Mamia kupoteza ajira vituo vya mafuta

Salary Slip

JF-Expert Member
Apr 3, 2012
46,888
143,985
Mamia kupoteza ajira vituo mafuta

Hali hiyo inatokana na kusuasua kwa mauzo ya bidhaa hiyo, huku chanzo kimojawapo kikitajwa kuwa ni matokeo ya hatua mbalimbali za Serikali ya awamu ya tano katika kubana matumizi.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kwa siku kadhaa umebaini kuwa tishio hilo ni kubwa zaidi katika baadhi ya vituo baada ya wastani wa mauzo yake kwa siku kuporomoka katika siku za hivi karibuni hadi kwa kiwango cha takribani asilimia hamsini.

Aidha, uchunguzi huo umebaini kuwa hadi sasa, tayari baadhi ya kampuni zinazomiliki vituo vya bidhaa hiyo zimeanza kuchukua uamuzi mgumu wa kuviuza au kuvikodisha kwa watu wengine.

“Hali ya biashara hii kwa sasa imekuwa ngumu… katika baadhi ya vituo wastani wa mauzo umeshuka hadi kufikia chini ya asilimia hamsini na hii maana yake ni kwamba kuna mamia ya watu wanaotegemea kushamiri kwa biashara hii watapoteza ajira zao endapo hali haitobadilika,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe.

Baadhi ya maofisa waliozungumza na Nipashe kati ya vituo vingi vya kuuzia mafuta vilivyotembelewa kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salam na kukiri kuwa hali kibiashara imekuwa ngumu kwa sasa ni wa vituo vya Oil Com kilichopo eneo la Sayansi-Kijitonyama;

TSN – Bamaga na Puma (Mwenge); GBP kilichopo eneo la Mbezi na kituo cha Total kilichopo Mlimani City.

Aidha, baadhi ya vituo vya mafuta vilivyotangazwa kuuzwa ni pamoja na vile vinavyomilikiwa na Kampuni ya Muro Investiment Ltd vilivyopo Kibaha, Mkuranga na Mlandizi mkoani Pwani.

HALI ILIVYO
Katika uchunguzi wake huo, Nipashe imebaini kuwa mauzo ya jumla kwa siku katika vituo vingi vya mafuta jijini Dar es Salaam yamepungua na hivyo kushusha mapato.

Baadhi ya wauzaji waliiambia Nipashe kuwa wateja waliokuwa na kawaida ya kujaza mafuta mpaka pomoni kwenye matenki ya magari yao (full tank) wamepungua kwa kiasi kikubwa na sasa wengi wao hununua kiasi kidogo cha mafuta.

Licha ya kutokuwapo kwa ushahidi wa kitaalamu utokanao na utafiti, baadhi ya wauzaji wamekuwa wakihusisha kushuka kwa wastani wa mauzo yao kwa siku na hatua za Serikali za kubana matumizi, zikiwamo zile za kudhibiti vikao, semina, warsha, makongamano, madhimisho ya sherehe mbalimbali na pia safari za nje.

Baadhi ya wauzaji hao waliiambia Nipashe kuwa hali imekuwa ngumu baada ya wastani wa mauzo kushuka na kutishia ustawi wa biashara hiyo kulinganisha na ilivyokuwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita licha ya wao kuuza kwa kuzingatia bei elekezi iliyowekwa na serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati, Maji na Mafuta (Ewura).

Bei elekezi ya Ewura kwa mwezi huu jijini Dar es Salaam ni Sh. 1,860 kwa lita ya mafuta ya petroli na Sh. 1,720 kwa lita ya mafuta ya dizeli.

Mmoja wa wauzaji katika kituo cha mafuta cha TSN kilichopo Bamaga aitwaye Christian Costantine, alisema kwenye eneo lake mauzo yameshuka kwa kiasi kikubwa kulinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka jana.

Akitoa mfano, alisema pale walipokuwa wakiuza kwa wastani wa lita 5,000 kwa siku, sasa wanauza kwa wastani wa kati ya lita 2,000 na 3,000 tu kwa siku.

“Sasa hivi inaonekana wazi kuwa hali ya uchumi ni ngumu. Hivi sasa tunategemea wateja wengi wanoagiza mafuta kwa bill (ankara)," alisema Constatine na kuongeza:

"Kabla ya kipindi hiki bodaboda walikuwa wanakuja kuchukua mafuta ya kuanzia elfu kumi (Sh.10,000), lakini hivi sasa, wengi wao wanachukua mafuta ya Sh. 5,000 na hata Sh. 2,000 tu. Hatuuzi kiasi kikubwa cha mafuta ukilinganisha na zamani,” aliongeza.

Meneja Msaidizi wa Kituo cha Oil Com kilichopo Sayansi, Faisal Aboubakar, alisema wateja wanaowategemea zaidi kwa sasa ni wale wanaolipa kwa kadi na kwamba, kwa ujumla biashara kwao siyo nzuri kulinganisha na ilivyokuwa hapo kabla.

“Sisi hapa tuna wateja wa aina mbili. Kuna wateja wanaokuja kuweka mafuta wakiwa na fedha mkononi na tuna wale wanaotumia kadi... na sasa tunategemea zaidi wateja wa kadi ambao huchukua mafuta mengi ijapokuwa kiasi chao pia hakilingani na zamani,” alisema.

"Wateja wetu wengine kama wale wa bodaboda wamepungua pia na hata wanapokuja, wanachukua kiasi kidogo tu cha mafuta,” aliongeza Aboubakar.
Meneja wa Kituo cha Total kilichopo Mlimani City, Ridhiwan Mohamed, alisema kituo chao hivi sasa kinakabiliwa na changamoto ya kupungua kwa wateja.

”Kituo changu sasa kinauza lita 20,000 mpaka lita 19,000, lakini kipindi cha nyuma tulikuwa tunauza hadi lita 30,000 kwa siku. Kwakweli hali imekuwa ngumu siku hizi,” alisema Mohamed na kuongeza:

“Yaani siku hizi tukiuza hata lita 25,000 kwa siku inakuwa kama ndoto kwa sababu ni nadra kutokea.”

Msimamizi Mkuu wa Kituo cha Mafuta cha Puma kilichoko eneo la Mwenge, Paul Msuya, alisema licha ya kituo chake kuwa kwenye eneo la makutano ya barabara ambalo magari mengi husimama, biashara imeshuka zaidi kulinganisha na mwaka jana.

Msuya alisema kipindi cha nyuma walikuwa wakiuza mafuta kwa wastani wa lita 10,000 kwa siku lakini sasa wanauza wastani wa lita 5,000 kwa siku na kwamba, wateja wao wengi ni pamoja na wale wa bajaji na bodaboda.

“Kuna baadhi ya wateja ambao ni wakwetu siku zote. Hawa huchukua kiwango cha mafuta kilekile tangu tumeanza kuwauzia. Lakini wale wateja wa kupita na kujaza mafuta (full tank) ndiyo wamepungua sana,” alisema Msuya.

Meneja wa kituo cha mafuta cha GBP kilichopo Mbezi, Rashid Saleh, alisema licha ya wao kuuza mafuta yao kwa bei ya chini zaidi, bado wateja wamepungua ukilinganisha na kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

“Tunauza mafuta ya petrol kwa Sh. 1,800 wakati bei ya Serikali ni Sh. 1,860 na tunauza mafuta ya dizeli kwa Sh. 1,660 wakati bei ya serikali ni Sh. 1,720. Pamoja na punguzo hili, wateja wetu bado wamekuwa wakipungua," alisema Saleh.

"Zamani tulikuwa tunauza lita 22,000 kwa siku, lakini siku hizi tunauza wastani wa lita 20,000 na 18,000 kwa siku.

Kiukweli, hali ya kiuchumi kwa wateja wetu imechangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa changamoto hii.”
Aidha, tangazo la kampuni ya Muro linavitaja vituo vyake vinavyouzwa kuwa ni vya Kibaha - Madafu, Dundani Mkuranga, Miwaleni Mlandizi na Vikindu - Mkuranga.

Hata hivyo, Nipashe haikuweza kuthibitisha kutoka katika vyanzo rasmi kuwa hatua hiyo ya kampuni ya Muro inatokana na kushuka kwa wastani wa mauzo kwa siku kama ilivyo katika vituo mbalimbali vilivyotembelewa na Nipashe jijini Dar es Salaam.

Endapo kila mkoa kati ya 30 utakadiriwa kuwa na vituo vya mafuta 20 na kila kituo kikiwa na wastani wa wafanyakazi watano, maana yake ajira za watu 3,000 zitakuwa shakani ikiwa hali ya biashara kwa siku itakuwa ya chini kama ilivyo katika vituo vilivyotembelewa na Nipashe.

Akizungumza na Nipashe, mmoja wa wafanyabiashara wa mafuta alisema kuwa endapo biashara ya mafuta itaporomoka kama ilivyo katika badhi ya vituo vilivyotembelewa na Nipashe, maana yake mamia ya watu wanaotegemea riziki zao kutokana na biashara hiyo watakuwa katika hatari ya kupoteza ajira.

“Ukweli ni kwamba mafuta ni kila kitu na biashara yake itaendelea kuwapo…lakini kama mauzo katika vituo yataendelea kushuka, maana yake wenye vituo watalazimika kuchukua hatua kadhaa ikiwamo kupunguza wafanyakazi na hilo litawaathiri wengi… hata madereva wa malori ya mafuta na wasaidizi wao watathirika,” alisema.

EWURA, TRA
Alipoulizwa kuhusu hali hiyo, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo, alisema mamlaka watafanya utafiti ili wajiridhishe kuhusu madai ya kupungua kwa wateja wa mafuta.

"Kuhusu taarifa uliyonipa, inabidi na sisi (Ewura) tufanye utafiti ili kupata ukweli wa taarifa hizo kwa kuangalia vituo vyote,” alisema na kuongeza:

"Haingiii akilini kusema biashara ya mafuta imeshuka wakati kuna magari mengi na foleni iko palepale (jijini Dar es Salaam). Kwa kifupi kuna sababu nyingi zinazoathiri biashara ya mafuta ikiwamo sehemu ambazo vituo hivyo vinawekwa.

"Unaweza kukuta mtu kituo chake cha mafuta kipo sehemu ambayo haina magari, hayasimami mara kwa mara halafu mwisho wa siku mtu huyu anakuja kulalamika kuwa biashara ya mafuta ni mbaya.

"Lakini pia tunachokijua ni kwamba uhitaji wa mafuta upo, tena mkubwa sana... kwa kweli kuhusu suala la biashara ya mafuta katika vituo vya mafuta kupungua tutalifanyia utafiti wetu na sisi ili tujue kama ni kweli."

Alipotafutwa na Nipashe kuzungumzia suala hilo jijini jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Richard Kayombo, alisema hivi sasa hawana takwimu sahihi za athari za kiuchumi kutokana na kupungua kwa wateja katika baadhi ya vituo vya mafuta.

"Kwenye biashara ya mafuta, sisi (TRA) huwa tunashughulika na mapato ya mwaka mzima. Hatujishughulishi na mapato ya mauzo ya kila siku ya vituo vya mafuta," alisema.

Tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, hatua kadhaa zimechukuliwa katika kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima ili fedha zitakazookolewa zitumike kwa ajili ya shughuli zinzowagusa moja kwa moja wananchi wa kawaida.

Katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2016/2017, Serikali imepanga kutumia Sh. trilioni 29.53.... Kati ya fedha hizo, Sh. trilioni 17.72 zitakuwa za matumizi ya kawaida, wakati Sh. trilioni 11.82, sawa na asilimia 40 ya bajeti nzima, zitatumika kwa shughuli za maendeleo.

Katika bajeti ya mwaka jana (2015/16), Bunge liliidhinisha Sh. trilioni 22.45. Kati yake, Sh. trilioni 16.7 zikiwa ni za matumizi ya kawaida ambayo ni sawa na asilimia 74.3 huku Sh. trilioni 5.76 sawa na asilimia 25.7 zikiwa za shughuli za maendeleo.


Chanzo: Nipashe

Hali ikiendelea hivi katika kila sekta,sijui serikali itakusanya wapi kodi ya kwenda kuhifadhiwa BOT kupitia account za taasisi na mashirika mbalimbali ya umma.
 
d6d49b04cefc61aa4a23aa953da2c4df.jpg


Ni wale wanaofanya Kazi kwenye vituo vya mafuta nchini..

Tatizo kubwa la kupunguza wafanyakazi ni kushuka kwa mauzo ya mafuta kwa 50%.

Nusu ya wafanyakazi Wa petrol station nchini watapoteza Ajira.

My take: ukisikia paa ujue imekukosa,Siku maslahi yako yakiguswa tutakusikia tu pole pole tuendelee kuisoma namba huku watawala wakituita wapiga dili..
 
Hii ni habari kuu katika gazeti la Nipashe la siku ya leo.

Habari inasema baadhi ya vituo mauzo yashuka kwa asilimia 50 na baadhi ya vituo vinapigwa bei.

Chanzo:Nipashe

Hali ikiendelea hivi katika kila sekta,sijui serikali itakusanya wapi kodi ya kwenda kuhifadhiwa BOT kupitia account za taasisi na mashirika mbalimbali ya umma.
atakaeichagua CCM 2020 ni tahira na punguani pekee
 
4 Reactions
Reply
Back
Top Bottom