Mambo Kumi (10) Ya Kufanya Mwezi Disemba Ili Mwezi Januari Uwe Wa Mafanikio Makubwa Sana Kwako.

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,781
3,074
Rafiki yangu mpendwa,

Mwezi disemba na mwezi januari ni miezi miwili ambayo watu wengi wamekuwa wanaipoteza kwenye maisha yao.

Wengi wanaupoteza mwezi disemba kwa kupunguza kasi ya mapambano, kwa kuwa mwaka unakuwa umefika ukingoni, wengi huona hakuna kikubwa wanachoweza kufanya hivyo wanasubiri mwaka mpya uanze.

Na mwezi januari huwa unapotea kwa sababu wengi huweka malengo yanayotokana na hisia, malengo ambayo hayatekelezeki na mwezi januari unapoisha wanakuwa wameachana na malengo hayo na kurudi kwenye maisha yao ya kawaida.

Kwa wale marafiki zangu waliopata nafasi ya kuwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA, huwa tunauanza mwaka mpya mwezi novemba ili kuepuka kupoteza miezi hii miwili. Wakati watu wanatulia mwezi wa disemba, sisi tunakuwa ndiyo tunachanja mbuga. Na wakati watu wanahangaika na malengo yasiyo sahihi mwezi januari, sisi tunakuwa tumeshapiga hatua kubwa.

Kwa wale marafiki zangu ambao bado hawajapata nafasi ya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, leo nimewaandalia mambo 10 ya kufanya mwezi disemba ili mwezi januari uwe wa mafanikio makubwa kwako.

Karibu sana rafiki ujifunze mambo haya kumi na uyafanyie kazi ili uweze kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.

1. Jikumbushe kusudi la maisha yako.

Kwa kelele za dunia ni mihangaiko yetu ya kila siku ni rahisi sana kusahau kusudi la maisha yako. Na ukishasahau kusudi la maisha yako, huna tofauti na meli ambayo haina uelekeo. Unaweza kwenda kasi sana, lakini haitakusaidia, kwa sababu unakuwa tayari umeshapotea.

Unapofika mwisho wa mwaka jikumbushe kusudi la maisha yako, jikumbushe kwa nini upo hapa duniani, jikumbushe nini kinakusukuma kutoka kitandani kila asubuhi.

Kusudi la maisha yako ndiyo linapaswa kukupa msukumo wa kufanya makubwa. Na unapolikumbuka mara zote, linakuwezesha kuchukua hatua sahihi ili kuweza kulitimiza.

Jikumbushe kusudi la maisha yako na jiulize yale unayofanya yanachangiaje kwenye kufikia kusudi la maisha yako.

2. Utafakari mwaka unaokwenda kuumaliza.

Watu wengi huwa wanauanza mwaka kwa matumaini makubwa, wanaweka malengo makubwa lakini huwa hayamalizi mwezi, wanaachana nayo na kurudi kwenye maisha ya kawaida.

Unapofika mwezi disemba ni wakati mzuri wa kuutafakari mwaka unaokwenda kuumaliza, kuangalia yale malengo na mipango uliyojiwekea na pia kuangalia kwa kiasi gani umeweza kutekeleza.

Kwa yale malengo uliyoachana nayo, jua tatizo ni nini, uliyaweka vibaya au uvivu na uzembe wako ndiyo umekufanya uachane nayo?

Angalia pia fursa mbalimbali ulizokutana nazo kwenye mwaka wako mzima, zile ulizofanyia kazi na zile zilizokupita.

Kwa kuutafakari mwaka unaokwenda kuumaliza, utaweza kuona wapi umefanya vizuri, wapi umekosea na marekebisho yapi ya kufanya.

3. Weka vipaumbele vya mwaka unaofuata.

Kabla hujaweka malengo yoyote, anza kwanza na vipaumbele. Watu wengi wanakosea kwenye kuweka malengo kwa sababu hawajui na pia hawana vipaumbele kwenye maisha yao. Hilo linawapelekea kuweka malengo ambayo hata hawajui wanayafikiaje, kwa sababu yanakuwa hayaendani na hayajapangiliwa vizuri.

Chagua vipaumbele vichache kwa mwaka unaofuata, angalia yale maeneo ambayo ni ya muhimu zaidi kwenye maisha yako, ambayo ukiyasimamia vizuri na kuyafanyia kazi, utaweza kupata matokeo bora sana kwenye maisha yako.

Kwa kujua vipaumbele vyako, utaweza kuweka malengo ambayo ni sahihi kwako na yanafikika.

4. Weka malengo yako kabla mwaka haujaanza.

Watu wengi wanakosea kuweka malengo kwa sababu wanayaweka kipindi ambacho siyo sahihi. Wakati wa mwaka mpya, watu wengi huwa wanakuwa na hisia kali za upya wa mwaka na kwa kuwa kila mtu anasema mwaka mpya mambo mapya, basi na wao wanajiunga na msafara huo.

Wengi wanajikuta wanaweka malengo ambayo siyo yao, wanapoona wengine wameweka malengo fulani basi na wao wanaona wanapaswa kuwa na malengo ya aina hiyo. Kitu kinachowapelekea kushindwa sana kwenye maisha yao.

Wakati sahihi wa kuyaweka malengo yako kwa mwaka mpya ni kabla mwaka haujaanza. Hivyo mwezi huu wa disemba, tenga muda na ukae chini ili kuweka malengo yako kwa mwaka unaofuata. Kupitia tafakari ya mwezi ulioisha uliyofanya, kupitia vipaumbele vya mwaka ulivyojiwekea, unaweza kuweka malengo ambayo ni bora sana kwako.

Weka malengo yako ya mwaka mpya mwezi disemba na wakati wengine wanakimbizana na malengo mwanzo wa mwaka, wewe unakuwa upo kwenye utekelezaji.

5. Kuwa makini msimu wa sikukuu usikuache mweupe.

Mwezi disemba ni mwezi ambao huwa kuna sikukuu nyingi, ni mwezi ambao wengi wana mategemeo makubwa ya kupumzika na kusherekea. Lakini unapaswa kuwa makini sana na kipindi cha sikukuu kwa sababu wengi hujisahau na kuuanza mwaka wakiwa kwenye madeni makubwa.

Hakikisha unajiwekea bajeti ya matumizi yako kwenye msimu wa sikukuu, na usizidishe kabisa bajeti hiyo. Hakikisha unaamua mapema kabisa ni vitu gani utagharamia kwenye msimu huo wa sikukuu na vipi utaachana navyo.

Na kama kuna sherehe ambazo hazina ulazima, zisikuumize kichwa, achana nazo. Hakuna utakachokikosa kwa kuachana na baadhi ya sherehe na mapumziko. Pia kama utaanza kufanyia kazi malengo yako mapema, utakuwa bize kupiga hatua na sikukuu hazitakuwa na madhara kwako.

6. Jitafakari hatua ulizopiga kiafya.

Huwa ni rahisi kuichukulia afya kwa mazoea, lakini pale afya inapotetereka ndipo tunagundua ina umuhimu kiasi gani. Mwezi disemba ni wakati sahihi wa kujitafakari hatua ulizopiga kiafya kwenye mwaka unaomaliza.

Angalia tabia zako kiafya kwa mwaka huo, je umekuwa unafanya mazoezi, ulaji wako umekuwaje, unajilindaje na magonjwa mbalimbali. Angalia uzito wako wakati unaanza mwaka na wakati unamaliza mwaka, je uzito umepungua au kuongezeka?

Unapopata majibu ya tafakari hii ya kiafya, weka malengo mapya ya kiafya kwa mwaka unaofuata. Weka malengo ya kufanya mazoezi zaidi, kula vyakula bora na andika kabisa kilo ngapi unapaswa kupunguza. Kwa wastani mtu mzima anapaswa kuwa na kilo 70, hivyo kama una uzito zaidi ya hapo, moja ya lengo lako kwa mwaka unaofuata ni kupunguza uzito wako. Kwa sababu uzito uliozidi ni chanzo cha magonjwa mengi.

7. Jua ukuaji binafsi uliofikia kwa mwaka unaoisha.

Watu wengi huwa wanaanza mwaka na kumaliza mwaka wakiwa vile vile, kinachobadilika ni wanakuwa wamepunguza siku zao za kuishi, kwa kukikaribia zaidi kifo chao.

Watu wengi wamekuwa hawakui kadiri siku zinavyokwenda, badala yake wanakuwa wamerudi nyuma. Na kurudi nyuma ni dalili tosha za kupotea na kushindwa kufanikiwa.

