Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali na. 7 ya mwaka 2019

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
613
1,776
MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MAREKEBISHO YA SHERIA MBALIMBALI NA.7 YA MWAKA 2019 (THE WRITTEN LAWS (MISCELLANEOUS AMENDMENTS) (NO.7) ACT, 2019)

(Chini ya Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la Januari, 2016)


A. UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, Naomba kuanza utangulizi wangu kwa kunukuu maneno ya aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Jaji, Barnabas Samatta, katika kesi ya Mwalimu Paul John Mhozya dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwalimu Paul John Mhozya vs Attorney General, (No. 1) [1996] TLR 130 kwamba “The notion, apparently harboured by some people in this country, that the President of the United Republic of Tanzania is above the law is subversive of the constitution and the laws. All Government leaders, including the President, are, like the humblest citizen, bound to comply with the laws of this country. The maxim ‘The king can do no wrong’ has no place in our law even if the word ‘President’ is substituted for the word ‘King’. Everyone and every institution or organisation in this country is enjoined to pay respect to the principle of supremacy of the law, see Article 26(1) of the constitutional.

2. Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri isiyo rasmi ni kwamba; Mheshimiwa Jaji Mkuu Mstaafu alisema na ninanukuu, “dhana iliyojengeka miongoni mwa watu, katika nchi hii kwamba Rais wa Jamhuri yuko juu ya sheria ni kinyume cha katiba na sheria za nchi. Viongozi wote wa serikali akiwemo Rais ni sawa na wananchi wa kawaida kabisa wanaotakiwa kutii na kufuata sheria za nchi hii. Usemi kwamba, ‘Mfalme hawezi kukosea, hauna nafasi kabisa katika sheria zetu, hata kama neno Rais likitumika kama mbadala wa neno mfalme, kila mwananchi na kila taasisi katika nchi hii inatakiwa kuheshimu msingi wa ukuu wa sheria.Tazama Ibara ya 26(1) kwamba “kila mtu ana wajibu wa kufuata na kuitii Katiba hii na sheria za Jamhuri ya Muungano”.

3. Mheshimiwa Spika, mswaada huu unakuja katika kipindi ambacho, Tanzania imegubikwa na giza nene la ukiukwaji uliokithiri wa misingi ya kidemokrasia na uvunjwaji wa sheria na katiba. Ni Tanzania pekee ambayo ina sheria zinazomzuia mwananchi kuchagua kiongozi anayemtaka na hivyo kuchaguliwa kiongozi. Ni kipindi ambacho wenye mamlaka wanawanyima wananchi fursa za kushiriki katika utawala wa Taifa kwa sababu wasimamizi wasaidizi wanaona vyama wanavyopitia wananchi hao kugombea havijasajiliwa na msajili wa vyama vya siasa, kinyume na kanuni za uchaguzi, sheria na Matakwa ya Katiba ya Nchi.

4. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitarajia kwamba, sambamba na muswada huu uliowasilishwa ndani ya Bunge lako Tukufu, Serikali ingeleta muswada hapa Bungeni ili kuipatia Tume ya Taifa ya Uchaguzi majukumu ya kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwa mujibu wa Ibara ya 74 (6) (e) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maratajio haya ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na wapenda Demokrasia hapa nchini, yanakuja baada ya TAMISEMI kushindwa kusimamia uchaguzi wa serikali za Mitaa kwa kuonesha waziwazi upendeleo kwa chama tawala na kuwaengua wagombea wa vyama vya upinzani takribani wote na baadaye kutangaza kupitia Waziri wa TAMISEMI kwamba, wagombea wote waliochukua na kurejesha fomu wameruhusiwa kushiriki mchakato wa uchaguzi, kauli hiyo ni kinyume na mamlaka ya Waziri aliyonayo kisheria na kikanuni na hivyo kuonyesha dhahili namna ambavyo uchaguzi huu unavyoendeshwa kwa matakwa na hisia za viongozi badala ya sheria na kanuni.

5. Mheshimiwa Spika, tamko la waziri wa TAMISEMI la kuwaruhusu wagombea walioenguliwa kuendelea kugombea lina mapungufu makubwa yafuatayo:

Kwanza, linakiuka sheria na kanuni za uchaguzi wenyewe kwasababu Waziri hana Mamlaka hayo,

Pili, tamko lake linadhibitisha kuwa wasimamizi wasaidizi wameondoa wagombea kinyume cha kanuni na sheria na kwa hiyo hawawezi kuwa na hadhi ya kuendelea kusimamia uchaguzi huu.

Tatu, kuwarejesha walioenguliwa bila kuangalia walionyimwa haki ya kuchukua fomu na kurudisha haiwezi kuwa suluhu ya tatizo lililopo.

6. Mheshimiwa Spika, hadi sasa msimamo wetu ni kwamba, hatutashiriki uchaguzi huo kwa kuwa kushiriki kwetu itakuwa ni kuhalalisha haramu kuwa halali. Tunapenda kuweka bayana kwamba, Waziri wa TAMISEMI hana uwezo na mamlaka kisheria kurudisha wagombea walioenguliwa na TAMISEMI yenyewe haina uhalali wa kimaadili (molar authority) wa kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema; namna pekee ya kufanya ni kuleta muswada Bungeni ili Bunge litunge sheria ya kuipatia Tume ya Taifa ya Uchaguzi majukumu ya kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwa kuwa NEC angalau ndiyo taasisi huru kuliko TAMISEMI, ilikuepusha mgongano wa maslahi katika uchaguzi huu.

7. Mheshimiwa Spika, Muswada ulioletwa mbele ya Bunge lako tukufu, unapendekeza marekebisho katika Sheria kumi na Moja. Sheria hizo ni Sheria ya Magonjwa ya wanyama, Sura ya 156, Sheria ya ustawi wa wanyama, Sura ya 154, Sheria ya Benki kuu ya Tanzania, Sura ya 197, Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura ya 134, Sheria ya Usimamizi na udhibiti wa VVU na UKIMWI, Sura ya 431, Sheria ya Usimamizi na uthibiti wa kemikali za viwandani na majumbani, Sura ya 182, Sheria ya Madini, Sura ya 123, Sheria ya Mazishi ya Viongozi wa kitaifa, Sura ya 149, Sheria ya Bandari, Sura ya 116, Sheria ya kuzuia ugaidi, Sura ya 19 na sheria ya Usajili na utambuzi wa watu Sura ya 36.

B. MAONI KATIKA MAREKEBISHO YA SHERIA MAHUSUSI

I. Marekebisho ya Sheria ya Magonjwa ya Wanyama (Sura ya 156)


8. Mheshimiwa Spika, Sehemu ya pili ya muswada ina rekebisha ya sheria ya Magonjwa ya Wanayama Sura ya 156. Kifungu cha 4 cha mswada kinarekebisha sheria mama kwa kurekebisha kifungu cha 62 cha sheria mama kwa kufuta maneno “three hundred thousand shillings or not more than five hundred thousands shillings or imprisonment for six months” na badala yake yawekwe maneno “five hundred thousands shillings but not exceeding ten million shillings or to imprisonment for a term of not less than six months but not exceeding twelve months”.

9. Mheshimiwa Spika, kiasi tajwa kama adhabu ni kikubwa sana na hakilingani na makosa. Kifungu hicho kinatokana na kifungu cha 62 cha sheria ya magonjwa ya wanyama ambacho kinasema mtu yoyote atakakwenda kinyume na matakwa ya sheria ya magonjwa ya wanyama atakuwa ametenda kosa.

10. Mheshimiwa Spika, kwa mfano makosa ambayo yanasemwa kutendeka chini ya sheria hii ya magonjwa ya wanyama ni pamoja na makosa ya kusafirisha mifugo kwa miguu au kwa kutumia usafiri nje ya eneo lililokaguliwa au kuwekewa kalandinga bila kibali. Mwananchi ambaye atakamatwa anaswaga Mbuzi wake wawili, kutoka eneo moja kwenda eneo lingine bila kibali huwezi kumtoza faini ya kati ya shilingi laki tano hadi milioni kumi na au adhabu ya kifungo cha miezi sita jela hadi waka mmoja. Adhabu lazima ilenge kurekebisha kuliko dhana ya sasa ya kutumia makosa kama chanzo cha mapato ya fedha kwa Serikali.

11. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 5 cha muswada wa sheria hii kinarekebisha kifungu cha 62 kwa kuongeza kifungu kipya cha 62A kinachohusu mfumo wa kufifilisha makosa, kwa maelezo ya kwamba jambo hilo litaepusha mchakato mrefu wa mashitaka na hivyo kuokoa gharama na muda na pia kupunguza mlundikano wa kesi.

12. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 5 cha mswada kinafanya marekebisho ya sheria mama kwa kuingiza kifungu kipya cha 62A (1) kinataka kuweka mazingira ya mtuhumiwa kukiri kosa kwa maandishi kwamba amefanya kosa kwa mujibu wa sheria ya magonjwa ya wanyama au sheria inayohusu idara nyingine, kifungu hiki kinampa mamlaka Mkurugenzi au Afisa aliyeidhinishwa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya kufifilisha makosa peke yake kabla ya kuanza kwa shauri mahakamani na kumtaka mtuhumiwa kulipa kiasi cha fedha kisicho zidi Milioni tano . Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba kifungu hiki kirekebishwe kwa kutoa mwanya uliopo kwenye maneno, “or any other sector legislation” kwa sababu sheria hii haihusiani na sheria za sector nyingine isipokuwa magonjwa ya wanyama pekee.

13. Mheshimiwa Spika, kifungu kidogo cha 62A (2) kinatoa mamlaka kwa Mkurugenzi kuongeza riba kwa mtu aliyeshindwa kulipa kiwango kilichotakiwa kulipwa kama ilivyoelekezwa kwe

nye kifungu cha 62A(1) hapo juu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona Serikali inataka kutumia njia hii kama mojawapo ya vyanzo vya mapato badala ya kuwa chombo cha kulea na kukuza sekta ya Mifugo nchini, kwa sababu mtu kushindwa kulipa faini aliyokiri inaweza kusababishwa na mambo mengi ikiwemo hali ngumu ya uchumi na umaskini ikizingatiwa inawezekana mtuhumiwa akawa ni mfugaji wa kawaida tu, hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani ilitegemea Serikali kutoa mwanya kwa mdaiwa kuongezewa muda wa kulipa badala ya kumuongezea riba.

14. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haikubaliana na kifungu cha 62A (3) kuwa mtu atakayeshindwa kulipa deni lililofifilishwa, Mkurugenzi anaweza kutekeleza amri ya kufifilisha sawa na na amri ya Mahakama na badala yake Kambi Rasmsi ya Upinzani Bungeni inataka uwepo utaratibu wa kusajili mahakamani hizo amri za kusisifilisha kama ambavyo tuzo nyingine zinasajiliwa mahakamani na jumuku la kutoa amri ya kutekeleza amri hizo litolewe na mahakama peke yake.

II. Marekebisho ya Sheria ya Ustawi wa Wanyama ( Sura ya 173).

15. Mheshimiwa Spika, sehemu ya III ya muswada huu unafanya marekebisho ya Sheria ya Ustawi wa wanyama Sura ya 173, kifungu cha 7 cha mswada kinafanya marekebisho ya kifungu cha 59 cha sheria mama ya Ustawi wa wanyama, sehemu ya VII inayohusu makosa na adhabu, ili kuongeza vitendo ambavyo ni makosa chini ya sheria hiyo. Kwa mujibu wa marekebisho haya itakuwa ni kosa mtu asipohakikisha kwamba wanyama waliochini ya uangalizi wake wanaishi bila njaa, kiu, woga, maumivu au majeraha.

16. Mheshimiwa spika, haieleweki ni kwa namna gani mfugaji anaweza kuadhibiwa ikiwa mnyama ambaye yuko chini ya uangalizi wake anaweza kupata woga, ambao hata mwangalizi mwenyewe hawezi na au kufahamu hata chanzo cha woga wa mnyama husika. Hata hivyo kiasi cha fedha kinachotajwa katika kifungu cha 7 cha muswada kwa kurekebisha kifungu cha 59(b) cha shilingi laki moja hadi milioni moja ni kiwango kikubwa sana kwa mfugaji wa kawaida na hivyo kinapaswa kupungua angalau kuwa kati ya elfu hamsini hadi laki tano.

17. Mheshimiwa Spika, tuangalie katika mazingira ambayo maeneo mengi ya malisho ya mifugo yanatwaliwa kwaajili ya matumizi mengine kama vile shughuli za madini, kilimo na kuwa hifadhi za wanyamapori na hivyo wafugaji kukosa eneo la malisho, jambo hilo ni wazi kabisa kuwa mifugo itakuwa na njaa. Aidha, katika mazingira ambayo mabadiliko ya tabianchi yameathiri maeneo mengi ya malisho na vyanzo vya maji kukauka. Je, katika mazingira kama hayo, mfugaji anatakiwa kuadhibiwa kwa mifugo kuwa na kiu au njaa?

18. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 8 cha muswada kinarekebisha kifungu cha 60(1)(a)kwa kufuta neno hamsini elfu na kuweka neno laki tano. Kiwango hiki cha fedha ni kiwango kinachotokana na dhana ya kufifilisha kwa makosa ambayo yameanishwa chini ya kifungu cha 59(1) ambayo mengine yameongezwa na marekebisho ya muswada huu, hata hivyo, maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhususiana na makosa ya kufifilisha ni yale yale. Aidha serikali iwekeze zaidi katika kuwajengea wananchi ufahamu wa kutovunja sheria za nchi katika sekta mbalimbali badala ya kuwavizia wafanye makosa ili Serikali ipate mapato yake.

III. Marekebisho ya Sheria ya Benki kuu ya Tanzania, (Sura ya 197)

19. MheshimiwaSpika, sehemu ya (iv) ya muswada huu unafanya marekekebisho sheria ya Benki kuu ya Tanzania, Sura ya 197, ambapo kifungu cha 10 cha muswada kinafanya marekebisho ya kifungu cha 34 cha sheria mama ya Benki kuu ya Tanzania. Kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha muswada huu, kifungu cha 34(1) cha sheria mama ya Benki kuu ya Tanzania kinarekebishwa ili kuweka matumizi sahihi ya neno “Serikali” ili kujumuisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

20. Mheshimiwa spika, Hata hivyo, marekebisho haya hayana msingi wowote kwa sababu, sheria namba 4 ya mwaka 2006 inayoitwa “The Bank of Tanzania Act, iliyochapishwa kwa amri ya Serikali katika Gazeti maalumu la Serikali ISSN 0856 – 0331X, Gazete No 5 la tarehe 8th June, 200

6 lenye kichwa cha habari kinachosema “ Act Supplement to the special Gazette of the United Republic of Tanzania No. 3 Vol 87 dated 8th June, 2006 Printed by the Government Printer, Dar Es Salaam, by Order of the Government” limeiandika sheria hii na kifungu hiki kama ambavyo Serikali inapendekeza sasa katika kifungu cha 10 cha muswada huu.

21. Mheshimiwa spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka serikali sasa kuliambia Bunge lako Tukufu nini dhamira ya kuleta mapendekezo haya ambayo tayari yako kwenye sheria za Tanzania, na ikiwa ni ukosefu wa umakini, uko wapi uwajibikaji wa Ofisi ya mwanasheria MKuu wa Serikali.

IV. Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi na uthibiti wa VVU na UKIMWI, Sura ya 431.

22. Mheshimiwa Spika, sehemu ya sita ya Mswada huu, unafanya marekebisho ya sheria ya Usimamizi na uthibiti wa VVU na UKIMWI ambapo jumla ya vifungu kumi vya sheria husika vinapendekezwa kufanyiwa marekebisho.

23. Mheshimiwa spika, kifungu cha 15 cha mswada huu kinapendekeza kufanya marekebisho kifungu cha 3 cha sheria mama, kwa kuongeza tafsili ya neno mtoto. Kwa mujibu wa mapendekezo haya Mtoto, kwa maana ya kupima virusi vinavyosababisha HIV ni mtu ambaye ana umri wa miaka chini ya 15. Aidha dhamira hasa ya mabadiliko haya ni kupunguza umri wa ridhaa ya upimaji kutoka miaka 18 ya awali hadi miaka 15 inayopendekezwa na serikali katika mswada huu.

24. Mheshimiwa spika, Kwa kuwa lengo ni hilo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba, kifungu cha 15 cha mswada huu ambacho kinarekebisha kifungu cha 3 cha sheria mama, kirekebishwe kwa kupunguza miaka kutoka 15 hadi miaka 12.

25. Mheshimiwa spika, ziko sababu mbalimbali za kufanya mapendekezo haya. Mosi, tayari Tanzania inazosheria nyingine ambazo zinatambua kuwa mtoto wa miaka 12 anaweza kuwajibika kisheria, Sheria ni pamoja na Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, ambayo kifungu cha 15(1)(2)(3) kinatambua kwamba mtu yoyote anaweza kufanya kosa la jinai akiwa na zaidi ya miaka 10 isipokuwa kwenye maswala ya kujamiiana ni kuanzia miaka 12, kwa hiyo marekebisho tunayopendekeza yataendana na kifungu hiki cha sheria hii.

26. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 33(2)(a) cha sheria ya kuthibiti na kuzuia Maambukizi ya VVU No 28/2008 kinatoa jukumu kwa mtu yoyote mwenye maambukizi ya VVU kumlinda mwingine dhidi ya Maambukizi, kifungu cha 4(1)(b) nacho kinatoa wajibu wa jumla wa kila mtu au taasisi kupambana na maambukizi ya VVU, sambamba na vifungu hivyo, kifungu cha 47 kinaeleza kusababisha maambukizi kwa mtu mwingine kwa kudhamiria itakuwa ni kosa ambalo kwa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Na.7 ya Mwaka 2019 ( yaani mswada huu ), kifungu cha 24(b) cha mswaada huu kinachorekebisha kifungu cha 47 cha sheria mama, kinaipatia mahakama uwezo wa kutoa amri ya kulipa fidia mtu atakayesababisha mwingine kuambukizwa VVU kwa makusudi. Ikimbukwe kwamba, vifungu vyote nilivyotaja hapo juu havitaji umri isipokuwa mtu, wajibu huu ni mgumu kutekelezeka kama unavyoelekezwa katika vifungu hivyo hasa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 15 ambao wameanza kujihusisha na vitendo vya ngono.

27. Mheshiwa Spika, mwaka 2009 Bunge lilitunga sheria ya mtoto namba 21, pamoja na kwamba kwa sheria hii mtoto ni mtu mwenye umri chini ya miaka 18, lakini kifungu cha 15 cha sheria hii kinampatia mtoto wajibu wa kulinda maadili pamoja na kutumia uwezo wake na akili yake kwa manufaa mapana ya jamii na taifa kwa ujumla. Sheria hii pia mtoto amepewa nafasi katika masuala mengine yanayomhusu kwa mfano, kifungu cha 39(2) (d) mtoto wa miaka 7 anaweza kufanya maamuzi na kuchagua anayetaka kuishi naye kati ya Baba au Mama, lakini katika masuala yanayohusu Afya yake kama upimaji wa VVU, Sheria ya UKIMWI Sheria inamkataza kupima VVU mpaka pale mzazi au mlezi atakapotoa ridhaa au atimize miaka 15 ambayo inapendekezwa sasa, ni miaka hii 15 ambayo tunapendekeza sasa ishuke hadi 12.

28. Mheshimiwa spika, kwa kuwa mtoto anahaki ya kutoa maoni na kushiriki kufanya maamuzi ya jambo lolote linaloathiri ustawi wake, upimaji wa VVU ni moja ya mambo yanayoathiri ustawi wake na hivyo ni maoni ya Kambi Rasm

i ya Upinzani Bungeni kwamba, Sheria ya UKIMWI inayomkataza mtoto kupima VVU bila ridhaa ya mzazi au mlezi wake inaathari za moja kwa moja haki yake ya kutoa maoni na kushiriki kufanya maamuzi. Kwa muktadha huo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba, kwa kubadili kifungu cha 15 cha mswada huu kinachohusu ridhaa ya upimaji kwa mtoto, itasaidia kuwapatia watoto nafasi ya ya kushiriki kufanya maamuzi kuhusu afya zao na wakati huo huo ikisadia utekelezwaji wa wa misingi ya sheria, ikiwemo sheria ya mtoto ya mwaka 2009.

29. Mheshimiwa Spika, Tukiangalia uzoefu kutoka nchi nyingine za Afrika, zikiwemo nchi ya Afrika kusini kupitia Sheria ya Mtoto Na. 38 ya mwaka 2005, kifungu cha 130(2)(a) kinaridhia mtoto kupima VVU akiwa na zaidi ya miaka 12 au chini ya miaka 12 ikiwa ana uelewa wa hatari, faida na athari za kijamii zinazohusiana na upimaji. Aidha nchi ya Afrika Kusini ilikwenda mbali zaidi kupitia kifungu cha 129 cha sheria hiyo, na kuruhusu ridhaa ya mtoto katika maswala mengine ya huduma za kiafya ikiwemo ridhaa ya matibabu na upasuaji kuwa miaka 12 na kuendelea.

30. Mheshimiwa Spika, Endapo Bunge lako tukufu litakubaliana na kupitisha marekebisho haya, Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza, kwa Afrika Mashariki kuwa na sheria ya hivi, nchi jirani ya Uganda, tayari inachokifungu kama hicho katika sheria yake ya kudhibiti na kuzuia UKIMWI ya mwaka 2014. Katika sheria hiyo, kifungu cha 10 (1) na (2) kinaruhusu mtoto wa miaka 12 kupima maambukizi ya VVU bila kupata ridhaa ya mzazi na au mlezi wake. Sheria hiyo ya nchi ya Uganda inakwenda sambamba na sera ya ushauri nasaha inayoeleza kwamba mtoto mwenye umri wa miaka 12 au zaidi anaweza kufanya maamuzi ya kupima VVU bila kuwa na ridhaa ya mzazi au mlezi. Nchi nyingine yenye kifungu kama hicho katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na kusini mwa jangwa la sahara ni pamoja na nchi za Rwanda Uganda, Lesotho, Malawi na Afrika Kusini.

31. Mheshimiwa Spika, Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani mwaka 2017 kuhusu kushushwa umri wa ridhaa ya kupima, unaonesha kwamba kadri sheria zinazohusiana na kupinguza umri wa ridhaa ya upimaji zinavyorekebishwa zinachangia kuongezeka kwa 11% upimaji wa VVU miongoni mwa watoto. Ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba, kwa kifungu cha 15 cha muswada huu kirekebishwe kutoka miaka 15 inayopendekezwa hadi miaka 12, kwa maslahi mapana ya Taifa hili.

32. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 18 cha mswada huu kinapendekeza kufanyia marekebisho kifungu cha 16 kwa kupendekeza kwamba, endapo mtu mwenye umri wa chini ya miaka 18 atapimwa VVU kwamba wazazi, walezi au mtu yoyote wa kuaminiwa na mpimwaji aweze kupokea majibu kwa niaba yake. Kifungu cha 16(2) (a) kilikuwa kina ruhusu mzazi au mlezi kupokea majibu ya vipimo vya VVU kwa niaba ya mtoto.

33. Mheshimiwa Spika, Ni mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba, kifungu hicho kibaki kama kilivyo kwenye sheria mama kwa sababu kitaathiri malengo ya Taifa. Tunapendekeza kwamba, watoto wenye ambao wanahitaji ridhaa ya wazazi ambao kwa maoni ya Kmabi Rasmi ya Upinzani ni watoto waliochini ya Miaka 12, hao tu ndiyo wapewe nafasi ya kujua majibu ya vipimo vya watoto wao, hali hii itaepusha watoto ambao wanaogopa kwamba ikiwa wazazi wao, walezi au mtu mwingine anaweza kujua hali ya afya zao basi hawatajitokeza kupima VVU na hivyo kukwamisha malengo ya serikali ya mapambano dhidi ya UKIMWI.

34. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 19 cha mswada kinafanya marekebisho ya kifungu cha 16 kwa kuongeza vifungu vipya vya 16A, 16B, 16C, 16D na 16E. Katika marekebisho hayo, Serikali inapendekeza Kurusu mtu kujipima VVU ikiwa ni pamoja na kueleza masharti yatakayo ambatana na upimaji huo.

35. Mheshimiwa spika, Pamoja na nia nzuri ya Serikali katika mapendekezo haya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba, kifungu cha 16 A (3) cha Muswada wa Marekebisho ya sheria mbalimbali No.7 ya mwaka 2019 kinachotaja kwamba; “A person below the age of eighteen years shall not undertake self-testing or be provided with self-testing kits” kiondolewe kwa sababu kifungu hicho kitawanyima watoto

wenye umri wa chini ya miaka 18 kijipima VVU katika mazingira ambayo, Takwimu za Tanzania HIV Impact Survey (THIS) 2016/2017, zinaonesha kwamba watoto wengi wanajihusisha na vitendo vya ngono kuanzia miaka 10 na kwamba maambukizi mapya kwa vijana wa miaka wa miaka 15 – 24 ni 40%.

VII. Marekebisho ya Sheria ya Madini, Sura ya 123

36. Mheshimiwa spika, sehemu ya nane ya muswada inapendekeza marekebisho katika sheria ya madini, Sura ya 123 kwa kile kinachosemwa na Serikali kwamba ni kuondoa changamoto ambazo zimejitokeza katika utekelezwaji wa shughuli za uongezwaji wa thamani madini.

37. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba mapema mwaka huu, Bunge lako Tukufu lilitunga na kupitisha sheria ya Marekebisho ya sheria mbalimbali Na.2 ya mwaka 2019, ambayo miongoni mwa sheria nyingine zilizofanyiwa marekebisho ilikuwemo sheria ya Madini, Sura ya 123. Kwa mujibu wa marekebisho hayo, sheria ya madini sasa inawataka wamiliki wa dealers licence kufanya biashara ya madini ndani ya soko la madini pekee, na hivyo kusababisha ugumu wa kufanya shughuli za uongezaji thamani madini katika masoko hayo.

38. Mheshimiwa Spika, kama Serikali ingekubali kupokea maoni mbadala huenda leo kabla hata ya mwaka kuisha yasingeletwa marekebisho haya, ni lazima sasa Serikali ijifunze kusikiliza maoni ya wadau na watu wengine kwa sababu mapendekezo yote yanalenga kubolesha na ni kwa maslahi mapana ya Taifa, kuliko Serikali kudhani kwamba kukubali ushauri ni kuonesha udhaifu.

39. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 42 cha muswada huu kinafanya marekebisho ya kifungu cha 73 kwa kufuta kifungu kidogo cha (3) cha sheria ya Madini. Hata kama Serikali ingesoma sheria yote kwa ujumla wake ingegundua kwamba, kwa kupendekeza marekebisho katika kifungu cha 73(3) ilipaswa pia kupitia muswada huu kupendekeza kufanya marekebisho ya kifungu cha 75(4)(b) cha sheria mama ya Madini, Sura ya 123.

40. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 42 cha muswada kinasema “the principle Act is amended in section 73, by-

(a) Deleting sub section 3; and

(b) Renumbering subsection (4) and (5) as subsection (3) and (4) respectively”.

38. Mheshimiwa Spika, Lakini kifungu cha 73(3) cha sheria ya Madini ambacho kimefutwa kinasema “An application for dealer licence in respect of gemstones shall be accompanied by commitment to acquire and utilize, in case of Tanzanian five lapidary machines and in the case of foreigner thirty (30) lapidary machines within three months from the date of grant of the licence.”

39. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 75 ambacho kinatoa muda wa kuhuisha leseni kinasema katika kifungu kidogo kwamba; “75(4) The holder of a dealer licence who applies in the proper manner shall be granted a renewal of his licence for a maximum period of twelve months unless:-

(a) he is in default;

(b) he is disqualified from holding or renewing a dealer licence under subsection (3) of section 73 or subsection (2) of section 78.

40. Mheshimiwa Spika, kama unavyoona hapo, ni dhahiri kwamba, kifungu hiki cha 75(4)(b) kinafanya marejeo kwenye kifungu cha 73(3) ambacho kwa mapendekezo ya kifungu cha 42 cha muswada kimefutwa. Kwa vyovyote vile kifungu hiki cha 75(4)(b) hakifanyi marejeo kwenye kifungu kipya cha 73(3) ambacho kimetokana na kuandikwa upya kwa kifungu kilichokuwa kifungu kidogo cha 4 na kifungu kidogo cha 5 ambacho sasa kinakuwa kifungu kidogo cha 4, kwa muktadha huo, kifungu cha 75(4)(b) kinapaswa kufutwa na Serikali wanapaswa kuingiza kifungu kipya kinachofanyia marekebisho kifungu cha 75.

41. Mheshimiwa spika, kifungu cha 43 cha muswada kinafanyia marekebisho sehemu ya V ya sheria mama ya Madini kwa kuongeza baada ya Kifungu cha 86B sehemu ndogo ya (iv) inayohusu utoaji wa leseni za ukataji na kung’arisha madini. Hata hivyo vifungu vya 86C, 86D, 86E havielezi kuhusu waombaji ambao watakuwa wameingia ubia. Kipindi cha leseni kinachotajwa chini ya kifungu kipya cha 86F kwa wenye leseni kubwa ni kidogo ukilinganisha na mtaji ambao utakuwa umewekezwa, ambao kwa mujibu wa kifungu kidogo cha (1) na (2) cha kifungu cha 8 cha sheria mama ya madini ni kati ya $100,00 hadi $100,000,000.

42. Mheshimiwa Spika, ni vigumu mwekezaji kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha kama hicho, halafu akanyimwa leseni ya kuendelea kwa sababu ambazo zinaelezwa katika kifungu kipya cha 86F(3). Pamoja na hayo, wakati Serikali ikifuta kifungu cha 73(3) ambacho kilikuwa kinamtaka mzawa kuwa na mashine 3 kabla ya kupewa leseni kifungu kipya cha 86G(2)(a) kinawataka wazawa ambao wanaomba leseni kubwa kuwa na mashine 10, kifungu hiki hakitoi nafasi kwa wazawa kuwekeza katika sekta ya madini na kutoa fursa kwao kuchangia uchumi wa Taifa lao. Ni maoni ya Kambi Raasmi ya Upinzani kwamba, Mashine zinazotakiwa zipunguzwe ili kuwawezesha wazawa ambao mitaji yao siyo mikubwa sana lakini wanapenda kuwekeza katika aina hii kushiriki kujenga uchumi wa Taifa lao.

C. HITIMISHO

43. Mheshimiwa Spika, Naomba kuhitimisha kwa kuwakumbusha viongozi wetu popote walipo kwamba, kamati kuu ya CHADEMA iliyokutana tarehe 7 Novemba, 2019 kutathimini mwenendo wa uchaguzi wa serikali za Mitaa 2019, iliazimia na kutangaza rasmi CHADEMA kujitoa katika mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kwa mukitadha huo, naomba kuwapongeza wagombea wetu wachache waliokuwa wameteuliwa kwa kuandika barua rasmi za kujitoa na kuwakumbusha waliobaki kama wapo, kuandika na kuwasilisha barua za kujitoarasmi kwenye mchakato huo ili CCM wapate ushindi wa kishindo wa 100% kama walivyo kusudia.

44. Mheshimiwa Spika, Baada ya kusema hayo naomba kuwasilisha!



SALOME WYCLIFFE MAKAMBA (MB)

K.N.Y MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI

KATIKA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

12 Novemba, 2019
 
Sasa hivi adhabu zimekuwa chanzo kikuu cha mapato. Badala ya kubuni adhabu kuzuia hasara, nchi inachekelea na kwenda mbali zaidi kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa imekusanya TZS kadhaa. So what? Mbona hatusikii kwamba wakosaji wamekiri kuwa hawarudii tena? Sasa hivi hata TRA isipokusanya mapato bado adhabu zinafanya kazi bila kuangalia athari za kuporomoka kiuchumi kwa raia.
 
Sheria zetu zimekuwa msaada kwa watendaji wa serikali kupata rushwa kutoka kwa wanao wahudumia.
 
Back
Top Bottom