Mambo ya Kuzingatia kwenye Kilimo cha Pamba

Mashima Elias

Member
Dec 22, 2010
18
52
IMG_20201117_125515.jpg

MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KWENYE KILIMO CHA PAMBA
Mwandishi: Mashima Elias
Ili kuongeza tija na Ubora wa Pamba Mkulima hana budi kuweka Juhudi katika kupata maarifa zaidi kuhusu kilimo cha pamba, maarifa haya unaweza kuyapata kwa wataalamu wa kilimo (Maafisa Kilimo) au kutoka kwa wakulima wengine wenye ujuzi wa pamba ama kwa Kutembelea maonesho ya Wakulima au kusoma makala mbalimbali za kilimo cha pamba zilizoandaliwa na wataalamu wa Kilimo, Taasisi za Kilimo na watafiti wa zao hili.
Ni kweli kuwa ongezeko la bei ya pamba linaweza kuongeza kipato cha Mkulima lakini pia Kufuata Kanuni za Kilimo bora cha pamba kunaweza kuongeza kipato vilevile, Wakulima wengi hawafikirii kuhusu kiasi cha mavuno wanachopoteza kwa kutozingatia kanuni za kilimo bora cha pamba, unaweza kuchukulia mfano tu badala ya Kupata Kilo 1200 kwenye ekari moja Mkulima anapata kilo 500 tu, tuchukulie bei ni Tsh.1000 mkulima atapata kati ya Tsh. 500,000/= Lakini anaweza akaongeza kipato chake hadi Tsh. 1,200,000/= kwa kupata kilo 1200 kama atazingatia ushauri wa wataalamu wa Kilimo.
Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia kwenye Kilimo cha Pamba ili Mkulima upate Faida Zaidi:

1. ANDAA SHAMBA MAPEMA
Katika hatua hii jitahidi kufanya yafuatayo:
I. Kama shamba lako lilikuwa limelimwa pamba hakikisha miti ya pamba imeng'olewa na imekusanywa na kuchomwa moto, usikata miti ya pamba na kuacha kisiki aridhini kwani kinaweza kuchipuka tena, Mkulima ufahamu kuwa kung'oa na kuchoma moto masalia ya pamba kwenye shamba lililokuwa limelimwa pamba itasaidia kupunguza mzunguko wa wadudu waharibifu wa pamba na vimelea vya magonjwa ya pamba hivyo kupunguza maambukizi kwenye msimu unaofuata.
II. Kama shamba lako halijalimwa zao la pamba liandae kwa kufyeka vichaka na kungo'a visiki.
Nyongeza: Katika hatua hii ya kuaanda shamba pia unaweza kumwaga mbolea ya samadi shambani kwako na zoezi hili lifanyike mwezi mmoja kabla ya msimu kuanza.
2.CHUKUA MBEGU BORA
Bodi ya pamba Tanzania huleta mbegu kila msimu hivyo hakikisha unaenda kuchukua mbegu hizo kwani ni Bora, epuka kupewa au kununua mbegu kutoka kwa mtu ambaye hana kibali cha kuuza au kusambaza mbegu za pamba kwani zinaweza kuwa zimekaa muda mrefu ama si bora kabisa kutokana na ukweli kuwa mbegu za pamba hufanyiwa utafiti mara kwa mara na maboresho kuendana na wakati na sifa stahiki.
Hivyo nakuomba zingatia kuchukua mbegu iliyothibitika na Bodi ya pamba kutumika katika msimu huo kwani ndiyo ufunguo wa kuelekea kwenye kupata mmea ulio bora na utakaokupa mavuno mazuri.
3. LIMA SHAMBA VIZURI
Udongo unatakiwa kulimwa kwa kina na kumwagika vizuri ili kuruhusu mbegu kuota na mizizi kupenya kwa urahisi kufikia virutubisho na kukuza pamba nzuri kwa mafanikio. Hivyo nashauri shamba lilimwe mara mbili hadi tatu, Kama unaweza kupiga haro (Kusawazisha) kwa trekta ni vizuri, Kama unatumia jembe la kukotwa na ng'ombe ni vyema kulima hadi uhakishe kuwa hakuna mabonge mabonge shambani.
Angalizo: Kuna maeneo mengine ya udongo wa kichanga ambao ni rahisi kwa mmomonyoko wa udongo hivyo ni vyema kuzingatia pia hilo kwa kutotifua sana udongo ili kuepuka mmomonyoko wa udongo unaoweza kupelekea virutubisho kusombwa na maji, sambamba na hilo kilimo cha matuta kinaweza kufaa zaidi katika maeneo hayo pamoja na maeneo ya miinuko inayotengeneza mitelemko mikali.
4. PANDA PAMBA MAPEMA, KWA MSITARI NA KWA IDADI YA MBEGU INAYOTAKIWA
Hakikisha unapanda mapema mara tu mvua zinapoanza kunyesha au kukaribia kunyesha. Pamba ikipandwa mapema itakua na kukomaa vizuri na hivyo kupata mavuno mengi. Kwa mikoa ya Simiyu, Shinyanga , Mwanza , Tabora , Mara , Kagera , Kigoma na Singida pamba ipandwe kati ya tarehe 15 Novemba na 15 Desemba.
Panda kwa msitari sentimita 60 kutoka mstari hadi mstari au Kutoka tuta hadi tuta na sentimita 30 shimo hadi shimo, lakini pia hakikisha unapanda idadi ya mbegu inayotakiwa ambayo ni kati ya mbegu 3 hadi 5 Kadili unavyoona inafaa kwa kuzingatia aina ya mbegu Ulizonazo kama ni zile zilizoondolewa manyoya panda 3 kama hazijaondolewa manyoya panda 5.
Faida za kupanda kwa mistari ni pamoja na Kurahisisha kazi ya palizi na unyunyiziaji wa Sumu za kuua wadudu waharibifu wa pamba, Kuwa na mimea ya kutosha lakini pia kuwa na uwiano sawa wa kupata virutubisho.
5. PUNGUZIA MICHE
Punguzia miche ya pamba na ibaki miwili (2) inayonawili na yenye afya. Zoezi hili lifanyike mapema hii itaifanya miche iweke matawi na kujiimarisha vizuri kwani miche mingi hunyang'anyana virutubisho na kuwa dhoofu.
6. PALILIA MAPEMA AU KWA WAKATI
Palilia Shamba la pamba mapema mara yanapoanza magugu kuota, Palizi ya kwanza ifanyike si chini ya mwezi mmoja tangu pamba kuota, Ukichelewa kupalilia pamba itazongwa na magugu ambayo yatachukua virutubisho na hivyo kuathiri pamba yako na kupelekea kupungua kwa mavuno.
7. WEKA MBOLEA
Mimea ya pamba kawaida inahitaji Nitrojeni, Fosforasi na Potasiamu ili iweze kukua na Kutoa matunda mengi, pamoja na virutubisho vingine ila hivi ni muhimu sana, Virutubisho hivi vinaweza kuwa vipo katika udongo kutegemeana na rutuba ya shamba lako hivyo unahitaji kuwa na uelewa pia kuhusu rutuba ya shamba lako. Mbolea ya Samadi ni bora zaidi katika kuboresha rutuba ya udongo wako kama inapatikana.
Nashauri iwekwe katika shamba mapema kipindi cha kuandaa shamba
8. ZUIA WADUDU NA MAGONJWA
Wadudu wanaweza kuwa shida kubwa katika uzalishaji wa pamba na kupelekea kupungua kwa mavuno, lakini unaweza kuwadhibiti kwa sumu, njia za kibaolojia, Sango, na kutumia Zao Mtego,aidha magonjwa ya pamba pia yanaweza kudhibitiwa kwa kwa kupanda mbegu zinazoweza kustahimili magonjwa.
Bodi ya pamba Tanzania huthibitisha viuawadudu kila msimu ambavyo vinaweza kutumika kudhibiti wadudu waharibifu wa pamba aidha Bodi ya pamba hutoa viua wadudu hivyo kwa wakulima kwahiyo ni vyema kuchukua na kukabiriana na visumbufu hivyo vya pamba mapema kabla uharibifu haujawa mkubwa, wadudu hawa ndiyo pia wanoleta baadhi ya magonjwa katika zao hili ijapo pia kuna magonjwa yanayosababishwa na virusi na Kuvu katika zao hili.
Ushauri wangu ni vyema Mkulima ukapata ushauri kutoka kwa wataalamu jinsi ya kutumia viuadudu.

Ukumbuke: Sumu za kuulia wadudu zinaweza kuwa njia rahisi na bora za kushughulikia visumbufu vya pamba lakini pia zina kasoro kadhaa ikiwa ni pamoja na kuharibu tindikali yako ya udongo na usawa wa lishe katika pamba vilevile hudhuru mazingira hivyo ni muhimu kuzingatia tahadhari zinazotolewa kwenye vifungashio na zinazotolewa na wataalamu wa kilimo na mazingira.
Angalizo: Viuadudu vya kemikali haviwezi kutumika kwa kilimo hai cha pamba.
9. VUNA PAMBA MAPEMA NA CHAMBUA
Vuna mapema pamba iliyokomaa na kupasuka vizuri na kuichambua Vizuri. Ukichelewa kuvuna pamba itaharibiwa na Mvua , takataka Vumbi, au Wanyama na hivyo kuharibu usafi na ubora wake.
10. UZA PAMBA YAKO KWA WANUNUZI WALIO NA KIBALI KUPITIA VYAMA VYA MSINGI
Ili uweze kupata bei nzuri hakikisha pamba yako unauza kwa kampuni zenye kibali cha kununua pamba kupitia chama chako cha Msingi (AMCOS), Epuka kuuza pamba yako kwa Machinga au wanunuzi wasio na kibali kuepuka kupunjwa kwa bei au Kipimo kwa mizani inayopunja.
Kwa Ushauri Zaidi Muone Afisa Kilimo aliye Karibu nawe
 
Back
Top Bottom