Mambo ya kuzingatia ili kuweza kulinda ajira yako

Zasasule

JF-Expert Member
Aug 12, 2009
1,002
103
  • Fanya kazi yako vizuri: Hili la kwanza linaweza kuwa wazi.Umeajiriwa kwa sababu mwajiri wako anahitaji msaada kutokana na ujuzi ulionao.Unategemewa kufanya kazi zako kwa juhudi na maarifa.

    Zingatia maelekezo,sera na kila kitu kinachohusiana na kazi yako.Timiza wajibu wako.Kama kazi yako inakwenda sambamba na vitu kama “deadlines”,hakikisha unafanikiwa ipasavyo katika hilo.
  • Punguza kulalamika: Pamoja na kwamba waajiri wengi wanasema kwamba wana sera huru zinazoruhusu wafanyakazi kuelezea kero zinazowakabili nk,ukweli ni kwamba waajiri hao hao hawapendi kuwa na mfanyakazi au wafanyakazi wanaolalamika kupita kiasi.

    Kila inapowezekana,jitahidi kutatua matatizo madogo madogo unayokumbana nayo kazini bila kukimbilia kwa “wakubwa” ukiwa na lundo la malalamiko. Endapo ni lazima kulalamika,fanya hivyo huku ukiwa na mapendekezo halisi ya jinsi ya kukabiliana na tatizo husika.
  • Kuwa na siasa zisizofungamana na upande wowote: Kila mtu ana utashi wake katika siasa za nchi.Na kwa vile mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi,utashi wa kisiasa au vyama vya kisiasa unazidi.Pamoja hayo,hakikisha kwamba katika maeneo ya kazi,unakuwa au unaonyesha kuwa na siasa zisizofungamana na upande wowote.Kwa maneno mengine,usilete ofisini ushabiki wa kisiasa unaoonekana kuzidi mipaka au hata kuingilia utendaji wako.

    Lakini pia usionyeshe kwamba huelewi kinachoendelea nchini.Baadhi ya waajiri huutumia wakati huu kukagua watu wanaoelewa kuhusu sera mbalimbali za nchi,vyama vya kisiasa nk ili kujua nani au mfanyakazi yupi anastahili kushika usukani japo wa idara fulani.

    Kumbuka katika nchi nyingi zinazoendelea(Tanzania ikiwemo) mambo mengi(kama vile biashara na uwekezaji) yana uhusiano wa karibu sana na siasa za kiuchumi za nchi husika.Usikae kando sana.
  • Elewa na kukumbatia utamaduni wa sehemu yako ya kazi: Kila sehemu ya kazi ina “utamaduni” wake. Ukitaka kulinda ajira yako ni muhimu ukaelewa na kuukumbatia utamaduni(culture). Mifano ya tamaduni mbalimbali za sehemu za kazi ni mingi ikiwemo uvaaji(dressing code),utaratibu unaofuatwa pindi vitu kama misiba au harusi vinapotokea,nk.

    Hakikisha kwamba unaelewa “corporate culture” ya sehemu yako ya kazi na kwenda nayo sambamba.Usipofanya hivyo,utakuwa “tofauti”.Ukiwa tofauti ni wazi kwamba kila mtu pale kazi atakuwa anasubiri kwa hamu siku utakayoondoka.
  • Epuka umbeya: Hili niliwahi kuliongelea katika mbinu za kuepuka migogoro makazini.Lipo pia katika mbinu za kulinda ajira yako.Umbeya katika sehemu za kazi upo na utakuwepo.Hii ni hulka yetu binadamu ambayo wakati mwingine ni ngumu kuepukika.Pamoja na hayo,umbeya ni jambo ambalo huchangia sana watu wengi kupoteza ajira zao kwani umbeya makazini sio tu kwamba ni chanzo cha migogoro bali pia ni upotezaji mkubwa wa muda na pia kitu kinachoshusha morali ya wafanyakazi wengine.

    Kama unataka kulinda ajira yako,ni vizuri ukajiepusha na majungu na umbeya.Funga mdomo,ziba masikio.Fanya kilichokupeleka mahali pale;kazi yako.Umbeya uache nyumbani kwako na mtaani.
  • Jiendeleze kielimu na ki-ujuzi: Kupata kazi kusiwe mwisho wa kujifunza.Endelea kupiga msasa ujuzi au elimu yako kwa aidha kujisomea(siku hizi unaweza kusoma kupitia mtandaoni,kwa wakati wako).Inapotokea nafasi yoyote ya kujiendeleza kielimu,usiilazie damu.

    Unaweza kujiendeleza kielimu kwa kujisomea majarida au tovuti mbalimbali zinazohusiana na sehemu yako ya kazi. Kama upo umoja wa taaluma yako au kazi yako,hakikisha kwamba unakuwa mwanachama.Unapopata nafasi ya kukutana na wenzako katika taaluma moja,hakikisha kwamba unaelewa kinachoendelea katika taaluma yako.
  • Kuwa mwenye shukrani: Ni wazi kwamba hakuna binadamu ambaye anaweza kufanya kila kitu mwenyewe.Kila mtu anahitaji msaada fulani katika maisha.Hali ni hiyo hiyo katika sehemu za kazi.

    Ni muhimu kuwashukuru wale wote ambao wanakusaidia pale kazini kwako kwa namna moja au nyingine.Kimsingi wafanyakazi wenzako wote, iwe ni wafagizi,ma-messenger,katibu muhtasi nk,wanakusaidia kwa namna moja au nyingine.Washukuru kila mara unapopata fursa ya kufanya hivyo.
  • Kuwa na mtizamo chanya(positive attitude):Penye wengi,pana mengi.Yawezekana kazini kwako pakawa na mambo fulani fulani ambayo kimsingi hayapendezi.Kunaweza kuwa na mfanyakazi au wafanyakazi ambao ni “visima vya majungu”.Jiepushe nao na wakati huo huo hakikisha kwamba unakuwa na mtizamo chanya.

    Ukiwa na mtizamo chanya katika kila jambo,utapendwa na wafanyakazi wenzako na hata wakuu wako wa kazi.Watu walio na mtizamo chanya,wana nafasi nzuri zaidi ya kulinda ajira zao kuliko watu ambao wanaonekana wazi kuwa na msimamo hasi(negative attitude).
  • Kuwa mwaminifu: Bila shaka hili linajieleza.Uaminifu katika kazi na maishani kwa ujumla ni silaha nzuri katika mambo mengi.Bado nakumbuka jinsi Rais mstaafu,Benjamin Mkapa,alivyowaasa vijana katika suala zima la kuwa waaminifu ili kwenda sambamba na changamoto za maendeleo ya kiuchumi.Ni kweli kabisa.

    Hakuna mwajiri anayeweza kuvumilia mfanyakazi ambaye sio mwaminifu.Hakikisha unakuwa mwaminifu kwa kutumia vizuri muda wa kazi.Unapokwenda nje kwa ajili ya chakula cha mchana(lunch) hakikisha kwamba unarudi katika muda uliopangwa.Acha kuiba muda wa kazi kwa kupiga piga ovyo simu zako binafsi.Mifano ipo mingi sana katika hili.
  • Jipende na ujitunze: Ili uweze kulinda ajira yako ni wazi kwamba ni lazima uwe na afya nzuri.Kwa hiyo ni muhimu ukapata muda wa kutosha wa kulala,kula vizuri, fanya mazoezi mara kwa mara.Ukifanya hivyo utakuwa umejiweka katika mazingira mazuri ya kutimiza yote yaliyotajwa hapo juu.
Ukizingatia hayo niliyoyataja hapo juu ni wazi kwamba utakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kulinda ajira uliyonayo.Pamoja na hayo,yaweza kutokea ukaipoteza ajira uliyonayo kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wako.Ni muhimu basi ukawa na “Plan B”.Linda ajira uliyonayo kwa hali na mali lakini usisahau kwanza;kuweka akiba ya kifedha benki au mahali pengine popote na pia kuwa na mbadala endapo ajira uliyonayo itatoweka.Siku zote lazima uwe umejianda
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom