Maoni ya Kuishi na ndugu kwa wana ndoa

royna

JF-Expert Member
Nov 18, 2010
479
335
Nimenukuu kwenye kitabu, nafikiri ni maoni ya mwandishi,
Sura ya Sita
Ndugu wa Karibu na wa mbali kwenye Ndoa
Wakati mwingine mtu huweza kufikiri matatizo yanayohusiana na ndugu kwenye ndoa huwa makubwa zaidi kwa watu wa kipato cha chini ukilinganisha na watu wenye uchumi mzuri. Hata hivyo kwa namna moja au nyingine wanandoa wengi hujikuta wanapata kero za ndugu zao kwa jinsi moja au nyingine.

Kuna uzoefu wa aina nyingi hasa tunapozungumzia uhusiano wa wanandoa na ndugu wa pande zote katika kuhusiana. Uhusiano huwa ni chanya (positive) ambao ni mzuri na hasi ( negative) ambao huwa una kashikashi. Mimi katika sura hii nitakazia zaidi uhusiano hasi maana uhusiano chanya siku zote huwa hauna shida. Katika mambo yanayoweza kusumbua ndoa nyingi, suala la ndugu huwa linajitokeza walau katika ndoa zilizo nyingi zinazoripoti migogoro. Migogoro ya ndugu kwenye ndoa huwa ipo ya aina nyingi, kuna ile inayoanza kabla wanandoa hawajaoana kwa mmoja wa wanandoa kukataliwa asioe au kuolewa kwenye ile familia. Haya yote huwa na mchango kwa mwanandoa mtarajiwa kwani hujiuliza aache mtarajiwa wake na kufuata familia au aoe/aolewe na kuacha matakwa ya familia. Uchaguzi wowote utakaofanywa na mwanandoa waweza kumuumiza, kwani kumuacha ampendaye si mtihani mdogo, lakini pia kuwaudhi wazazi ni mtihani mkubwa zaidi. Kwa lugha nyingine, mgogoro huu unapaswa kutatuliwa kwa hekima kubwa ambayo wanandoa watarajiwa pamoja na familia wamejaliwa nayo kwani yasipotafutiwa ufumbuzi mbadala huleta migogoro ya kudumu kati ya wanandoa na wanafamilia. Tatizo lingine ambalo wanandoa hukutana nalo ni lile la ndugu wanaotaka kuingilia maamuzi ya wanandoa hao kwa jinsi moja au nyingine. Hawa mara nyingi huwa ni ndugu wa upande wa kiume ambao kisaikolojia huwa wanakuwa hawajamuachilia kijana wao kuwa mtu mzima wa kujitegemea. Mara chache familia ya mke huweza kufanya hivi pia, japo kwa sababu ya mfumo dume wa Afrika si jambo linalotokea mara nyingi. Jambo hili lisipoangaliwa huleta migogoro sana kwa wanandoa, kwani hufika kipindi mwanandoa hajui au anajichanganya afuate ya nani, ushauri wa ndugu au maamuzi ya mwenza. Mimi hushauri si vibaya kuwa rafiki wa wanandoa na hata kushauri lakini ni vema kuacha wao wawe waamuzi wa mwisho katika mambo yao. Na kwa wanandoa pia, ni vizuri ninyi mkawa na malengo mamoja katika mazingira yoyote, Pia si vema kutumia maneno makali kwa ndugu wanapowaingilia maana mara nyingi nia yao huwa ni nzuri, japo wao wanakuwa hawajui kwamba kwa kufanya hivyo itachangia migogoro. Hivyo ni vizuri kuendelea kuwaheshimu ndugu hata katika mazingira haya, wakati mwingine kuwasikiliza bila kuwajibu kwa ubaya, na wakati mwingine kunyamaza kwa adabu (si ukaidi) na kuendelea na mambo yenu ili kuwafanya wao pia wawaelewe taratibu taratibu si kwa pupa. Ndugu wengine waleta migogoro ni wale ndugu ambao kwa sababu moja au nyingine huja kuishi na wanandoa. Kama umeelewa vizuri sura inayochambua mtazamo utagundua kabisa kuwa ndugu wajapo kuishi kwa wanandoa huwa wana mtazamo wao juu ya kuishi pale, na wanandoa nao huwa wana mtazamo wao juu ya wageni wao. Kama mitazamo na malengo ya wageni hawa na mitazamo yao ikiwa tofauti na wanandoa hawa utegemee migongano japo kwa kiasi kidogo. Katika makundi haya kuna watu ambao huja kusalimia kwa muda mfupi na kuondoka, kuna wanaokuja kusalimia kwa muda mrefu, kuna wanaoukuja kutafuta maisha (shule,kazi) ambao hawaondoki hadi malengo yao yatimie, kuna