Maoni Yangu: Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni Chombo Huru Kiutendaji. Ninayo Maajabu Nane (8) ya Tume ambayo Hayazungumzwi

Lugumgya

JF-Expert Member
Dec 10, 2019
629
1,997
Tukiwa tunaelekea katika Mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2020, kumekuwa na mtazamamo wa muda mrefu kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania si chombo huru, na kwamba inafanya kazi kwa upendeleo na mnufaika mkubwa wa upendeleo huo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mtazamo huo unaweza kuwa na ukweli kulingana na ukweli wa kweli kwamba, kila binadamu amepewa karama yake ya kuchambua na kuangalia mambo kwa upekee wake. Ninachoona mimi si lazima Polepole, Mnyika au Sakaya akione sawa na mtazamo wangu na kinyume chake.

Mimi kama mtanzania, nimeona nitoe maoni yangu juu ya chombo hiki ambacho kimsingi ndiyo kielelezo cha Demokrasia nchini. Maoni nitakayo yatoa ni kwa uelewa wangu, ambapo naamini kutokana na michango yenu naweza kujifunza na kufungamana na wale, wanye maono kuwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi si chombo huru. Kwa sasa mimi naamini kuwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ni chombo huru.

*Tume ya Taifa ya Uchaguzi nini?*

NEC ni chombo huru kilichoanzishwa chini ya ibara ya 74 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. Inao Wajumbe 7 ambao huteuliwa na Rais, Mkurugenzi wa Tume, ambaye huteuliwa na Rais kwa mujibu wa Ibara ya 74 (7) na Sekretariati ambao ni Watumishi wa Tume. Kazi ya Sekretarieti ni kuratibu na kusimamia shughuli zote za utendaji wa Tume za kila siku.

*Majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi*

Kuhusu Majukumu ya Tume ya Tume ya Uchaguzi naomba tusome Ibara ya 74 (6) na 78 (1) ya Katiba ya JMT, Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, sura 292 na kifungu cha 4C cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura 343.

*Muhtasari wa Mfumo wa Siasa Tanzania*

Itakumbukwa kuwa kabla ya kupata uhuru mwaka 1961,Tanganyika (Tanzania Bara) ilikuwa na Mfumo wa Vyama vingi vya Siasa, ambapo vyama vitatu ambavyo ni Tanganyika African National Union (TANU),United Tanganyika Party (UTP) na African National Congress (ANC) vilishiriki kwenye chaguzi.

Kwa upande wa Zanzibar kulikuwa na vyama vya Afro Shiraz Party (ASP), Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP), UMMA Party na Zanzibar Nationalist Party (ZNP) ambavyo vilishirki kwenye chaguzi kabla ya mwaka 1964.

Mfumo wa vyama vingi ulifutwa rasmi mwaka 1965 na kubaki na mfumo wa chama kimoja baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964, ambapo ni vyama viwili tu vilibaki. Vyama hivyo ni Chama cha TANU kwa upande wa Tanzania Bara na chama cha ASP kwa upande wa Tanzania Visiwani, ambavyo viliamua kuungana Mwaka 1977 na kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mnamo mwaka 1992 Mfumo wa Vyama Vingi ulirejeshwa tena chini, na ndipo tarehe 13, Januari 1993 NEC ikaanzishwa. Tangu kuanzishwa kwake, imesimamia Chaguzi kuu tano zilizofanyika mwaka 1995,2000, 2005,2010 na 2015 zikihusisha vyama vingi vya Siasa. Itakumbukwa kuwa, Vyama hivyo vinasajiliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, kupitia Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura 258. Mpaka Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 jumla ya Vyama 22 vya siasa vilikuwa vimepata usajiliwa kudumu.

*Mfumo wa Uchaguzi Tanzania*

Katiba ya nchi inatoa haki kwa kila mwananchi kushiriki katika shughuli za utawala za nchi kwa kuchagua au kuchaguliwa (Ibara 21 ya Katiba ya JMT, 1977). Kila Mtanzania aliye na umri wa miaka 18 na kuendelea ana haki ya kupiga kura kuchagua kiongozi anayempenda, regardless of Chama.Ukimpenda Mbowe, chagua, Ukimpenda JPM, Chagua, Ukimpenda Rungwe, Chagua, Ukimpenda Paschal Mayalla, Chagua, ukimpenda Dr. Shika, Chagua, lakini kama wamepitishwa kugombea nafasi na vyama vyao vya siasa.

Kwa mujibu wa vifungu vya 35 F(8) na 80 (1) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 Tanzania inatumia mfumo wa Uchaguzi ambao mgombea anayepata kura nyingi halali kuliko mgombea mwingine ndiye hutangazwa kuwa mshindi (First-Past-the Post).

Tatizo huanzia hapa First –Past-the Post, matokeo yakitoka tu, NEC inaanza kuoneka ni Wakala wa Chama fulani. Hata ile michakato shirikishi yote iliyofanyika kwa kushirikisha na vyama vyote husaulika na kuonekana kwamba NEC inapendelea Wagombea wa chama fulani na inatangaza kwa shinikizo.

*Je, ni kweli NEC inafanya kazi kwa shinikizo na kwamba si chombo huru kiutendaji kama inavyosemwa na baadhi ya wadau wa Uchaguzi?*

Kwa maoni yangu NEC ni chombo huru ambacho hakifanyi kazi kwa shinikizo bali kinatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria. Sababu zangu ni hizi hapa chini, fuatana nami;

1. *Uanzishwaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi* Kimsingi NEC ni idara huru inayojitegemea. Hii ni kwa mujibu wa ibara 74 (7) ya Katiba ya JMT, 1977. Kadhalika ibara ya 74 (11) ya Katiba ya JMT, inaeleza kuwa katika kutekeleza majukumu yake ya kikatiba, NEC haitalazimika kupokea maelekezo au amri kutoka kwa mtu yeyote au Idara yoyote ya Serikali au kufuata maoni ya chama chochote cha siasa.

Katiba tayari inaipa NEC makucha ya kutekeleza majukumu yake bila kuingiliwa, na kama inatokea Viongozi wa Tume kwa namna moja ama nyingine wanatekeleza majukumu yao kinyume na matakwa ya Katiba huo ni ukiukwaji mkubwa wa Katiba ya nchi

Kikwazo pekee ninachokiona katika Katiba ni kutoruhusu makosa ya kimaamzi ya chombo hiki huru kuchunguzwa katika mahakama yoyote -Ibara 74 (12) ya Katiba ya JMT,1977. Lakini kwa ujumla wake kama Viongozi watatekeleza wajibu wao kwa weledi, NEC ni chombo huru kabisa.

2.*Uandikishaji na Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura*. Jukumu la kuandikisha na kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga ni la Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Hii ni kwa mujibu wa Ibara ya ya 74 (6) na 78 (1) ya Katiba ya JMT. Aidha Kifungu cha 15 (5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343, kinaitaka NEC kufanya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara 2 kati ya Uchaguzi mmoja na Uchaguzi mwingine. Mfano Katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 NEC iliandikisha jumla ya Wapiga Kura 23, 161,440 (Bara 22,658, 247, Visiwani 503,193)-(Taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, 2016).

Wapiga kura wote walioandikishwa na Tume ilikuwa ni kwa ajili ya Vyama vyote vinavyoshiriki Uchaguzi. Tume haiandikishi wanachama wa chama chochote cha Siasa, bali Tume inaandikisha Wapiga Kura ambao ni Wanachama au si wanachama wa Vyama vya Siasa. Lakini katika Uandikishaji huu Tume haiandikishi wapiga kura kwa kufata itikadi za kivyama, ni Uandikishaji huru.

Wapiga kura hawa hawa walioadikishwa na Tume ndo huwapigia kura akina Joseph Mbilinyi, Joseph Kasheku “Msukuma”, Tundu Lissu, Job Ndugai, Khangi Lugora na Zitto Kabwe. Na mchakato wa Uandikishaji hufanyika Kweupe kabisa.CCM kwa kuwa madarakani haina uwezo wala nguvu kisheria za kuiambia NEC kwamba usimuandikishe Mbowe, wala Lipumba kwa kuwa wanajulikana kuwa ni wafuasi na wenyeviti wa vyama pinzani. Never!

