Manispaa ya Moshi: Kuungua kwa Bweni la Kaloleni Islamic ni hujuma za watu wenye nia ovu

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,495
9,275
Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro imesema, matukio ya kuungua mara kwa mara mabweni ya Shule ya Seminari ya Wasichana ya Kiislamu ya Kaloleni ni hujuma.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Michael Mwandezi alisema hayo wakati akikagua athari za moto uliotokea Oktoba 8, mwaka huu, saa 1:15 usiku.

"Imefika mahali sasa tunaamini matukio haya ni mpango unaoratibiwa na baadhi ya watu wenye nia ovu, haiwezekani imepita siku 40 pekee tangu tukio la pili la moto la Agosti 26 mwaka huu, sasa umetokea tena, tunalaani matukio haya"alisema Mwandezi.

Alisema ingawa vyombo vya dola vinachunguza kubaini chanzo si cha tukio hilo mazingira ya matukio hayo yanashawishi kudhani kuwa matukio hayo yanapangwa.

"Lazima tuwaze mbali, haiwezekani wanafunzi hao ambao waliunguliwa bweni mwezi mmoja uliopita, wamehamishiwa hapa na moto umewafuata tena...huu ni mpango, tutawasaka wahusika, mbaya zaidi hata yale magodoro walipewa msaada yameungua tena"alisema.

Baadhi ya wanafunzi walisema walihisi harufu ya kiberiti kilichowashwa katika chumba cha kuhifadhi magodoro, kabla ya kulipuka kwa moto huo ulioteketeza bweni la Madina.

Wanafunzi 83 wa vidato vya kwanza, pili na tatu walinusurika.

Mwandezi aliomba wadau wajitokeze kuwasaidia wanafunzi hao kurejea katika hali yao ya kawaida kwa kutoa misaada ikiwemo ya magodoro, vitanda, madaftari, vitabu na sare za shule.

Mwanafunzi wa kidato cha tatu, Salma Maeda, alisema wakati anakwenda bwenini alisikia harufu ya kiberiti kilichowashwa na baadaye wakaona moto.

Mwanafunzi Pili Shamte wa kidato cha kwanza, alisema walishuhudia moto ukianza wakapiga kelele kuomba msaada na kwamba, baadhi yao walipoteza fahamu na kukimbizwa zahanati ya shule.

Wanafunzi wameomba wapewe likizo ya wiki moja au mbili ili serikali ifanye uchunguzi wa tukio na wao waende kununua sare nyingine na mahitaji mengine kwa kuwa vitu vyote zikiwemo nguo, vitabu, madaftari na magodoro vimeungua.

"Tunaomba msaada maana vitu vyote vimeteketea na nguo tulizobaki nazo ni hizi tulizovaa, hatuji kesho yetu ikoje, tunaomba tusaidiwe maana haitapendeza baadhi yetu wanavaa sare na sisi tunavaa nguo za kawaida madarasani"alisema Pili.

Mkuu wa shule hiyo, Husein Shaban alisema hadi sasa tathmini halisi ya hasara haijajulikana na timu ya wataalamu wakiwemo wa serikali wanafanya uchunguzi.

Alishukuru jitihada zilizofanywa kwa kuzima mtoto huo ingawa tayari uliathiri sehemu kubwa ya mabweni hayo na kwamba baada ya tukio masomo yalisimama kwa muda na yanatarajiwa kuanza tena leo Oktoba 12.

Alisema watoto wote wapo salama licha ya mshtuko waliopata na kwamba walipewa ushauri wa kisaikolojia ili kuwarejesha katika hali ya kawaida.

Mkaguzi kutoka Jeshi la Zimamoto mkoani Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi alisema walifika eneo la tukio saa 1.49 usiku na kwamba moto ulianzia katika chumba cha kuhifadhi magodoro na walifanikiwa kuudhibiti usihamie katika majengo mengine.

Alisema bado chanzo cha tukio hakijajulikana na kwamba uchunguzi unaendelea, na ameshauri kuongezwa ukubwa wa lango kuu la kuingia shuleni ili kurahisisha kutolewa msaada wa haraka.
 
Naanza kuamini maneno ya yule aliyesema kwamba huenda ikawa ni hujuma ili kuwaaminisha na pia kuwaogopesha wadau kwamba upande ule shule zao si salama
Baada ya kuona watu wameelevuka sasa na wanahitaji elimu yenye manufaa hapa na huko mbele tuendako ,
Tujitafakari
 
Hii ni michezo tu kuna kitu kinapangwa huko mbeleni usishangae ukasikia kuna shule ya kikatoliki imechomwa moto then ukasikia ni waislamu wanalipa kisasi ndio hapo migogoro inapoanzia
 
Hii ni michezo tu kuna kitu kinapangwa huko mbeleni usishangae ukasikia kuna shule ya kikatoliki imechomwa moto then ukasikia ni waislamu wanalipa kisasi ndio hapo migogoro inapoanzia
Duh Mungu aepushe tusifike huko.
 
Back
Top Bottom