Maoni yangu kuhusu Withholding Tax kwa Nyumba za kupanga

Abdul Nondo

JF-Expert Member
Oct 28, 2016
515
2,874
Hapo awali ni wapangaji wa nyumba, pango na maofisi kwa ajili ya ya Biashara (commercial/business Building) ndiyo waliokuwa wakitakiwa kulipa kodi iitwayo withholding tax ya asilimia kumi (10%) kwenda TRA.Na wanaokatwa kodi hii ni wamiliki wa pango au jengo hilo la Biashara 10% kutoka katika fedha anayolipa mpangaji kwa miezi anayopanga.

Sheria ya income tax kifungu cha 82(2)(a) "The Income tax Act 2019",kiliweka wazi kuwa mtu asilipishwe kodi hiyo withholding tax ya pango la jengo au nyumba kama halitumii Kwa biashara.

Hivyo wapangaji wa fremu za maduka,maofisi na biashara zinginezo tu ndiyo waliotakiwa kulipa Kodi ya withholding tax ya 10% TRA.

Mwaka huu 2022 ,Bunge kupitia sheria ya fedha ya 2022, (The Finance Act, 2022) ilifanyia marekebisho ya sheria ya Kodi yaani The Income Tax Act 2019 na kufuta kifungu cha 82(2)(a) kilichokuwa kimetoa maelekezo kuwa wanaopaswa kulipa Kodi ya withholding tax ya 10% ya pango ni wale tu wanaopanga nyumba Kwa madhumuni ya biashara.

Kufuatia marekebisho haya,sheria sasa inataka pia kila mpangaji hata wale wanaopanga nyumba kwa ajili ya makazi binafsi (residences) yaani wapangaji wanatakiwa kulipa asilimia 10 ya Kodi ya nyumba ya kila mwezi kwenda TRA kama withholding tax na utaratibu uliotolewa na TRA ni kwamba ni wapangaji ndio wanapaswa kulipa fedha hiyo 10% kutoka katika kiasi cha fedha anachotakiwa kumlipa mwenye nyumba kwa miezi husika na kumpelekea risiti mwenye nyumba kuwa asilimia 10 imekwisha lipwa TRA.

Sheria hii ya Withholding tax imemfanya mpangaji kama wakala wa serikali katika upatikanaji wa kodi hii (Withholding agent /withholder) kwa kuzuia kiasi cha fedha 10% kabla ya Mwenye nyumba au mmiliki hajapokea fedha husika kwa mpangaji, hivyo 10% ya fedha ile inazuiwa na mpangaji kama wakala wa kodi hii kwa serikali (Withholding Agent) na mwenye nyumba ambaye ni (Witholdee) kupewa kodi ya nyumba (rent) pungufu baada ya kodi ya serikali (withholding tax) kukatwa.

Napenda kukubali kwamba kodi hii ya Withholding tax sio mpya ,ipo muda mrefu kwa wamiliki wa majengo ya Biashara (Commercial/ Business Buildings),na ni Mpya kwa wamiliki wa majengo ya makazi (Residential buildings).

Hivyo utekelezaji wake unaweza kuwa tofauti na wenye ugumu ikiwa changamoto mahususi nitakazozianisha kama hazitafanyiwa kazi.

1.Wapangaji wengi wa majengo ya Biashara walikuwa wanaweza kulipa Kodi hii Kama (Withholding Agent) sababu wengi wana TIN (Namba ya utambulisho wa mlipakodi).

Ingawa serikali imesema kwa sasa kila mtanzania ajisajili awe na TIN ,bado naona changamoto hiyo na hadi sasa hakuna jitihada zozote ,na kwa namna hii ili mpangaji wa chumba au nyumba aweze kulipa kodi hii ni lazima awe na TIN ,hivyo kuna kazi kazi inapaswa kufanyika ili wapangaji wote kwa hatua hii wawe na TIN .

2. Changamoto ya pili, Uelewa bado ni mdogo sana .Kwetu hili jambo ni geni sana na ndio mara ya kwanza kwa wapangaji wa nyumba kutakiwa kushikilia 10% ya Kodi anayotakiwa mlipa mmiliki. Hivyo ni jambo geni kwa mpangaji na ni Jambo geni pia hata kwa mwenye nyumba/mmiliki wa nyumba.

a) Wapangaji wengi hadi sasa wanajua kodi hii (Withholding tax) wanakatwa wao, sababu elimu bado ipo chini sana .

b) Wamiliki/Wenye nyumba hawajapewa Elimu ya kutosha juu ya wajibu wao wa kulipa hiyo Kodi (Withholding tax 10%) kutoka katika kipato(rent au kodi) anayolipwa na mpangaji wake. Hivyo bila elimu ,uelewa katika hili hakuna mwenye nyumba atakubali mpangaji ashikilie 10% ya kodi alafu mwenye nyumba apewe hela pungufu na risiti ya malipo ya kulipa Kodi TRA , mpangaji atafukuzwa na mwenye nyumba atatafuta mpangaji mwingine.

c) Wamiliki wa Nyumba wanaweza kuongeza Kodi za nyumba kwa wapangaji ili kufidia Kodi hii,Kama serikali haitaweka utaratibu wa kudhibiti hili wenye nyumba katika upandishaji wa nyumba kiholela.


Ushauri wangu.

Kodi hii ili ikusanywe bila changamoto isiitwe wala isiwe Withholding tax ,iwe aina nyingine ya kodi kwa wenye nyumba wanaopangisha au Wamiliki wa Nyumba wanaopangisha na Kodi hii akatwe mwenye nyumba mwenyewe kwa njia ambayo serikali itaona inafaa ,na Mpangaji asiwe wakala wa kuzuia kodi hii (Withholding Agent) , Mpangaji alipe Kodi ya nyumba yote kwa Mwenye nyumba ,na Mwenye nyumba ndio awekewe utaratibu wa kulipa hiyo fedha Kama Kodi (Tahadhari:Isiwe aina ya Kodi ya Withholding tax) sababu utekelezaji wake utakuwa mgumu na utaleta mgogoro kati ya mwenye nyumba na mpangaji ikiwa Kodi hii itakuwa ni Withholding tax.

Ila ikiwa serikali inaona hakuna njia nyingine zaidi ya hii kwa kuita Kodi hii Withholding Tax ,napenda kushauri namna ambayo angalau itasaidia ili kutekeleza ,

Njia ya kurahisha makusanyo ya fedha hii, mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) washirikiane na Halmashauri kupitia watendaji wa mtaa (MEO) na kata (WEO).

(a)Moja, kutambua nyumba zote katika mtaa na kata zinazopangisha (zenye wapangaji) .

(b) Pili, kuwaita wenye nyumba wote(wasimamizi wa nyumba) na wapangaji katika mtaa husika na kufanya nao kikao kuwaeleza utaratibu na sheria hii.

(c)Tatu,kutengeneza by- laws katika Halmashauri zitakazotaka wapangaji wote kuwa na TIN na wenye nyumba wote kuwa na TIN pamoja na mikataba yote ya kupangishiana (mpangaji na mwenye nyumba) iwe na sehemu ya kusaini ya Afisa Mtendaji/Mwenyekiti wa serikali ya mtaa ili kabla ya mkataba kuanza kufanya kazi. Afisa Mtendaji wa mtaa au Mwenyekiti apate kuthibitisha mkataba wao baada ya kujiridhisha kwamba Kodi ya Withholding Tax (10%) imelipwa na kwa kuoneshwa ushahidi wa TRA(Tax evidence).

d) TRA ishirikiane na iwatumie Afisa watendaji au wenyeviti wa mtaa kufuatilia (Auditing) nyumba ambazo zinapangisha wapangaji ili kujiridhisha kama kodi hiyo ya Withholding Tax 10% kama inalipwa na kama mikataba ya kupangishiana ilipita ofisi ya serikali ya mtaa.

Hii itasaidia kuondoa mgogoro kati ya wapangaji na wenye nyumba na itarahisha kodi hiyo kulipwa ,ila kwa namna ilivyosasa ni vigumu sana kodi hiyo kulipwa labda iwe tunajifurahisha ila kama kweli tuna lengo la kukusanya kodi hii ,tuangalie utaratibu na pia TRA iangalie namna ya kuwashirikisha Halmashauri kupitia serikali za mitaa .

Elimu ,Elimu ,Elimu , Elimu,Elimu,Elimu.

Elimu bado ipo chini sana kuanzia kwenye umuhimu wa kumiliki TIN kwa kila mtanzania mwenye umri wa miaka 18 .

Elimu bado ipo chini sana kuhusu kulipa Kodi hii Withholding tax .

Sioni utekelezaji wa hili ikiwa hakuna utaratibu na njia za kutatua changamoto zilizopo.

Ahsante.

Abdul Nondo.
 
Mzee Nyerere Ninampa lawama hapo Tu kwenye Elimu ya Tanzania maana mwenzake Kenyata aliwekeza kwenye Elimu matokeo yake Leo kila eneo kuna majanga Sasa angalia watu hawajui k.k.k hadi leo
 
Back
Top Bottom