Mambo unayohitaji kujua katika ndoto unazoota sehemu ya nane(jambo la 8) by Christopher Mwakasege

Principal Focus

JF-Expert Member
Jan 4, 2013
924
1,000
Jina la Yesu litukuzwe milele na milele!
Tunaendelea tena na somo hili la: “Mambo unayohitaji kuyajua kuhusu ndoto unazoota ili iwe vyepesi kufanikiwa kimaisha”
Leo nataka nikujulishe kimafundisho juu ya jambo la 8 katika mfululizo wa somo hili ya kwamba “Usisahau kutumia Damu ya Yesu ili kuondoa sumu iliyoingia maishani mwako kwa kupitia kwenye ndoto”.
Yesu Kristo alipokuwa anashiriki “chakula cha Bwana na wanafunzi wake- siku ya pasaka -alisema: “Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi” (Mathayo 26:28)
Hii inatupa kujua ya kuwa, ikiwa damu ya Yesu ina uwezo wa “Kuondoa” dhambi: ina maana basi ya kuwa – ina uwezo pia wa kuondoa chochote kinachokuja kikiwa kimeambatana na dhambi!Kufuatana na Warumi 5:12, 17 – shetani alipata nafasi ya kuingia, na kuingiza vitu vyake – katika maisha ya mwanadamu, kupitia kwenye mlango wa dhambi, pale kwenye bustani ya Edeni.Ikiwa ni hivyo – inakuwa ni sahihi kabisa tukiamini ya kuwa, damu ya Yesu inaweza kutumika kuondoa dhambi, pamoja na chochote kile ambacho shetani anakiingiza katika maisha ya mwanadamu!
Tunapojifunza somo la leo – nataka tuangalie jinsi ambavyo unaweza kuitumia damu ya Yesu, kuondoa sumu yoyote ambayo shetani anaingiza kwenye maisha ya mtu, kwa njia ya ndoto.
Mtu mmoja aliniandikia akitaka nimwombee baada ya kuota ndoto ifuatayo: Aliota ameumwa na nyoka kidole cha pili cha mguu wake. Na alipoamka toka usingizini alikuta kidole kile alichoumwa na nyoka katika ndoto aliyoota, kilikuwa kinauma na kinatoa damu.Mtu yule alienda kanisani kwao kwa ajili ya maombi, na alipoombewa walikemea pepo la mauti toka ndani yake. Lakini, hata baada ya maombi yale, maisha yake na uchumi wake viliyumba sana, na kujikuta mara kwa mara, akifukuzwa toka kwenye nyumba alizokuwa anapanga kwa ajili ya kuishi.
Swali la msingi alilojiuliza, na ambalo lilimfanya ahitaji maombi zaidi, ni kutaka kujua ni kwa nini hata baada ya pepo la mauti kukemewa na kutolewa toka ndani yake, bado maisha yake yalikuwa magumu sana!
Nikikupa maelezo kwa kutumia mfano huu ufuatao utaelewa vizuri: Mtu akiumwa na mbu na akimwambukiza ugonjwa wa malaria, hatapata uponyaji kwa kumuua mbu aliyemuuma! Ni lazima pia “aondoe” mwilini mwake “vijidudu” vilivyowekwa na mbu yule kwenye damu yake, na pia “kuondoa” ugonjwa wa malaria alioupata kwa kutokana na vijidudu vile!
Nyoka aliyemuuma mtu yule kwenye ndoto aliyoota, aliacha “sumu” kwenye “maisha” yake! Alipoamka toka usingizini – yule nyoka hakuwepo – ila maumivu yalikuwepo, na damu ilikuwa inatoka kutoka kwenye kidole alichoumwa! Kwa hiyo – nyoka aliondoka – lakini “sumu” ilibaki ndani ya mtu yule! Na unaweza kuona ya kuwa sumu ile ilibeba “mauti” iliyofanya uchumi wake ufe: na ilibeba “hali ya kukataliwa”, iliyofanya awe anafukuzwa kwenye nyumba alizokuwa anapanga!
Bila kuondoa sumu ile ya nyoka na madhara yake kwenye maisha yake, hali mbaya ya uchumi wake isingeondoka; na hali ya kukataliwa isingeondoka!Nilipomwombea mtu huyu – nilitumia damu ya Yesu kuondoa “sumu” ya nyoka aliyemuua – na madhara yake kwenye uchumi wake, na madhara yake kwenye eneo la yeye kuishi.
Kumbuka: Kufuatana na Mathayo 26:28 – “damu ya agano” – yaani damu ya Yesu – ina uwezo wa “kuondoa” dhambi, na kile ambacho shetani anakileta katika maisha ya watu!
Mtu mwingine aliomba nimwombee baada ya kuota ndoto hii: Aliota ndoto ya kuwa kuna mtu anakata kwa kisu kidole gumba cha mguu wake wa kulia. Akaamka toka usingizini kwa mshtuko na akauombea mguu wake usiku ule ule – maana alipoamka alisikia maumivu makali toka kwenye kidole alichoota kuwa kinakatwa na kisu!
Mtu yule alishangaa sana kuona ya kwamba, baada ya miezi mitatu tangu aote ndoto ile, lile eneo la kidole kilichokuwa kinakatwa na kisu kwenye ndoto – pametokea alama nyeusi iliyokuwa inamwasha sana.Ni dhahiri ya kuwa aliombea kidole chake baada ya kuamka toka usingizini, lakini maombi yake hayakugusa “sumu” iliyoingizwa kwenye maisha yake kwa njia ya “kisu” kilichotumika kwenye ndoto aliyoota!
Mimi aliponishirikisha juu ya ndoto hiyo – nilimwombea kwa kutumia damu ya Yesu kuondoa ile “sumu” iliyosababisha kidole kiwe cheusi na kuwasha. Kumbuka: “pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo” (Waebrani 9:22). Lakini kufuatana na Mambo ya Walawi 8:23,24 – “kidole gumba cha kulia” kinasimama kama eneo linaloguswa wakati ulimwengu wa roho unapofuatilia hatua za mtu katika kumtumikia Mungu.
Ni dhahiri kwa kutumia ndoto ile, shetani alitaka “kukata” na “kuzuia” hatua za mtu yule katika kumtumikia Mungu. Nilimwombea pia jambo hilo kwa damu ya Yesu!Na maombi hayo niliyoomba kwa kutumia damu ya Yesu yalimsaidia kuponya kidole cha mtu yule; na kuponya, na kuutunza utumishi aliokuwa nao katika Kristo Yesu.
Unaposhughulika na ndoto za namna hii, ambazo zinaweka na kuacha “sumu” kwenye maisha yako, au ya mtu mwingine – kumbuka hatua zifuatazo:
1. Omba toba kwa ajili ya jambo lolote lililosababisha mtu aote ndoto ya jinsi hii;
2. Kemea pepo la shetani lolote litakalokuwa limeingia kwenye maisha ya mwota ndoto ile, ili liondoke kwenye maisha yake;
3. Weka mkono wako juu ya eneo lililopata madhara kwenye ndoto (kama vile – kidole), huku ukisema “Namwaga damu ya Yesu ya agano jipya kwenye eneo hili (huku ukilitaja hilo eneo), ili kuondoa sumu na madhara yake vilivyopitia hapo kwa njia ya ndoto aliyoota;
4. Ikiwa kumetokea “ugonjwa” au “madhara” ambayo uliyaondoa kwenye hatua ya 3 hapo juu, kumbuka kuomba “mbadala” wake ili utokee hapo. Kwa mfano ikiwa “sumu” ilileta ugonjwa – omba damu ya Yesu iweke uponyaji! Ikiwa “sumu” iliharibu uchumi – basi omba damu ya Yesu itengeneze uchumi ulioharibika!
Hii ni kwa sababu, kwa damu ya Yesu ya agano jipya, Biblia inasema;” aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili” (Waebrania 10:9)!
Mungu azidi kukubariki tunapoendelea kushiriki pamoja katika somo hili.
 

MNFUMAKOLE

JF-Expert Member
Nov 14, 2014
505
500
Nimewahawi kuota nimekatwa mguu wa kushoto! hadi sasa mguu wa kushoto unaniuma kuanzia kidele kikubwa hadi upande wote wa kushoto! yaaani kuanzia mguuni hadi kichwani! sasa nimejifunza kitu! asanteni sana kwa kutushirikisha hili!
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom