Mara zote kuwa na shukrani kwa yote uliyonayo maishani

ROBERT HERIEL

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
4,567
2,000
MARA ZOTE KUWA NA SHUKRANI KWA YOTE ULIYONAYO MAISHANI

Kwa Mkono wa, Robert Heriel

Bila Shukrani maisha hayamfai mtu. Hayana maana yoyote, bila Shukrani maisha ni UTUMWA na mzigo mzito wenye maumivu makali mno. Kushukuru ni kuishi, kunamfanya mtu aishi Kwa Raha na furaha.

Pasipo kushukuru maisha yafaa nini?

Ni kweli maisha sometimes yanatisha, yanatupitisha katika njia ngumu zinazoumiza Nafsi zetu na kuacha majeraha makubwa ya uchungu yasiyofutika maishani kwetu. Kuna wakati maisha hukufanya ujute kuzaliwa, ukufuru Mungu na hata kulaumu wengine. Lakini ukijifunza kushukuru Kwa Yale uliyojaliwa basi moyo wako utaweza kuhimili mikikimikiki ya maisha.

Ni kweli wapo waliozaliwa Mafukara; wanaoshinda njaa na Kula mlo duni, miili Yao imefubaa, Afya zao zimezorota, wapo hoi huku magonjwa yakiwaandama kwani njaa rafiki Ake ni Maradhi, usilaumu, usilalamike, shukuru Kwa kuwa na uwezo wa kupata hamu ya Kula. Wapo wenye vyakula lakini hawana hamu ya Kula. Na wapo wenye hamu ya Kula pamoja na chakula lakini Maradhi Fulani huwasumbua, hivyo hawakifurahii chakula.

Wakati Fulani nikiwa mdogo, nikiwa nalelewa na Bibi yangu, hatukuwa na chakula kizuri chakutamanika, ingawaje kilikuwa chakula chenye kushibisha, nilikichukulia poapoa, kuna wakati nilikuwa nikilalama kuwa kila siku tunakula chakula hicho hicho(ugali), maneno yangu hayakuwa mazuri, Bibi alinambia nijifunze kushukuru kwani kuna wengine wanakosa hata hiki tunachokula.

Baada ya miaka mingi kupita, nikiwa nimekua kijana sasa, nilikumbuka maneno ya Bibi, uwezo wa kununua chakula nikipendacho ninao, lakini ishu ipo kwenye Meno, Taikon anamatatizo ya Meno. Kwa. Kweli chakula nikitamu lakini sikifurahii, wenye matatizo ya Meno mtaelewa nazungumzia nini.

Ndipo nikakumbuka kuwa, shukuru Kwa yote uliyonayo katika maisha yako.

Usiwe mtu wa kulalamika.

Shukuru kwa sura uliyonayo hata Kama unaiona ni mbaya, ipende hivyo hivyo na ubaya wake kwani kuna watu wanatamani wangekuwa Kama wewe.

Shukuru Kwa maumbile yako, uwe mrefu au mfupi, mnene au mwembamba, mweupe au mweusi, mshukuru Sana Mungu, kwani wapo watu wanavitafuta ulivyo navyo lakini kamwe hawezi kuvipata.

Kushukuru ni Dalili ya Upendo, kujali na kuthamini.

Asiyeshukuru Hana upendo ndani yake, hathamini wala hajali.

Maisha ni kweli yanaweza yakawa yanaogopesha, lakini wewe usiwe mwoga, maisha huwaogopesha wasio na Shukrani, wasiorizika na Yale waliojaliwa na Muumba.

Wanaoiogopa kesho ni Wale walioshindwa kushukuru Kwa Leo na Jana. Huna haja ya kuigopa kesho kwani kesho ni mtoto wa leo. Na Leo ni Baba WA kesho. Hakuna kesho pasipo leo. Ikiwa ndivyo hivyo, ndio maana ukaambiwa uwaheshimu Baba yako na Mama yako ili siku zako zipate kuwa nyingi katika USO wa Dunia. Kwa maana leo ndio Baba na ndio Mama, unapaswa uiheshimu, uishukuru, na uilipe fadhila ili mtoto wake akizaliwa ambaye ni Kesho uwe Salama.

Maisha ni Raha, iwe unapitia katika njia yenye milima mikali na miamba iliyochongoka, Shukuru Sana Kwa maana hakuna visa vizuri vya kusisimua Kama vya waliopitia njia ngumu.

Kujifunza kushukuru ni kujifunza kuishi Kwa furaha katika maisha yako.

Maisha yako ni yathamani kuliko Fedha, kuliko Nyumba, kuliko kitu chochote. Kupewa maisha pekee unapaswa ushukuru.

Shukuru kuwa vile ulivyo; uwe mjinga shukuru, uwe na akili shukuru.
Uwe masikini shukuru, uwe tajiri shukuru.
Uwe na nyumba shukuru, usiwe nayo shukuru.
Shukuru! Shukuru! Shukuru Kwa kila kitu.

Kushukuru ni kujivunia Yale uliyonayo.
Mke/mume uliyenaye mshukuru Mungu.
Awe mzuri au mbaya mshukuru Mungu.

Hata Kama anakusumbua mshukuru Mungu, ukiweza kufanya hivyo nakuhakikishia maisha yako yatabadilika mara, na utaelewa ninachokiandika.

Watoto ulionao mshukuru na jivunie nao. Iwe wazuri au Wabaya. Shukuru.

Siku zote Shukrani inatabia ya kumshangaza mtu Kwa mambo MAZURI.

Kazi uliyonayo mshukuru MUNGU. Iwe inakipato duni au kikubwa wewe shukuru.
Iwe inadharaulika au inaheshimika shukuru tu.

Ilimradi uitende Kwa nguvu zako zote, Kwa akili zako zote na Kwa moyo wako wote. Kazi hiyo hiyo wanayoidharau itawa-Suprise mpaka wakuite mchawi maana ndio tabia za watu walioshindwa kuita watu wachawi. Hata Yesu aliitwa Belzebubu yaani Mkuu wa mashetani.

Mshukuru Mungu Kwa elimu uliyonayo. Mshukuru MUNGU Kwa kukosa kwako elimu Kama hauna Elimu. Iwe ulifanya uzembe au mazingira magumu ya nyumbani ndio yakufanya ukakosa elimu, we mshukuru Mungu. Usijilaumu wala kumlaumu yeyote.

Shukrani hufungua akili. Humfanya mtu aangalie mbele nini atafanya atoke pale alipo. Na akili ikifunguka baraka hufunguka, Kwa maana pasipo akili hakuna baraka, akili ndio humfanya mtu aweze kuziona baraka na kuzitumia.

Watu wanaolalamika na kulaumu hujikuta akili zao wakizifunga na hivyo wanashindwa kutumia baraka walizogewa.

Neno usihukumu usije ukahukumiwa huenda wengi wetu wanachanganya maana,
Lakini maana yake ni kuwa usilaumu wengine, usijione wewe ndio uko sahihi/mwenye haki usije ukalaumiwa/Nafsi yako ikajilaumu baadaye.

Furahia maisha yako.
Penda familia yako.
Mshukuru Mungu kwa yote aliyokupa.
Mshukuru kwa kukupa familia nzuri Kama hiyo.
Hata Kama mke/mume anakusumbua, ukijifunza kumshukuru MUNGU kwa mkeo/mumeo licha ya ubaya wake nakuhakikishia maisha yako yatabadilika.

Siongei Kama motivation speaker hapa, naongea uhalisia wa Mambo.
Nafahamu ugumu wa kushukuru na kujivunia wakati wa Hali ngumu,
Nafahamu ugumu wa kujivunia na kushukuru Kwa kuwa na Mke/mume mkorofi.
Nafahamu ugumu wa kushukuru na kujivunia udhaifu wa maumbile yasiyovutia Kama ubaya wa Sura, ufupi uliopitiliza, urefu uliopitiliza, unene au wembamba uliopitiliza, kibamia au Bwawa miongoni mwa mengine. Lakini yakupasa ujitahidi kushukuru kwani Kwa namna hiyo ndipo utakapoipata furaha yako.

Taikon niishie hapa, maana kuna watu watasema andiko hili ni refu.

Ni Yule Mtibeli

Robert Heriel
Taikon wa FASIHI
Kwa sasa Dar es salaam
 

Craig

JF-Expert Member
Feb 9, 2013
1,169
2,000
Mkuu Taikon nakuelewa sana Ila jitahidi kufupisha bandiko, manake kadri linavyokuwa refu ndiyo nina sahau mapema Hoja zote.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom