Gibborim
JF-Expert Member
- Oct 7, 2019
- 388
- 877
Mkuu, Hapana SIYO KWELI. Marekani alipambana na kila taifa lenye vinasaba vya kikomunisti hapa duniani, liwe kubwa au dogo, taifa la Uchina likiwa juu kabisa ya orodha. Historia ibaki kuwa historia ,tusiizungumze bila kutoa uthibitisho maana tutakuwa tunafanya HISTORICAL REVISIONISM.China imekuja kuwa tishio kwa marekani miaka hii ya 2000s.Huko nyuma labda uniambie USSR/Russia,Huko nyuma marekani hakuwahi kuwekeza nyuvu kupambana na china kama livyowekeza kwa USSR.Sasa ukiniambia walishindwa sijui una maana gani.
Marekani alianza kupambana na Uchina tokea mwaka 1946 kwenye The Chinese Civil War akiiunga mkono Serikali ya kitaifa ya Uchina ya Chiang Kai-Shek dhidi ya vikosi vya kikomunisti vya Mao Tse-Tung.Asilimia 57 ya vifaa vya kijeshi vya Chiang kuanzia ndege hadi mizinga vilitolewa na serikali ya Marekani.
Mwaka 1948 bunge la Marekani lilipitisha sheria iitwayo The Chinese Aid Act ambayo ilihalalisha Marekani kumsaidia kijeshi Chiang kupambana na vikosi vya kikomunisti vya Mao Tse-Tung. Wakati huko Ulaya wanapata The Marshall Aid chini ya The Marshall Plan ili kumkabili USSR, Chiang alipewa The China Aid ili kuzuia wakomunisti wasichukue nchi. Hili halikusaidia kitu maana serikali ya Chiang ilibagazwa vibaya na kukimbilia uhamishoni kule Taiwan.
Mwaka 1951 baada ya kuzidiwa na vikosi vya wakomunisti wa Uchina kwenye vita ya Korea General Douglas MacArthur alitaka kutumia silaha za nyuklia dhidi ya Uchina na Korea Kaskazini akiamini kwamba angeshinda vita ndani ya siku kumi tu na kumrudisha Chiang madarakani kutoka Taiwan lakini President Harry Truman akaogopa na kumfuta kazi.
Uchina akashinda akajitanua Korea Kaskazini na tokea mwaka 1953 hajaondoka kule mpaka leo hii. Marekani kwa kuwaogopa wakomunisti wa Uchina aliamua kujenga kambi za kijeshi za kudumu kule Japan ambako akaamua hadi kuwatoa wahalifu wa kivita kama Nobusuke Kishi na kuwapa madaraka ili wamsaidie kupambana na Uchina.
Huyu Nobusuke Kishi alikuwa babu yake na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe na kabla ya hapa alihukumiwa na The Special Military Tribunal for Far East kwa makosa ya vita ya pili ya dunia. Juhudi zote hizi za Marekani ziliashiria kwamba Uchina alikuwa ni tishio kubwa kwa maslahi ya taifa la Marekani tokea kitambo.
Marekani aliitenga Uchina ya kikoministi kiuchumi na kidiplomasia. Mao Tse-Tung alishawahi andika barua kwa maraisi wa Marekani kuomba amani na ushirikiano wa kibiashara na Marekani lakini hakujibuwa mpaka miaka ya 1970 ambapo Raisi Nixon alifanya mazungumzo na Waziri Mkuu Zhou Enlai.
Marekani aliamini kabisa kumtenga Uchina kungezuia ustawi wake wa kisayansi na kiteknolojia lakini mwaka 1964 aliwaacha midomo wazi baada ya kufanya jaribio la kwanza la mabomu ya kiatomiki kule Lop Nur. Jaribio hili liliwavuruga Marekani na Washirika wake kwasababu walikuwa wanapigana na wakomunisti kule Vietnman.
Waliwahi hadi kufanya mazungumzo yasiyo rasmi na Serikali ya Warusi ili kumzuia Uchina asitengeneze zaidi silaha za kiatomiki. Lakini unadhani ameweza ?
Mwaka 1972 Marekani akashindwa tena kumzuia Uchina kupata kiti ndani ya baraza la ulinzi la UN, baada ya Taiwan kunyang'anywa na kufukuzwa. Zaidi ya hapo mwaka 1979 Marekani akaamua kukubali kuitambua rasmi Serikali ya Kikoministi ya Uchina ili kumfanya asishikamane na Urusi wakati wa vita baridi.
Mwaka 1993 Marekani aliweka vikwazo vyenye kiwango cha dola za kimarekani milioni 500 dhidi ya Uchina, akizuia vifaa maalumu vya kutengeneza Satellite kuuzwa Uchina akidhani atawazorotesha wachina lakini hakufanikiwa leo hii wao ndiyo wa kwanza kurusha The First Quantum Satellite nje ya dunia.
Historia inaonyesha kuwa Marekani alianza kuhangaika na tishio la Uchina punde tu baada ya vita ya pili ya dunia kuisha mwaka 1945 na siyo mwaka 2000 kama unavyosema hapa.
Miaka zaidi ya mia mbili iliyopita Mfalme Napoleone Bonaparte wa Ufaransa aliwahi kusema hivi kuhusu taifa la Uchina" China is a sleeping giant. Let her sleep, for when she wakes she will move the world"