Mama na mtoto wafikishwa kortini kwa tuhuma za mauaji ya ndugu yao wa damu

JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Feb 7, 2022
1,006
2,703
Mama na mtoto wake wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa madai ya kumuua Beatrice Magombola ambaye ni ndugu yao wa damu moja.

Washitakiwa hao ni Alphonse Magombola (34) mkazi wa Bunju B Mpakani na Sophia Mwenda (61) mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam.

Marehemu Beatrice na Alphonse ni mtu na mdogo wake na Mwenda ni mama yao mzazi.

Akisoma hati ya mashitaka, Wakili wa Serikali Faraja Ngukah alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Ritha Tarimo kuwa watu hao wanashtakiwa kwa mauaji ya ndugu yao.

Ngukah alidai kuwa washtakiwa hao Desemba Mosi, 2020 wakiwa eneo la Kijichi ndani ya Temeke, Dar es Salaam, walimuua Beatrice Magombola.

Baada ya washtakiwa hao kusomewa shitaka lao, mshtakiwa wa kwanza alidai kuwa kwamba kutokana na mateso ya muda mrefu kuanzia Machi 17,2022 na kuendelea, aliumia mguu wake wa kulia.

"Kutokana na kupigwa kwa muda mrefu mguu wangu wa kulia umepata hitilafu. Naomba nipatiwe matibabu," alidai Alphonse.

Hakimu Tarimo alimweleza Wakili Ngukah kama amesikia alichokidai Alphonce na kujibu kwamba amesikia na kueleza kwamba huko mahabusu (Magereza) atakakopelekwa kuna matibabu, kwa hiyo atapata huduma hiyo na kama shida yake ni kubwa atapelekwa hospitali ya rufani.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu alimhoji Alphonse kama ifuatavyo;

Hakimu: Umesema toka lini upo mahabusu?

Alphonsce: Tangu Machi 17, 2022.

Hakimu: Tangu muda huo ulishawahi kupelekwa mahakama yoyote ile?

Alphonce: Sijawahi, nilikuwa Oysterbay Polisi.

Hakimu: Uliwahi kupewa dhamana?

Alphonce: Hapana sikupewa dhamana.

Naye mshitakiwa wa pili, Mwenda, alidai Aprili 18, 2022 alitakiwa aende kliniki, hakupelekwa kutokana na hali hiyo macho yake yanamuuma kwa sababu alifanyiwa upasuaji wa macho, kwa hiyo anaomba apatiwe matibabu.

Pia alidai kwamba Machi 18, 2022 alikamatwa na kukaa Kituo cha Polisi Mabatini siku tatu na baadaye akahamishiwa kituo kingine na kudai kuwa alipigwa sana hadi kupata maumivu ya mguu, mkono na nyonga kwa hiyo anaomba apatiwe matibabu.

Kutokana na malalamiko hayo, Hakimu Tarimo alisema Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji isipokuwa Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka kwa hiyo, ameandika malalamiko yao kwa sababu ya kuweka kumbukumbu.

Kuhusiana na matibabu, Hakimu Tarimo aliwaeleza kwamba mahabusu zote zinatoa matibabu, kwa hiyo watatibiwa na kama hali itakuwa mbaya basi watatibiwa nje ya mahabusu na ana hakika watatibiwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 28, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa. Upelelezi haujakamilika na washitakiwa wamerudishwa mahabusu kwa sababu shitaka la mauji halina dhamana.


Source: IPP
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

0 Reactions
Reply
Top Bottom