Mambo ya msingi unayopaswa kuyafahamu kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii kibiashara (3)

Status
Not open for further replies.

Sam Gidori

Senior Member
Sep 7, 2020
165
414

Tangazo_.png

Mambo 10 ya kuzingatia unapoandaa chapisho la tangazo la kibiashara mtandaoni​

Mitandao ya kijamii imebadilika kutoka kuwa majukwaa ambayo watu hukutana kufahamiana na kujadili masuala mbalimbali ya kijamii, hadi kuwa majukwaa ya kibiashara ambayo unaweza kukutana na wateja wako, kuwafahamisha kuhusu biashara au huduma unayoitoa na kuuza bidhaa zako mtandaoni.

Katika sehemu ya pili ya makala haya, tuliangalia mitandao tofauti ya kijamii unayoweza kutumia kulingana na mahitaji yako ya kibiashara. Baada ya kufahamu tofauti ya mitandao hiyo, ni vyema kuangalia jinsi unavyoweza kutengeneza machapisho yenye ushawishi kwa ajili ya kutangaza bidhaa au huduma yako mtandaoni.
Unapaswa kufahamu kuwa mitandao ya kijamii inatoa fursa ya kutangaza bidhaa yako kwa njia mbili: njia ya kwanza haina gharama yoyote, ikiwa utaamua kutangaza biashara yako kwa kutengeneza machapisho ya kawaida mtandaoni. Njia hii ni rahisi kwa kuwa haina gharama yoyote, lakini uwezo wa machapisho yako kuwafikia watu wengi itategemea wingi wa watu waliofuata akaunti au ukurasa wako (followers).

Njia ya pili ni kwa kutumia matangazo ya kulipia. Njia hii itawezesha machapisho yako kuwafikia wateja wengi zaidi, ikitegemea ukubwa wa eneo la kijiografia utakalokuwa umechagua kwa chapisho lako kuonekana na watu utakaokuwa umechagua walione chapisho lako, bila kusahau bajeti ya fedha utakayokuwa umeiwekeza katika kulipia chapisho lako. Lakini katika makala haya, tutaangazia zaidi jinsi ya kuandaa matangazo yasiyo ya kulipia.

Watu wengi hawapendi matangazo. Utafiti unaonesha kuwa asilimia 70 ya watumiaji wa mtandao wanakerwa na matangazo. Lakini sio matangazo yote yanakera mtandaoni. Asilimia 83 ya watumiaji wa mtandao wanakubaliana na kauli ya "Sio matangazo yote ni mabaya, lakini natamani kuondoa matangazo yote yanayokera!" Hii inaonesha kuwa watumiaji wengi wa mtandao hawachukii matangazo, lakini wanatumia matangazo mabaya.

Unapoandaa tangazo lako mtandaoni, lengo lako ni kuwafikia wateja wengi watakaosoma tangazo lako na kuvutiwa na bidhaa au huduma, kisha kushawishika kununua au kutumia bidhaa yako. Ili kufanikisha lengo hilo, yapo mambo 10 ya kuzingatia kila mara unapoandaa tangazo lako.

1. Bainisha lengo la tangazo
Kabla ya kuchapisha tangazo lako, jiulize, unataka kufikia lengo gani baada ya watu kuliona tangazo hilo. Lengo linaweza kuwa kuwafanya wateja wako kuifahamu bidhaa yako, kuongeza wafuasi katika akaunti yako, kupata watu wengi zaidi wanaotembelea tovuti yako, nk. Kuwa na lengo madhubuti kutakusaidia kuandaa tangazo linalowaelekeza wateja wako katika kufikia lengo lako.

2. Aina ya wateja unaotaka kuwafikia
Wateja wako watapokea matangazo yako kwa namna tofauti. Tangazo linalowalenga wazee halitafanana na tangazo la urembo linalowalenga wanawake. Unapaswa kuwaelewa wateja wako na kuandaa mpangilio wa tangazo lako kuhakikisha kuwa pale mlengwa anapoliona tangazo lako atalihusianisha na hali yake na kuona kuwa bidhaa au huduma yako inamfaa, kisha kuchukua uamuzi wa kununua.
Wateja wako wamegawanyika katika makundi tofauti tofauti: jinsia, umri, eneo la kijiografia wanaloishi, kipato chao, kiwango chao cha elimu, nk. Hivyo unapoandaa tangazo, hakikisha unaangalia vigezo vyote kuhusu mgawanyiko wa wateja wako.

3. Picha au video inayoambatana na tangazo lako
Ni wazi kuwa picha moja huweza kubeba thamani ya maneno 1000. Katika matangazo, hili huonekana zaidi. Picha au video inayoambatana na tangazo huweza kumshawishi mtu kufanya maamuzi kwa haraka zaidi kuliko maneno utakayokuwa umeyatumia, ndiyo maana matangazo mengi hutumia picha au video za watu maarufu ili kuongeza ushawishi na thamani ya bidhaa au huduma inayotangazwa. Ni muhimu kutumia picha unayodhani itakuwa na uhusiano wa moja kwa moja na maisha ya mteja wako. Mfano, utakapotumia picha yenye sura ya mzungu kutangaza juisi ya muwa, utakuwa umekosa uhalisia wa tangazo lako na maisha ya wateja wako.

4. Maelezo mafupi kuhusu biashara yako
Usiwaache wateja wako wakijiuliza maswali kuhusu chapisho lako, lakini usitegemee wateja wako kusoma maelezo marefu kuhusu biashara yako pia. Maelezo kuhusu biashara yako ni sehemu ambayo inahitaji ubunifu mkubwa. Jitahidi kuweka maelezo mafupi yenye ushawishi yasiyozidi mistari minne, ikiwezekana epuka kufikia "See More."

5. Tengeneza ofa inayoshawishi
Wateja wanapenda kupatana bei, na ni rahisi zaidi kwa mteja kufanya biashara na wewe tena pale utakapomwekea mazingira ya kumridhisha mwanzoni. Katika kumtengenezea mazingira ya ushawishi, unaweza kutumia 'vivutio' kama vile bei ya ushindani, muda wa bure wa majaribio ya bidhaa (trial period), kumfikishia mteja bidhaa bure, nk. Unapotengeneza ofa yako, hakikisha unaitangaza kwa ujasiri, na hii humjengea mteja imani katika bidhaa yako pale anapoona unampa ofa fulani na unaitangaza kwa kujiamini.

6. Eleza faida atakayoipata mteja baada ya kutumia bidhaa/huduma yako
Njia moja ya kumshawishi mteja kununua bidhaa au kutumia huduma yako ni kumfanya aone faida atakayoipata kutokana na kutumia bidhaa yako zaidi ya kile unachodhani unakifanya. Unaweza kuainisha huduma/ bidhaa unayoitoa, kazi ya bidhaa/huduma hiyo, kisha eleza matokeo ya kazi na faida atakazozipata mteja kutokana na bidhaa/huduma ulizoainisha.
Unapofikiri kuhusu faida, si lazima iwe faida ya vitu vinavyoshikika, inaweza kuwa furaha, raha, kuokoa muda, nk.

7. Waondolee wasiwasi wateja wako
Ni kawaida kwa mtu kuwa na wasiwasi anapotoa fedha kwa ajili ya kununua bidhaa mtandaoni. Kuna biashara nyingi feki mtandaoni na bidhaa zenye ubora hafifu, hivyo watu wengi huogopa kupoteza fedha zao kwa wezi wa mtandaoni. Biashara yako haina tofauti na ile ya wezi wa mtandaoni, hivyo ni wajibu wako kumfanya mteja akuamini na kununua bidhaa yako, na si ile ya mwizi mtandaoni.
Moja kati ya njia ya kuwaondolea wasiwasi wateja wako ni kwa kuwapa uhakika wa fedha zao baada ya kununua bidhaa yako. Mteja anakuwa na imani zaidi pale mteja anapokuwa na uhakika wa kutopata hasara baada ya kufanya biashara.

8. Washawishi wateja wako kufanya uamuzi "Sasa"
Unapoandaa tangazo la kibiashara, unakuwa na lengo la kubadili mawazo ya wateja wako na kuwafanya kununua au kutumia bidhaa/huduma yako. Lakini uamuzi huo hautakuwa na maana ikiwa wateja wako hawatachukua hatua ya kununua au kutumia bidhaa/huduma yako. Watu wanaweza kuliona tangazo lako na kulifurahia, lakini wakaamua kulifanyia kazi baadaye, kisha wakaendelea na mambo mengine na kusahau kuhusu tangazo lako. Hivyo unapaswa kuwashawishi wateja wako kufanya maamuzi SASA, na si baadaye.
Unaweza kutengeneza uharaka huo kwa njia ya kuweka muda wa kumalizika kwa ofa hiyo ya kuvutia, ndani ya saa kadhaa, siku au wiki. Ikiwa mteja ataona kuwa hataweza kupata bidhaa hiyo baada ya muda wa ofa kuisha, atalazimika kuchukua hatua sasa.
Unaweza pia kuwashawishi wateja wako kununua bidhaa yako kutokana na ulazima wa kuwa na bidhaa hiyo msimu fulani utakapofika. Mfano, unaweza kumshawishi mteja kununua mwamvuli sasa ili asipate tabu katika msimu wa mvua unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Bila kujali njia utakayoitumia, ni muhimu sana kuwashawishi wateja wako kuwa muda wa kuchukua hatua ni SASA, na si wakati mwingine.

9. Tangazo liwe na wito unaoeleweka (Call-to-action)
Tangazo zuri la biashara mtandaoni ni lile linalomtaka mteja kuchukua hatua baada ya kuliona, kulingana na lengo lako na aina ya wateja wako.
Kuweka lengo bayana linasaidia kuondoa mkanganyiko kwa mteja kuhusu hatua anayopaswa kuchukua baada ya kuona tangazo lako. Mfano, ikiwa unataka mteja kupenda ukurasa wako, basi mwelekeze kupenda ukurasa wako, na si kumwelekeza kupenda ukurasa na kununua bidhaa ndani ya tangazo moja. Hakikisha kiungo kinachoambatana na tangazo lako kinamwelekeza mtumiaji kufanya unachomwelekeza kufanya.

10. Mawasiliano yaliyokamilika
Baada ya kufanikiwa kumshawishi mteja kufanya maamuzi ya kununua/kutumia bidhaa au huduma yako, mteja atahitaji kuwasiliana na wewe kwa ajili ya kuhitimisha kuagiza bidhaa yako. Mawasiliano yanaweza kuwa namba ya simu, barua pepe, au kiunganishi kinachompeleka mteja katika tovuti yenye fomu itakayomwezesha kununua bidhaa hiyo. Jambo la kuzingatia katika kuweka mawasiliano yako ni kuhakikisha kuwa mteja anakuwa na urahisi wa uharaka wa kuwasiliana na wewe au kituo chako cha biashara. Kukosa mawasiliano kunaweza kumfanya mteja kubadili mawazo na kuacha kununua bidhaa yako, hivyo kupoteza maana ya kazi yote iliyofanyika awali.

Ubora wa tangazo la biashara mtandaoni unazingatia uwezo wa tangazo hilo kumshawishi mteja kuchukua maamuzi ya kununua bidhaa au kutumia huduma inayotangazwa katika tangazo husika. Tangazo la biashara siku zote linaendana na ubora wa huduma inayotolewa. Hivyo, lengo la kwanza la tangazo la biashara mtandaoni ni kumshawishi mtumiaji wa mtandao kulitazama na kushawishika kuwa mteja wa bidhaa au huduma inayotangazwa. Mteja ataridhika zaidi ikiwa atahudumiwa kwa ubora unaolingana na tangazo aliloliona mtandaoni.

Unaweza pia kusoma:
 
Matangazo ya biashara siku hizi yamepungua pia sababu inajulikana
 
Status
Not open for further replies.
Back
Top Bottom