Marekani yamjibu Lipumba

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,825
287,847
Marekani yamjibu Lipumba

na Edward Kinabo
Tanzania Daima~Sauti ya Watu

SERIKALI ya Marekani imekanusha madai yaliyotolewa juzi na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, kuwa nchi wahisani zimeshindwa kuwakemea viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi na badala yake zimekuwa zikiwasifia.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima jana, Msemaji Mkuu wa Ubalozi huo nchini, Jeffery Salaiz, alisema Marekani kama moja ya nchi wahisani, haijawahi kusifia watuhumiwa wa ufisadi nchini na kamwe haitarajii kufanya hivyo.

Alisema Profesa Lipumba ana uhuru wa kutoa maoni yake sawa na ilivyo kwa mtu mwingine yeyote, lakini Marekani haikubaliani na madai hayo, kwani imekuwa ikichangia sana mapambano dhidi ya ufisadi nchini.

Alisema Marekani, mara kadhaa imekuwa ikitoa kauli za kutaka mamlaka zinazohusika kuhakikisha fedha zilizoibwa zinarejeshwa na watuhumiwa wanawajibishwa, ikiwa ni pamoja na kuchunguzwa, kufunguliwa mashitaka na kufungwa wakipatikana na hatia.

Alisema kitu ambacho Marekani imekuwa ikisifia kwa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tatu ni hatua iliyopigwa katika sera za mageuzi ya kiuchumi hata uchumi mkubwa kuweza kukua kwa kiwango cha kuridhisha, tofauti na miaka ya nyuma.

“Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, alifanya mageuzi ya kiuchumi na ameacha uchumi ukikua katika kiwango cha kuridhisha, ingawa bado kazi zaidi inahitajika katika kudumisha na kukuza uchumi huu. Hizi ndizo juhudi ambazo Marekani imekuwa ikisifia na si ufisadi,” alisema.

Alisema Marekani inaunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania hususan uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, chini ya Rais Kikwete, kwa kujenga mazingira yanayotoa uhuru zaidi kwa vyombo vya habari, wanaharakati, vyombo vya usalama, Bunge na wadau mbalimbali, kuzungumza kwa uwazi kuhusu ufisadi, kuchunguza, kutoa ushahidi na kushawishi kuchukuliwa kwa hatua.

“Suala la ufisadi lipo katika kila nchi, ikiwemo Marekani. Sisi tunaamini katika utawala wa sheria, tunaamini kuwa utawala wa sheria ndio nguzo ya utawala bora wa kupambana na ufisadi na tumekuwa tukishirikiana na Tanzania katika hili,” alisema.

Alisema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Marekani imetoa jumla ya dola milioni 11.5 kwa Tanzania kwa ajili ya kutekeleza programu mbalimbali za kuzuia ufisadi.

Ametaja programu ambazo zimekuwa zikitekelezwa chini ya ufadhili huo kuwa ni programu ya kujenga uelewa wa wanahabari kuhusu rushwa, kuimarisha Tume ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), kuwezesha jamii kufuatilia fedha za walipa kodi kupitia Mfumo wa Ufuatiliaji wa Matumizi ya Fedha za Umma ‘PETS’ na programu ya kutoa mafunzo dhidi ya rushwa kwa mawakili na watendaji wa mahakama.

Alipoulizwa kuwa haoni kuwa ufisadi ambao Mkapa na viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tatu na Nne wanahusishwa nao, umechangiwa sana na sifa ambazo wahisani wamekuwa wakitoa, alisema nchi yake imekuwa tu ikipongeza mazuri yanayofanywa na serikali na kutaka hatua zichukuliwe kwa yale yaliyo kinyume na misingi ya utawala bora.

“Marekani inafuatilia kwa karibu jinsi hali ya mambo inavyokwenda nchini, hususan vita dhidi ya mafisadi, lakini haiwezi kutoa kauli kila siku bali hufanya hivyo pale inapobidi,” alisema.

Juzi Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, katika mkutano wake na waandishi wa habari, aliwalaumu wahisani kwa kushindwa kuwakemea viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi na kudai kuwa, wamekuwa wakiwasifia kuwa wanaendeleza utawala bora na utawala wa sheria.

Lipumba alisema wafadhili walimsifia hata Rais Mkapa kuwa aliongoza mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na kujenga misingi imara ya utawala bora.

Mkapa na viongozi kadhaa wa serikali yake wakati ule, wamekuwa wakihusishwa na kashfa mbalimbali za ufisadi.

Mbali ya Mkapa, tuhuma za ufisadi zimekuwa zikiwaandama baadhi ya viongozi wa serikali na katika hatua fulani, baadhi ya viongozi wamelazimika kujiuzulu uongozi baada ya majina yao kuhusishwa katika tuhuma mbalimbali za namna hiyo.

Miongoni mwa waliojiuzulu ni aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na waliokuwa mawaziri wengine watatu, Nazir Karamagi, Dk. Ibrahim Msabaha na Andrew Chenge.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna hatua zaidi zilizochukuliwa dhidi ya watuhumiwa wanaohusishwa na kashfa tofauti za ufisadi, licha ya serikali kuahidi kufanya hivyo.
 

“Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, alifanya mageuzi ya kiuchumi na ameacha uchumi ukikua katika kiwango cha kuridhisha, ingawa bado kazi zaidi inahitajika katika kudumisha na kukuza uchumi huu. Hizi ndizo juhudi ambazo Marekani imekuwa ikisifia na si ufisadi,” alisema.

Alisema Marekani inaunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania hususan uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, chini ya Rais Kikwete, kwa kujenga mazingira yanayotoa uhuru zaidi kwa vyombo vya habari, wanaharakati, vyombo vya usalama, Bunge na wadau mbalimbali, kuzungumza kwa uwazi kuhusu ufisadi, kuchunguza, kutoa ushahidi na kushawishi kuchukuliwa kwa hatua.

Naam... Hata JF inajifalagua vilivyo ndani ya awamu hii ya nne
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom