Maprofesa wakosoa wagombea vyama vya upinzani kuenguliwa

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
PROFESA Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (RUCU), amekosoa kuenguliwa kwa wagombea wa vyama vya upinzani katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

WhatsApp%20Image%202020-07-15%20at%205.13.29%20PM.jpeg

Amesema kinachotokea sasa kwenye mchakato huo kwa baadhi ya wagombea kuenguliwa kilianzia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ambao ulilalamikiwa.

Msomi huyo alikuwa akizungumza na Nipashe kuhusu mchakato wa uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Jumatano Oktoba 28, mwaka huu.

Alisema ili uchaguzi uwe huru na haki kama ambavyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekuwa ikitangaza kila mara, ni lazima wahakikishe vyama vyote vinapewa haki ya wagombea wao kushiriki.

“Hii ni mbinu iliyotumika uchaguzi wa serikali za mitaa, wapinzani wakaenguliwa. NEC ilivyotangaza uchaguzi utakuwa huru na haki hatukutegemea hili lijirudie tena.

“Haiwezekani wagombea wanaoonekana fomu zao zina matatizo wawe wa upinzani tu.

Mbona wa CCM hakuna anayerudishwa? Haiwezekani uchaguzi uwe huru na haki kama mfumo wenyewe hauruhusu uwe hivyo, hatuna tume huru," alionya.

Profesa Mpangala alisema kuwa, ili uchaguzi uwe huru na haki, wagombea wote wanatakiwa watendwe haki sawa, bila hivyo siyo wa haki.

Wakati Profesa Mpangala akisema hayo, Profesa Alexander Makulilo kutoka Idara ya Sayansi ya Utawala ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), aliiambia Nipashe jana kuwa siyo jambo la ajabu kwa chama tawala kupata wagombea wanaopita bila kupingwa kutokana na kuwa na faida ya kutekeleza ilani.

“Mimi kwangu sioni ajabu kuwapo na wagombea waliopita bila kupingwa. Hii siyo mara kwanza, uchaguzi wa vyama vingi ulianza tangu 1995, tukawa nao mwaka 2000, 2005, 2010, 2015, wagombea katika nyadhifa za ubunge, udiwani wamekuwa wakipita bila kupingwa.

“Faida ambayo chama tawala inapata ni kwamba kinakuwa kimetekeleza sera na ilani, chama cha upinzani kinakosa ‘advantage’ (faida) hiyo kwa sababu kinakuwa hakijatekeleza ilani, sababu hakikushinda uchaguzi," alisema.

Hata hivyo, msomi huyo alisema ni vigumu kwa mtu ambaye ni mpya kupita bila kupingwa ingawa wakati mwingine inatokea kama wananchi wamechoka na mbunge aliyekuwa madarakani.

“Mfano, rais akipita kwenye jimbo la mbunge wa upinzani akikuambia tunabadilisha matumizi ya fedha za fungu fulani, ujue ni serikali iliyopo madarakani,” alisema.

Profesa Makulilo alisema ifahamike kuwa zipo sababu mbalimbali za mtu kupita bila kupingwa ambazo ni pamoja na kutotimiza masharti ya sheria ambazo ukishindwa kuzizingatia, mpinzani wako anatangazwa mshindi.

Alisema sheria zilizopo zimeweka fursa kwa watu kukata rufani na kuweka mapingamizi ili NEC kwa kutumia kanuni na sheria, mtu akileta ushahidi wake ukaonekana ni sahihi, basi uamuzi unatenguliwa.

Kuhusu malalamiko ya baadhi ya wagombea kuporwa fomu, Profesa Makulilo alisema kuwa kwenye uchaguzi, kuna mambo mengi na mnapokuwa mnashindana mtu anaweza akaamua kusema lolote.

Alishauri wenye malalamiko ya aina hiyo kuyapeleka kwenye vyombo husika ambavyo vitachuja na kutoa uamuzi na kama hawajaridhika na uamuzi wa NEC, kuna fursa ya kwenda mahakamani.

“Watu wasizue taharuki, wafuate sheria, ukishindwa NEC unaona umeonewa, unakwenda mahakamani mpaka haki inapatikana,” alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Richard Mbunda, alisema alipata fursa ya kumsikiliza Msimamzi wa Uchaguzi Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.

Alisema msimamizi huyo alieleza kuwa, kutokana na utaratibu waliopewa na NEC walijitahidi kuwapelekea wagombea walioteuliwa na vyama vyao watu wa kuwakagua ujazaji wa fomu kabla ya siku ya mwisho ambayo ni juzi.

“Hii ina maana katika mazingira kama haya, mtu hawezi kuja na fomu kwamba haijajazwa vizuri au kuwa na matatizo au upungufu.

“Kama huu ndiyo utaratibu uliotolewa na NEC, basi ulikuwa ni mzuri na ungeepusha malalamiko ya watu kuiangalia NEC kama chombo kinachotumika na chama tawala, hii ni namna ambavyo NEC inatakiwa kujitathmini.

“Lakini, wakati mwingine unaweza kukuta wasimamizi wa uchaguzi wanafanya mambo wakidhani kwamba wanakisaidia chama tawala kumbe wanakipaka matope na kuipaka matope serikali katika mchakato ambao ulitakiwa uwe huru na wa haki na CCM ingeshinda bila kelele zozote," alisema.

Dk. Mbunda alisema kuenguliwa kwa wagombea wa upinzani ni jambo linalofikirisha na NEC inatakiwa kujitathmini namna ambavyo inaendesha mambo yake.

Jana, NEC ilipiga marufuku vitendo vya baadhi ya wagombea kujitangaza kupita bila kupingwa, ikifafanua kuwa ni tabia mbaya kwa kuwa inachochea vurugu.

Imeandikwa na Romana Mallya na Thobias Mwanakatwe
 
Hapa aliyeongea point za msingi ni mzee mpangala na dr.mbunda huyo muha makulilo wa hapo udom naona anatafuta uteuzi.
 
CCM ni moja ya vyama vya kisiasa vilivyodumaa. Kwa miaka yote hii tangu kizaliwe mwaka 1977, bado kinaendesha siasa za kizamani na zilizopitwa na wakati. Hongera nyingi ziwafikie Profesa Gaudence Mpangala wa RUCU na Dr. Richard Mbunda wa Udsm.

Mnastahili kuwa Wanazuoni tofauti na wale wasomi njaa wanaopindisha ukweli kwa makusudi, ili tu kulinda matumbo yao.
 
CCM ni moja ya vyama vya kisiasa vilivyodumaa. Kwa miaka yote hii tangu kizaliwe mwaka 1977, bado kinaendesha siasa za kizamani na zilizopitwa na wakati. Hongera nyingi ziwafikie Profesa Gaudence Mpangala wa RUCU na Dr. Richard Mbunda wa Udsm.

Mnastahili kuwa Wanazuoni tofauti na wale wasomi njaa wanaopindisha ukweli kwa makusudi, ili tu kulinda matumbo yao.
Pamoja na siasa za zamani inazoendesha bado vyama vya upinzani vimeshindwa kuitoa
 
Back
Top Bottom