Marekani, Uingereza zawaonya Kibaki, Raila

Sokomoko

JF-Expert Member
Mar 29, 2008
1,915
127
Marekani, Uingereza zawaonya Kibaki, Raila
Na Waandishi Wetu, Dar na Nairobi


MAREKANI na Uingereza, zimewaonya Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Mtarajiwa Raila Odinga na kuwataka kumaliza tofauti zao kwa haraka na kutangaza Baraza la Mawaziri.


Katika taarifa yake iliyotolewa jana mjini Nairobi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Condoleezza Rice alisema, viongozi hao hawana sababu ya kuendelea kuchelewesha utekelezaji wa mkataba wa serikali ya Mseto kwa kuhakikisha kuwa, kunakuwa na mgawanyo sawa wa madaraka.


Rice alisema kuwa, uharaka huo unahitajika kwa sasa kwa viongozi hao kutambua kuwa suala la kuunda Baraza hilo la Mawaziri ni shughuli muhimu kwa ustawi wa taifa hilo kwa sasa.


" Iwapo mkataba huu hautatekelezwa kikamilifu, Marekani itasimama kwa upande wake kutoa hukumu kulingana na ucheleweshwaji wa utekelezaji wa mkataba huo, pamoja na sheria zilizopitishwa hivi karibuni, ”" alisema Rice katika taarifa yake hiyo.


Aliongeza kuwa, alizungumza na Kibaki na Raila kwa simu kwa siku mbili zilizopita na kumhakikishia, wako tayari kutekeleza makubaliano hayo na kutangaza Baraza hilo la Mawaziri.


Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Miliband, aliungana na Rice akielezea kusikitishwa kwake na urasimu unaofanywa na viongozi hao, kiasi cha kuchelewesha Baraza hilo la Mawaziri kwa makusudi.


Miliband, alikumbushia hali tete ya usalama iliyolikumba taifa hilo na kuwa nchi yake itahakikisha inasimamia utekelezwaji wa makubaliano yaliyofikiwa, baina ya viongozi hao chini ya msuluhishi, Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan.


“Kila upande ni lazima ujue jukumu lake katika kuharakisha utekelezaji wa makubaliano hayo, pia wafuasi wa Kibaki ni lazima watambue kuwa suala la mgawanyo sawa wa madaraka zikiwemo nafasi muhimu halizuiliki,” alisema Miliband.


Spika wa Bunge la Kenya, Kenneth Marende, alieleza matumaini yake kuwa anaamini viongozi hao watatangaza Baraza hilo la Mawaziri mapema, kabla ya kuanza kwa kipindi cha Bunge Jumanne wiki ijayo.


Akizungumza katika maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya Rwanda yaliyotokea miaka 14 iliyopita, Marende, alitoa mwito kwa Kibaki na Raila kuharakisha kutangaza baraza hilo na kuwataka wananchi wa Kenya kulinda amani ya nchi yao, hasa katika kipindi hiki wanaposubiri kutangazwa kwa baraza hilo.


" Nina imani, ninatarajia baraza litakuwa tayari kabla ya kuanza kwa Bunge, lakini pia ni wajibu wetu wananchi kuwa na subira, hasa tunapojifunza kutoka Rwanda, tukijua yaliyowapata miaka 14 iliyopita yanaweza kutokea kwetu pia,” alisema Marende.


Aliwaasa Kibaki na Raila kutambua kuwa, wakifuata kikamilifu dhana ya mgawanyo wa madaraka kama ilivyo kwenye makubaliano ya mkataba huo hakuna tatizo linaloweza kuendelea katika kugawana madaraka hayo.


Jumatatu wiki hii, Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), kilitangaza kujitoa kusitisha mazungumzo juu ya kuundwa kwa baraza hilo, kikidai kuwa Rais Kibaki na wafuasi wake wamekuwa wakikiuka makubaliano waliyofikia awali juu ya mgawanyo wa madaraka na wizara, kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba wa serikali ya mseto.


Mkataba huo, uliosainiwa chini ya usimamizi wa Annan ulituliza machafuko yaliyoikumba nchi hiyo, baada ya kutangazwa matokeo ya Urais yenye utata ya uchaguzi mkuu uliofanyika Desemba 27, mwaka jana.


Vurugu za aina hiyo, zilianza kuibuka tena juzi katika eneo la Kibera na Kisumu, muda mfupi baada ya ODM kutangaza kusitisha mazungumzo juu ya Baraza la Mawaziri.

Source: Mwananchi newspaper.
 
Back
Top Bottom