Mambo ya kuzingatia unapoendesha pikipiki

Ben Zen Tarot

JF-Expert Member
Dec 13, 2014
3,905
6,689
Pikipiki au kwa jina maarufu bodaboda, zinatumiwa na watu wengi sana kwa usafiri. Licha ya pikipiki kutumiwa kama usafiri, wengine huzitumia kama chanzo cha kipato chao cha kila siku.

Hata hivyo kila mmoja amewahi kusikia au kushudia juu ya changamoto kubwa ya ajali inayokabili usafiri wa pikipiki au bodaboda. Wengine wamepata majeraha, kupoteza maisha, kupoteza mali au hata kupata ulemavu wa kudumu.

Pasipo shaka sasa ni wakati wa kutazama ni nini hasa chanzo cha ongezeko kubwa la ajali za pikipiki ili kikabiliwe.

Ikiwa unaendesha pikipiki au unataka kuongeza maarifa yako, basi fahamu mambo 10 ya kufanya ili kuepuka ajali unapoendesha pikipiki au bodaboda.

1. Pata elimu sahihi ya kuendesha pikipiki
Pikipiki ni chombo cha kitaalamu kinachohitaji maarifa sahihi ya kukitumia. Ajali nyingi zinatokana na watu kuendesha pikipiki bila maarifa sahihi ya kutumia chombo hicho pamoja na kanuni muhimu za usalama barabarani.

Hivi leo kijana hujifunza pikipiki kichochoroni kwa siku mbili na kuingia kwenye barabara kuu za mji, hili limefanya wengi kugongwa au kugonga watumiaji wengine wa barabara.

Ni muhimu kuhudhuria mafunzo stahiki ya kuendesha chombo cha moto ili kuepuka ajali.

2. Tumia pikipiki bora na salama
Vifaa badia au feki vimetawala soko. Baadhi ya pikipiki zimetengenezwa kwa viwango duni, jambo ambalo linaweza kusababisha ajali.

Ni muhimu kuhakikisha unatumia pikipiki bora ambayo haitakuletea hatari kama vile kukatika breki au kupasuka gurudumu kirahisi. Unaweza kuzingatia haya yafuatayo:

Nunua pikipiki kutoka kwa watengenezaji wanaoaminika.

Fanyia matengenezo pikipiki yako kwa wakati.

Kagua pikipiki yako vyema kabla ya kuanza safari. Hakikisha kila kitu kinafanya kazi vyema.

3. Usitumie kilevi
Kilevi au pombe ni chanzo kikubwa cha ajali. Ili kuepuka ajali unapoendesha pikipiki, ni muhimu kuepuka matumizi ya pombe kwani hukufanya ushindwe kumudu vyema pikipiki yako uwapo barabarani.

4. Vaa kofia ngumu
Usalama wa mtumiaji wa usafiri wa pikipiki au bodaboda, unategemea kwa kiasi kikubwa uvaaji wa kofia ngumu. Kofia ngumu hukinga kichwa chako mara upatapo ajali, pia kofia ngumu hukulinda na athari za kimazingira kama vile upepo na vumbi.

Ili kuepuka kifo au majeraha makubwa wakati wa ajali, ni vyema kuhakikisha unatumia kofia ngumu.

5. Tambua hali ya hewa
Usafiri wa pikipiki huathiriwa sana na hali ya hewa. Ni muhimu sana kuchunguza hali ya hewa ya eneo unalotaka kwenda kabla ya kuanza safari.

Kumbuka unapokwenda eneo lenye mvua unaweza kukutana na changamoto ya utelezi ambayo inaweza kusababisha ajali.

6. Beba mzigo sahihi
Bodaboda au pikipiki siyo gari. Kuna tabia ya baadhi ya watu hupenda kubeba mizigo mingi au abiria kupita kiasi cha uwezo wa pikipiki zao.

Hili huwasababishia kupata ajali kwani hushindwa kumudu pikipiki zao wanapokutana na kitu cha ghafla barabarani. Hakikisha huzidishi mzigo kwenye pikipiki yako ili kuepuka ajali.

7. Epuka mwendo kasi
“Mwendo kasi unaua.”

Chanzo cha ajali nyingi za pikipiki ni madereva wa pikipiki kuendesha pikipiki zao kwa mwendo mkubwa. Hili huwafanya washindwe kuzimudu mara kunapotokea kitu cha ghafla barabarani. Ikiwa huna haraka sana, basi nenda kwa mwendo wa wastani ili ufike salama kule uendako

8. Endesha kwa kujihami
Unapoendesha pikipiki epuka mawazo kama vile “ananiona” au “ni haki yangu kupita”. Kumbuka pikipiki ni rahisi zaidi kugongwa na kupata madhara makubwa kuliko gari.

Hakikisha unajihami, akili yako yote inakuwa barabarani huku ukichukua tahadhari za kiusalama. Hakikisha maamuzi na matendo yote unayoyafanya ni salama.

9. Kuwa makini unapompita mwingine (overtake)
Chanzo kingine kikubwa cha ajali za barabarani kwa magari na pikipiki ni kupita (overtake) vyombo vingine. Kumbuka kuovertake ni jambo linalohitaji umakini mkubwa, la sivyo utagongana na gari au pikipiki nyingine. Unaweza kuzingatia haya yafuatayo:

Overtake mahali sahihi. Usiovertake kwenye kona, kwenye mteremko mkali au mlima, mahali usipoona vizuri au mahali ambapo haparuhusiwi.

Punguza mwendo wakati wa kuovertake.

Mjulishe dereva mwingine kuwa unataka kuovertake.

Usiovertake kwa kushtukiza.

10. Tambua hatari za barabarani
Kuna hatari mbalimbali zinazoweza kuwepo barabarani. Pikipiki huathiriwa zaidi na hatari za barabarani kuliko gari, hivyo ni vyema kuwa makini.

Kwa mfano kukanyaga jiwe au tunda lililooza barabarani kunaweza kukusababishia ajali mbaya. Hivyo ni vyema ukajihadhari na vitu kama vile mashimo, mawe, makopo, kamba au waya n.k.

Pasipo shaka, ajali za pikipiki zinaweza kuepukika au kupunguzwa kwa kiasi kikuwa ikiwa madereva pamoja na watumiaji wa pikipiki watazingatia mambo yaliyoelezwa hapa.
 
.... Punguza mwendo wakati wa kuovertake........ HAPO SASA UNATAKA WAFE WENGI ZAIDI.
Natumaini alikua anamaanisha, punguza mwendo kabla ya kufanya overtake. Hii itakupa muda wa kuona kama upande wa pili kupo shwari pia nyuma yako hakuna anayekuja kwa mwendo mkali, imagine unaovertake huku nyuma yako linakuja bus kwa speed kali waweza poteza umakini.
 
Zamani nilikua nikiona bodaboda wanavyopita katikati ya foleni za magari nilikua naogopa naona wanahatari sana ila tokea nimenunua pikipiki namimi nimejikuta napita katikati ya magari kwenye foleni na bila hofu yeyote, hii kitu imenifanya nione gari sio usafiri wa haraka tena ukiwa unaenda katikati ya jiji

kikubwa ni kutembelea kwenye gia sahihi mkono wa clutch uwe attention muda wote kwakua breki itahusuka anytime, kifupi pikipiki hazisababishi ajali ukiwa makini ila madereva ndio wanaoleta ajari.
 
Good analysation naongezea kitu kmoja daima iwe usku au mchana washa taa kubwa ya mbele boda huwa haionekan mana inafanana na baiskeli ikiwa mbali...

Hii husababisha wenye magar weng ku overtake huku mbele akikutana na boda maana huwa hazionekan kirahs hasa mchana had mkaribiane..so always washa taa ya mbele
 
Kuna mwamba anaendesha boda kwenda Moshi from Dar kila Krismasi. Mwaka huu hatoboi. RIP in advance
 
zamani nilikua nikiona bodaboda wanavyopita katikati ya foleni za magari nilikua naogopa naona wanahatari sana ila tokea nimenunua pikipiki namimi nimejikuta napita katikati ya magari kwenye foleni na bila hofu yeyote, hii kitu imenifanya nione gari sio usafiri wa haraka tena ukiwa unaenda katikati ya jiji, kikubwa ni kutembelea kwenye gia sahihi mkono wa clutch uwe attention muda wote kwakua breki itahusuka anytime, kifupi pikipiki hazisababishi ajali ukiwa makini ila madereva ndio wanaoleta ajari.
Inabidi uwe makini kwa wale wanaovuka barabara
 
Back
Top Bottom