Chagamoto ni kwamba Tume imekuwa haifanyi Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura mara mbili kati ya Uchaguzi mmoja na mwingine. Lakini jambo hili halina dhumuni la kuathiri au kupendelea chama chochote Cha Siasa.

3. *Ugawaji wa Majimbo ya Uchaguzi*. Kwa mujibu wa Ibara ya 75(4) ya Katiba ya JMT, 1977 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina Jukumu la Kuchunguza na kuigawa JMT katika majimbo ya Uchaguzi. Katika Uchaguzi wa mwaka 2015 kwa mfano, Tume ilianzisha majimbo Mapya 25, ambapo jumla ya majimbo ya Uchaguzi yalifikia 264 (bara 214, visiwani 50).

Katika majimbo haya hakuna jimbo lilioanzishwa maalumu kwa ajili ya chama fulani cha siasa. Majimbo yalianzishwa kwa ajili ya Vyama Vyote vya Siasa na kwa ajili ya ushindani huru wa kisiasa.

Kuna jambo hapa kwamba, Tume ikiona kuwa CCM inaenda kushindwa, huja na mkakati wa Kuanzisha Jimbo jipya ili kufungua milango kwa CCM kuwa na Wabunge wengi Bungeni. Sasa sijui Siku kukiwa na hisia kuwa CCM inaenda kushindwa kitaifa itabidi NEC ianzishe nchi nyingine ndani ya nchi moja? Illogical!

Katika kuongeza majimbo Tume haijiongezei tu; angalia katiba ya JMT 1977, Ibara ya 75 (1), vigezo vingine ni Wastani wa Idadi ya Watu, Ukubwa wa Eneo wa Jimbo husika, Jimbo lisiwe ndani ya Wilaya/Halmashauri Mbili, nk. Na siyo kutokana na hisia za CHADEMA, CCM au ACT-Wazalendo kushindwa au kushinda.

4. *Watendaji wa Uchaguzi*. Kuna watendaji mbalimbali wa Uchaguzi katika mchakato wa Uchaguzi. Hapo napo kumekuwa na malalamiko mengi. Kati ya Watendaji hawa kuna Watumishi wa Tume walioko Makao Makuu. Lakini kutokana na kuwa wachache Tume hulazimika kuazima watumishi kutoka idara mbalimbali za Serikali.

Sambamba na hilo Tume imepewa jukumu la Kuteua watendaji mbalimbali wanaosimamia shughuli za Uchaguzi katika ngazi ya Halmashauri, Jimbo, kata na Vituo vya Kupigia Kura. Hii ni kwa mujibu wa vifungu 7(1) na 7(2) na kifungu 8(1) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343, na vifungu 9(1) na 9(2) vya Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura 292.

Watendaji hawa ni pamoja na Waratibu wa Uchaguzi Mkoa, Wasimamizi wa Uchaguzi katika Halmashauri, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi Ngazi za Jimbo, Maafisa
Uchaguzi katika kila Halmashauri, Wasimamizi Wasaidizi katika Ngazi ya Kata, Watendaji katika Vituo Vya Kupiga Kura.

Mtakumbuka kuwa Watendaji wa Tume Makao makuu, kwa sasa wanaajiriwa na Sekretarieti ya Ajira ya Utumishi wa Umma kulingana na Kibali. Unatuma maombi, unafanya usaili. Hakuna sifa ya Uanachama wa Chama Cha Siasa ili uweze kuajiriwa na Tume. Lakini mara tu unapoajiriwa na Tume, unatakiwa kukana Chama chako na kuwa mtu huru.

Changamoto ni kwamba itikadi iko kwa mtu mwenyewe ndani yake. Ila utendaji unafanyika kwa mujibu wa Sheria na si kwa mujibu wa matakwa ya idara fulani ya Serikali au chama fulani. Wale wanaoazimwa pia, hawaazimwi kwenye vyama, wanaazimwa kwenye idara huru za Serikali. Kipindi cha Uchaguzi maombi hutumwa kwa Mkurugenzi Halmashauri husika, ukikidhi Vigezo unapewa nafasi ya kuwa mtendaji wa Uchaguzi kwa wakati huo.

Ushiriki wa Wakurugenzi nafikiri ambao wanalalamikiwa sana kwenye Majimbo ni suala la utashi na weledi tu. Lakini sheria na kanuni zipo, ndiyo maana kuna mwanya wa kwenda mahakamani kupinga maamzi ya Ubunge. Kwa hiyo hapa pia uwanja upo sawa. Hawa, Wakurugenzi ndiyo waliomtangaza Vedastus Mathayo, Esther Bulaya, Halima Mdee, Peter Msigwa na Geroge Simbachawene kuwa Wabunge katika majimbo yao.

5. *Uteuzi wa Wagombea*. Uteuzi wa Wagombea kiti cha Rais na Makamu wa Rais hufanywa na Tume kwa Mujibu wa kifungu Cha 30 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343.

Mfano katika Uchaguzi Mkuu 2015 jumla ya Wagombea 11 walichukua fomu lakini ni Wagombea 8 tu waliorudisha fomu zao na wote 8 waliorejesha fomu zao walikidhi Vigezo kwa mujibu wa Ibara ya 39(1) ya katiba ya JMT, 1977. Hawa ni Wagombea wa Vyama 8 tofauti vya siasa ikiwemo ACT-Wazalendo, ADC, CCM, CHADEMA, CHAUMMA, TLP, NRA na UPDP.

Kama Tume ingekuwa inafanya kazi kwa shinikizo ingewakata wagombea wa vyama vyote vilivyokuwa na Nguvu kama CHADEMA na kubakiza UPDP chini ya Dovutwa au NRA chini ya Kasambala ili kuipa CCM nafasi rahisi ya Kushinda.

Lakini kutokana na vyama vyote kukidhi vigezo kwa mujibu wa sheria Wagombea wote waliruhisiwa kuchukua fomu na kushiriki Uchaguzi unaoratibiwa na kusimimaiwa na Tume. Ni katika kuhakikisha kuwa Tume inatenda haki, Kifungu cha 40 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 kinatoa nafasi ya kuweka pingamizi kwa wagombea walioteuliwa katika nafasi ya kiti cha Rais ndani ya saa 24 baada ya muda wa uteuzi kumalizika.

Kwa upande wa Ubunge, Wabunge hujaza Fomu Na.8 za uteuzi na Fomu Na.10 za Maadili, ambazo hutolewa na Msimamizi wa Uchaguzi. Kifungu cha 40 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 kinatoa nafasi ya kuweka pingamizi kwa wagombea walioteuliwa katika nafasi ya Ubunge. Pingamizi hupokelewa, husikilizwa na kuamuliwa na Msimamizi wa Uchaguzi.

Ili kutenda haki kama mlalamikaji au mlalamikiwa hakuridhika na maamzi ya Msimamizi wa Uchaguzi, anaruhusiwa kukata Rufaa katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 40(6), Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343. Kwa Mfano katika Uchaguzi Mkuu 2015, Tume iliwarejesha Wabunge 14 kati ya 57 waliokata rufaa kupinga maamzi ya Wasimamizi wa Uchaguzi. Kati ya hawa 14, wanufaika walikuwa CHADEMA 7, ACT-Wazalendo 3, ADA-TADEA 1, CUF 2 na SAU 1.

6. *Zoezi la Kampeni za Uchaguzi*. Tume ina wajibu wa Kuunda Kamati ya Kuratibu Ratiba ya Kampeni kwa Upande wa Wagombea Rais. Kamati hii si ya Chama Kimoja ni ya Vyama Vyote vilivyo na Mgombea wa Urais.