Kwa mwezi disemba, kaa chini na tafakari ukuaji binafsi uliofikia kwa mwaka unaoisha. Ni vitabu gani umesoma kwa mwaka huo, vitu gani vipya umejifunza, ujuzi upi mpya umeongeza na hatua gani za tofauti umeweza kuchukua kwenye maisha yako, kazi yako na hata biashara yako.

Kama mwaka unaanza na kuisha hujasoma kitabu hata kimoja, hujaongeza ujuzi wowote, kwa hakika umepoteza mwaka huo. Weka mapema lengo la ukuaji binafsi kwa mwaka unaofuata, vitabu utakavyosoma na hata ujuzi mpya utakaojifunza.

Hakikisha kila mwaka wako unapoisha, unaweza kuangalia nyuma na kuona vitu vipya ulivyojifunza na hatua mpya ulizopiga kwenye maisha yao.

8. Pitia namba zako kifedha.

Watu wengi wamekuwa wanaweka malengo yao ya kifedha, kisha kuyasahau na kuendelea na maisha yao mengine. Wakifiri labda kwa miujiza fulani malengo hayo yatajitekeleza yenyewe.

Wengi wanaendesha maisha yao bila ya kujua kiasi halisi cha fedha wanachoingiza, matumizi yao, akiba na hata uwekezaji.

Mwezi disemba ni wakati mzuri kwako kupitia namba zako kifedha. Namba muhimu sana kupitia ni kipato chako halisi, matumizi yako yote, akiba unayoweka na uwekezaji unaofanya.

Kwa msingi tu, kipato kinapaswa kuwa kikubwa kuliko matumizi, unapaswa kuwa na akiba ya dharura na unapaswa kuwekeza sehemu ya kipato chako, kwenye eneo ambalo linazalisha faida kwa ajili ya baadaye.

Kama lengo lako la mbeleni ni kufikia uhuru wa kifedha, lazima uwe makini sana na namba zako kifedha. Kupitia namba zako kifedha linapaswa kuwa zoezi unalofanya mara kwa mara na siyo mwanzo na mwisho wa mwaka pekee.

Weka malengo yako ya kifedha, kiasi gani cha kipato unataka kuwa nacho, matumizi yako ya msingi ni yapi, akiba utaweka kiasi gani na uwekezaji utakaoufanya ni upi.

9. Boresha mahusiano yako na watu wa karibu.

Mahusiano yetu na wale watu wa karibu kwetu ni muhimu sana kwa maisha yenye utulivu kwetu na hata kwa mafanikio yetu. Haya ni mahusiano ambayo tunapaswa kuyaboresha kwa kuyalinda na kuyapalilia.

Unapofika mwisho wa mwaka, tafakari hali ya mafanikio yote muhimu kwako, angalia yapi yanahitaji kuboreshwa zaidi ili uweze kupiga hatua zaidi.

10. Tenga muda wa kuwa na wewe zaidi.

Tumekuwa tunagawa muda wetu kwa kila mtu anayeutaka, ila tunajinyima sisi wenyewe. Muda wote kwa masaa 24 tunapatikana kwa ajili ya wengine, simu ikiita na tukachelewa kuipokea tunaona tumekosa makubwa, ujumbe ukaingia na tukachelewa kujibu tunaona kama dunia itasimama.

Hakuna kitu muhimu kama kupata muda wa kuwa na wewe mwenyewe, muda wako binafsi, wa kukaa na wewe na kutafakari maisha yako yanavyokwenda na hatua unazopiga.

Ni katika muda huu utaweza kujipima malengo na mipango uliyonayo na hatua unazochukua na kuona kama upo kwenye uelekeo sahihi au ambao siyo sahihi. Ni wakati huu ambapo unaweza kujua vipi vipaumbele muhimu kwako na wapi pa kufanya marekebisho ili kufika kule unakotaka kufika.

Hakikisha unajitengea muda wa kuwa na wewe mwenyewe, muda ambao hutakuwa na usumbufu wowote na utaweza kutafakari na kuyapitia maisha yako.

Rafiki yangu mpendwa, hayo ndiyo mambo kumi muhimu sana unayopaswa kuyafanya kwezi disemba kama unataka mwezi januari na mwaka mzima unaofuata uwe mwaka wa mafanikio makubwa kwako.

Nina imani utayafanya mambo haya na mwaka wako utaweza kuwa wa kipekee sana kwako. Nikutakie kila la kheri katika utekelezaji wa haya ambayo tumejifunza hapa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
 
Back
Top Bottom