Manowari zaiokoa meli ya Tanzania

Msharika

JF-Expert Member
May 15, 2009
947
69
MELI ya Tanzania mv Barakaale 1 imenusurika kutekwa nyara na maharamia.

Manowari ya kivita ya Marekani ya USS Farragut imezuia shambulizi hilo katika Bahari ya Hindi.

Taarifa iliyotolewa jana na Ubalozi wa Marekani nchini, maharamia walitaka kuiteka meli hiyo Jumapili iliyopita. Maharamia hao walikamatwa, na kwa mujibu wa CNN walikuwa wanane.

“Baada ya kupokea taarifa ya kuomba msaada kutoka kwa nahodha wa mv Barakaale, helikopta aina ya SH-60B Seahawk, kutoka USS Farragut iliwasili na kuzuia mashambulizi mawili dhidi ya meli hiyo ya Tanzania,” taarifa hiyo ilisema.

Manowari Farragut ni sehemu ya kikosikazi cha kimataifa, kijulikanacho kama Combined Task Force 151, kilichoundwa Januari mwaka jana kwa lengo la kuzuia na kupambana na uharamia.

Lengo ni kulinda usalama wa vyombo vya usafirishaji majini na kuhakikisha kuwa vinakuwa na uhuru wa kupita katika eneo hilo kwa faida ya nchi zote.

Hata hivyo, habari zilizopatikana jana kutoka CNN zilisema jaribio hilo la utekaji nyara lilitokea katika eneo la Ghuba ya Aden.

Msemaji wa kikosi namba tano cha Marekani, Luteni Corey Barker alisema,watuhumiwa hao baadaye walichukuliwa na manowari hiyo ya Marekani.

Meli hiyo ya Tanzania ilishambuliwa katika eneo hilo hatari na kuvitaarifu vyombo vingine kwa njia ya redio kuhusu tukio hilo kabla ya helkopta kuwasili.

“Wakati wa shambulizi hilo … mabaharia walitumia mbinu za kujihami” ambazo zilisababisha watuhumiwa hao kudondoka baharini wakati wakijaribu kuingia ndani ya meli hiyo, kikosikazi hicho kilisema.

Mtuhumiwa mmoja aliokolewa na mashua ndogo ya maharamia, lakini alijaribu tena kuingia katika meli bila mafanikio.

Kuwasili kwa helkopta kuliwafanya maharamia hao kukimbia, huku helkopta hiyo ikiifuatilia mashua hiyo na kufyatua risasi kwenye tanga na mashua hiyo kusimama, taarifa ya kikosikazi ilisema.

Baada ya kusimama, askari wa USS Farragut waliingia kwenye mashua na kuwakamata maharamia hao wanane.

Kamanda Bernard Miranda wa majeshi ya wanamaji ya Jamhuri ya Singapore ambaye ndiye mkuu wa kikosikazi hicho, aliwapongeza mabaharia wa Barakaale kwa mbinu zao.

"Nahodha wa Barakaale alifanya kinachotakiwa kwa kukataa kusimamisha meli yake kwa kuiyumbisha na maharamia hao kushindwa kuiparamia,” Miranda alisema katika taarifa yake.

Kikosikazi hicho kiliundwa Januari mwaka jana,kinaendesha shughuli zake katika Ghuba ya Aden na maeneo ya pwani ya Somalia.

Ingawa idadi ya vitendo vya uharamia imekithiri katika eneo hilo, hususan mwaka jana, kikosi hicho kilisema juzi kuwa matukio ya utekaji yaliyofanikiwa yamepungua kwa asilimia 40.

Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Begum Tagi, alikiri kuwa wizara hiyo ina taarifa za tukio hilo, lakini kupitia tovuti ya Marekani.

Akaongeza kuwa bado inasubiri taarifa kutoka vyombo vya ndani kama vile Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra).

“Ni kweli tumesikia taarifa hizi kupitia tovuti ya Marekani ambayo imeonesha meli hiyo inapeperusha bendera ya Tanzania, lakini hatuna taarifa kupitia vyombo vyetu, ila kama wenye meli hiyo watatupatia taarifa pia itakuwa ni vizuri,” alisema Tagi.

Matukio ya uharamia katika pwani ya Somalia yamekuwa yakilenga meli nyingi za mizigo ikiwa ni pamoja na mafuta ambapo maharamia wa kisomali wamekuwa wakidai kikombozi.

Fedha hizo inadaiwa zimekuwa zikitumiwa na waasi wa Somalia wa kikundi cha Al Shabaab kwa ajili ya kupambana na majeshi ya Serikali dhaifu ya nchi hiyo.

Hii ni mara ya kwanza kwa meli ya Tanzania kushambuliwa na maharamia hao wa kisomali, ambao mwaka jana walifanikiwa kuteka nyara meli iliyokuwa na shehena za silaha za Kenya, lakini wakaiachia baadaye
 
Back
Top Bottom