Crashwise
JF-Expert Member
- Oct 23, 2007
- 22,227
- 8,739
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI MHESHIMIWA SUSAN ANSELIM JEROME LYIMO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KATIKA WIZARA HIYO KWA MWAKA WA FEDHA 2016/17.
1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii, kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia sote uhai na kutuwezesha kuliona Bunge la 11 tukiwa salama. Pili napenda kumshukuru kwa dhati kabisa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (Mb) kwa imani kubwa aliyo nayo kwangu kwa kuendelea kuniteua kuwa Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa vipindi vitatu mfululizo. Ninaahidi kuendelea kuchapa kazi kwa bidii, na kwa hakika sitaiangusha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika wajibu huu niliopewa wa kuisimamia Serikali katika sekta ya Elimu nchini.
Mheshimiwa Spika, naishukuru familia yangu ikiongozwa na mume wangu Boniventure Ngowi na wanangu wote. Kipekee namshukuru sana Naibu Waziri wangu Dr. Suleiman Ally Yussuf kwa ushauri wake. Vilevile nawashukuru sana BAWACHA Mkoa wa kichama wa Kinondoni kwa kunichagua kuwawakilisha hapa kama kawaida sitawaangusha.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee napenda kuwapongeza viongozi wote wakuu wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kwa kazi kubwa na nzuri walioyoifanya ya kuwaongoza watanzania kuchagua mabadiliko katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015.
Mheshimiwa Spika, pamoja na ukiukwaji mkubwa wa haki na demokrasia uliofanywa na vyombo vya dola dhidi ya upinzani katika uchaguzi huo, ikiwemo kuvamia, kuwakamata na kuwanyang’anya vifaa vya kazi wataalamu wa UKAWA waliokuwa wakijumlisha matokeo ya uchaguzi huo, bado wananchi walionyesha imani kubwa sana kwa upinzani kwa kuupigia kura nyingi; na kwa mara ya kwanza katika historia ya vyama vingi hapa nchini, upinzani umepata viti 116 ikiwa ni ongezeko la asilimia 23.3 kutoka viti 89 vilivyopatikana katika uchaguzi Mkuu wa 2010.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kura za rais, licha ya mbinu zote zilizofanywa na vyombo vya dola kuchakachua ushindi wa upinzani, bado upinzani kupitia UKAWA umeongeza kiwango chake cha ushindi hadi kufikia asilimia takriban 40 tofauti na miaka iliyopita. Ushindi huu umetokana na kuporomoka vibaya kwa Chama cha Mapinduzi katika ngazi ya Rais kutoka ushindi wa asilimia 80 mwaka 2005 hadi asilimia 61.17 mwaka 2010 na kufikia asilimia 58 mwaka 2015. Kwa hesabu hizi ni wazi 2020 CCM itakuwa historia kama vile ilivyokuwa kwa chama cha KANU nchini Kenya na vyama vingine katika nchi za kiafrika vilivyoondolewa madarakani kwa kukataliwa na wananchi kutokana na utawala wa ki-imla wa muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, kuporomoka huku ni matokeo ya wazi kabisa kuwa chama hiki kimepoteza mvuto kwa wananchi kutokana na kushindwa kuondoa umasikini pamoja na kushindwa kusambaza huduma toshelezi za kijamii hasa elimu na afya kwa miaka yote ya utawala wake wa miaka 55 sasa.
Mheshimiwa Spika, kutokana na aibu hii ya kushindwa kuondoa umasikini kwa wananchi; na kutokana na hofu ya Serikali kuhojiwa na bunge kuhusu utendaji wake; sasa Serikali hii ya awamu ya tano inayojinasibu kwa kauli mbiu ya ‘hapa kazi tu’ imeamua kulinyamazisha bunge kwa kupiga marufuku vyombo vya habari kurusha moja kwa moja mijadala inayoendelea bungeni kuhusu utendaji wa Serikali na kuhusu mgawanyo wa fedha za umma katika bajeti ya serikali. Aidha, kutokana na hofu ya kukosolewa kutokana na kutojiamini katika mambo inayoyafanya; Serikali sasa imeanza kuingilia hotuba za Wasemaji Wakuu wa Upinzani na kuzifanyia censorhip kinyume kabisa na Kanuni za Bunge hili.
Mheshimiwa Spika, Kanunu ya 99(9) ya Kanuni za Bunge toleo la Januari, 2016, inasema kwamba: “Baada ya Waziri kuwasilisha hotuba ya bajeti kwa mujibu wa fasili ya kwanza; Mwenyekiti wa Kamati iliyopitia makadirio husika na Msemaji wa Kambi ya Upinzani watatoa maoni yao kwa muda usiozidi dakika 30 kila mmoja”.Kanuni haijaelekeza kwamba watatoa maoni yao baada ya kupitiwa na Kamati ya Kanuni. Kwa hiyo Mheshimiwa Spika; kitendo kilichofanyika tarehe 16 Mei, 2016 cha kuiondoa mezani hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili ikachakachuliwe na Kamati ya Kanuni, ni kinyume kabisa na Kanuni za Bunge; na ni kinyume kabisa na mila na desturi za uendeshaji wa mabunge ya Jumuiya ya Madola.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakemea kwa nguvu zote na inaitaka Serikali kuacha mara moja tabia hii ya kuingilia shughuli za kikanuni za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kutumia mgongo wa Bunge.
2. ELIMU YETU NA HATMA YA TANZANIA
Mheshimiwa Spika, dhambi kubwa na mbaya kuliko zote kuwahi kufanywa na Serikali hii ya CCM ni kuwanyima Watanzania elimu bora; kupandikiza elimu nyepesi, potofu na tegemezi kwa vizazi vingi vya taifa hili; dhambi ya kuwachanganya na kuwavuruga watoto wa Taifa hili kwa sera dhaifu, mitaala isiyo na dira na vitabu visivyokuwa na tija kwa maendeleo yao na ya Taifa lao.
Mheshimiwa Spika, Nchi yetu ipo hivi ilivyo kwa sababu ya elimu duni. Umaskini, ujinga na maradhi vinavyotesa Taifa hili ni matokeo ya elimu mbovu iliyotolewa na Serikali ya CCM kwa zaidi ya miaka 55 tangu tupate uhuru. Taifa linalotoa elimu bora halifanani hata kidogo na jinsi Tanzania yetu ilivyo.
