Mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kupanga kiwango cha kodi

MAMESHO

JF-Expert Member
Jul 5, 2011
1,361
1,614
MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA WAKATI WA KUPANGA KIWANGO CHA KODI

Ndugu msomaji, karibu tujifunze kwa pamoja mambo ambayo ni muhimu kutazamwa wakati wa kupanga kodi kwa maana huwa zinaathiri maisha yetu ya kila siku. Ni dhahiri kuwa jambo la kodi linazungumzwa kwa namna nyingi, kugusa hisia, mitazamo, na kupima kama lina athari chanya au hasi kwa walengwa. Nachukulia nilichoandika hapa kuwa mawazo yangu binafsi. Natumaini mtajifunza kutoka kwangu, nami nitajifunza kutoka kwenu.

Kodi ni moja ya uthibitisho wa nguvu za utawala. Kodi ipo tangu enzi na enzi; kwa mfano wakati wa Usultani Zanzibar kodi ilikuwa inalipwa kwa mfumo wa bidhaa au huduma. Kwa wakazi na waliokuwa wanafanya biashara au wasafiri wanaopita kisiwani hapo walilazimika kulipa kodi aina mbali mbali. Kwa mfano mwaka 1828-1840 palikuwa kitovu cha biashara. Bidhaa kuu zilikuwa pembe za ndovu, vitambaa, viungo vya chakula na watumwa. Kodi hiyo ilisaidia sana katika maendeleo ya mji wa Zanzibar na kuufanya kuwa kitovu cha biashara Afrika ya Mashariki.

Siku hizi serikali zina mifumo ambayo ni ya kisasa ya ukusanyaji wa kodi. Kodi inaamuliwa iwe kiasi gani, kwa ajili ya nini na ilipwe vipi. Hivyo namna hiyo, huwa inagusa kwenye maisha yetu ya kila siku.

Awali, hili huwa linafanywa na mamlaka husika ambayo imepewa nguvu hiyo. halafu bunge letu huwa linapitisha mapendekezo ya taasisi hizo. Huwa inazingatiwa ni kwa kiasi gani ukusanyaji wa kodi utaathiri walipa kodi, kwa upande mwingine inakuwa ni chanzo cha mapato kuwezesha serikali kuweza kutoa huduma kwa jamii. Kwa upande mwingine hupunguza fedha za ziada kwa watu binafsi na faida za biashara hivyo pengine kukawa na athari kuhusu ajira, matumizi na uwekezaji.

Kwa hiyo mambo muhimu ya kuzingatia ni uwiano sahihi, uhakika, ufanisi na urahisi. Unaweza kusoma zaidi mwandishi Adam Smith (1977) kwenye kitabu chake kinaitwa “The Wealth of Nations” (utajiri wa Mataifa). Kuhusu uwiano sahihi ni kwamba kodi iendane na uwezo wa mlipakodi kulipa na hali ya kiwango cha maisha. Uhakika ina maana kuwa mlipakodi afahamu ni kwa nini na vipi ametozwa kodi hiyo.

Urahisi una maana kuwa zoezi la kukusanya na kulipa liko rahisi kiasi gani. Hapa mlipaji anaweza kulipa moja kwa moja kwa kutumia akauti yake ya akiba au hundi. Mlipaji anapewa siku kadhaa kuweza kukamilisha ulipaji wake. Mlipaji anaweza kulipa kwa kutumia simu au vifaa vya kieletroniki, kwa huduma hii mlipaji anaweza kutozwa gharama ndogo ya utumaji pamoja na tozo ya serikali. Kwa walipakodi ambao wanashindwa kulipa kodi yote kwa mara moja kunakuwa na makubaliano ambayo wanaweza kulipa kwa awamu pengine kila mwezi, au baada ya miezi kadhaa. Vilevile kuna huduma za kieletroniki za kutuma taarifa za kodi ambazo ni rahisi kutumia. Ni vyema ukusanyaji usiathiri mgawanyo na matumizi ya rasilimali za uchumi. Ufanisi utaonekana kwa mfumo mzima unayoendeshwa, ni vizuri usiwe ni mfumo wa gharama kubwa kuliko kodi zenyewe zinazokusanywa au kuvuka kiwango cha bajeti iliyopangwa kwa ajili ya makusanyo.

Mfumo mzuri wa kodi kwa sasa
Mara nyingi mfumo wa kodi unalenga makundi ya walipa kodi au aina fulani ya matumizi na kutogusa baadhi ya maeneo. Wakati mwingine mfumo wa kodi unakosa uwazi, unaweka gharama kwenye bidhaa (kama mafuta, umeme, vifaa vya ujenzi) ambazo ni vigumu kuainishwa kwenye stakabadhi za malipo.

Wakati mwingine mamlaka za kodi zinashindwa kutumia sheria au kuwashtaki wale wanaokwepa kodi kwa namna ambayo itapunguza gharama. Kwa mfano: inaweza kuwatumia mawakala kufanya baadhi ya kazi na hivyo kulazimika kuwalipa gharama za juu.

Kodi na uchumi
Je serikali inaweza kutoza kodi na kupunguza athari kwenye uchumi? Kwa ujumla kodi (katika mapato, uzalishaji, au matumizi ya bidhaa) huleta athari kwa maana hubadili maamuzi kwamba mhusika au kampuni ipate kiasi gani kama kodi isingekuwepo. Hivyo kiwango cha kodi kinaweza kuchochea au kufifisha shughuli fulani za uchumi.
Kwa mfano kodi za uzalishaji wa bidhaa mara nyingi hufanya wazalishaji kuongeza bei ya bidhaa hivyo kujumuisha gharama kwa watumiaji. Wakati bei zinapopanda, wanunuzi wanapungua kwa hivyo wafanyabiashara wanapata mapato kidogo na watumiaji wanatumia kidogo.

Kodi ya mapato binafsi
Kodi hii inapunguza nguvu ya manununzi. Watumiaji wananunua bidhaa chache kuliko ambavyo wangenunua kama kusingekuwa na kodi. Hivyo kupunguza matumizi ya kifahari na yasiyo muhimu kwanza hivyo huathiri viwanda vya bidhaa hizo za kifahari kuliko vingine.

Maendeleo ya uchumi na ukuaji
Kodi ina athiri kwenye ukuaji wa uchumi na maendeleo. Ifahamike kuwa masoko ya kimataifa yako huru, mtaji huenda kwenye nchi ambazo kodi zake ni nafuu ziaidi ya zile ambazo kodi zake ziko juu.
Wakati kodi ya mapato binafsi iko juu, watu hutumia Zaidi muda wao kupumzika kuliko kufanya kazi za ziada. Wakati kodi kwenye akiba ikiwa juu watu wengi hutuma Zaidi fedha zao kuliko kuziweka akiba kwa ajili ya matumizi ya baadae. Kwa ujumla, athari za maamuzi ya wafanyabiashara na makampuni hufanya pesa kidogo iwepo kwa ajili ya uwekezaji na jitihada zinakuwa ndogo kwenye shughuli za biashara.

Hitimisho
Andiko hili limeonyesha kuwa mambo manne yaliyoainishwa ni muhimu sana wakati wa kupanga kiwango cha kodi limegusia kwa uchache mifumo na ukuaji wa uchumi. Je unadhani vitu gani vingine ni muhimu au sio muhimu wakati wa kupanga kiwango cha kodi. Karibu unieleze nami niweze kujifunza jambo kutoka kwako.



Kuhusu mwandishi

Mtanzania, Mwenye Shahada ya kwanza ya chuo kikuu, Mjasiriamali.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom