Manabii na mitume wa leo jiaandaeni na mjifunze kuwatumikia kondoo

Ignas lyamuya

JF-Expert Member
Jan 17, 2019
777
856
WALIANDALIWA VEMA KATIKA VYUO VIKUU VYA MANABII

Watu wengi wanafikiri kuwa manabii waliotumiwa na Mungu wakati wa Agano la Kale walikuwa mbumbumbu na kwamba hawakuwa na elimu na wala hawakusoma falsafa na theologia. Haya ni mapokeo potofu na upotofu huu ndio unaowafanya baadhi ya watu wafikiri kuwa kuwa mhubiri wa Neno la Mungu au kuwa kiongozi wa Kanisa leo hakuhitaji elimu kubwa. Lakini mtu anaweza kujiuliza maswali kadhaa ili kujua kama kweli manabii wale walikuwa ni mbumbumbu au maamuma!

Hivi watu mbumbumbu wangewezaje kuandika vitabu virefu vyenye mpangilio mzuri wa hoja nzito zinazogusa mambo ya kiuchumi, kijamii, kiutawala na kisiasa? Hivi maamuma wa falsafa angewezaje kutoa andiko la kifalsafa kama alivyofanya Nabii Habakuki? Hivi mtu mbumbumbu angewezaje kutoa ujumbe uliojaa hoja za sayansi ya siasa, kidiplomasia, na uhusiano wa kimataifa kama walivyofanya Nabii Amos na Nabii Ezekieli? Mungu angewezaje kupitisha ujumbe uliokuwa na mikakati ya kijeshi kwa manabii mbumbumbu kama Mikaya na wengine wengi?

Majibu ya maswali hayo ni kuwa manabii waliotumika wakati wa Agano la Kale walikuwa ni watu makini na walioandaliwa kupitia vyuo vya kinabii na kusomea theologia na falsafa ya wakati wao. Chuo cha Betheli kilikuwa maarufu sana (2Wafalme 2:3). Chuo hicho kilikuwa kinawaandaa manabii kwa kuwafundisha theologia na falsafa ya wakati ule! Chuo kingine kilikuwa Yeriko (2Wafalme 2:5) na Chuo kingine kilikuwa Gilgali (2Wafalme 4:38). Inawezekana Nabii Eliya, Nabii Elisha, na Nabii Mikaya waliandaliwa katika vyuo hivyo na baadaye kila mmoja kwa wakati wake alifundisha katika vyuo hivyo.

Maneno yanayotumika kama 'wana wa manabii' hayana maana kuwa walikuwa ni watoto wa manabii au wafuasi wa manabii. Tafsiri inayoweza kuvitendea haki vifungu hivyo ni kuwa wale walikuwa ni wanafunzi wa unabii au wanachuo wa unabii au wana jumuiya ya chuo cha unabii. Kitendo cha Nabii Eliya kumuachia joho Nabii Elisha kinaweza kumaanisha kuwa Nabii Eliya ndiye aliyekuwa Mkuu wa Chuo na Elisha Makamu wa Mkuu wa Chuo, hivyo Nabii Eliya alipotwaliwa ndipo Nabii Elisha akawa ndiye Mkuu wa Chuo kimojawapo au vyote.

Makala hii imelenga kuwatia moyo na kuwahamasisha wale wote wanaojisikia kuitwa kumtumikia Mungu ili waone umuhimu wa kupata maandalizi katika vyuo maalum vya mafunzo ikiwemo kufanya mazoezi na kupata uzoefu chini ya uangalizi wa watumishi wa Mungu walio waaminifu na wazoefu. Ni vizuri watu wakaelewa kuwa hakuna njia ya mkato katika utumishi. Hatuoni ushahidi wo wote katika Biblia unaoonyesha kuwa Mungu aliwaita watu katika huduma ya unabii, ukuhani, au utume pasipo kuwapa maandalizi ya kutosha. Kupitia vyuo hivyo vya manabii, 'wana wa manabii' au 'jumuiya ya manabii' waliweza kwa pamoja kuwajibishana na kugundua imani au mafundisho potofu. Walikuwa na utaratibu maalum wa kuwapata viongozi wao kama ilivyokuwa kwa Elisha! Haikuwezekana kabisa kwa nabii kujiweka wakfu yeye mwenyewe kwa ajili ya huduma pasipo kuwekwa wakfu na manabii wengine.




Sent from my iPhone using JamiiForums
 
Back
Top Bottom