Mheshimiwa Spika, hizi ni zama za kuelezana ukweli, hata mkitufungia humu Bungeni wananchi wasituone ‘Live’ bado Ukweli utaendelea kupasua kuta za Bunge hili na kuwafikia Watanzania. Mwanafasihi mashuhuri wa nchi yetu, Afrika ya Mashariki na Barani Afrika, Hayati Shaaban Robert, katika kitabu chake cha KUSADIKIKA aliandika hivi, “Msema kweli hukimbiwa na Rafiki zake, nikipatwa na Ajali kama hiyo sitawaonea Wivu wale wanaodumu na marafiki zao siku zote. Siwezi kuikana Kweli kwa kuhofia Upweke wa kitambo na kujinyima Furaha ya milele inayokaribia kutokea baada ya kushindwa kwa Uongo” mwisho wa kunukuu. Maneno haya ndio msimamo wangu na wa Kambi kwa ujumla wake, kwani siku zote wabunge wa Upinzani tumeonekana kama maadui na kunyanyapaliwa na Serikali hii ya CCM kwa sababu kusema ukweli kuhusu madhaifu ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, nchi zilizoendelea zinafanya mambo mengi ya kimaendeleo kwa kuwatumia wataalam wao wa elimu ya juu – University graduates. Wataalam wa vyuo vikuu wanatengenezwa kwa kutegemea pia elimu bora ya msingi na sekondari. Tanzania nayo ina vyuo vikuu. Lakini leo ipo haja ya Bunge hili kujiuliza nini hasa maana ya Chuo kikuu – “A University is an institution of higher learning where people's minds are trained for clear thinking, for independent thinking, for analysis and for problem solving at the highest level, is the centre for advancing the frontiers of knowledge". Kwamba: Chuo Kikuu ni taasisi ya elimu ya juu inayoandaa watu kuwa na fikra pevu, fikra huru kwaajili ya kuwa na uwezo mkubwa wa kiuchambuzi na kwaajili ya kutatua matatizo kwa kiwango cha hali ya juu, ni kituo cha kuendeleza maarifa.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa na Mawaziri wengi tu waliopita vyuo vikuu, lakini bado wameliingiza Taifa hili kwenye hasara kubwa kwa maamuzi mabovu, kwa kuingia mikataba isiyojali maslahi ya taifa na kwa utendaji usio na ufanisi. Hivi hawa wana-fit kweli kwenye definition hii ya Chuo Kikuu? Ukweli ni kuwa hata Serikali yenyewe haiwaamini wataalam wake wanaozalishwa na vyuo vikuu hasa kwenye Sekta ya Sayansi na Teknolojia. Na hili lipo wazi; leo Tanzania ina madini, gesi na mafuta, lakini watafiti, wachimbaji na wavunaji wakubwa wa raslimali hizi, wenye mashine kubwa na za kisasa, na zenye kutumia teknolojia ya hali ya juu si Watanzania.
Mheshimiwa Spika, Mwanafalsafa Herbet Spencer aliwahi kusema, namnukuu “The great aim of education is not knowledge but action” – kwamba “lengo kuu la elimu si ufahamu, bali vitendo”. Tafiti zinaonyesha ni 39% tu ya wahitimu wa vyuo vikuu wanaajirika kutokana na kile kinachoitwa kukosa ujuzi “lack of skills”. Kambi ya Upinzani inauliza hivi ni lini serikali itawekeza vizuri kwenye elimu katika ngazi zote?!!
3. BAJETI YA UTEKELEZAJI WA ELIMU BURE
Mheshimiwa Spika, kupitia Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, iliyofuatiwa na Tamko la utekelezaji katika Waraka namba 5 wa Mwaka 2015, imeagiza kufutwa kwa ada za masomo katika shule za sekondari kuanzia Kidato cha 1 –IV na michango ya aina yoyote kwa shule za msingi.
Mheshimiwa Spika, Kabla ya agizo hili la elimu bila ada na uchangiaji wa elimu katika shule za umma ulifanywa kwa ushirikiano baina ya serikali pamoja na wazazi. Hata hivyo upatikanaji wa pesa shuleni ulikuwa wa shida. Mathalani serikali iliweza kupeleka wastani wa Tsh. 4,000/= hadi 5,000/= tu kama ruzuku kwa shule za msingi badala ya Tsh 10,000/= zilizotakiwa kwa kila mtoto kwa mwaka. Aidha, Serikali iliweza kutoa wastani wa Tsh 12,000/= hadi 15,000 kwa kila mtoto kwa mwaka kama ruzuku kwa shule za sekondari badala ya 25,000/= zilizostahili (BRN report 2015).
Mheshimwa Spika, kwa kuzingatia hali hiyo, ili serikali iweze kugharamia utoaji wa elimu pasipo wazazi kuchangia ni lazima katika mpango wake wa bajeti kuanzia bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/17 itenge kiwango cha fedha kama kugharamia elimu kama ifuatavyo:-
§ Shilingi bilioni 161.5 kwa ajili ya ruzuku elimu ya msingi na awali kwa wanafunzi 8,987,031 kwa shilingi 10,000 kila mwanafunzi.
§ Shilingi bilioni 40 kwa ajili ya ruzuku elimu ya sekondari kwa wanafunzi 1,575,254 kwa shilingi 25,000 kila mwanafunzi kwa shule za umma.
§ Shilingi bilioni 31 kufidia ada ya shilingi 20,000/=kwa kila mwananfunzi katika shule za sekondari za umma kwa wanafunzi 1,575,254.
§ Shilingi 198 kufidia program za uji ambazo zilikuwa zinachangiwa na wazazi maana hivi sasa wazazi hawachaji chochote na shule nyingi zimeacha kutoa uji kwa wanafunzi.
§ Shilingi bilioni 1,438 kwa ajili ya kutatua changamoto za miundombinu kwa shule za msingi na sekondari kama vile vyoo, madarasa, madawati na ukamilishaji wa maabara za shule ya kata.
Mheshimiwa Spika,kwa minajili hiyo, ili kugharamia utoaji elimu bure serikali inapaswa kufidia pesa za ada iliyokuwa ikitolewa na wazazi kwa shule za sekondari na fedha ya gharama za chakula (uji) kwa wanafunzi wa shule za msingi kuanzia darasa la awali mpaka la saba. Serikali pia inapaswa kulipia gharama za uboreshaji na ujenzi wa miundombinu inayohitajika kwa mwaka. Shule nyingi zina mrundikano wa wanafunzi zaidi ya 400 kwa darasa la kwanza walioandikishwa mwaka 2016.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa uchambuzi uliofanywa na Haki Elimu katika jedwali namba 1, 2 na 3 hapo chini, kwa kuzingatia takwimu za idadi ya wanafunzi, shule na mahitaji, kila mwaka serikali itapaswa kutenga kiasi cha fedha kisichopungua shilingi bilioni 1,797.5 (takriban shilingi trililioni 1.8) nje ya mahitaji mengine ya kisekta ili kugharamia elimu bila malipo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuhakikisha kiwango hicho kinajumuishwa katika bajeti ya sekta ya elimu ya Mwaka wa Fedha 2016/2017 ili kutekeleza kwa ufanisi azma yake ya utoaji wa elimu bure, vinginevyo utakuwa ni usanii mtupu, na dhana ya elimu bure inaweza kuwa chanzo kingine cha anguko kuu la ubora wa elimu nchini.
Jedwali 1: Gharama za kufidia ada na ruzuku shuleni kwa ajili ya vifaa, gharama za mitihani na gharama za uendeshaji
Kiasi (Tshs)
Idadi ya wanafunzi
Jumla
Msingi
10,000
8,987,031
Bil. 90
Sekondari
25,000
1,575,254
Bil. 40
Ada Sekondari
20,000
1,575,254
Bil. 31.5
Jumla ya Ruzuku Msingi na Sekondari
Bil 161.5
Chanzo: (BEST 2015)
Jedwali 2: Gharama za kufidia ujenzi wa miundombinu uliokuwa ukichangiwa na wazazi
Upungufu
Gharama (Tshs)
Jumla
Madawati
1,170,827
80,000
Bil.90
Matundu ya vyoo
150,000
1,000,000
Bil. 150
Madarasa
95,945
12,000,000
Bil.1,150
Maabara
Shule 1,560
30,000,000
Bil. 47
Jumla kuu ya gharama za kufidia ujenzi wa miundombinu
Bil.1,438
Chanzo: (BEST 2015)
Jedwali 3: Gharama za kufidia utoaji uji shuleni
Watoto wa darasa la awali
Bei ya Uji kwa siku
Siku za Masomo
Idadi ya wanafunzi
Jumla
Sh. 100
198
992,356
Bil 20
Wanafunzi wa msingi (Darasa la I – VII)
Sh.100
198
8,987, 031
Bil. 178
Jumla ya fidia utoaji uji shule za awali na msingi
Bil 198`
Jumla Kuu
Bil 1,797.5
4. CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WALIMU NCHINI
Mheshimiwa Spika; Elimu bora inategemea sana morali ya walimu na sio madawati au madarasa yenye viyoyozi. Pamoja na uhalisia kwamba Serikali hii ya CCM imekuwa ikiwatumia sana walimu kutekeleza majukumu mengine tofauti na kufundisha kama vile uendeshaji wa sensa ya watu na makazi; uandikishaji wa wapiga kura na usimamizi wa mazoezi ya kupiga na kuhesabu kura, lakini baada ya shughuli hizo, Serikali huwa inawasahau kabisa.
Mheshimiwa Spika, walimu wanakabiliwa na changamoto nyingi sana jambo ambalo linakwamisha matamanio ya kuinua ubora wa elimu nchini. Tumelisema hili tangu bunge la tisa, bunge la kumi na sasa bunge la kumi na moja lakini Serikali haionekani kuzipa kipaumbele changamoto hizo ili kuzitatua.
Mheshimiwa Spika,Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutatua changamoto zinazowakabili walimu kama ifuatavyo:
i. Kuongeza posho ya kufundishia kwa walimu ili kufidia muda wa mwalimu kufanya kazi kwani ualimu ndio kada pekee inayofanya kazi kwa saa 24 hasa nyakati za kutunga na kusahihisha mitihani, kupanga matokeo n.k.
ii. Kujenga vyumba vya madarasa vya kutosha na kuviwekea samani za kutosha ili kupunguza mlundikano wa wanafunzi darasani na hivyo kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunza.
iii. Kuwapandisha madaraja kwa wakati sambamba na kuwapandishia mishahara walimu waliokidhi vigezo vya kupandishwa madaraja ili kuwapa motisha wa kufundisha.
iv. Kuwe na chombo kimoja cha ajira kwa walimu, na kwa maana hiyo; Tume ya Walimu ianze mara moja kazi ya kutatua kero za walimu.
v. Muda wa mafunzo kwa vitendo (BTP) kwa walimu uzingatiwe ili walimu-wanafunzi waweze kupata uzoefu wa kutosha wa kufundisha kuliko inavyofanyika hivi sasa ambapo mafunzo hayo yanafanyika chini ya wiki nane kila mwaka.
vi. Serikali ishughulikie kero ya Walimu wanaostaafu na kutolipwa stahiki zao mapema na pia kutorudishwa makwao kwa mujibu wa kanuni za utumishi.
vii. Serikali iwalipe walimu posho ya mazingira magumu ya kazi ili kuvutia kufanya kazi maeneo ya vijijini.
viii. Ajira mpya ziingizwe kwenye payroll mapema ili kuondoa kero ya kucheleweshwa kwa maslahi ya walimu kutokana na majina yao kutokuwepo kwenye payroll.
5. SERA YA VITABU
Mheshimiwa Spika,
Mwaka 1991 Serikali ya Tanzania ilitangaza sera mpya ya vitabu iliyoruhusu wachapishaji binafsi (private publishers) kuchapisha vitabu vya shule na vyuo nchini. Uamuzi huo ulifanyika baada ya miaka mingi ya ukosefu wa vitabu kutokana na kutaifishwa kwa makampuni ya uchapishaji na kuanzishwa kwa mashirika ya uma ya uchapishaji (km TPH, EAEPL) ambayo yalilenga kuchapisha vitabu ambavyo vingeandikwa na Taasisi ya Elimu.
Mheshimiwa Spika, Uamuzi huo wa kuondokana na dhiki na mahangaiko ya kukosekana kwa vitabu vya shule uliwekewa utaratibu maalumu wa utekelezaji ukiratibiwa na kitengo cha Book Management Unit (BMU), makao makuu ya Wizara ya Elimu. Baadae Wizara ya Elimu iliunda kitengo cha kudhibiti ubora wa vitabu kiitwacho, Educational Materials Approval Committee (EMAC).
Mheshimiwa Spika, Tangu 1991 wachapishaji wazalendo wamepiga hatua kubwa katika fani hii. Wanachapisha vitabu bora vya kiada vya ngazi zote za elimu. Tatizo la kutokuwapo kwa vitabu vya kiada halipo tena. Tatizo sasa ni kwamba serikali hainunui vitabu vya kutosha na kwa muda. Pia wachapishaji wanachapisha vitabu vya hadithi mbalimbali kwa ajili ya watoto wa ngazi zote za msingi na sekondari – hususan chini ya CBP kwa mfano kuna aina za vitabu (titles) zisizopungua 350 za vitabu vya hadithi na rejea pale CBP. Pia wachapishaji hao wametoa machapisho mengine kama kamusi, atlasi, chati mbalimbali, n.k.
Sera mpya ya vitabu ya mwaka 2014
Mheshimiwa Spika, Sera mpya iliyotangazwa na Kamishna wa Elimu kupitia Waraka wa Elimu Namba 4 wa mwaka 2014 inafuta sera ya Serikali ya vitabu ya mwaka 1991 na kurejesha majukumu ya uandishi na uchapishaji wa vitabu vya shule mikononi mwa Taasisi ya Elimu. Sera hiyo inadai kuwa wachapishaji binafsi wanaweza kuchapisha vitabu vya ziada – ambavyo anaviita ‘reference books’.
Mheshimiwa Spika, Mwaka jana (2015) Taasisi ya Elimu iliendesha semina kwa walimu wakuu wa shule za msingi nchini kote kuhusu ufundishaji unaotekeleza mitaala mipya hususan darasa la kwanza na la pili kwa utaratibu wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK). Walimu waliopewa semina waliahidiwa kupatiwa vitabu vipya vinavyokidhi mitaala mipya mwezi Januari au Februari 2016 ili waanze kuvitumia madarasani. Shule zimesubiri vitabu hivyo hadi sasa, karibu nusu ya mwaka, bila kupatiwa vitabu hivyo.
Mheshimiwa Spika,Inasemekana vitabu hivyo vipya vya Taasisi ya Elimu havifai. Pia tumesikia kuwa baadhi ya wafanyakazi waliohusika katika usimamizi wa kazi hiyo wamesimamishwa kazi. Lakini hadi sasa watoto wako madarasani wakisubiri vitabu vipya vya Taasisi ya Elimu.
Mheshimiwa Spika, Mwandishi ni msanii kama alivyo mchoraji, mwimbaji, mchezaji wa ngoma au mwigizaji. Kundi hili lina watu wenye vipaji maalumu. Uandishi siyo kazi anayoamriwa au kupangiwa mtu kuifanya ila naifanya kwa utashi wake. Pia haitegemei elimu ya mtu, kwa mfano, Shaaban Robert alikuwa na elimu ya darasa la IV tu lakini aliandika vitabu vilivyo bora sana ambavyo vinatumika hadi vyuo vikuu.
Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Elimu ina mwelekeo wa ukuzaji mitaala na siyo kuandika na kuchapisha vitabu. Ilichukua muda mrefu hadi Wizara ya Elimu ya miaka ya 1990 kutambua hivyo. Ni heri Wizara ya Elimu ikabidhi jukumu la uandishi na usambazaji wa vitabu kwa wachapishaji binafsi.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na kadhia hii ya vitabu kukosekana mashuleni, Kambi rasmi ya Upinzani inapendekeza yafuatayo:
(a) Serikali irejeshe Sera ya Vitabu ya 1991 ambayo ina mafanikio makubwa
(b) Serikali iweke pembeni mitaala mipya ya TIE ya 2016 na badala yake iunde Tume ya Elimu itakayotathmini Mfumo na Utendaji wa Elimu nchini na kutoa mapendekezo mapya
(c) Vitabu vilivyopo tangu mfumo mpya wa elimu wa 1991, viendelee kutumika shuleni hadi tume imalize kazi yake.
6. UAMUZI WA KISIASA UNAVYOATHIRI UBORA WA ELIMU NCHINI
Mheshimiwa Spika, Serikali ya CCM kwa muda mrefu sasa imekuwa na tabia ya kufanya uamuzi wakisiasa katika masuala ya elimu na kuweka kando utafiti au ushauri wa kitaalamu jambo ambalo limeathiri sana ubora wa elimu nchini.
Mheshimiwa Spika, mifano iko mingi; kwa mfano mwaka 2014, Serikali ya CCM iliwashusha walimu wakuu wa shule mbalimbali za Sekondari za Serikali nafasi zao za ukuu wa shule eti kwa sababu walifunga shule kutokana na ukosefu wa chakula uliosababishwa na wazabuni wa chakula mashuleni kushindwa kusambaza vyakula kutokana na ukosefu wa fedha kwa kuwa Serikali ilikuwa haiwalipi wazabuni hao.
Mheshimiwa Spika, mfano mwingine ni kuhusu matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012 yaliyokuwa mabaya kuliko yote kutokea ambapo zaidi ya asilimia 95 walipata daraja la 0 na IV. Hali hii ilipelekea Serikali kufanya ‘standardization’, uamuzi ambao kimsingi ulikuwa ni wa kisiasa ili kuwafurahisha wanafunzi na wazazi ili waendelee kuipigia kura CCM. Haikuishia hapo, Serikali baadaye ikapanua magoli kwa kubadili mfumo wa upangaji wa matokeo kutoka madaraja (division) kwenda GPA (wastani). Jambo hili halikukubalika sio tu na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni bali hata wadau mbali mbali wa elimu. Leo hii baada ya kelele nyingi za wadau wa elimu; Serikali imerudi tena kwenye utaratibu wa zamani wa madaraja.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea kuionya Serikali kuacha siasa katika masuala muhimu kama ya elimu kwani yanachangia sana katika kuporomoka kwa elimu nchini. Aidha, ili kuondokana na maamuzi ya kisiasa kwenye elimu, tunarudia kupendekeza tena kwamba Serikali ianzishe chombo cha udhibiti wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi (Tanzania Education and Training Regulatory Authority - TETRA) kitakachoweka viwango vya ubora wa elimu kwa mujibu wa mitaala iliyopitishwa na Serikali, kudhibiti utungaji, usahihishaji na upangaji wa matokeo ya mitihani, kudhibiti gharama za elimu (ada na michango mingine) baina ya shule na taasisi nyingine za elimu za uma na binafsi ili kuwa na mfumo mmoja wa elimu unaoeleweka kuliko sasa ambapo kuna tofauti kubwa za kimfumo baina ya shule na taasisi za elimu binafsi na zile za umma. Haiwezekani Wizara hii iwe ndio mtungaji ya sera elimu, mtoaji wa elimu, mdhibiti wa elimu, mtungaji na msahihishaji mitihani huku ikiwa pia mmiliki wa baadhi ya shule. Haki itatoka wapi?!!
7. UKIUKAJI WA KATAZO LA SERIKALI LA KUONGEZA ADA KWA SHULE ZISIZO ZA SERIKALI KWA MWAKA WA MASOMO 2016
Mheshimiwa Spika; Pamoja na mkanganyiko uliopo kuhusu ada elekezi na katazo la Serikali la kuongeza ada kwa shule zisizo za Serikali kwa mwaka wa masomo 2016, zipo baadhi ya shule zisizo za Serikali zimeendelea kuongeza ada kwa mwaka huu wa masomo 2016 na kwenda mbali zaidi kuwatoza wazazi faini ya hadi shilingi laki moja kwa kuchelewa kulipa ongezeko hilo ndani ya siku saba.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa kwamba shule ya awali ya AL MUNTAZIR UNION NUSERY SCHOOL ya Dar es Salaam imeongeza ada kutoka shilingi 1,580,000/= mwaka 2015 hadi kufikia shilingi 1,980,000/= mwaka 2016 sawa na ongezeko la shilingi 400,000/=. Aidha, shule ya msingi ya AL MUNTAZIR BOYS PRIMARY SCHOOL ya Dar es Salaam imeongeza ada kutoka shilingi 1,820,000/= mwaka 2015 hadi shilingi 2,480,000/= mwaka 2016 sawa na ongezeko la shilingi 460,000/=
Mheshimiwa Spika, pamoja na barua mbalimbali zilizoandikwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar na Kamishna mwenyewe ambayo kopi yake tunayo bado shule hii imeendelea kukaidi. Hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua, hii shule ya AL MUNTAZIR inapata wapi nguvu ya kukaidi maagizo ya Serikali waziwazi? sambamba na hilo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa msimamo wake kuhusu katazo lake la ongezeko la ada kwa shule zisizo za Serikali, na namna inavyolisimamia utekelezaji wa agizo hilo.
8. UPANGAJI WA BAJETI YA WIZARA YA ELIMU
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto ya muda mrefu ya upangaji wa matumizi katika sekta ya elimu. Mara zote upangaji wa bajeti ya sekta umeshindwa kuzingatia uwiano unaokubalika kati ya matumizi ya kawaida na yale ya maendeleo. Uchambuzi wa bajeti ya wizara unaonesha kuwa kati ya shilingi bilioni 897.6 za bajeti ya Wizara zilopangwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo, shilingi bilioni 427.5 ambazo ni sawa na asilimia 47.6% zimepangwa kwa ajili ya kugharamia mikopo ya elimu ya juu.
Mheshimiwa Spika, athari ya kupanga fedha za mikopo katika bajeti ya maendeleo ili bajeti ya maendeleo inaonekane kuwa kubwa lakini kimsingi fedha inayokwenda kutekeleza miradi halisi ya maendeleo ni kidogo sana na hivyo kutokidhi mahitaji.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji, kama mkopo wa mafunzo ni uwekezaji kwa nini bajeti za mafunzo ya maofisa wa Wizara (Training domestic na Training outside) yako kwenye bajeti ya Matumizi ya Kawaida? Mafunzo kwa ajili ya walimu 7000 wa sayansi na lugha katika kasima 4001 ya SEDP yako katika bajeti ya matumizi ya kawaida. Kwa nini bajeti ya mafunzo ya Program 20 kasima ndogo 2001 ambayo ni shilingi bilioni 3.9 na Program 70 kasima ndogo 7001 yako kwenye bajeti ya matumizi ya kawaida? Upangaji huu wa bajeti ni kushindwa kuwa na msimamo unaowiana na hii husababisha miradi mingi ya maendeleo katika sekta ya elimu kutotekelezwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuwa na vigezo vya bajeti ya maendeleo katika wizara hii tofauti na ilivyo sasa ambapo fedha zinazoonekana dhahiri kuwa ni za matumizi ya kawaida zinawekwa kwenye bajeti ya maendeleo ili bajeti iungwe mkono wakati ki-uhalisia hakuna maendeleo yenye tija yatakayofanyika kutokana na upungufu mkubwa wa fedha za maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kama Serikali inadai kwamba mikopo ya elimu ya juu ni fedha za maendeleo kwa kigezo kwamba huo ni uwekezaji kwenye maendeleo ya rasilimali watu; basi isiwadai wanafunzi wanaopewa fedha hizo kugharamia elimu ya juu kwa kuwa ni uwekezaji kama uwekezaji mwingine wa miradi ya maendeleo ambayo serikali hugharamia bila kudai kurudishiwa fedha hizo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haioni sababu ya Serikali kuwadai wahitimu wa vyuo vikuu kurejesha fedha waliyokopeshwa kugharamia elimu waliyoipata kwa sababu gharama hiyo wataifidia kupitia kodi ya mapato (Pay As You Earn) pindi watakapoajiriwa. Kodi hiyo itakuwa ndio faida (economic returns) ya kuwalipia wanafunzi wa elimu ya juu ambayo inachangia moja kwa moja kwenye pato la taifa na uchumi kwa jumla. Serikali itambue pia kwamba fedha inazowakopesha wanafunzi wa elimu ya juu inatokana pia na kodi waliyolipa wazazi wa wanafunzi hao.