wagonjwa wanokuja kutibiwa kisha warudi n.k. Wageni hawa wanapotembelea familia hizi, kwa sababu moja au nyingine wanapaswa kujua kuwa tayari wako chini ya utawala wa wanandoa, na wanapaswa kuishi kulingana na matakwa ya wanandoa hawa ili waweze kukidhi mahitaji yao yaliyowaleta katika familia hiyo na kuondoka kuiacha hiyo familia na utaratibu wake. Kinachotokea, hali huwa haiwi kama matazamio ya watu wengi yalivyo. Wageni hawa hutaka kuanzisha utawala mwingine ndani ya familia husika, jambo ambalo huweza kuleta mkanganyiko, na kama wanandoa hawa si thabiti, hujikuta wamejiingiza katika migogoro hii kisha kuwagawa na kuwapunguzia umoja wao wa kimapenzi. Matatizo machache yaletwayo na wageni hawa ni uvivu (kupenda wafanyiwe kila shughuli na msichana wa kazi) jambo ambalo ni uonevu mkubwa maana, mgeni aongezekapo na ukubwa wa familia huongezeka, hivyo na kazi huongezeka ambazo zinapaswa kusaidiana kati ya mama mwenye nyumba, msichana na wageni (kama wageni hao si wazazi ,wagonjwa au wasiojiweza). Tatizo lingine ambalo huchangiwa na wageni wa namna hii ni ukaidi uliozidi kipimo kwa wenyeji na kufikiri wameonewa kwa kila jambo. Mimi hushauri wageni hawa kuwa kwa sababu wewe umepita hapo kutafuta maisha, jifunze kuishi na wanafamilia hao kwa mfumo wao kisha uende zako, alimradi haiathiri imani yako (ambayo ni muhimu sana). Lakini pia kwa wanandoa ni vizuri kuwaelewa wageni hao kwamba kinachowatofautisha ni ujuzi wa maisha na mtazamo, hivyo kuchukuliana ni muhimu zaidi, huku wanandoa wakikumbuka kuwa wao wanapaswa kushikana zaidi. . Mpendwa msomaji motisha (motivation) huishi ndani ya mtu husika. Kinachokusukuma wewe kuamini na kuona jambo hivyo sicho kinachomsukuma mgeni au ndugu kuona na kuwaza anavyowaza. Ni kwa sababu hiyo mimi nashauri kuwa tofauti zenu zisiwe chanzo cha ninyi kukosa raha na amani. Maana mwisho wa siku utaona kuwa tofauti zenu zinasababishwa na nguvu inayowazidi nyote, si yeyote kati yenu amependa sana kuwa na tabia na msimamo alio nao. Mnahitaji kuwa waelewa zaidi katika kumaliza tofauti zenu, na kupunguza kukasirishwa, maana siku zote anayeumia ni anayekasirika si anayekasirisha. Kusaidia ndugu ni baraka kubwa, ninaamini katika historia ni vigumu kupata mtu ambaye alikuwa maskini sana kwa sababu alisaidia watu, na badala yake huona wengi waliobarikiwa kwa sababu ya kutoa. Ninaamini ndiyo maana hata Biblia imeandika kuwa ni bora kutoa kuliko kupokea. Kikubwa katika kusaidia ni muhimu kuzingatia kuwa kutoa kusizidi uwezo. Si vema kuwalaza watoto wako na njaa kwa sababu umempa mtu kitu ambacho wangekula wao. Kutokana na makwazo yanayosababishwa na ndugu na jamaa watu wengi wameamua na kufikiri kuwa waache kabisa kusaidia ndugu au wawasaidie wakiwa mbali na si kuishi nao kwa karibu. Mimi nafikiri ni vema tukakubaliana kuwa kwa sasa, Afrika hakuna kitu kiitwacho ‘extended family’ maana watu wote ni ndugu, hivyo mimi nafikiri ni mapema sana kwa wanajamii kukwepa kusaidia ndugu wanaowazunguka. Hili kwa sehemu kubwa linagusa zaidi watu wa kutoka katika familia maskini, ambayo unakuta kwa sababu moja au nyingine ni mtu mmoja au wachache tu ndiyo wamejikwamua kidogo kiuchumi. Najua wakati mwingine ni ngumu kidogo na unasikia kuwa uache lakini mimi nina sababu kadhaa za kusema hivyo: Kwanza kabisa ni vizuri ukawaza kuwa ni kwa nini wewe ndo umekuwa na nafasi nzuri katika familia yenu kuliko wengine, ni kwa sababu yamkini Mungu aliona wewe utakuwa unawajibika zaidi (more responsible) kuliko wao. Si vibaya pia kuwaza kuwa