Kamati hiyo hupitia na kujadili Mapendekezo ya Ratiba ya Mikutano ya Vyama husika. Mapendekezo hayo yakisha kubaliwa Tume hulazimika kusambaza Ratiba hiyo kwa Waratibu wote wa Uchaguzi wa mikoa, ambao pia hulazimika kufikisha kwa Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi. Nakala nyingine hupewa IGP, ambaye atahusika kuwasambazia RPCs na OCDs kwa ajili ya Ulinzi na Usalama katika mikutano ya Kampeni. Kamati hii hupanga siku za kukutana kwa wiki na hulazimika kukutana bila kujali ratiba kama kuna dharura.

Kwa Upande wa Ubunge na Madiwani, Vyama vyote vyenye Wagombea katika ngazi husika, hulazimika kuwasilisha Mapendekezo ya Ratiba ya Kampeni za Uchaguzi kwa Msimamizi wa Uchaguzi.

Vyama ambavyo uhitaji kufanya mabadiliko ya tarehe na Maeneo ya kufanyia kampeni hulazimika kutoa taarifa kwa Wasimamzi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi. Mabadiliko yakikubaliwa hupelekwa kwa Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Polisi Wilaya ili watoe Ulinzi katika Mikutano ya Kampeni.

Hapa naona kuna mazingira sawa, kama kuna makosa yanatendeka na watendaji waliopewa jukumu la kusimamia zoezi la Uchaguzi kwa niaba ya Tume hayo ni makosa yanayotokana na utashi wao na wala si kwa idhini ya Tume au Time kutokuwa kwa huru.

7. *Upigaji Kura na Uhesabauji Kura*. Zoezi la kupiga kura ni kwa wapiga kura walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la wapiga kura. Bado hakuna Sheria inayomlazimisha Mtanzania kupiga kura lakini ni haki ya kila Mtanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18.

Ili uweze kupiga Kura sharti uwe umejiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura na uwe na Kadi halali ya Mpiga kura. Na Mazingira ya Chumba cha Kupigia Kura yana Uwakilishi (Mawakala) wa Vyama vya Siasa ambavyo vinashiriki.

Mawakala hao si Wa Tume, bali ni wa Vyama vya Siasa. Hao jukumu lao kubwa ni kuhakikisha kuwa wanalinda Maslahi ya Wagombea wa Vyama vyao vya Siasa katika Vituo vya Upigaji Kura. Je, katika mazingira huru kama haya Tume inaingiaje kwanye lawama?

Kwa Upande wa Uhesabuji kura, baada ya Zoezi la Uchaguzi kukamilika Vituo vya Kupigia Kura hubadilika na Kuwa Vituo vya Kuhesabia Kura. Kura za Rais zinaanza kuhesabiwa, Wabunge na mwisho Madiwani.

Katika kila kituo kuna taratibu za kufuata ambazo ni pamoja na;
i. Kukagua Masanduku kama lakiri hazijafunguliwa na kukata lakiri hizo kwa chini;
ii. Kumimina kura zote kwenye meza na kuhesabu kura moja moja kwa sauti inayosikika kwa kila mtu mwenye uwezo wa kusikia;
iii.Kuandika katika ‘drafting pad’ idadi ya kura zote zilizo patikana katika kila sanduku;
iv. Kukunjua karatasi moja baada ya nyingine kwa kuonyesha upande wa juu wa picha za Wagombea;
v. kuhesabu kwa sauti ili kila mmoja aweze kuandika idadi iliyopatikana;
vi.Kubainisha kura zenye mgogoro;
vii.Kujaza matokeo ya Uchaguzi kwenye Fomu za Matokeo, 21A, 21B, 21C kwa Rais, Wabunge na Madiwani Mtawalia;
viii.Kubandika mahali pa wazi Fomu za Matokeo ya Urais, Wabunge na Madiwani na kuwapatia Mawakala nakala za Taarifa za matokeo ya Uchaguzi.

Kumbuka, katika hatua hii Mawakala wa Kuhesabu Kura hutakiwa kujaza Fomu Na.16 katika kila hatua ya kuhesabu kura kuonesha kama kuridhika au kutoridhika. Hata katika Usafirishaji wa Masanduku Mawakala wa Vyama Wanakuwepo.