9. CHANGAMOTO ZA KIBAJETI ZA UKAGUZI NA UHAKIKI WA UBORA WA ELIMU NCHINI.
Mheshimiwa Spika,ni dhahiri kwamba moja ya sababu zinazochangia kushuka kwa viwango vya ubora na ufaulu katika shule zetu za umma ni kutokuwepo kwa ukaguzi na ufuatiliaji. Kwa mujibu wa Takwimu za Elimu Tanzania (BEST 2015) ni asilimia 19.1 tu ya shule za msingi na asilimia 21.4 pekee ya shule za sekondari ambazo hukaguliwa kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, tafsiri ya takwimu hizo ni kwamba, serikali huchukua takribani miaka mitano kukamilisha ukaguzi wa shule zote za umma zilizopo. Kwa maneno mengine ni kwamba, shule hukaguliwa mara moja kila baada ya miaka mitano!
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, katika bajeti ya Mwaka 2016/2017, jumla ya shiligi bilioni 24.1 zimetengwa kwa ajili ya idara ya ukaguzi na vitengo vyake kwa ajili ya matumizi ya kawaida lakini takribani shilingi bilioni 22 zimetengwa kwa ajili ya mishahara na maslahi mengine ya watumishi katika matumizi ya kawaida. Hivyo kiasi cha takribani shilingi bilioni 2 pekee ndicho kilichobaki kwa ajili ya shughuli halisi za ukaguzi kama ununuzi wa mafuta ya gari, posho za wakaguzi, ukarabati wa magari, mawasiliano na programu za mafunzo au uelimishaji.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuona umuhimu wa ukaguzi na uhakiki wa ubora wa elimu na hivyo kutenga fungu rasmi katika mwaka mpya wa fedha 2016/17 lenye fedha za kutosha kukagua angalau asilimia 80 ya taasisi za elimu zinazostahili kukaguliwa hapa nchini.
10. MWONGOZO WA UTEKELEZAJI WA SERA MPYA YA ELIMU
Mheshimiwa Spika, Itakumbukwa kwamba sekta ya elimu sasa inasimamiwa na Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, iliyozinduliwa Februari 2015 na kuanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2015/2016. Katika sera hii serikali imeazimia kutekeleza, pamoja na mambo mengine; utoaji elimu msingi na sekondari bila ada, kuongeza ubora wa elimu kwa kuimarisha ukaguzi shuleni, kuboresha miundombinu na kuhakikisha kuna upatikanaji wa vifaa stahili vya kujifunza na kufundishia pamoja na kuongeza ubora wa walimu kwa kutoa mafunzo, motisha na kuimarisha udhibiti wa taaluma ya ualimu.
Mheshimiwa Spika, ili Sera hii iweze kutekelezwa kwa ufanisi, inahitaji itengenezewe miongozo (Guidelines) na Mpango wa utekelezaji (Strategy). Hata hivyo pamoja na kwamba baadhi ya matamko ndani ya sera hii yamekwishaanza kufanyiwa kazi (mfano utoaji elimu bure), bado mpango wa utekelezaji wa sera hii haujakamilika mpaka hivi sasa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa maelezo mbele ya bunge hili kwa nini mkakati wa utekelezaji wa sera ya elimu haujakamilika na kuanza kutumika hadi leo huku baadhi ya matamko yakiwa yameanza kutekelezwa?
11. WANAFUNZI WALIOHAMISHWA KUTOKA VYUO VYA ST.JOSEPH
Mheshimiwa Spika,kwa muda mrefu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliiomba Serikali kuhamisha vijana hao kutokana na mazingira mabovu ya kujifunzia na kufundishia. Hii ni pamoja na ukosefu wa walimu wenye sifa na program zisizo na ulinganifu na Vyuo vingine. Nilifuatilia jambo hili hadi kufanya ziara katika Vyuo hivi na kujionea hali mbaya isiyokubalika. Baada ya kupiga kelele nyingi humu Bungeni, Naibu Waziri aliahidi kwenda pamoja na TCU kuona hali halisi katika vyuo hivyo. Jambo la kustaajabisha ni kwamba walituletea ripoti ya hovyo na ya kisiasa zaidi na kusema kuwa hali ni shwari; lakini jambo linaloshangaza zaidi ni kwamba leo wanafunzi wale wamehamishwa .
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa majibu ya kina ni kwani nini mwaka jana watendaji wa TCU na wa Wizara walisema hakuna tatizo na watendaji hao hao mwaka huu wameona kuna tatizo la msingi na kuwahamisha wanafunzi wa vyuo hivyo?. Je, wanafunzi hao watalipwa nini kwa muda waliopoteza?. Na ni nini hatma ya vyuo hivyo??
Mheshimiwa Spika, jambo linalokera zaidi ni baadhi ya vijana hawa sasa wamekwama kwenye vyuo waliovyohamia kwa kuwa kozi walizokuwa wanasoma zinatofautiana na pia kutokana na kuwa na mihula tofauti wengi wao wanalazika kurudia mwaka wa masomo ausemista.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji ni kwanini TCU ilivisajili vyuo hivi na kuvipa ithibati? Pili ni kwanini vyuo hivi vina mihula tofauti na vyuo vingine? Na pia ni fedha kiasi gani zimepotea katika kuwalipia mikopo vijana hawa na sasa hawajui ni lini watahitimu masomo yao? Ni nini hatma ya vyuo hivyo na ni mfumo gani wa elimu yetu unaoruhusu wahitimu wa kidato cha nne kujiunga na vyuo vikuu kwa kisingizio cha special programs?!!
Mheshimiwa Spika, kitendo cha Waziri wa Elimu kuivunja bodi ya TCU jana tarehe 25 Mei, 2016 kutokana na kudahili wanafunzi wasio na sifa kujiunga vyuo vikuu siku moja kabla ya mjadala wa hotuba yake ya bajeti ya Elimu ni kujaribu kwa hila kulizuia bunge kujadili kwa kina udhaifu mkubwa wa Serikali kupitia TCU katika kusimamia ubora wa Elimu ya juu hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ni hatua gani za ziada itachukuwa kwa wajumbe hao wa bodi kwa kuwa wamewaharibia wanafunzi maisha yao na kupoteza fedha za umma kutokana na maamuzi yao?
12. MABORESHO YA MFUMO WA ELIMU NCHINI
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikitoa angalizo kuwa mfumo wetu wa elimu umepitwa na wakati; hivyo upitiwe upya na kufanyiwa maboresho ili uendane na mabadiliko yanayotokea katika nyanja mbalimbali duniani.
Mheshimiwa Spika, elimu ya nchi yetu imekumbwa na matatizo mengi ya ki-mfumo jambo ambalo pamoja na madhaifu mengine limechangia sana kushuka kwa ubora wa elimu ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa matatizo yanayoikumba sekta ya elimu hapa nchini yamekuwa yakijirudia rudia; na kwa kuwa mara kadhaa serikali imekuwa ikifanya maamuzi ya kisiasa zaidi kukabiliana na changamoto zinayoikumba sekta ya elimu jambo ambalo halijatoa ufumbuzi wa kudumu wa kuondokana na changamoto hizo; na kwa kuwa wadau wote wa elimu wana matamanio ya kuona ubora wa elimu yetu unaongezeka; Hivyo basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kwa hatua ya sasa kuunda tume ya kitaalamu kwa ajili ya kuupitia upya mfumo wa elimu inayotolewa Tanzania ili pamoja na kukuza ubora wake lakini pia elimu hiyo iweze kwenda sambamba na kasi kubwa ya mabadiliko ya kiuchumi duniani.
13. DHANA YA UGATUZI KAMILI WA MADARAKA (DECENTRALIZATION BY DEVOLUTION) NA MKANGANYIKO WA USIMAMZI WA SEKTA YA ELIMU NCHINI
Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa dhana ya ugatuzi kamili wa madaraka, yani D by D, huduma nyingi za kijamii zikiwemo afya na elimu zimeshushwa katika ngazi ya Serikali za Mitaa na Wizara za sekta husika zimeachwa na jukumu la kusimamia sera za sekta husika na kusimamia taasisi chache tu kulingana na itakavyopangwa na wizara husika.
Mheshimiwa Spika, pamoja utaratibu huo kutajwa kuwa una nia njema ya kuwapa wananchi madaraka zaidi kupitia serikali zao za mitaa, lakini utaratibu huo umeleta mkanganyiko mkubwa sana katika usimamizi wa sekta ya elimu nchini.
Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu tuliona jinsi matatizo ya walimu yalivyokuwa yanashindikana kutatuliwa kutokana na kuwa na mamlaka nyingi mno zinazoshughulika na walimu hadi tukafikia uamuzi wa kupendekeza kwamba kuwe na chombo kimoja kitakachoshughulikia masuala ya walimu yani TETRA – Tanzania Education and Training Authority, jambo ambalo mpaka sasa halijatekelezwa na Serikali. Hata hivyo, haiwezekani kutokana na mfumo wa D by D, waziri awe na mamlaka tu na vyuo vya ualimu na vyuo vikuu na kuacha taasisi nyingine zote za elimu na kazi zake katika mamlaka nyingine.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuangalia upya mfumo wake wa ugatuzi madaraka ili usilete mwingiliano wa kiutendaji katika ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa lakini pia kuweka mfumo ambao kutakuwa na chombo kimoja kikuu cha kitaifa kitakachoshughulikia kwa ukamilifu masuala ya elimu kuliko ilivyo sasa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuona matatizo ya ugatuaji hapa nchini, niliamua kusoma vitabu vingi vinavyohusu dhana ya ugatuzi na nimegundua kuwa Tanzania hatutekelezi kabisa dhana ya D by D bali tunachofanya ni D by C yaani Decentralization by Deconcentration na ndio maana mambo hayaendi, Hivyo basi nashauri serikali isome vitabu vinavyoelezea dhana hii ili waielewe kwa undani.
14. UBUNIFU KATIKA SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Spika, hakuna Taifa duniani lililoendelea bila kuwekeza kwenye Sayansi na Teknolojia. Ni ukweli usiopingika kuwa, Sayansi na Teknolojia vinachangia sana katika maendeleo ya Taifa lolote. Mageuzi ya Sayansi na Teknolojia yanaleta hamasa ya ubunifu, pamoja na kuvutia zaidi ushiriki wa sekta binafsi katika kuendeleza Sayansi ya Teknolojia na ubunifu. Ni wazi mageuzi haya yanahitaji fedha nyingi hasa za utafiti. Jambo la kusikitisha ni kwamba, Serikali haitoi fedha kwa ajili ya utafiti; kwa mfano, bajeti ya 2015/2016 sekta hii ilikuwa na upugufu mkubwa na hata baada ya agizo la tengeo la1% ya pato ghafi la Taifa (GDP). Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze ni kiasi gani cha pato ghafi la Taifa limetengwa kwa ajili ya utafiti katika bajeti ya 2016/17?
Mheshimiwa Spika, Inasikitisha sana kuona COSTEC ambacho ni chombo pekee cha kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu utafiti, sayansi na Teknolojia kilichoanzishwa na sheria Namba 7 ya mwaka1986 lakini bado Serikali haijaweza kuipata Tume hii walau 1% ya pato ghafi la Taifa. Mathalani kwa mwaka huu Tume imetengewa 0.04% ya Bajeti yote ya Serikali. Halafu tunategemea nchi itaendelea kwa utaratibu huu?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuipa kipaumbele Tume hii ili iweze kufanya tafiti zake na kusaidia Taasisi nyingine. Haiwezekani kasma 8001 inayohusu Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ipate asilimia 4 tu ya bajeti ya Wizara. Ndio sababu inayopelekea wabunifu kushindwa kuendeleza ubunifu wao na hivyo kuishia mitaani.
Mheshimiwa Spika, tulielezwa hapa kuwa COSTEC iliishauri kutoa mwongozo wa matumizi na Teknolojia ya kisasa itwaayo (Unmanned Aerial Vehicle UAV) itumiayo helicopters zinazoendeshwa bila rubani (drones). Teknolojia hii ni muhimu sana kwa ajili ya udhibiti wa majangili kuandaa mipango miji, upimaji ardhi na katika matukio kama mafuriko. COSTEC ilishauri Serikali kuainisha Teknolojia hii kama kipaumbele cha kufanya utafiti na hivyo Tanzania kuwa mstari wa mbele ikiwa taasisi zake zataitumia. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Serikali kulieleza Bunge hili kama ilitekeleza ushauri iliopewa na COSTEC kuhusu teknolojia hiyo.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2015/2016 Sekta hii ya Sayansi na Teknolojia ilipata fedha kidogo sana huku tukitamba tuko kwenye karne ya Sayansi ya Teknolojia. Kwa mfano mwaka jana iliyokuwa Wizara ya Sayansi na Teknolojia na Mawasiliano ilipokea hadi Aprili, 2015 shilingi bilioni 4.79 fedha za maendeleo sawa na 18.46% ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge lako tukufu.
15. MAREJESHO KANDAMIZI YA MIKOPO YA ELIMU YA JUU
Mheshimiwa Spika, yapo malalamiko ya Wahitimu wa vyuo vikuu walionufaika na mikopo ya elimu ya juu kwamba utaratibu unatumika wa kufanya marejesho ya mikopo hiyo ni kandamizi na hauzingatii mazingira magumu ya ukosefu wa ajira wahitimu hao wanayokumbana nayo mara tu baada ya kuhitimu elimu ya chuo kikuu. Kwa mujibu wa taarifa ya baadhi ya wahitimu wa elimu ya juu ni kwamba; badala ya Bodi ya mikopo kudai marejesho ya mkopo peke yake, bodi hiyo imeweka gharama nyingine juu ya mikopo hiyo.
Mheshimiwa Spika; Bodi ya mikopo imeweka kiwango cha adhabu kwa wanaochelewa kurejesha mkopo (penalty amount) na kiwango cha kulinda kuporomoka kwa thamani ya shilingi (retention of value charges). Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni haikubaliani na kiwango kilichowekwa na bodi cha kulinda kuporomoka kwa thamani ya shilingi (value retention fee) ya taktriban asilimia 50 ya deni lote.
Mheshimiwa Spika, ufuatao ni mfano wa hati ya madai ya marejesho wa mkopo kwa mhitimu wa chuo kikuu. Inasomeka kama ifuatavyo: “Kindly be informed that the deductions for the loans board will begin effectively May, 2016 and the deduction Percentage will be 8% from the basic salary.
If you have a complaint in accordance to this information, kindly see from HESLB
Chek no
Index
Full name
Principle
Amount
Penalty
Loan
Admin fee
Value
Retention fee
Total
Loan
Amount
Outstanding debt
6,946,000.
694,600
69,460
2,833,344
10,543,404
10,543,404
CHANZO: HESLB
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kufuta gharama ya ‘Value Rentention Fee’ inayowatoza wahitimu wanaporejesha mikopo ili kuwapunguzia ukali wa maisha wahitimu hao ukizingatia wengi wao bado hawajapata ajira na waliopata ajira bado mishahara yao ni midogo. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni bado inasimamia msimamo wake wa kuitaka Serikali kutowadai wahitimu wa elimu ya juu kwa kuwa fedha inayowapatia ni bajeti ya maendeleo ya wizara husika kama ilivyo kwa wizara nyingine na hivyo Serikali haipaswi kudai fedha hizo kama ambavyo haidai kurejeshewa fedha inazotoa katika miradi mingine ya maendeleo.
16. UNYANYASAJI WA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU
WANAOHISIWA KUUNGA MKONO UPINZANI
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na tabia mbaya sana ya baadhi ya wakuu wa vyuo vikuu hapa nchini kuwanyanyapaa na kuwadhalilisha na hata kudiriki kuwafukuza chuoni wanafunzi ambao kwa hisia zao wanafikiri wanaunga mkono harakati za vyama vya upinzani.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa kwamba aliyekuwa kiongozi wa Serikali ya Wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dodoma amesimamishwa masomo kwa hisia tu kwamba alikwa mfuasi wa CHADEMA. Aidha, aliyekuwa makamu wake, tena msichana, aliamriwa na uongozi wa chuo hicho kukabidhi madaraka yake, kwa uongozi mwingine wa serikali ya wanafunzi ambao haukuchaguliwa na wanafunzi (uliteuliwa na utawala wa chuo) kinyume kabisa na katiba inayoongoza Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho.
Mheshimiwa Spika, mwanafunzi huyu (msichana) alitakiwa kupongezwa na uongozi wa chuo kwa kuthubutu kugombea nafasi hiyo na kuonyesha uwezo mkubwa wa uongozi, lakini alisakamwa na uongozi wa chuo na kutishiwa maisha, jambo lilomfanya afungue shauri mahakamani kupinga kulazimishwa kuachia madaraka. Hata hivyo, zilipoonekana dalili za yeye kushinda, chuo kilimwandikia barua ya kumfukuza chuo kabla ya hukumu.
1. Mheheshimiwa Spika, hukumu imetoka na huyo mwanafunzi ameshinda kesi. Utawala wa chuo hicho umedharau amri ya Mahakama ya kumrejesha na kumpa ushirikiano kiongozi huyo halali wa Serikali ya Wanafunzi kwa nafasi ya Makamu wa Rais; mwanafunzi huyo ananyanyapaliwa na uongozi wa chuo kikuu cha Dodoma jambo ambalo kwa vyovyote vile litaathiri masomo yake ikizingatiwa kwamba zimebaki wiki chache kabala hajafanya mtihani wa kuhitimu shahada yake ya kwanza. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa maelezo mbele ya bunge hili ni kwa nini haijamchulia Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma hatua za kinidhamu kwa kuendeleza unyanyapaa na unyanyasaji wa wazi kwa wanafunzi wa chuo hicho kwa hisia zake tu kwamba wanafunzi hao ni wafuasi wa CHADEMA/UKAWA? Ina maana UDOM ni kwa ajili ya wanafunzi wa CCM? TUME YA WALIMU (TEACHERS SERVICE COMMISSION)
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kwa muda mrefu imekuwa ikipinga utaratibu wa walimu kuwa chini ya mamlaka tofauti za ajira jambo linaloleta mkanganyiko kwao hasa pale wanapokuwa na madai mbalimbali kuhusu maslahi yao. Walimu walikuwa wakipata tabu kujua ni mamlaka ipi kati ya Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma au Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, au Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi .
Mheshimiwa Spika, Baada ya kelele nyingi, hatimaye serikali ilileta muswada wa Sheria ya kuanzisha Tume ya Utumishi wa Walimu (Teachers Service Commision) mwezi Julai, 2015. Nia ya Serikali kuleta muswada ule ililenga kuwalaghai walimu ili waipigie CCM kura katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015, na ndio maana uliletwa Julai, 2015 tena kwa matangazo na mbwembwe nyingi hadi kufikia hatua ya Rais wa wakati huo Jakaya Mrisho Kikwete kuupigia kampeni kwa Chama cha Walimu (CWT) na wadau wengine wa elimu tofauti na njia za kawada za Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii kukutana na wadau ili mradi tu ionekane kwamba Serikali ilikuwa inawajali walimu sana.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuwaarifu walimu wote nchini kwamba Seriakali hii ya CCM haijawahi kuwa na nia ya dhati ya kutatua kero zake, ila inakaa na walimu kimkakati tu kwa malengo ya kubembeleza kura zao, na wakishapiga kura hizo matatizo yanaendelea kubaki palepale ndio maana hadi leo pamoja na Tume hiyo ya Utumishi wa Walimu kutengewa fedha bado wajumbe hawajateuliwa ikiwa ni miezi tisa tangu sheria hiyo itungwe; Pili vifungu vingi vya Sheria hiyo ni vya muundo na majumumu ya tume hiyo pamoja na makatazo na adhabu na haionyeshi kero za walimu zitashughulikiwa namna gani. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ilete Bungeni muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria hiyo ili vifungu vyote vyenye mapungufu viweze kufanyiwa marekebisho ili sheria hiyo iwe bora na yenye kutatua kero za muda mrefu za walimu.
17. KUHAMISHWA KWA MAFUNZO YA WALIMU KUTOKA KURUGENZI YA WALIMU YA WEST HADI NACTE (NATIONAL COUNCIL FOR TECHNICAL EDUCATION)
Mheshimiwa Spika, tangu tupate uhuru, nchi imekuwa ikifanya mipango na mikakati ya kutoa elimu bora kwa ajili ya wananchi wake. Serikali imekuwa inaweka vyombo au taasisi mbali mbali kutekeleza jukumu la utoaji ya elimu. Ili kuhakikisha tunaenda vizuri, serikali imekuwa inafanya mapitio ya utoaji wa huduma hasa elimu. Mapitio hayo (reviews) yamekuwa yanategemea kwanza; utafiti wa kisayansi, na pili ushirikishwaji mpana wa wadau wote.
Mheshimiwa Spika, Jambo la kushangaza ni kuwa bila utafiti wowote wa kisayansi wala ushiriki wa wadau wa elimu kwa niaba ya wananchi, MAFUNZO YA UALIMU (Teachers Education) yamehamishwa kutoka Kurugenzi ya Ualimu ya WEST na kupelekwa Mafunzo ya Elimu ya Ufundi (NACTE).
Mheshimiwa Spika; malengo na makusudi ya mafunzo ya walimu yanatofautiana sana na malengo na makusudi ya mafunzo yanayotolewa chini ya NACTE.
Mheshimiwa Spika, Makusudi ya Elimu ya Ufundi ni inayotolewa chini ya NACTE ni kama ifuatavyo; naomba kunukuu:-
§ Technical Education objective is to prepare graduates for occupations categorised as skilled crafts below engineering profession and hence employees are called technicians guided by 1996 National Technical Education Policy.
§ NACTE quality controls and regulates technical education.
Mheshimiwa Spika, matokeo ya kufanya uhamisho huu ni sawa na kuweka mafunzo ya Ualimu kama fani ya ufundi tofauti na Ualimu kama taaluma inayojitegemea kama sheria, Uhasibu au ununuzi ambazo zote zina bodi zake.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani ina mtazamo kwamba, uamuzi huo wa Serikali usipobatilishwa, basi Changamoto zafuatazao zitatokea.
i. Kuongezeka kwa gharama za uendeshaji kutokana kubadilika kwa muundo wa utawala (organizational structure).
ii. Kutakuwa na shida ya kupata wanafunzi wa kujiunga na vyuo kwa vile vyuo vikuu navyo vinawaangalia hao hao kutoa vyeti na diploma.
iii. Kutokwepo harmonization kati ya TCU na NACTE juu ya mafunzo ya walimu hasa ubora wake.
iv. Ugumu wa kuendesha vyuo kwa vile serikali haitapeleka fedha tena.
v. Falsafa (philosophies) mbali mbali za vyuo vya bainafsi na umma na hivyo kuongeza kwa mkanganyiko.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa majibu mbele ya Bunge hili juu ya maswali yafuatayo:-
i. Kulikuwa na sababu gani (rationale) ya kuhamisha mafunzo ya walimu toka Kurugenzi ya Mafunzo ya Wizara ya Elimu kwenda NACTE?
ii. Je, kuna utafiti gani wa kisayansi uliofanyika kuhalalisha mabadiliko hayo?
iii. Je, wadau walihusihwa kuhusu jambo hili?
iv. Kuna faida na hasara gani ya kufanya huu uhamisho huo?
v. Kuna mikakati gani iliyowekwa kuhakikisha kuwa ubora wa elimu hautaathirika?
vi. Kuna mikakati gani iliyowekwa kuhakikisha uandiskishaji wa walimu wanafunzi kukidhi mahitaji ya vyuo husika?
vii. Vyuo hivi vitawezaji kuwa endelevu bila ruzuku ya serikali?
viii. Je, mitaala itawezaje kuwa harmonized kwa ajili ya vyuo vyote?
18. MAPENDEKEZO YA JUMLA YA KUBORESHA SEKTA YA
ELIMU NCHINI
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa imebainika dhahiri kwamba elimu ya Tanzania imekuwa inaporomoka kwa sababu ya uwekezaji hafifu katika rasilimali watu katika sekta hiyo – yaani taaluma na mafunzo kwa walimu; na kwa kuwa imebainika pia kwamba mitaala mibovu isiyokidhi viwango imechangia sana kushuka kwa ubora wa elimu hapa nchini; hivyo basi , Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwa Serikali kufanya mambo yafuatayo:
1. Kuboresha Mitaala elimu ili ishabihiane na mahitaji ya jamii na mabadiliko makubwa yanayoendelea kutokea duniani katika nyanja mbalimbali.
2. Kuelekeza na kusimamia matumizi ya kitabu kimoja cha kiada ili kufanya vijana wetu wasitofautiane katika ufahamu wa mada zinazofundishwa kwani wanafanya mitihani mmoja.
3. Kusimamia utungaji na uchapaji wa vitabu na kuhakikisha kuwa vina ubora wa hli ya juu kwani vitabu ndio kiongozi kwa walimu.
4. Kuongoza majadiliano na wadau wa elimu na kuweka msimamo juu ya Lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu kwani bado ni tatizo kubwa. Haiwezekani katika nchi moja baadhi ya shule zitumie Kiswahili na nyingine Kiingereza.
5. Kuwekeza katika Vifaa vya kufundishia na kujifunza ili kuondoa vikwazo katika utekelezaji wa mataala.
6. Kuboresha Miundo mbinu na mazingira ya shule. Miundo mbinu iliyopo bado ni mabovu sana; ukosefu wa vyoo, madarasa n.k. watafiti wamesema ni asilimia nne tu ya shule za sekondari nchini ndizo zinazokidhi vigezo vya chini kabisa vya hadhi ya sekondari. Hii ni takribani shule 160 tu kati ya shule za sekondari zaidi ya 4000 zilizopo nchini.
7. Mafunzo kwa walimu ni muhimu mno ili waendane na mabadiliko yanayojitokeza. Taarifa ya CAG inafafanua kwa undani tatizo hilo kwamba ni walimu 61,531(31%) tu kwa shule za msingi na 11% kwa walimu wa Sekondari.
8. Mazingira ya walimu ni mabaya sana kama nilivyoeleza awali hivyo, tunaamini mwalimu ni wakala mzuri wa kubadilisha hali mbaya ya elimu nchini. Bila kurekebisha maslahi ya mwalimu hata uwekeze vipi kwa kujenga madarasa kwa dhahabu vitakuwa kazi bure, sambamba na hili pawepo usimamizi thabiti kuhakikisha walimu wanatimiza wajibu wao.
9. Motisha kwa walimu ninajua baadhi ya walimu wanajituma sana hivyo, Serikali iwatambue na kutunzwa ili kuwatia moyo na kuwahamasisha wengine.
10. Kuajiri walimu wenye sifa stahiki – yaani waliofuzu na kufaulu vizuri katika taaluma inayokidhi mahitaji katika shule husika,
19. HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, aliyekuwa Rais Marekani, Abraham Lincoln aliwahi kusema, namnukuu;
“The philosophy of the school room in one generation will be the philosophy of government in the next” - kwamba “Falsafa ya elimu inayotolewa darasani kwenye kizazi cha leo ndiyo itakayokuwa hatma ya serikali yetu ya kesho”. Kama tutaendelea kuzalisha wahitimu wanaotokana na elimu duni inayotolewa, iliyogubikwa na maamuzi mabovu ya kisiasa na vitendo vya ufisadi, ni dhahiri kuwa Taifa letu halitaweza kupata viongozi bora wa kuliongoza huko tuendako.
Mheshimiwa Spika, wakati wa kuchukua hatua za kunusuru elimu yetu ni sasa. Ni lazima tubadilike. Matatizo ya nchi hii hayataweza kamwe kutatuliwa kwa elimu hii duni tunayopandikiza kwa watoto wetu. Tunahitaji mapinduzi na mageuzi makubwa ya kielimu kuitoa Tanzania hapa ilipo na kuipeleka kwenye level nyingine. Suala la kuwa nchi ya uchumi wa kati, nchi ya viwanda, litaendelea kuwa ni hadithi za Bulicheka tu ikiwa hatutaondoa mapungufu mengi yanayokabili mfumo wetu wa elimu.
Mheshimiwa Spika, napenda kumalizia hotuba yangu kwa kusema kwamba, sera ya elimu bure ilianzishwa na CHADEMA. Ipo katika ilani ya uchaguzi ya CHADEMA chini ya mwavuli wa UKAWA tangu mwaka 2005, 2010 na hatimaye 2015. Lengo lilikuwa ni kutoa huduma ya elimu bure kwa ukamilifu wake kuanzia shule za awali hadi chuo kikuu. Maigizo ya ilani ya CHADEMA yaliyofanywa na CCM, yameishia kuondoa ada tu na michango midogomidogo ya uendeshaji wa shule hadi kidato cha nne tu, huku kukiwa na sintofahamu kubwa juu ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika shule hizo. Hali hii inapelekea kuporomoka zaidi kwa elimu.
Mheshimiwa Spika, kuna msemo usemao, ‘If education is expensive try ignorance’, tafsiri yake ni kwamba; kama elimu/ kuelimika ni gharama basi jaribu ujinga. Tanzania tumeamua kujaribu ujinga, kwa kutowekeza vya kutosha katika elimu na ndio maana elimu yetu imeporomoka na kufikia hapa ilipo.
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Elimu katika awamu ya kwanza Marehemu Jackson Makwetta alisema kwamba: “Tanzania ni kama mama mjamzito ambaye siku zake za kujifungia zimefika lakini hajifungui, hivyo Tanzania inahitaji mabadiliko vinginevyo itaendelea kudidimia kielimu na kiuchumi.” Kwa sababu hiyo; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuutazama upya mfumo wa elimu sasa kwa kuunda tume maalum ya kuupitia upya na kutoa mapendekezo ili Taifa liweze kuwa na mfumo bora wa elimu unaokidhi viwango vya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.
Susan Anselm Jerome Lyimo (Mb)
WAZIRI KIVULI NA MSEMAJI MKUU WA
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUDI
26 Mei, 2016