Elections 2010 Mama Salma, ukishangaa ya Momba utayaona ya UWT

Dingswayo

JF-Expert Member
May 26, 2009
4,019
2,923
Na Mashaka Mgeta

24th October 2010

Akiwa njiani kutokea Sumbawanga mkoa wa Rukwa, Mama Salma Kikwete ambaye ni mke wa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amepokewa kwa salaam ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).


Wanawake waliokuwa katika vijiji kadhaa katika wilaya mpya ya Momba, wakasimama kandoni mwa barabara na kila Mama Salma alipowasalimia (kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na kusomwa kwenye vyombo vya habari), hawakusita kumuitikia.

Walionyesha heshima kubwa kwa Mama Salma. Hawakunyamaza kimya badala yake waliitikia kwa ishara, pale waliponyoosha mikono yao, wakaachanisha vidole ili kuruhusu viwili miongoni mwao vijenge umbo la V, wakavielekeza kwa mke wa Rais Kikwete.
Nilipoisoma habari kuhusu tukio, hilo nilikumbuka andiko lililopo kwenye Biblia, kitabu kitakatifu ambacho msingi wa imani yangu umejijenga hapo (huku nikiheshimu imani za wengine), pale Yesu alipoingia katika mji wa Jerusalem.

Wayahudi walikwenda kumlaki (Yesu), na kutokana na desturi yao, walibeba majani ya miti ya mizeituni, wakaimba na kusema ``hosana, hosana, juu mbinguni…mbarikiwa anayekuja kwa jina la Bwana, hosana juu mbinguni.'

Mama Salma si mfano wa Yesu, lakini kwa historia ya matukio, alikuwa anaingia mkoani Mbeya na akapokewa na wanawake. Yesu alipokewa na Wayahudi walionyanyua matawi ya Mzeituni ambayo wataalamu waBbiblia wanaweza kutoa tafsiri yake kwa usahihi, lakini (Mama Salma) akaonyeshwa alama ya V inayoaminika kutumiwa na Chadema.

"Nimeshangaa kuona haya katika mkoa wa Mbeya…nilipofika karibu na Tunduma, wanawake walininyooshea vidole viwili wakati kila ninapopita, wananishangilia," Mama Salma alikaririwa akisema.
Lakini katika utimilifu wake, tukio la wanawake wa Momba kumnyooshea vidole viwili Mama Salma, lilistahili kuwepo ambapo pamoja na mambo mengine, tafsiri yake ni kuelezea kuchoshwa na taasisi zinazohusika katika maendeleo na ustawi wao.

Wamechoshwa na mipango ya serikali ya CCM, wamechoshwa na mfumo wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) usiowajali wanawake wakulima na wafanyakazi.
Hawaoni matumaini ya kuboresha maisha yao, maisha ya watoto wao, wazazi wao, waume zao na jamii wanamoishi. Hawayaoni matumaini mema. Kesho kwao ni heri ya jana!

Ninaamini Mama Salma alipaswa kuwashangaa wanawake wa Momba. Kwa sababu pengine katika ziara zake mikoa kadhaa nchini, amekuwa akikutanishwa na wanawake waliopo `matawi ya juu'.
Wafanyabiashara, wanasiasa waliojikusanyia fedha kutokana na ushiriki wao wa karibu katika miradi ya kijamii, ndugu na marafiki wa watawala.

Ni wanawake wa aina hiyo ambao (pengine) kila Mama Salma alipoingia mjini, alikuta gharamza zote zimelipiwa. Haitaji kulipia malazi, chai ya asubuhi, chakula cha mchana na jioni, usafiri nakadhalika.
Wanawake waliopo `matawi ya juu' na ambao wanaiishi hali hiyo kutokana na ukaribu wao na watawala, wanachangia, wanalipia…Mama na ujumbe wake wanapita tu!

Sitaki kuhalalisha kwamba huo ni ukweli na uhalisia wa matukio ya ziara za Mama Salma, la hasha. Lakini mazingira yaliyopo yanaweza kuwa kigezo cha kuhalalisha hilo.

Kwa hiyo wanapoibuka wanawake wa vijijini katika wilaya mpya ya Momba kumuonyeshea vidole viwili, tena wakivipunga juu hewani badala ya dole gumba linalotumiwa na CCM ambayo yeye (Mama Salma) ni mwanachama wake, ajue kuwa hiyo ni salaam.

Ni salaam na ishara kwamba wanawake wa vijijini wanaelezea undani wa imani yao, kwamba imejikita katika kile kinachowakilishwa na alama waliyomuonyeshea Mama Salma.

Anashangaa! Kwa nini anapowasalimia wanawake wa vijijini, badala ya kumshangilia kama sehemu nyingine, wanamnyooshea alama za vidole viwili. Anapoiona hali hiyo, ni kwamba wanawake hawaridhishwi na CCM na kama hawaridhishwi na CCM, ni kwamba hawaridhishwi na utendaji kazi wa serikali ya CCM.

Huo tayari unakuwa mfano wa mzigo. Mzigo ambao haumstahili mtu yeyote isipokuwa Rais wa nchi.
Ni kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwamba unapopita mahali ukawakuta watu wanalia kwa sababu ya njaa, unajua kwamba huo ni mzigo wa Raisi.

Bila shaka kama Mwalimu Nyerere angekuwepo hai, kisha akashiriki ziara ya Mama Salma na kuwashuhudia wanawake wa Momba wakinyoosha vidole viwili, angemnong'oneza (Mama Salma) na kusema: "huo ni mzigo wa Raia."

Kwa hali hiyo Mama Salma anapaswa kuishirikisha UWT ili kujadili na kupata kiini cha mapokezi ya vidole viwili kutoka kwa wanawake wa vijijini. Kwamba kutokana na ushawishi wake ndani ya chama na serikali, UWT ina nafasi gani kuhakikisha kwamba matarajio ya wanawake yanafikiwa pasipo kuhusisha itikadi za kisiasa?

Kwa maana ile kuwa mwanachama wa Chadema, CCM, CUF ama taja chama chochote kingine, haimuondolei mwanamke haki ya kupata mahitaji muhimu ambayo bila shaka ni sehemu ya malengo, dira ama mwelekeo wa UWT.

Haitoshi kwa Mama Salma kuwashangaa wanawake wa vijiji vya Momba waliompokea kwa alama ya vidole viwili, bali aingie ndani na kuyaona yanayofanywa na UWT ili kufikia matarajio ya wanawake nchini.
Anaweza kukuta UWT ambayo yeye ni mwanachama wake, haitendi kwa kadri inavyostahili. Haiwafikii wanawake hasa katika ngazi za msingi. Pengine wamebaki kuwa kikundi cha watu wachache wenye maslahi yanayofanana, wakinuia na kushirikishana pamoja.
Kama hali itakuwa hivyo, asishangae atakapoendelea kupokewa na wanawake wanaoonyesha alama tofauti ikiwemo vidole viwili vinavyotengeneza alama ya V.


Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi wa NIPASHE. Anapatikana katika simu namba 0754691540 ama barua pepe:mashaka.mgeta@guardian.co.tz au mgeta2000@yahoo.com.


CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
 
Back
Top Bottom