wangeweza kuwa hao ndugu zako unaowasaidia ndiyo wenye uwezo kiuchumi na wewe ungeomba kwao.Waandishi wa vitabu vya “The Power of Positive Thinking” na ‘Rich Dad Poor Dad’ kwa mazingira tofauti wanatoa moyo kwa wasomaji kuwa na bidii katika kutoa na kusaidia, kwa sababu wanaamini ipo nguvu inayosaidia kufanikiwa katika kutoa. Pili ninaamini pia kuwa unaweza kuwa na watoto ambao unajua uthamani wao. Ninaamini pia umewalea katika mazingira ambayo ungependa waendelee kuishi hivyo hata utakapokuwa haupo. Si vibaya pia kukumbuka kuwa hakuna binadamu mwenye kujua atakufa lini. Wakati mwingine ni vizuri kufanya wema duniani kwa ajili ya kuwekeza kwa ajili ya watoto. Mara nyingi unapopanda mbegu njema huvuna mazao mema. Kwa kuwasaidia watoto wa watu wengine, na wewe wa wa kwako watakuja kusaidiwa hivyo hivyo na watu wengine ukiwa haupo. Si lazima mtu uliyemsaidia akusaidie maana hufanyi hivyo ili akulipe bali unamtendea wema nawe utatendewa wema hivyo hivyo. Kuna wakati mwingine watu unaowasaidia au uliowasaidia wanaweza wasionyeshe moyo wa shukrani na hata kukusema au kukutendea vibaya, unapaswa kujua kuwa si makosa yao wafanyapo hivyo (kumbuka mtazamo), Biblia inatufundisha kutenda mema na inasema kuwa tutalipwa tusipozimia mioyo. Hivyo usikate tamaa wala usiache kutenda mema kwa watu na ndugu maana hiyo ni kama mbegu iliyopandwa shambani, wakati wa kuvuna utafarijika. Pia kuacha kusaidia watu wengine si kuwatendea haki maana na wewe kwa namna moja u nyingine waweza kuwa ulisaidiwa na watu, au wazazi wako waweza kuwa walisaidiwa na watu, kumbuka msaada ni msaada tu, hata kama ulipata tu siku moja ya kulala kwa watu ni msaada, hivyo ni vema na wewe usaidie wengine. Mimi ushauri wangu huwa ni badala ya kuwaepuka ndugu, wanandoa watafute njia mbadala ambayo ni salama na ambayo inapunguza msongo kwao na ndugu. Kuna wanandoa ambao kwa sababau moja au nyingine wameamua kuwasaidia ndugu zao wakiwa mbali au wasingependa waje waishi hapa kwao. Mimi sina shida ni uchaguzi gani mnafanya ila ninasisitiza kuwa kwa sababu moja au nyingine ni vema kusaidia ndugu. Katika uchaguzi wa kusaidia ndugu mahali walipo, kama ni wanafunzi wanasoma kuna changamoto zake, kwamba kama wanafanya hawako chini ya uangalizi wako wanaweza pia wasifanye vizuri kama matazamio yako yalivyo, kwasababu mazingira (external environment) yana mchango mkubwa kwenye utimiaji wa malengo ya mtu. Kwa wale utakaoamua kuwaleta nyumbani ni vema ukatafuta maelekezo sahihi wakajua ni jinsi gani ya kuishi hapo nyumbani. Usipofanya hivyo mapema, mnaweza kupata migongano katikati kwani mgeni atataka kufanya vitu kwa utaratibu wake, na ninyi mkawa na utaratibu tofauti. Kwa wale ambao ni wadogo na mna nia ya kuishi nao, ni vizuri kuhakiki kuona kama kweli wako tayari kuishi na ninyi, kama hawako tayari ni vizuri kuona kama wameelewa; na kama bado wanaonekana hawako radhi, ni vema kuwa makini, maana pia siyo salama kuishi na watu wasiopenda kuishi na ninyi kwenye nyumba moja. Kwa familia zenye watoto wadogo, ni vema pia kuwafanya wakaelewa ni jinsi gani ninyi mnapenda waishi na watoto wenu, maana kila familia ina mazingira tofautitofauti ya kulea watoto. Usipomuelekeza mgeni wa kutoka kijijni vizuri ambaye amekuja mjini, usishangae kuona mtoto kalishwa milo mitatu kama mtu mzima. Japokuwa zoezi la kufahamiana inabidi lifanyike kwa uangalifu mkubwa sana ili mgongano usitokee siku za mwanzo wa kuishi pamoja. Kama zoezi likifanikiwa mwanzo wa kuishi pamoja, mnaweza kupunguza migongano kwa sehemu kubwa sana. Kwa wale wageni ambao si wanafunzi wamekuja kuishi muda mrefu kwa sababu moja au nyingine ikiwemo kutafuta maisha, kwa mfano kuna watu ambao wanaweza hata kuacha wake zao na kuja kuishi kwako kwa ajili ya kutafuta maisha. Ni vizuri kujua malengo ya watu hawa kuja kuishi hapo kwako. Kama wana muda maalumu wamepanga na mambo mengine ya msingi ni vema ijulikane mapema. Nasema hivi kwa sababu mtu mwenye familia anapoiacha familia yake na kuja kuishi kwako, bila malengo wewe pia unakuwa unawakosea watu wanaomtegemea maana kiongozi wa familia ana jukumu la kutunza familia yake, na kuiacha kwenda kuishi mahali bila malengo si kuwatendea haki. Lakini kama ni kwenda kutafuta maisha; hilo ni suala tofauti. Umakini inabidi uangaliwe unapokuwa unawaelekeza wageni hawa maana kwa wengine inaweza ikaharibu uhusiano kabisa. Msaada wa umakini wa kuangalia ndugu:
  • Unapotoa msaada, jifunze kuwasaidia watu ambao wana uhitaji wa kweli, siyo tu kusaidia kila mtu ilimradi anahitaji msaada, kuna ambao wanapenda tu kuomba msaada, hata kama msaada huo watautumia vibaya.
  • Usiwasaidie watu walioacha familia zao kuja kwako bila malengo, kwa nia ya kukimbia majukumu yao, au wanafurahia tu kuishi kwako, bali uwafundishe na uwatengenezee mazingira ya kutafuta pesa ili ziwasaidie kuangalia familia zao.
  • Kama inawezekana jiepushe na kuishi na watu wengi sana kwa wakati mmoja, wasaidie na uishi nao kwa zamu, kusaidia hakupaswi kuwa mzigo bali kunapaswa kuwa baraka.
  • Wahitaji yatima na wahitaji wajane wapewe nafasi ya kwanza katika kuwasaidia maana wao wanaweza kwa nafasi zao wakawa wahitaji zaidi kuliko wengine.
  • Jitahidi kadri uwezavyo kutengeneza mazingira mazuri na mwenza wako mnaposaidia ndugu, maana ndoa yenu ina thamani kubwa hivyo ni vema kutokuruhusu masuala ya kusaidia ndugu yalete migongano kwenu.
  • Ndugu waishio kwenu ambao wameanza kujitegemea (kwa mfano wamemaliza vyuo na kuanza kazi) wahamasishwe na kujengewa mazingira ya kuweza kujitegemea wenyewe ili waweze kuwapa wahitaji msaada wengine nafasi.
  • Kuna wale watu ambao ni wavivu, wanaopenda tu wakae kwako bila kufanya lolote au kujipatia kipato hapo nyumbani, wanapaswa kupewa ushauri taratibu sana, kuwa uvivu ni mbaya, na kwamba wao pia ni viongozi wa familia watarajiwa, kwa kuwa wavivu watakuwa mzigo kwa wenza wao kwa siku za usoni.
  • Kuna wale wachache wenye tabia za ajabu ajabu sana, ambao kwa sababu moja au nyingine wanataka kuharibu amani ya familia walipofikia. Wanataka kunyanyasa wasichana wa kazi, au watoto, hekima inahitajika sana jinsi ya kuishi nao, maana wanaweza kuwa chanzo cha kuharibu familia ya walipofikia.
Wazazi Ni vema tukakumbushana kuwa katika makundi haya, wazazi wanatakiwa kuangaliwa kwa adabu, heshima na umakini tofauti. Wanandoa wanaweza kukubaliana ni jinsi gani wawaangalie wazazi kihisia na kifedha. Kuna wazazi wale ambao hawana matatizo ya kifedha mnaweza kuwatia moyo tu kwa kuwaheshimu, na kuwazawadia kwa chochote maana wazazi hujisikia vema na vizuri watoto wanapowakumbuka. Bali kwa wale wenye wazazi wenye uhitaji mkubwa wa kifedha ni muhimu kuwafikiria kwa umakini, na kuwawekea mikakati endelevu ya jinsi ya kuwawezesha kuishi na msongo mdogo zaidi wa kifedha, maana kuwasaidia wazazi ni baraka. Yote katika yote, jifunze kutoa kulingana na uwezo wako, na utoe kwa hiari. Unapotoa huku unanung’unika, unazuia baraka ambazo zingepita kwako kupitia unaowasaida.
 
Hii kitu ni ndefu sana...ina maana miandishi yote hiyo ni maoni tu?
 
Back
Top Bottom