Katika mazingira haya ya Uwazi, kosa la Tume liko wapi hadi ionekane haiko huru?

8. *Kutangaza matokeo ya Vyama Vyote katika Ngazi zote*. Kwa mujibu wa kifungu cha 35 F (7) Cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343, Tume ndiyo Chombo chenye dhamana ya Kutangaza Matokeo ya nafasi ya Urais, na Kifungu cha 81(a) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343, Msimamizi wa Uchaguzi ndiye mwenye Jukumu la kutangaza Matokeo ngazi ya Ubunge. Vilele kifungu cha 82(a) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura 292, Msimamizi wa Uchaguzi au Msimamizi Msaidizi wa ngazi ya Kata ndiye mwenye jukumu la kutangaza Matokeo ngazi ya Udiwani.

Itakumbukwa kuwa Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi wanatekeleza Majukumu ya Tume. Katika zoezi la Uchaguzi ni Watendaji wa Uchaguzi wa Tume. Na hivyo hufanya kazi kwa mujibu wa sheria na siyo kwa Utashi wao.

Ni katika kutekeleza majukumu hayo Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi katika Uchaguzi Mkuu wa
Mwaka 2015 waliweza kuwatangaza Wabunge 195 wa CCM, Wabunge 35 wa CHADEMA, Wabunge 32 wa CUF, Mbunge 1 wa ACT-Wazalendo na Mbunge 1 wa NCCR-Mageuzi.

Aidha, ni hao hao Watendaji waliweza kuwatangaza madiwani 2,875 wa CCM, 801 CHADEMA, 212 CUF, 32 ACT-Wazalendo, 23 NCCR-Mageuzi, Wawili TLP na Mmoja NLD.

Kama Tume si huru na inafanya kazi kwa shinikizo, hizo Takwimu walipewa na Serikali au Idara gani ya Serikali kama si matokeo huru yaliyotokana na Utendaji huru wa Tume?. Kama wanafanya kwa kuelekezwa maana yake hata vyama vingine visingepata idadi iliyopatikana.

Hakuna mtoa Maelekezo anaweza kuelekeza utangaze Madiwani 1000+ wa Upinzani au Wabunge 69 wa Upinzani. Hakuna! Hakuna Mtoa Maelekezo anayeweza kuelekeza Vyama vya Upinzani vipate asilimia 41.54 ya Kura zote za Urais. Hakuna!

Hivyo, kutokana na Maeneo 8 hayo niliyaangazia naamini kuwa Tume ya Uchaguzi ni huru.

Napokea kukosolewa na kuelimishwa ili niweze kupanua uelewa wangu kuhusu Tume kuwa Huru au kutokuwa Huru.

Naomba kuwasilisha.

Lugumya

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Hongera kwa uzi wako mkuu.
Naomba kukuuliza maswali machache tu.
1. Nini maana ya neno huru?
2. Nini maana ya Tume huru?
3. Eleza sifa/vipimo vya Tume huru?
4. Tume huru inaundwa na nani?
5. Hao watu wanaounda Tume huru wanateuliwa na nani?
6. Kwenye hiyo Tume huru kuna wawakilishi/wajumbe toka vyama vya upinzani?
7. Naomba ufanye utafiti katika mataifa mengine mfano Marekani ili ujue Tume huru inapatikanaje.
 
Mleta mada hata ungeeandika na kukesha hapa jukwaani ni kama kupoteza muda wako bure. Hiyo katiba unayoitetea ni ya mwaka 1977 enzi za mfumo wa chama kimoja.

Kuna katiba pendekezwa ambayo ilikuwa kwenye hatua ya kupigiwa kura japo maoni yetu yalichakachuliwa na bunge la ccm, lakini muundo wa tume ya uchaguzi haukuwa huu.

Rais huyu alikataa hiyo katiba mpya iliyokuwa kwenye hatua ya kura, akidhani uwepo wa katiba mpya ni hisani yake au ni wajibu wa rais. Kumbe lengo la kuikataa katiba mpya, ni ili anajisi chaguzi za nchi hii.

Hatuidai tume huru ya uchaguzi kwa bahati mbaya, mwenendo mzima wa uchaguzi tunafahamu, na tuna ushahidi usioacha shaka kuwa tume hii ys uchaguzi kutokana na muundo wake haiko huru. Andika kwa kupamba na kuweka vifungu vya hiyo katiba, lakini tume hii sio huru fullstop.
 
No wonder common sense isn't common to all...
Otherwise ungejua kuwa maelezo yako yote ni upumbavu (kwa sauti ya Hayati Mwl. JKN)!
Mpumbavu na mjinga hujibu hoja kwa matusi na kejeli mwerevu hujibu hoja kwa hoja acha upumbavu na ujinga kuwa mwerevu jibu hoja au lete hoja yako.

Sent from my Infinix X624 using Tapatalk
 
Sidhani kama kigezo cha kuteuliwa kuingia kwenye ujumbe wa tume huwa uanachama wa chama flani, bali ni raia wa Tz akiwa timamu wa akili na anaoutaalamu husika! Kimsingi, haitatokea mjumbe wa tume asiwe na nashasha na chama hata kimoja!

Lakini akiwa ktk kutimiza majukumu yake, mapenzi na chama yanawekwa kando na kuweka mpira kati! Kwa bahati mbaya, ili hiyo tume iwe huru machoni pa Mbowe et al, inabidi mwanachama wao wanayemjua awe ndie bosi wa tume yenyewe!
 
Sidhani kama kigezo cha kuteuliwa kuingia kwenye ujumbe wa tume huwa uanachama wa chama flani, bali ni raia wa Tz akiwa timamu wa akili na anaoutaalamu husika! Kimsingi, haitatokea mjumbe wa tume asiwe na nashasha na chama hata kimoja! Lakini akiwa ktk kutimiza majukumu yake, mapenzi na chama yanawekwa kando na kuweka mpira kati! Kwa bahati mbaya, ili hiyo tume iwe huru machoni pa Mbowe et al, inabidi mwanachama wao wanayemjua awe ndie bosi wa tume yenyewe!

Umejaribu kuandika mawazo yako lakini ebu tueleze uhalisia upoje?
 
Tume ya Uchaguzi Tanzania SI HURU.

Baadhi ya sababu na uthibitisho kuwa SI HURU ni:-

- Timu moja kupewa Mamlaka ya KUTEUA REFA SI SAWA.

- Kwa vyovyote vile iwavyo, Wateule watafanya kazi kwa kumnufaisha MTEUZI WAO.

Mifano hai:-

Jecha na Zanzibar,

Mkurugenzi wa Kinondoni na Uchaguzi wa Marudio ulio sababisha MAUAJI.

Maeneo waliyoshinda WAPINZANI, Matokeo yalitangazwa kwa MBINDE, Kuna maeneo Watu waliuawa, kuumizwa, kufunguliwa MASHITAKA YA KUKOMOA.

NIKUTEUE MIMI,

MSHAHARA NIKULIPE MIMI,
POSHO, GARI NIKUPE NIMI,

WEWE UMTANGAZE MPINZANI AMESHINDA, H!!!!!!!!!!!!!!!!!!!?

Madudu ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Hayo ni baadhi ya uthibitisho kuwa TUME YA UCHAGUZI SI HURU NA KWAMBA INAELEKEZWA CHA KUFANYA NA MTEUZI

AU Wateule wanayafanya hayo kumfurahisha ALIYEWATEUA.
 
Tume sio huru acha propaganda zako kwani nani haijui katiba,Rais Mstaafu Mkapa alikiri ktk kitabu chaku kuwa haja ya Tume huru,Tume ingekuwa huru Jecha angefuta Uchaguzi wa Zanzibar?

Sent using Jamii Forums mobile app
Hayo ni Maoni yangu Mkuu, wewe njoo na ya kwako! Sema si huru kwa sababu 1,2,3. Unasema bila hata pointi moja, hukusudii kunipa maarifa juu ya Tume kutokuwa Huru.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom