Mambo muhimu ya kujiuliza mfanyakazi unayetaka kudhulumiwa mafao yako kwenye hii sheria angamizi.

Amalinze

JF-Expert Member
May 6, 2012
6,784
5,283
Katika nchi hii kuna mambo ya ajabu sana, na hili ni mojawapo. Wafanyakazi katika sheria hii mpya wana mambo muhimu ya kujiuliza:

Upitishwaji wa Sheria Hii Mpya
Sheria zote zinazopelekwa bungeni ikiwa pamoja na marekebisho yake, wadau hupewa na nafasi ya kuzijadili na kutoa maoni yao kabla ya kujadiliwa bungeni. Kwa nini mabadiliko ya sheria hayakujadiliwa, yakapitishwa kinyemela bila ya kupata maoni ya wenye mifuko yao? Wamiliki wa mifuko hii ni wafanyakazi, wala si serikali maana serikali haichangii chochote katika mifuko hii.

Uzuri ya Mabadiliko Haya
Wafanyakazi ni watu wenye akili timamu, si punguani wala si watoto kiasi cha kuonekana kuwa kuna watu wengine wanaojua uzuri na faida ya mabadiliko haya zaidi ya wafanyakazi wenyewe. Wafanyakazi wana haki ya kuamua kwa utashi wao juu ya nini kilicho na manufaa kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye, haki hiyo haipo kwa serikali wala bunge au chombo kingine chochote. Kama mabadiliko haya yanafanywa kwa manufaa ya wafanyakazi kwa nini manufaa hayo yasipelekwe kwa wafanyakazi ambao ndiyo wadau wakubwa, wakayadili na kuona faida badala ya kuyapitisha kwa siri?

Wafanyakazi Kunyang'anywa Pesa Yao
Mifuko hii inatunza fedha za Wafanyakazi, si fedha ya serikali. Lakini mifuko inavyoendeshwa hapa Tanzania, imefanywa kuwa ni pesa za serikali na hivyo serikali kuamua kuzitumia pesa hizo kadiri inavyotaka au hata kuiwekea sheria na kanuni bila ya ushiriki kamilifu wa Wafanyakazi ambao ndiyo wachangiaji wa mifuko hii. Serikali imeifanya mifuko hii ndiyo hela ya serikali ya kuendeshea miradi mikubwa ya maendeleo bila kuangalia faida watakayopata wachangiaji wa mifuko hii kwenye hiyo miradi ya maendeleo. Mifuko hii haipo kwaajili ya kuendesha serikali au kugharamia miradi ya serikali, jukumu lake la kwanza ni kuangalia manufaa ya wanachama wake ambao ni Wafanyakazi lakini haki hii ya msingi ya wanachama wa mifuko hii imeporwa na serikali.

Njama za Kuwaibia Wafanyakazi
Faida zinazotajwa na wanaotetea mabadiliko haya ni za kinadharia sana. Katika nchi ambayo ni 6% tu ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi ndiyo walioajiriwa kwenye sekta rasmi, uhakika wa mfanyakazi kuwa katika ajira wakati wote mpaka kufikia umri wa miaka 55 au 65 ni mdogo sana. Wafanyakazi wengi kwenye sekta binafsi wanafanya kazi kwa mikataba ya muda mfupi, na baada ya kumaliza mikataba yao hakuna uhakika wa kupata ajira tena. Mathalani mfanyakazi ameajiriwa mara moja kwa kipindi cha miaka 2, ni vipi atanufaika na mabadiliko haya? Na wakati huo atakapofikisha miaka 55 (kama atafika) atapata nini wakati thamani ya shilingi inaporomoko kila siku na huku mfumko wa bei ukikua kwa kasi ya ajabu? Ndiyo maana mabadiliko haya hayana manufaa kwa wanachama wa mfuko bali ni njia nyingine ya kupokonya hela ya mfanyakazi kwa kutumia lugha ya udanganyifu. Kilio cha wafanyakazi wa Tanzania ni kodi kubwa ya PAYEE, badala ya serikali kusikiliza kilio hiki cha wafanyakazi, imezidi kuwapokonya hata kile kidogo walichokuwa nwakipata wamalizapo mikataba yao ya kazi. Baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakitumia mafao haya kuanzishia miradi midogo midogo, wengine huyatumia kwa kujisomesha na wengine hata kuwasomesha watoto wao ambao kwa vipato vyao vya mwezi wanashindwa kufanya hivyo.

Serikali kwa sasa inachukua karibu 20-30% ya mshahara wa mfanyakazi kama PAYE, sasa imeamua kuchukua tena 20% ya mshahara wa mfanyakazi. Hii ina maana sasa serikali itakuwa ikichukua karibu 40-50% ya pesa yote ya mfanyakazi.

Hoja ya Kuiga Mfumo wa Mataifa Mengine
Kati ya sababu zinazotolewa ni kuwa mfumo huu mpya unafuata maelekezo ya ILO na jinsi nchi nyingine zinavyofanya. Undumilakuwili wa serikali ni kama ifuatavyo. Tumekuwa tukiongelea matumizi mabaya ya fedha za umma yanayofanywa na serikali na watendaji wake. Kwa mfano katika serikali kukifanyika kikao wanalipana posho ya malazi na chakula, na posho ya kukaa. Posho hii ya kukaa hailipwi na nchi yoyote iliyoendelea, ukiwauliza kwa nini wasifuate taratibu zinazofuatwa na mataifa mengine, jibu ni kuwa 'sisi ni taifa jingine na hivyo hatulazimiki kufuata taratibu za mataifa mengine'. Mataifa ya wenzetu kiongozi yeyote ambaye taasisi yake inakumbwa na kashfa, lazima mkuu wa kitengo hicho huwajibika, lakini hapa kwetu ukiwauliza kwa nini tusifuate mfumo huo wa wenzetu, tunaambiwa hutulazimiki kufuata mifumo hiyo maana sisi ni Taifa huru ambalo halilazimiki kufuata taratibu za mataifa mengine, na yapo mengi ya namna hiyo. Inapokuja kwenye suala la kumkamua mfanyakazi, ukiuliza juu ya kodi kubwa anayokatwa kwenye PAYE, utapewa takwimu za kodi za mataifa mengine (hapo haielezwi tena kuwa sisi ni Taifa huru lisilohitaji kufuata juu ya nini mataifa mengine yanafanya). Kwenye hili la mifuko ya jamii nalo wafanyakazi wanaambiwa kuwa ndivyo mataifa mengine yanavyofanya. Wakati katika uhalisia mataifa hayo yana uhakika mkubwa wa ajira kwa watu wake, yana umri mkubwa zaidi wa tegemeo la kuishi, sarafu zao ni imara, na mfumko wa bei upo chini sana ukilinganisha na Tanzania. Serikali iache kuendekeza mambo yanayowadhulumu wafanyakazi wakati huo huo ikiyatetea yale yenye kuwanufaisha viongozi wa serikali.

Wafanyakazi Wanatakiwa Kufanya Nini?

Wafanyakazi Wamiliki Mifuko Yao
Wafanyakazi, katika katiba mpya wahakikishe inaingizwa kwenye katiba mpya kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii ni mali ya wafanyakazi na itasimamiwa na wafanyakazi wenyewe kwa kupitia vyama vyao vya wafanyakazi. Mifuko hii itakapokuwa chini ya wafanyakazi wenyewe itaweza kufanya kazi kwa manufaa ya wanachama wake, itaweza kuanzisha vitega uchumi ambavyo vitamwezesha mwanachama kuwa na gawio la faida maisha yake yote kwa kutegemeana na kadiri alivyochangia. Kwa kiasi cha pesa kinachopatikana kwenye mifuko hii kuna uwezekano mkubwa wa wafanyakazi wanapoondoka kazini kupewa pesa yao yote waliyochangia, na bado wakaendelea kushikilia hisa katika vitega uchumi kutokana na faida zilizopatikana. Hili litaondoa wajumbe wa bodi na wakurugenzi wanaoweza kuteuliwa kwa manufaa ya kisiasa na kisha wakaamua kuwatumikia waliowateua kuliko wanachama wa mifuko.

Kudai Ripoti ya Mchakato wa Mabadiliko ya Sheria
Wafanyakazi kwa kupitia vyama vyao vya wafanyakazi wadai taarifa juu ya mchakato wa namna mabadiliko yalivyofikiwa. Kama ikigundulika kuwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi walishirikishwa lakini wao hawakuwashirikisha wafanyakazi, viongozi wote wa wafanyakazi wafukuzwe kwenye nafasi zao. Kama hilo halitawezekana, basi wafanyakazi wote wajitoe kwenye uanachama wa vyama vyote vya wafanyakazi na kuunda vyama vingine vyenye kufanya kazi kwa manufaa ya wanachama wake na siyo kwa manufaa ya serikali.

Njia za Kisiasa
Wenzetu katika mataifa yaliyoendelea, ikifika wakati wa uchanguzi makundi mbalimali huweka bayana matakwa ya kundi lao, na hutoa tamko kuwa, 'sisi kama kundi mojawapo la kijamii, tutamchagua kiongozi au chama kitakachosimamia au kufanya mambo 1) -----, 2) ----n.k.'. Wafanyakazi wa Tanzania, sasa ni wakati wa kuungana na kuachana na ushabiki wa kisiasa na badala yake kama kundi mojawapo la kijamii kuangalia maslahi ya kundi letu. Ifike mahali, kama wafanyakazi wa Tanzania tutamke kuwa, 'wafanyakazi wote tutakiunga mkono chama au mgombea ambaye atashusha PAYE kwa 25% kutoka ilipo sasa na kwa namna yeyote ile mtu asilipe PAYE inayozidi 20% ya mshahara wake. Pili tuseme kuwa tutamchagua kiongozi au chama kitakachokuwa tayari kuiachia mifuko ya kijamii irudi kwa wanachama wake na iendeshwe na wanachama wenyewe.

Wafanyakazi wa Tanzania tukiendekeza siasa na ushabiki wa vyama, wanasiasa wataendelea kuwachezea wafanyakazi miaka yote huku wao wasiozalisha wakijipangia maslahi mazuri na mazingira ya malipo starehe huku mchangiaji mwenyewe akibakia hoi bin taabani.
 
Back
Top Bottom