luak na Aggrey Idri walitoweka January 2017
Marekani imewawekea vikwazo maafisa watano wa ngazi za juu za Usalama wa Taifa wa South Sudan, NSS, kwa kuhusishwa na utekaji na mauaji ya wakosoaji wawili wa serikali ya Rais Salva Kiir miaka mitatu iliyopita.
South Sudan imekuwa ikikana kujua kilichowasibu Mwanasheria mtetezi wa haki za binadamu, Dong Samuel Luak na mwanachama wa chama cha upinzani cha SPLM-IO, Aggrey Idri, walionyopolewa kwenye mitaa ya Nairobi, Kenya na watu wasiojulikana na kupotea January 2017.
Hata hivyo jopo la wataalam wa Umoja wa Mataifa liliripoti kuwa limedhihirisha ushahidi unaobainisha Serikali ya South Sudan ndio iliwateka, kuwasafirisha mpaka Makao Makuu ya Usalama wa Taifa wa South Sudan, mjini Juba, na hatimaye kwenye kambi ya mafunzo ya usalama wa taifa, Luri, iliyoko kwenye shamba linalomilikiwa na Rais Kiir, ambako waliuliwa.
Watano hao ni pamoja na Bw. Abud Stephen Thiongkol, ambae alikuwa Mkuu wa mahabusu ya Luri, na ndie anaeminika kuidhinisha wauawe . Wengine ni Malual Dhal Muorwel, Kamanda Mkuu wa Kambi ya Usalama ya Luri, John Too Lam, Mwambata wa Kijeshi wa Ubalozi wa South Sudan, Kenya, ambae pamoja na mtajwa mwingine, Michael Kuajien, walikuwepo Nairobi wakati wa utekaji. Pia yupo Angelo Kuot Garang, mwanausalama wa South Sudan aliyetumia passport ya Australia kurudi Afrika Mashariki kusimamia zoezi la utekaji wa wawili hao.
Ripoti ya jopo la wataalam hao wa Umoja wa Mataifa ilisema ilipata ushahidi wa vyanzo mbali mbali vilivyoshabihiana na vya kuaminika, wakiwepo watu waliowaona Bw. Luak na Bw. Idri katika mahabusu za Usalama wa Taifa mjini Jeba katika nyakati tofauti, kabla ya kuhamishiwa kwenye kambi ya Luri ambako inaaminika waliuliwa kwa kupigwa risasi Januari 30, 2017.
Vikwazo vya kiuchumi vya Marekani kwa watu binafsi vinatwaa mali yeyote ya mhusika iliyoko kwenye himaya ya Marekani, na inapiga marufuku Waamerika kufanya nae miamala. Sheria ya vikwazo pia inazuia taasisi zozote duniani zinazofanya biashara na Marekani kujihusisha na mhusika aliyeko kwenye vikwazo.
Wanaharaki wa haki za binadamu wa jumuiya ya Kimataifa wamesema wamepokea hatua hiyo ya Marekani kama mwanzo wa mchakato wa kuwafikisha wahusika mbele ya vyombo vya sheria.