Maofisa wa Tanzania waenda Kenya kuchunguza wafungwa

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,006
Tanzania yaenda Kenya kuchunguza wafungwa
Shadrack Sagati
Daily News; Friday,January 09, 2009 @21:15​

Serikali imetuma maofisa wake katika magereza mawili Kenya kwa ajili ya kuchunguza madai ya kuteswa, kunyanyaswa na baadhi yao kuuawa, yaliyotolewa na wafungwa Watanzania walio katika magereza hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliliambia gazeti hili jana kuwa wafungwa hao wamewasilisha malalamiko yao katika ubalozi wa Tanzania ulioko mjini Nairobi, Kenya.

Gazeti hili juzi liliandika habari za wafungwa hao wapatao 30 ambao wamefungwa katika Gereza la Kamiti mjini Nairobi ambao wanadai kuteswa na askari jela hadi wenzao wawili kuuawa na askari hao.

Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Nyasugala Kadege, amekuwa anatafutwa na gazeti hili ili aweze kuzungumzia suala hilo, lakini mara zote amekuwa akipokea simu na kudai yuko katika kikao na hawezi kuzungumza.

Membe katika kulifafanua suala hilo, jana alisema wafungwa hao waliwasilisha malalamiko katika ubalozi wa Tanzania Jumamosi iliyopita namna wanavyoteswa na askari wa Kenya ikiwamo kunyimwa chakula.

“Kutokana na malalamiko haya, sisi tumelazimika kuwatuma maofisa wetu waende kwenye magereza haya wakachunguze madai haya ya wafungwa Watanzania,” alisema Membe. Waziri huyo alisema maofisa hao watakwenda kuzungumza na wafungwa katika magereza ya Naivasha na Kamiti ili kupata ukweli wa mambo kuhusu madai hayo ya kuteswa kinyama.

Alisema serikali haiwezi kukaa kimya, kwani malalamiko hayo yametolewa na Watanzania; licha ya kuwa ni wafungwa, lakini wana haki ya kupewa haki kama binadamu wengine. Membe alisema wameiomba Serikali ya Kenya kuwaruhusu na kutoa ushirikiano kwa maofisa hao wa Tanzania katika kipindi ambacho watakuwa katika uchunguzi huo.

“Tunaamini Serikali ya Kenya itawaruhusu na hawatapata kikwazo chochote, ili waweze kujiridhisha na madai hayo ya unyanyasaji,” alisema Membe ambaye hata hivyo hakueleza idadi ya maofisa hao na siku ambayo wataanza uchunguzi huo.

Aliongeza kuwa mara baada ya uchunguzi huo, serikali itapokea taarifa na wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje watatoa tamko kuhusu matokeo ya uchunguzi huo. Alisema hatua nyingine ambayo serikali itafanya, ni kuona uwezekano wa kuwarudisha nyumbani wafungwa hao kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo kimataifa.

Membe alisema zipo taratibu ambazo ni lazima zifuatwe katika suala la kuwarudisha nyumbani wafungwa na akaongeza kuwa mchakato huo unahusisha wizara mbalimbali, ikiwamo ya Mambo ya Ndani. Waziri huyo alisema hata hivyo wafungwa ambao vifungo vyao ni vifupi, hakuna haja ya kuwarudisha nyumbani, bali wanaotumikia vifungo vya muda mrefu, ipo haja ya kufanya mchakato huo.

“Tunafanya hivyo si kwa vile sisi jela zetu ni ‘Paradiso’, hapana, ila tunaamini kuwa wafungwa wanastahili kuthaminiwa kama binadamu wengine,” alisema Membe. Hata hivyo, alionya kuwa suala hilo linaweza kuchukua muda mrefu si la kuharakisha kutokana na taratibu zake zilivyo kutokana na mikataba ya kimataifa inavyoelekeza.

Alipoulizwa iwapo Serikali ya Kenya itagoma kuruhusu maofisa hao kuchunguza suala hilo, Membe alijibu kuwa kuna taratibu za kimataifa ambazo zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kushirikisha vyombo vya kimataifa vinavyohusika na suala hilo.

Alisema malalamiko ya namna hiyo yaliwahi kutolewa na wafungwa hao miaka miwili iliyopita na serikali ilipotuma maofisa wake kuchunguza, waliruhusiwa na Serikali ya Kenya. “Ni kweli baada ya uchunguzi tulibaini kuwapo wafungwa wa Kitanzania waliofia gerezani, lakini walifariki dunia kwa ugonjwa si kuteswa,” alisema Membe.
Alisema malalamiko ya juzi ni mapya, hivyo serikali inalazimika kuyashughulikia haraka ili kujiridhisha.

Gazeti hili ndilo ambalo liliandika habari za wafungwa walioko katika Gereza la Kamiti mjini Nairobi kunyanyaswa na mamlaka za nchi hiyo, hali inayowalazimu kuiomba Serikali ya Tanzania kuwarejesha nchini ili watumikie adhabu zao wakiwa nyumbani. Wafungwa hao wanalalamika askari wa magereza nchini humo kuwanyanyasa kwa kuwapiga na kuwanyima chakula. Waliwataja wenzao wawili Hamis Kiando na Sultan Alipo huenda wameuawa kwani hawaonekani gerezani.

Baadhi ya wafungwa walioko katika gereza la Kamiti ni Haji Hassani, Rajabu Jata, Kanali Mohamed, Salehe Ali Issa, Iddy Nyembo, Musa Machota, Steven Kibuta, Time Zakaria, Ramadhan Kipato, Mussa Khamis na Abdallah Mohamed. Wengine ni Abeid Salum, Kassim Kessy, Ali Shindo, Said Kiondo, Khamis Salim, Ndamwene Hassan, Kefu Pashua, Said Ali, Saisal Islam, Mohamed Bahari, Kiando na Alipo.
 
Nimependa jinsi serikali inavyoanza kujua thamani ya raia wake isiwe hapa karibu hata huko ughaibuni serikali iwe inachukua hatua...(Ujifunze kwa wenzetu wanatuma jeshi na ndege kuchukua raia wao.....kama kuna matatizo.....
 
Back
Top Bottom