Mapinduzi, historia ya zanzibar na vuguvugu la sasa

WaMzizima

Senior Member
Jun 25, 2009
152
41
Baada ya viongozi, asasi na sisi wananchi wa kawaida kuendelea kuzozana na kupigiana kelele huku wazenj wengi wakiendelea kulaumu kila kitu kuanzia umaskini wao hadi kuporomoka kwa maadili kwenye muungano (kitu ambacho si kweli) ni wazi waamue kuitisha hiyo kura ya maoni haraka iwezekanavyo ila kumaliza mzizi huu wa fitina. Kufanya hivyo hawahitaji serikali ya muungano kuamua, maamuzi hayo yamo ndani ya uwezo wao wa kikatiba hivyo bora wafanye hivyo mapema. Ila hapa ningependa kuweka tena hii mada hapo chini ya uchambuzi wa historia ya Zanzibar ilipotoka hadi tulipo leo ili watu wengine ambao hawajui historia ya visiwa hivi wapate uelewa kabla ya kuamua hitma ya muelekeo na mustakabali mzima wa visiwa vya Unguja na Pemba.

Historia hupenda kujirudia haya mambo yamechanganya toka wakati wa mkoloni, mimi ningependa kuangalia zaidi historia ya Zanzibar kuanzia tuseme about 1960, wakati waingereza wakijitayarisha kuwaachia wazalendo kujiendesha. Kama ilivyokuwa Tanganyika kipindi hiki Znz wakafanya uchaguzi, tofauti na Tanganyika ambako Tanu walishinda kwa kura nyingi na Nyerere ku​wa waziri mkuu mambo visiwani ilikuwa tofauti.


CHAGUZI ZA MWANZO


Uchaguzi wa mwanzo Januari 1961 ZNP na ASP kila kimoja kilipata viti 11 ingawa ASP walidai kuwa wameibiwa kura (Kumbuka CUF 95,00,05??), hivyo wakoloni wakatayarisha uchaguzi mwingine Juni mwaka huo na kuongeza viti kuwa 23. ZNP kwa kuungana na ZPPP wakapata viti 13 na ASP ikapata 10 ingawa walishinda kura nyingi. Fujo zikaibuka watu wakauwawa (Pemba 00??) ASP wakadai faulu ya wizi wa kura na vilevile kudai kuwa mipaka ya majimbo ya uchaguzi yalipendelea ZNP, kwamba majimbo yao ASP yalifanywa kuwa makubwa kwa makusudi.


Baada ya kutwaa madaraka ZNP/ZPPP ikapiga marufuku baadhi ya vikundi, na kujaza serikalini watu wao na kufukuza wale ambao iliona wanalalia upande wa ASP.(Kumbuka CCM Znz baada ya uchaguzi 00,05 na madai ya Kuonewa wanachama wao toka CUF??)


Kabla ya Uhuru uchaguzi mwingine ukafanyika tena 1963 na kama 1961 mambo yakawa vilevile majimbo yakaongezwa na kuwa 31, ingawa mseto wa ASP ya Karume na Umma Party cha Babu walishinda 54% ya kura walipata viti 13 na ZNP/ZPPP kuchukua vilivyobaki. ZNP chini ya Shamte wakaongeza ubaguzi wao serikalini na mashirika ya umma (CCM baada ya 95,00??) wakawafukuza kazi wanajeshi na polisi wenye asili ya bara, wakapiga marufuku Umma party na Babu akakimbilia Dar.


Uhuru kamili toka kwa waingereza ulipotangazwa mnamo 10 disemba, 1963 ZNP/ZPPP wakawa wameshika hatamu kwenye usultani wa kikatiba (constitutional monarchy) huku sultani Jamshid akiwa kiongozi wa nchi na Shamte waziri mkuu.


INGIA JOHN OKELLO


Huyu bwana hatajwi sana siku hizi kwenye siasa za Zanzibar, lakini mzaliwa huyu wa Uganda ndio alikuwa kinara wa mapinduzi ya Januari 64. Bado wasomi wa historia wanazozana kuhusu Karume na Babu kama walihusikaje kwenye mapinduzi haya...Ingawa Babu amekiri mara kadhaa kutojua kwake kwa haya mapinduzi yaliyochochewa na Okello. Inadaiwa pia kuwa Okello alimpeleka Karume Dar ili awe salama wakati huo ingawa ni wazi Karume alikuwa na shughuli nyingine tofauti Bara kipindi hicho.


Kipindi hicho kulikuwa na tetesi ya mapinduzi ambayo Babu, Hanga na kwa kushirikiana na Kambona walikuwa wanaanda kuipindua serikali , hivyo basi Okello akawawahi kwa kushirikiana na mgambo na vijana wa ASP youth league na polisi waliofukuzwa kazi waliweza kuteka vituo vikuu vyo polisi mji mkongwe na kuteka redio na uwanja wa ndege. Jamshid, Shamte na baraza la mawaziri walifanikiwa kutoroka Znz kwa kutumia meli ya sultani Seyyid Khaliffa kwenda Dar na baadae Sultani alienda Portsmouth, UK alipo hadi leo...sijui kwa nini hakwenda kwa babu zake Oman mi sijui sababu alikimbilia kwa wakoloni zake wa mwanzo. Anyway Okello akaanza vitisho redioni na kuamrisha vikosi vyake kuwakamata waarabu na wahindi visiwani, kukawa na umwagaji mkubwa wa damu ambao hadi leo hatujui idadi kamili, ubakaji, wizi na uharibifu mkubwa wa mali.


Angalia video hii ya kasheshe kipindi hicho


Arab Massacre in Zanzibar - YouTube




Hii video ni sehemu ya sinema ya kiitaliani inaitwa Africa Addio. Kwa kweli kuna ubishi wa idadi kamili ya vifo kuanzia 1,000 hadi wengine wanadai 20,000 SMZ haijawahi kutoa tamko wala kuunda tume huru kuchunguza mauaji haya ya mapinduzi.


Cha msingi tunajua kilichotokea baada ya mapinduzi Karume akarudi na kuwa Rais, likaundwa baraza la mapinduzi Babu akawa waziri wa mambo ya nje Hanga makamu wa rais. Muda si mrefu Okello akazuiwa kuingia Znz wakati anarudi safari toka Dar mwishowe alirudi uganda ambako inaaminika Idi Amin aliimmaliza 1972, baada ya yeye Okello kudaiwa kusema kuwa sasa Uganda ina field marshall wawili, yaani yeye na Amin.


Hata hivyo kama haya mapinduzi ambayo SMZ inadai ni matakatifu mbona nabii wake mkuu yaani Okello hawamuenzi? yaani Znz vijana wengi siku hizi hawajui Okello ni nani, na wala hawajui ushirika wake katika mapinduzi yao. Hakuna kumbukumbu (barabara au square) wala hatajwi mashuleni kwao.


Je Okello ni Shujaa (Hero) au Haramia (Villain)? only history will tell...


MUUNGANO BAADA YA MAPINDUZI


Ingawa wengi naona humu wanadai kuwa muungano uliletwa kuzuia ujio tena wa Sultani, historia inaonyesha tofauti. Mapinduzi kwa kiasi kikubwa yaliungwa mkono na weusi wengi Znz hasa unguja ikumbukwe wakati huo idadi ya watu znz ilikuwa kama 300,000 huku weusi na washirazi kama 230,000 waarabu 50,000 na wahindi/waasia 20,000. Ingawa idadi kubwa tu ya watu walikuwa ni mchanganyiko, lakini weusi walikuwa wanatengwa ZNP hawakuwa na waziri mweusi kwenye baraza lao na vilevile kazi nyingi za juu serikalini walipewa waarabu na wahindi. Weusi kwenye sekondari hawakuzidi 12%...Hivyo basi sera za mwanzo za ASP na Umma za kuongeza nafasi za kazi, shule pamoja na kujengea weusi makazi bora pamoja na kuwaongezea huduma za afya ziliwapa wapenzi wengi.


Tatizo likawa kama kwenye serikali nyingine za kiafrika upinzani ukapigwa marufuku, uhuru binafsi na wa kujichanganya ukawa duni, uhuru wa vyombo vya habari nao vilevile ikawa hakuna.


Ingawa Karume alikuwa popular lakini bado alikuwa na wasiwasi na vuguvugu la Umma party na sera zao za mlengo wa shoto(ukomunisti), na hii ndio inaaminika kuwa sababu kubwa ya kuungana na Tanganyika na si tishio la kurudi sultani. Wengine wanasema baada ya mkutano kati ya Obote, Kenyatta, Karume na Nyerere kuhusu kuunda Shirikisho la afrika mashariki kuvunjika, basi Nyerere na Karume wakaamua kuunda muungano wao bila kujali Kenya na Uganda.


Ukweli halisi hatuwezi kujua maana wote ni marehemu.


UAMSHO NA HARAKATI ZA SASA??


Tatizo kwenye vuguvugu la sasa ni jee hawa wanaitaka Zanzibar ipi? ile baada ya Uhuru chini ya sultani na ya kibwanyenye au ya Karume kabla ya muungano ya mrengo wa kushoto na ukandamizwaji au kuachana na hizo na kujaribu mpya kabisa. Kwa wafuatiliaji wa siasa za Zanzibar tangu awali utaona kuanzia wakati wa ZNP na ASP hadi sasa kati ya CUF na CCM siku zote visiwa hivi vina siasa kali za mfarakano mkubwa...kwamba CUF ndio ZPPP ya leo ni suala la kuwaachia wenyewe wajadili, lakini ni wazi kuwa Pemba ndio ngome kuu ya CUF kama ilivyokuwa kwa ZPPP. Na CUF vilevile inadai Zanzibar huru ingawa inaendelea kufaidi matunda ya muungano.


Uamsho wanapiga tu makelele na ni wazi wanafadhiliwa na wazito toka Oman, ila ni vyema wajue kuwa waarabu si wafadhili wazuri siku zote, angalia kama wangekuwa wafadhili wazuri wasingeruhusu waarabu/waislamu wenzao ambao hawana mafuta kuwa maskini wa kutupwa na kuteswa (i.e Yemen, Palestine, Somalia, Mauritania n.k.)


Vilevile serikali zao hivi sasa haziko imara, pili ujuzi wao wa kuendesha NGO/ asasi binafsi si mzuri na sera za wazi hawana zaidi ya kufadhili makundi ya kigaidi. Mi nafikiri mwisho Uamsho itabadilika na kuwa chama kipya cha siasa Znz na kuwa chama cha upinzani, ambacho kitakuwa kitu kizuri maana hivi sasa Znz hawana upinzani rasmi baada ya CUF kuungana na CCM kwenye SMZ, ingawa muungano huo wa CUF/CCM utadumu muda gani hatujui.


Tusubiri hiyo kura ya maoni na baada ya hapo tuone kama Znz itaweza kukwepa siasa za kuumizana na kupigana bakora, ambazo hazijalishi status ya Serikali kuanzia wakati wapo huru (61,63,64) au ndani ya muungano (72 mauaji ya karume, 95,00 mauaji pemba)...Kumbuka historia hupenda kujirudia. Tuombe liwalo lolote liwe la kheri maana Znz na Tanganyika ni ndugu na kheri visiwani ni kheri bara, aidha kwenye muungano au nje ukweli huu wa udugu utakuwepo tu siku zote.


Karl Marx alisema "History repeats itself, first as tragedy, second as farce"




Yetu macho


Nawakilisha
 
Back
Top Bottom