Mapambano dhidi ya Covid-19 Tanzania na kwingineko Afrika: Watafiti na wanasayansi wetu mko wapi na munasemaje?

Dr Mathew Togolani Mndeme

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
201
808
Ninaandika uchambuzi huu kwa dhumuni moja kubwa: Kutimiza jukumu la kitaalamu linalowahitaji wanatafiti/ wanasayansi/ wasomi kutoa elimu kwenye jamii na kushiriki kujadili mambo magumu na mepesi yanayoikabili kwa mtazamo wa kisayansi.

Katika vita vya kijeshi dhidi ya aadui wa nchi, tunatanguliza makamanda na wanajeshi wetu mbele na sisi wananchi wote kwa ujumla, chini ya maelekezo na dira ya viongozi wetu, tunashirikiana nao kwa hali na mali kutafuta ushindi na kupunguza madhara ya vita kwenye maisha na uchumi wetu. Ili viongozi (hasa Amiri Jeshi Mkuu na wasaidizi wake) watoe maelekezo na dira zenye kupelekea ushindi na kutuacha salama, ni lazima wawasikilize sana wanajeshi walioko uwanja wa vita (field) na wataalamu wa kupanga mikakati ya kijeshi (military strategists) maana ndio wanaelewa vema aina ya adui wanayepambana naye na uwezo wake.

Kwa minajili hiyo, ninaamini kwamba, katika mazingira ya vita ya kisayansi yanayoikumba dunia kama ilivyo sasa dhidi ya adui Covid-19, watafiti na wanasayansi wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kuongoza mapambano na kutoa tafakuri zinazoweza kutumiwa na viongozi/wanasiasa katika kufanya maamuzi na kuchukua hatua ambazo mwisho wa siku zitaonesha TIJA na kutuletea ushindi. Wanasayansi na watafiti wanapoamua kunyamaza kimya na kuwaachia viongozi/wanasiasa jukumu hili zito, ni sawasawa na makamanda wa jeshi na “military strategists” kunyamaza kimya na kusubiri maelekezo ambayo kwa sehemu kubwa yanaweza yasizingatie mikakati ya kijeshi, uwezo wa adui, na hali ilivyo katika uwanja wa vita.

Katika kufuatilia na kujifunza yanayoendelea kwenye vita dhidi ya Covid-19 hapa kwetu Tanzania na kwingineko Afrika kusini mwa jangwa la Sahara, jambo moja kubwa liko dhahiri. Sisi kama jamii ya kiafrika kwa ujumla wetu, tumekua na hofu na taharuki kubwa juu ya uhatari wa Covid-19. Sina nia ya kupuuza msingi na uhalali wa kutaharuki huko. La hasha. Hata mimi nadhani kuna saa ninapata hofu hasa kwa sababu ninafuatilia kwa karibu usiku na mchana machapisho na data za janga hili na a kujaribu kuchakata ili kupata uelewa wa kisayansi

Ninatambua vema kwamba inatisha sana tunaposikia idadi ya watu walioathirika na kufariki katika nchi nchingine. Hali hii inatufanya tujione tuko kwenye hatari zaidi hasa kutokana na changamoto nyingi zinazotukabili huku tukiwa na uwezo mdogo kitaalamu, miundombinu, vifaa, teknolojia na rasilimali nyingine. Hata hivyo, taharuki hii ina madhara makubwa kwetu kuliko faida. Haitusaidii hata kidogo. Kubwa zaidi ni ukweli kwamba taharuki imeaathiri uwezo wetu wa kuwa na fikra huru (independent thinking) na kufanya maamuzi kisayansi kwa muktadha wa mazingira na hali yetu ya maisha (making decisions based on scientific evidence in the context of environment). Hili linadhirika zaidi na namna tunavyokabiliana na mlipuko hasa kwa kuiga au kulazimisha serikali zetu kuiga njia zinazotumiwa na mataifa ya magharibi bila kuziweka kwenye muktadha wa maisha na mazingira yetu.

Kwa mfano, kila anayerejea uhatari wa Covid-19 na hivyo kupendekeza au kuitaka serikali kuchukua hatua zaidi, anarejea hali iliyoko Italia, Hispania au hata Marekani kama kielelezo cha uhatari na kwamba “tusipokua makini”, hali yetu itakua mbaya kuliko yao. Nimesikiliza watu wengi na kusoma maandishi mengi ya watu wanaoshangaa nchi za kiafrika ambazo hadi sasa hazijafunga mipaka watu wasiingie wala kutoka nchini; hazijasimamisha usafiri wa umma kama nchi zingine; hazijatangaza karantini ya nchi nzima itakayowazuia watu kutoka ndani ya nyumba zao hadi hali itakapokua salama; nk. Mtazamo huu umeongezewa uzito baada ya kauli iliyotolewa wiki jana na Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyozitahadharisha nchi za kiafrika kujiandaa kukabiliana na madhara makubwa zaidi ya Covid-19. Tahadhari hii ilitolewa kwa msingi kwamba mifumo yetu ya afya (Health systems) ni mibovu na dhaifu sana na haina uwezo wa kukabiliana na majanga makubwa. Ila nini usahihi wa hofu hii na tahadhari tunayopewa?

Ninapoweka hofu ya Covid-19 na mijadala inayoendelea katika minzania ya tafakuri tunduizi, ninapata maswali kadhaa:
  • Jamiii yetu ina elimu ya kutosha kwa kiasi gani kuhusu maambukizi ya Covid-19?
  • Jamii ina elimu msingi ya kisayansi kwa kiasi gani kuhusu magonjwa ya mlipuko kwa ujumla wake na namna ya kukabiliana nayo?
  • Wanasayansi na watafiti wetu wanasemaje kwenye hili? Kwa kuzingatia taaluma na tafiti zao, wana mawazo gani tofauti na haya ya jumla na ya mikumbo yaliyotamalaki kwenye jamii?
  • Serikali na jamii yetu, imetoa nafasi na uhuru kwa kiasi gani kwa wanasayansi na watafiti wetu kujadili mambo yanayotukabilia bila hofu ya kukosea au kukosolewa?
  • Nje ya mifumo ramsi ya kutoa elimu, sisi kama nchi, tumetoa uhuru na nafasi kiasi gani kwa wanasayansi na watafiti wetu kutoa elimu kwenye jamii ili kujenga jamii yenye mwanga na uelewa mpana wa dunia tunayoishi kwa sasa?
Nikitafakari maswali haya ninapata nadharia kadhaa za harakaharaka zinazohitaji uchambuzi wa kina na tafakuri pana zaidi. Nitaje chache:
  • Majadala wa tataizo la Covid-19 umetawaliwa na watu wasio na uelewa wala utaalamu wa kutosha kuhusu magonjwa wala sayansi ya kukabiliana na milipuko. Wengine hawana kabisa lakini ndio wamekua na sauti kubwa kuliko wenye utaalamu.
  • Wataalamu wetu (wanasayansi na watafiti) huenda wameamua kunyamaza au huenda hawajui kwamba wamenyamaza…huenda kwa sababu wanajiona hawana nafasi kwenye vita hii; au jamii haioneshi kuwahitaji kwenye vita vya aina hii; au siokawaida mawazo na elimu zao kutumika.
  • Mlipuko wa Covid-19 umetuweka wazi kwamba sisi ni nchi ya watu ambao haiongozwi na elimu au sayansi (we are not a knowledge-based society, and we might be far from be one of the kinds). Iwapo watafiti na wanasayansi wetu wanaacha mjadala wa kisayansi kutawaliwa na yeyote na maisha yakaendelea tu, basi ni wazi elimu sio kipeumbele kutuongoza katika kufikiria, kuchambua, kuchanganua, kuchakata na kutafuta majibu ya maswali magumu tuliyonayo au majawabu kwa matatizo yanayotukali.
  • Tafakuri namba 2 na 3 hapo juu zinaweza kupimwa kwa kutazama vyombo vyetu vya habari ambavyo ni mhimili wa 4 wa dola. Tutazame wamekua wakiwahoji kina nani tangu tatizo hili lianze? Wanapohoji huwa wanahoji nini hasa? Wanaohoji wana uwezo gani wa kuhoji na kuuliza maswali magumu na yenye tija? Wanapowasikiliza viongozi na wataalamu wakitoa maelezo, maelekezo na miongozo, vyombo vyetu vya habari vinauliza maswali gani?
  • Kuna uwezekano mkubwa wanasayansi na watafiti wetu hawaoni ni kwa namna gani wanaweza kutimiza wajibu wao wa kushiriki mijadala iliyoko kwenye jamii, kujibu maswali ya kisayansi, na kutoa elimu bila kuonekana wanangiliana na mamlaka za kiserikali.
Ninafarijika kwamba nchi yetu ina wanasayansi na watafiti wengi waliobobea kwenye maeneo mengi yenye changamoto kwenye jamii. Tunawahitaji wote kweney kupambana na Covid-19.

Mathalani, ninaona hili la Covid-19 limefanywa kama ni jambo linalowahusu madaktari na manesi tu. Tunadhani wao pekee ndio wana maelezo sahihi na majibu ya maswali yote kwenye kukabiliana na mlipuko. Mtizamo huu sio sahihi na tunawaonea bure.

Katika kubiliana na Covid-19 tunahitaji elimu, uchambuzi, na tafakuri za:
  • Wataalamu wa wagonjwa (epidemiologists) watusaidie kuelewa Covid-19 ni nini, tunakabiliana nayo vipi, kwa nini, na tunashiriki vipi. Watueleze hatua sahihi za kisayansi za kukabiliana na mlipuko hata kama umma kwa mtizamo wao wanaona hazifai.
  • Wataalamu wa takwimu (statisticians and biostatisticians) wachambue data zilizopo na watupe tafsiri yake.
  • Wataalamu wa uchumi (economists) watueleze nini mweleko wa hali tuliyonayo na madhara au faida za kiuchumi za hatua tunazochukua kwa mtu mmoja mmoja na uchumi wa nchi kwa ujumla. Pia watuambie tunaweza kufanya nini kupunguza makali ya athari hizo.
  • Wataalamu wa hesabu (mathematicians) watusaidie na wasaidiane na wataaamu wengine kuchakata data na kutoa utabiri wa kitalaamu wa hali tuliyonayo.
  • Walaamu wa afya ya jamii (public health specialists) watoe elimu za kujikinga na magonjwa, usafi, na njia sahihi tunazoweza kuzitumia kulingana na mazingira yetu.
  • Wataalamu wa saikolojia na sosholojia kutoa tafsiri na elimu juu za kukabiliana na msongo wa mawazo, hofu, wasiwasi, taharuki, unyanyapaa, kubadili tabia, nk.
  • Wataalamu wa mifumo ya digitali watusidie kubuni au kutuelekeza kwenye mifumo ya kukabiliana na milipuko na watupe elimu ya kutumia mifumo hii kurahisisha udhibiti.
  • Watalaamu wa uhandhisi waje na mawazo, mbinu na mikakati ya kujenga miundombinu bora ya kusaidia sasa na baadaye kukabiliana na milipuko.
  • Walaamu wa eleimu wasaidie namna nzuri ya kutoa elimu kwa jamii kulingana na tofauti zetu za kielimu, mazingira, uchimi, rika, nk
  • Orodha ni dhefu.
Nimalizie makala yangu kwa kuuliza tena swali: Watafiti na wanasayansi wetu muko wapi na munasemaje na munatushauri nini katika vita ya Covid-19?

Imeandikwa na Mathew Mndeme (mmtogolani@gmail.com)
  • Mwanasayansi/mtafiti wa mifumo ya digitali katika ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa
  • Mwanafunzi wa uwasilishaji wa tafiti za kisayansi katika jamii (Scholarly/ Scientific Communication)
 
Hongera mkuu, uchambuzi makini sana na umemalizia vizuri kuwa nini kifanyike au kuboreshwa. Ukweli elimu bado inahitajika sana kwa kuhusisha wadau mbalimbali kama ulivyoainisha. Hofu ipo lakini maangaiko ya maisha yanafanya watu wengi wasiichukulie corona serious.
 
Mathew Togolani Mndeme
Hii thread yako ni fikirishi na inatoa elimu na kuuliza maswali ambayo yana umuhimu mkubwa sasa kuliko wakati mwingine wowote.

Ili kufahamu ni kwa kiasi gani jamii ya Kitanzania inatambua wanasayansi na kuzingatia kazi zao za kitafiti, tuangalie upande mwingine wa shilingi; yaani asilimia ya Watanzania wanaoamini kwa dhati katika ushirikina, matendo ya kimiujiza na mambo mengine ambayo hayana ushahidi wa kisayansi.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya Pew mwaka 2010, zaidi ya 90% ya Watanzania walithibitika ni waumini katika ushirikina na katika imani zingine potofu:
witchcraftbelieffigures.jpg

Chanzo: 93% believe in #Witchcraft in #Tanzania
(Kiujumla, kiasi cha imani katika ushirikina katika nchi kinaendana na hali ya ubora wa elimu inayotolewa).

Kutokana na hizi takwimu, mambo mawili yanajitokeza. Kwanza, ni ushahidi uliopo wa jinsi Watanzania wanavyochangamkia ufumbuzi wa mkato mkato wa matatizo unaodaiwa kutolewa kimiujiza kama "kikombe cha Babu" na huduma mbalimbali za "manabii" na "mitume" wa siku hizi.

Pili, kwa vile lengo la wanasiasa wetu ni kuungwa mkono na kupata ufuasi, haishangazi katika kipindi hiki cha maambukizi ya koronavirus wanasisitiza zaidi ibada na maombi kama njia ya kukabiliana na huu ugonjwa kuliko kuzingatia maelekezo ya kisayansi yanayotolewa na wataalam wa afya.

Katika kujibu swali lako, wanasayansi na watafiti wetu wana nafasi kiduchu katika mapambano dhidi ya coronavirus hapa nchini.
 
Back
Top Bottom