Mama Asha Suleiman Iddi awataka WanaCCM kutokimbia vikao

aleesha

JF-Expert Member
Oct 17, 2016
775
1,117
MKE wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, mama Asha Suleiman Iddi, amewataka wana CCM kuchukua tahadhari kwa baadhi ya wagombea waliojitokeza kuwania nafasi za uongozi baada ya kuanza kuvikimbia vikao vya chaguzi zinazoendelea.

Mama Asha, ambaye ni Mjumbe wa Uchaguzi Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilaya ya kaskazini ‘B’, aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa uchaguzi wa wilaya hiyo, uliyowashirikisha wanachama wa jimbo la Kiwengwa, Mahonda, Bumbwini na Donge.

Alisema baadhi ya waliojitokeza kuwania nafasi za uongozi katika ngazi ya shina, matawi hadi wadi, wameanza kukimbia vikao vya juu vya uchaguzi wakati ni wajumbe muhimu katika uchaguzi huo.

Alisema hali hiyo inaashiria kwamba hawako tayari kukitumikia chama jambo ambalo linaweza kukisababishia chama kutokuwa na mipango bora ya ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.

“Asietaka kuchagua wenzake asigombee kwani inanisikitisha kuona watu tuliowapa kura kuwa viongozi katika wadi, shina na matawi, leo hii hawapo katika uchaguzi huu wa wilaya na wao ndio walioomba kazi ya kukitumikia chama,” alisema.

Alisema nia ya CCM sio kutoa ajira bali ni kupata viongozi wazuri watakaoonesha thamani ya chama na kuendelea kubaki madarakani.

Hata hivyo, aliwataka kutokuwa chanzo cha kuharibu uchaguzi, kutokana na tabia iliyojengeka katika mkoa huo kwa wanawake kutopendana kwa kuendeleza vitendo vya chuki na fitina.

Mwenyekiti wa UWT mkoa huo, Miza Kombo Ali, alisema amepata mshtuko baada ya kuona idadi kubwa ya waliopewa nafasi za uongozi katika ngazi mbali mbali katika wilaya hiyo, hawashiriki katika chaguzi zinazoendelea.

Alisema ni vyema kwa wananchama hao kuona umuhimu wa kushiriki vikao vinavyoendelea, ili waweze kuwachagua viongozi waliobakia.

Mapema Katibu wa UWT willaya hiyo, Khadija Juma Khamis, alisema hali ya uchaguzi katika wilaya hiyo ni vizuri na hakuna rufaa iliyowasilishwa ofisi kwake.

Chanzo: Zanzibar Leo
 
Back
Top Bottom