Mambo ya kufanya ili Mtoto akusikilize na akuheshimu

tramadol

JF-Expert Member
Oct 10, 2015
5,383
4,317

Msomaji mmoja wa safu hii aliniandikia hivi majuzi akidai mwanae hamsikilizi. Kwa mujibu wa mzazi huyu, pamoja na kufanya jitihada za kumwelekeza mwanae mambo muhimu ya kimaisha, bado kijana wake huyo haonekani kusikiliza. Anasema, kadri anavyomwadhibu mwanae, ‘ndivyo anavyozidi kuwa mkaidi…’

Mzazi huyu, inavyoonekana, amepoteza mamlaka yake kama mzazi. Mamlaka kimsingi ni uwezo wa kusema kitu na kikasikika bila kulazimika kutoa adhabu. Unapokuwa na mamlaka maana yake unayo nguvu ya ushawishi inayomfanya mtoto awe tayari kukuiga, kukusikiliza, kukuelewa na kufanya kwa hiari yake yale unayomwelekeza.

Ni ukweli ulio wazi kuwa ushawishi wa mzazi kwa mtoto wake hauji hivi hivi. Ushawishi ni matokeo ya jitihada za muda mrefu zinazofanywa na mzazi ili kuwekeza katika uhusiano na mwanae tangu mapema. Tutazame maeneo manne yanayoongeza ushawishi wa mzazi kwa mtoto.

Kuaminika
Mamlaka yako mzazi kwa mwanao yanategemea kiwango cha imani alichonacho kwako. Kukuamini maana yake, kwanza, hana mashaka na nia yako njema kwake na pili, anaamni anayo nafasi ya pekee kwako kama mzazi wake.

Kwa kawaida, mambo madogo madogo sana ndiyo humfanya mtoto aongeze imani yake kwako. Kwa mfano, kutumia sehemu ya muda wako kwa ajili yake kwa kufanya mazungumzo na matembezi naye, kufurahia yale mema yanayomgusa zaidi, humfanya mtoto akuamini. Kuaminika kunakwenda sambamba na vile unavyoonesha kumthamini kama mtu anayestahili heshima.

Msimamo usioyumba
Hakuna kitu kibaya kama kutokueleweka unataka nini. Kutokueleweka kunakotokana na kubadilika badilika, kunatuma ujumbe mbaya kuwa huna uhakika na usahihi wa kile unachokidai kwake. Hali hii ya kutokutabirika kwako humfanya atake kuendelea kujaribu bahati yake kwa sababu tayari ana wasiwasi na mamlaka yako kama wazazi.

Ili kujihakikishia mamlaka ni muhimu kuwa na msimamo wa pamoja na mzazi mwenzako. Kupingana wazi wazi na msimamo na maamuzi ya mzazi mwenzako mbele ya mwanao huwapunguzia mamlaka yenu kama wazazi na ni kutengeneza mazingira ya kujaribiwa kwa mamlaka yenu mara kwa mara.

Kuishi unayoyasema
Mtoto hujifunza zaidi kwa yale unayoyafanya kama mzazi kuliko yale unayoyasema. Mamlaka yako kama mzazi yanategemea na namna maneno yako yanavyooana na yale unayoyafanya. Mtoto anapokuona ukifanya yale yale unayomzuia yeye anakupunguzia alama za ushawishi wako kwake.

Hakikisha unaishi maneno yako. Tenda unayoyasisitiza. Unapomwambia ashukuru anapopewa kitu, kuwa mfano kwa kuwa mtu wa shukrani. Unaposisitiza aombe msamaha, jitahidi kuonesha mfano kwa kuomba msamaha pale unapojikwaa.

Mstahi anapokosea
Unafanya nini pale unapogundua mwanao amekosea? Unamkemea kwa ghadhabu tu kwa sababu ni mtoto? Ni vizuri kuelewa kuwa watoto, kama sisi tulio watu wazima, wanatamani sana kutendewa kwa staha. Unapomtendea kwa staha unamfanya ajione analo deni la kukulipa heshima unayostahili.

Hakuna sababu ya kumkemea mtoto kupita kiasi hata kama unajua ni kweli amekosea. Hakuna sababu ya kumvunjia heshima kwa kumdhalilisha mbele ya rafiki zake. Unapofanya hivyo, ni rahisi kujenga kisasi cha utoto. Usipomstahi mwanao, unapoteza mamlaka yako kwake.

Kwa ujumla, mamlaka yako kama mzazi ni zao la maisha yako yanayohalalisha kusikilizwa. Ukijenga uhalali kama mzazi, hutalazimika tumia nguvu nyingi kutafuta ushiwishi kwa mwanao.
 
Wanasema watoto wanaweza wasiwe wasikilizaji wazuri lakini kamwe hawajawahi kushindwa kufuata au kuiga wanachokiona kwa wazazi/ walezi wao.

Msisitizo ni hapo kwenye kuishi kwa kadri ya unachokiamini na kukihubiri.
 
Ukiwa na pesa, kila anachotaka mtoto wewe unampa tu, lazima akuheshimu


Hii inaweza isiwe sahihi nyakati zote.
Mzee wangu hakuwa na pesa kuasi kikubwa cha kutupatia kila tulichotaka lakini hadi mauti inamkuta namheshimu na sijawahijutia kuwa mwanawe.
 
Dunia ya kisasa na mambo ya kisasa. Mshua wa zamani haki ya nani ungemsikiliza tu na kumheshimu kwa sababu hakukuwa na namna. Shida ni hiki kizazi kipya kilichodekezwa hiki. Kizazi cha swaga za instagram.
 
Back
Top Bottom